Wednesday 23 November 2011

Ubepari wa ulaji riba na ufisadi hautufai…

Ahmed Rajab
NINAYAANDIKA haya nikiwa London,Jiji ambalo siku mbili hizi naona limejiinamia.
Kwa kawaida siku kama hizi huwa ni siku za kushangilia majani yanapopukutika na kubadilika rangi kuwa ya dhahabu badala ya kijani. 
Badala yake Jiji hili limeshika tama, likiwaza yaliyowasibu Wagiriki na  Wataliana.
Mambo yamechacha barani Ulaya na ya huko si hasha yakatambaatambaa na kufika katika fukwe za Uingereza. Wagiriki na Wataliana wote wameziona serikali zao zikiporomoka baada ya nchi mbili hizo kuelemewa na milima ya madeni.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou, ambaye ni mtoto wa waziri mkuu na pia mjukuu wa waziri mkuu (babu yake aliwahi kuwa waziri mkuu mara tatu) alilazimika kujiuzulu ili aipe nafasi serikali mpya ya umoja wa kitaifa ijaribu kuunusuru uchumi wa Ugiriki. 
Yumkini moja ya njia zitazoufanya uchumi wa nchi hiyo upate afueni kidogo ni kwa Ugiriki kujitoa kwenye kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya yuro ya Ulaya.
Waziri Mkuu wa Italia naye, Silvio Berlusconi, aliyekuwa waziri mkuu mara nne kuanzia mwaka 1994 alilazimika pia kuuacha wadhifa huo. 
Berlusconi amepata sifa au ila ya kuwa kichekesho cha Ulaya kwa kashfa za uasherati zilizomvaa.  Hatosahaulika kwa hafla zake za usiku wa manane ambapo anasemekana haikuwa fedheha kwake kuwafanya wasichana wabichi wawe wanacheza dansa wakiwa uchi. 
Mwenyewe akiziita hizo hafla zake kuwa ni ‘bunga bunga’. Kwa vile sasa hana kinga ya uwaziri mkuu huenda akaishia korokoroni kwa ufisadi huo na wa rushwa.
Berlusconi ameondoka madarakani lakini Wataliana wanapata taabu kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa iliyo imara.  Hivyo, Italia huenda ikarejelea mtindo wake wa miaka ya 1960, 1970 na ile ya 1980 uliokuwa ukizifanya serikali za akina Aldo Moro, Mariano Rumor, Giulio Andreotti au za akina Francesco Cossiga, Arnaldo Forlani, Giovanni Spadolini au Amintore Fanfani ziwe zinaporomoka kila baada ya miezi michache au kama zimekaa sana basi kila baada ya mwaka au miaka miwili.
Masoko ya sarafu katika nchi za Magharini yametanabahi kwamba kitisho kwa chumi za nchi hizo hakitoki Ireland, wala hakitoki Uhispani au hata Ugiriki. Zinatambua sasa kwamba kitisho kubwa kwa nchi zilizo kwenye ukanda wa yuro kinatoka Italia.
Kweli deni la Ugikiri si dogo — ni kama yuro bilioni 350.  Lakini deni la Italia ni kubwa mno, takriban yuro trilioni mbili (idadi ambayo hata mtu hajui aiandike vipi kwa tarakimu).
Endapo Italia itanyimwa mikopo zaidi hatua hiyo itazua kuyayuka kwa fedha katika eneo zima la Bara la Ulaya. 
Hayo yatakuwa maafa makubwa si kwa Ulaya tu bali pia kwetu Afrika ambako chumi zetu zimekuwa kama mikia ya chumi za Ulaya.
Kwa hali ya mambo ilivyo sasa, kuna wasiwasi mkubwa kwamba Ufaransa huenda ikazifuata nyayo za Ugiriki na Italia na ikateleza.
Hapa Uingereza juujuu, bila ya shaka, mambo yanaonekana kama ni shwari.  Lakini wenye kuhodhi nyenzo za uchumi si nchini Uingereza tu bali pia hata Marekani na bila ya shaka huko Ujerumani na Ufaransa wanatambua fika kwamba hawana lao jambo.
Imekuwa kama kuna maradhi, tena maradhi mabaya ya kuambukiza, katika chumi za nchi za Magharibi kwa ujumla.  Ubepari umeachwa uchi; rabakitana. Na unachusha.
Mfumo wa wenye nguvu duniani umebiringitia juu chini. Miaka 150 iliyopita hakuna asiyejuwa nani aliyekuwa na nguvu kati ya Bara la Ulaya na China.
Wakati wa Vita ya Kwanza ya Kasumba pale Uingereza ilipoishinda China, Uingereza iliilazimisha China iilipe fidia. 
Si hayo tu bali Uingereza ikanyosha kono lake na kuitwaa Hong Kong. Isitosheke; ikaanza kuwalazimisha Wachina waziweke wazi bandari zao kwa wafanyabiashara Wakiingereza. Hali kadhalika Waingereza wakaitaka China isitumie sheria zake kuwahukumu raia wa Uingereza.
Madola mengine ya Magharibi nayo yakaanza kuitapia China. Yakaanza kuishurutisha iwape uhondo na marupurupu kama hayo waliyopata Waingereza.
Wakati mmoja Wachina waliishika meli iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza na China ikakataa kuomba radhi. Tukio hilo likawapa Waingereza kisingizio cha kuingia tena vitani.  Ndipo ilipoanza Vita ya Pili ya Kasumba. 
Wafaransa nao wakajitosa vitani kuwasaidia Waingereza. Pamoja na Waingereza wakauteka mji wa Beijing na wakazichoma moto kasri kadhaa ambazo mfalme wa China akizitumia kupumzikia katika majira ya kiangazi.
Wafaransa haohao sasa hawana haya na wanaitaka China ilidhamini kifedha Bara la Ulaya.  Kwa ufupi, wanataka China iliokoe Bara la Ulaya na hasa zile nchi zilizo kwenye ukanda wa sarafu ya yuro.
Wachina wanasema hawajui kwa nini wavuke misitu na nyika kwenda kuokoa chumi za Ulaya au kutoa dawa ya kuyaponyesha maradhi ya Ulaya. 
Wafaransa bila ya shaka ni wajanja na wanajua wanachokitaka: wanainyatia ile akiba ya sarafu za kigeni ya China zenye thamani ya dola za Marekani trilioni 2.3.
Na hapa ndipo tunapopaswa kumdhukuru Mzee Karl Marx.  Sikatai kwamba mwanafalsafa huyo alikosea katika baadhi ya utabiri wake.  Wala sikatai kwamba nadharia zake za kisiasa, hasa kuhusu mambo ya utawala zilikwenda kombo.
Hata hivyo, anapohitaji kupongezwa natumpongeze.  Ilikuwa ni yeye aliyesema mwanzo kwamba misingi ya ubepari si thabiti; haiko imara. Matokeo ya hali hiyo ndiyo tunayoyashuhudia hivi sasa barani Ulaya na pia Marekani ambako kima cha wasio na ajira kimepanda kuzidi asilimia 9. Hukohuko Marekani pia kila uchao umasikini unakithiri.
Ubaya wa mambo ni kwamba nchi kama yetu inaona fahari kuzikumbatia sera za kiuchumi zinazowanufaisha wachache sana katika jamii.  Si hayo tu lakini wakubwa wetu wanazikumbatia sera hizo pamoja na maovu yake mengine kama vile ufisadi na ule utamaduni wa jamii ya mtu kumla mtu, chambilecho Julius Nyerere.
Aghalabu hao wenye kuwala wenziwao ni wale walio kwenye madaraka wenye kuyatumia madaraka yao kujinyakulia utajiri ambao mara nyingi huwa ni mali ya umma.
Waliokuwa wakisema Umarx umepitwa na wakati sasa wanasemaje wakiuona utabiri wa Marx kila siku unathibitika kuwa ni wa kweli?  Wala wasihoji kwa kuitaja China na kusema kwamba China imepiga hatua kwa sababu imeukanya Umarx.
Marx hakutaka nchi ziwe masikini.  Lengo lake daima lilikuwa kutaka pawepo na ustawi wa jamii na utajiri wa kiutu. Tafauti ya nadharia yake ni kwamba akitaka wafanyakazi, wenye kuzalisha mali kwa jasho lao, ndio wawe wenye kuuhodhi utajiri. 
Marx hakutaka pawepo jamii ya mabepari wachache wenye kuwanyonya wafanyakazi walio wengi. Akitaka pawepo uadilifu katika mahusiano ya kiuchumi.
Kila siku zikienda tutazidi kushuhudia kuporomoka kwa mfumo wa kibepari wenye kutegemea ulaji wa riba, unyonyaji na ufisadi.  Na kila siku zikizidi tutafungua macho na kuwashuhudia waathirika wakichukua hatua za kuuhujumu mfumo huo.
Hili vuguvugu tuliloliamkia ghafla hivi karibuni takriban katika nchi nyingi za Magharibi za maandamano dhidi ya mabenki ni mojawapo tu ya ushahidi huo.  Halijafika bado kwa kasi Afrika lakini utabiri wangu ni kwamba haliko mbali.
Kama halitochukua umbo kama hilo la Ulaya na Marekani basi huenda likachukua umbo jingine.  Uwezekano huo upo hasa sasa ambapo Marekani, Ufaransa na nchi za Ulaya zikiwa zinajitutumua na kujivimbisha kijeshi barani Afrika toka katika eneo la Sahel hadi Pembe ya Afrika.
Jingine litaloweza kuchochea hali hiyo ni ule uporaji wa ardhi za kilimo barani Afrika unaofanywa na makampuni ya kigeni kwa kushirikiana na vibaraka wa mabepari wenye kutawala sehemu nyingi barani Afrika.
Huko kujifurisha kijeshi kwa Marekani na nchi nyingine za Magharibi barani Afrika pamoja na uporaji wa ardhi na maliasili za Bara hilo ni ishara nyingine kwamba ubepari wa Kimagharibi unatapatapa na unatafuta njia za kujiokoa. Ndiyo maana wengine tunaushikilia ukomredi wetu.
Source: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment