Muswada
wa Katiba mpya
Ahofia
mabavu ya dola kuteka mamlaka ya wananchi
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe
Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Mashirika ya Umma, ametoa maoni yake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Katiba
mpya, unaotyarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano ulioanza mapema wiki hii
bungeni mjini Dodoma. Ili kufahamu zaidi kuhusu maoni ya Zitto, endelea kusoma
makala haya.
KAMA kuna jambo moja ambalo
huunganisha Taifa ni Katiba ya Taifa hilo. Katiba huweka misingi mikuu ya nchi
na namna ya kujenga na kuendesha Taifa. Hivyo Katiba inapaswa kuwa ni matokeo
ya mwafaka wa kitaifa kwenye masuala yote ya msingi ya nchi husika. Tanzania
imekuwa ikiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara. Kabla ya hapo kulikuwa na Katiba
ya Uhuru ambayo ilitokana na mwafaka wa wapigania Uhuru wa nchi yetu, baadaye
Katiba ya Jamhuri ya Tangayika na kisha Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar, kabla ya kubadili jina na kuitwa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Ukiachana na Katiba ya Uhuru, Katiba
nyingine zote hazikutokana na mwafaka wa kitaifa bali matakwa ya tabaka la
watawala. Katiba ya kudumu ya mwaka 1977 ni zao dhahiri kabisa la utawala wa
chama kimoja ambacho kilikuwa na dhamira ya kushika hatamu za uongozi. Kutokana
na hali hii haikuchukua muda kwa wasomi mwaka 1983 kuanza harakati za kuifanyia
mabadiliko makubwa. Kati ya matokeo ya mabadiliko hayo ni kuwamo kwa Haki za
Msingi za Binaadamu katika Katiba katika mabadiliko ya mwaka 1984, miaka saba
tu tangu kuandikwa kwa Katiba ya kudumu.
Takribani mwaka mzima huu kumekuwa
na madai ya kuandikwa kwa Katiba mpya. Madai haya si mapya kwani huibuka na
kusinyaa kila baada ya Uchaguzi Mkuu. Itakumbukwa kwamba mwishoni mwa miaka ya
1990 kundi la vyama vya siasa liliunda Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA)
ili kudai kuandikwa kwa Katiba mpya.
Hata hivyo, safari hii sauti ya
mabadiliko imekuwa ni kubwa sana kiasi cha Serikali kusikia na hivyo kupeleka
bungeni muswada wa Marejeo ya Katiba kwa lengo la kuandika Katiba mpya ya nchi
yetu. Muswada huu umeleta kelele nyingi na manung’uniko mengi sana kutoka kwa
makundi mbalimbali ya jamii kuanzia vyama vya siasa, viongozi wa dini na Asasi
za Kijamii. Baadhi ya Asasi za Kijamii zimeunda Jukwaa la Katiba ili kuweza
kuratibu vizuri juhudi za kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Sababu kubwa ya kupingwa kwa Muswada
wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ni kwamba mchakato umewekwa
kwenye Dola mno na hasa kwenye Urais. Rais anateua tume ya kukusanya maoni,
Rais pia ndiye anateua Bunge la Katiba. Watu wengi tungependa kuona mchakato
unakuwa kwa wananchi zaidi. Serikali imefanya marekebisho kadhaa na kupanua
wigo wa mjadala wa Katiba na pia kumhusisha kikamilifu Rais wa Zanzibar katika
mchakato.
Baadhi yetu tunaona kama nafasi ya
Zanzibar katika mchakato imepewa nguvu kubwa kupita kiasi. Nadhani Zanzibar
inastahili kupata nafasi hii katika mchakato wa Katiba. Jambo ambalo ni vizuri
tulitilie maanani ni kwamba Muungano wa Mwaka 1964 ulihusisha nchi mbili huru
zenye hadhi sawa mbele ya sheria za kimataifa. Linapokuja suala la kuandika
Katiba ya Muungano, pande mbili za Muungano zinakuwa na hadhi sawasawa. Kwamba
Zanzibar ishiriki kwenye masuala ya Muungano tu ni hoja inayojadilika iwapo tu
Katiba ya Muungano ingetofautisha kinagaubaga taasisi za kimuungano na zisizo.
Kwa mfano Sura ya Bunge katika Katiba ni lazima ijadiliwe na pande zote mbili
ingawa Bunge wakati mwingine hupitisha miswaada ambayo si masuala ya Muungano.
Aina ya Muungano wetu inatulazimisha kufanya hivi tunavyofanya sasa. Mkataba wa
Muungano ni lazima uheshimiwe kama ulivyo sasa.
Katiba mpya yaweza kuweka
makubaliano mapya lakini muswada wa sasa ni lazima utambue nafasi halali ya
Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya sasa na Hati za Muugano. Suala hili ni la
kisheria na sio suala la idadi ya watu au ukubwa wa eneo la nchi husika. Nchi
ya Ushelisheli yenye watu 80,000 ina nafasi sawa na Tanzania yenye watu 42
milioni katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika
(AU) na Umoja wa Mataifa (UN). Zote zina kura moja tu. Huu ndio ukweli na
hatuna budi kukubaliana nao.
Muswada unampa mamlaka Rais wa
Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar kuteua Tume ya Katiba. Tume hii
ma-Rais hawatapata ushauri wa mtu mwingine yeyote kwa mujibu wa kifungu cha (6)
na vifungu vidogo (1), (2) na (3). Wanasiasa wakiwamo wabunge, wawakilishi,
viongozi wa vyama ngazi za taifa, mkoa au wilaya hawatakuwa na sifa za
kuteuliwa.
Inawezekana kabisa waandishi wa
muswada walikuwa na mantiki ya kuuondoa mchakato kwenye mikono ya wanasiasa. Nia
hii njema haikufikiriwa vizuri hata kidogo. Njia hii haijengi mwafaka. Tume hii
sio ya wataalamu, ni tume inayopaswa kuwa na sura ya kitaifa. Nafasi ya
wanasiasa katika mchakato wa kukusanya maoni ni muhimu sana katika kuhalalisha
mchakato wenyewe. Tume lazima ionekane ni Tume ya Taifa na sio Tume ya ma-Rais.
Hivyo kipengele hiki cha kuwanyima sifa wanasiasa kinapaswa kufutwa katika
muswada. Wabunge na wawakilishi kwa kuwa ni sehemu ya Bunge la Katiba wasiwemo
katika tume, lakini viongozi wengine wa kisiasa wawe na haki ya kuteuliwa kuwa
wajumbe.
Lakini pia Rais ateue Tume kutokana
na maoni kutoka katika makundi yenye maslahi ya karibu na Katiba ya nchi na
hivi ni vyama vya siasa. Ninapendekeza kwamba katika wajumbe 30 wa tume ya
kukusanya maoni ya Katiba, 10 watokane na vyama vya siasa vyenye wabunge kwa
uwiano wa CCM wawili, CHADEMA wawili, CUF wawili, NCCR wawili, TLP mmoja na UDP
mmoja. Kila chama cha siasa chenye wabunge kupitia kiongozi wake bungeni
kipeleke majina ya watu wanaowapendekeza kuwa katika Tume ya Katiba na kutokana
na mapendekezo hayo, Rais atawateua kuwa wajumbe. Masharti mengine ya nusu
kutoka kila upande wa Muungano yazingatiwe.
Muswada unapendekeza kuwapo kwa
mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume. Kifungu cha cha saba kifungu kidogo
(1), (2) na (3) kinaweka utaratibu wa kupatikana kwa mwenyekiti na makamu
mwenyekiti wa tume. Muswada unasema uteuzi wa mwenyekiti na makamu utazingatia
kwamba mmoja atoke upande mmoja wa Muungano na mwingine upande wa pili wa
Muungano. Ingawa muswada hausemi waziwazi lakini ni dhahiri kwamba mwenyekiti
wa tume atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa
Zanzibar. Sitaki kujenga hoja kwamba mwenyekiti na makamu wachaguliwe na
wajumbe wa tume kutoka miongoni mwao lakini ni dhahiri mwenyekiti wa tume
anapaswa kuwa mtu mwenye heshima kubwa hapa nchini. Ningependekeza kwamba
ma-Rais wateue wenyeviti wenza badala ya mwenyekiti na makamu wake ili kuweka
nafasi sawa kwa pande mbili za Muungano. Hapa nchini tunao Watanzania ambao
wamefanya kazi iliyotukuka katika nyadhifa mbalimbali na sasa ni wastaafu wasio
na nia yoyote ya madaraka ya kisiasa wanaoweza kuongoza vizuri kabisa tume hii.
Ni mapendekezo yangu kwamba Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Sinde Warioba
wawe wenyeviti wenza wa Tume ya Katiba. Uzoefu wao katika uongozi na kuijua
kwao nchi kutasaidia sana kuhakikisha kwamba mchakato wa kukusanya maoni na
kisha kuandika Katiba unakuwa na mafanikio kwa kuzingatia misingi ya taifa
letu.
Muswada unapendekeza kwamba hadidu
rejea za tume zitolewe na ma-Rais. Kifungu cha nane cha muswada kuhusu hadidu
rejea nadhani hakina mantiki sana. Madhumuni ya muswada yanasema pamoja na
mambo mengine muswada unaweka masharti kuhusu hadidu rejea za tume. Wakati huo
huo muswada unasema hadidu rejea zitakuwa ni hati ya kisheria itakayozingatiwa
na tume katika kazi zake.
Mantiki ni kwamba hadidu rejea
zinapaswa kuwa sehemu ya muswada kama ‘schedule’ ili kuzipa nguvu ya
kisheria badala ya tangazo katika gazeti la Serikali. Hadidu rejea zikiwa ni
sehemu ya muswada zitajadiliwa na Bunge na kupitishwa hivyo kuwa ni jambo
ambalo limefikiwa kwa mwafaka wa wawakilishi wa wananchi.
Muswada unataka uamuzi wa kura ya
maoni kuhusu Katiba uwe ni kukubaliwa na nusu ya Watanzania katika kila upande
wa Muungano. Nadhani hapa tunacheza na Katiba ya nchi. Katiba ya nchi inapaswa
kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura wa pande zote za Muungano yaani
kila upande theluthi mbili. Hii itaipa Katiba uhalali (legitimacy) na
hivyo kuheshimiwa na wananchi na watawala. Kuna woga gani uliopo kutaka Katiba
ikubalike na nusu ya wapiga kura? Mifano ya nchi nyingi duniani Katiba inapaswa
kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura. Hata jirani zetu wa Kenya ilikuwa
hivyo na hata kura ya maoni kuhusu mwafaka huko Zanzibar ilikuwa hivyo. Kwa kuwa
Katiba ni chombo cha mwafaka wa kitaifa, muswada utamke kwamba Katiba mpya
itakuwa imepita iwapo theluthi mbili ya wapiga kura watapiga kura ya ndio.
Raia Mwema
No comments:
Post a Comment