Umoja wa Kiislamu wa Elimu,
Uchumi na Maendeleo Zanzibar (UKUEM), umesema unaunga mkono msimamo wa serikali
ya Muungano na Zanzibar wa kupinga mashoga na wasagaji kutambuliwa kisheria.
Katibu Mtendaji wa Umoja huo, Sheikh Mohammed Mohammed,
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Zanzibar jana,
alisema umoja huo unaunga mkono msimamo uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed
Shein, wa kupinga suala hilo.
Msimamo huo wa serikali unafuatia tishio lililotolewa na
Waziri Mkuu wa Uingereza David Camelon kuzitaka nchi ambazo zinapata misaada
kutoka nchi hiyo kuingiza katika Katiba haki za kuwatambua mashoga na mahusiani
ya jinsia moja ama sivyo zinaweza kunyimwa misaada hiyo.
Sheikh Mohammed alisema kwamba vitendo vya ndoa za jinsia
moja vinakwenda kinyume na mila na utamaduni wa mwafrika pamoja na misingi ya
imani za dini hivyo siyo busara kuruhusu kuwepo kwa sheria kama hiyo.
Alisema kwamba matatizo ya kiuchumi isiwe sababu kwa nchi
maskini kulazimishwa kufuata sheria zinazo kwenda kinyume na mila na utamaduni
wa wananchi wake.
“Bado tunasema kuwa huu ni mwanzo mzuri wa kukabiliana na
viongozi wanaotaka kueneza ufisadi kwa kutumia uwezo wao wa kiuchumi
kulazimisha mila na silka zao zikubalike hata kama zinakwenda kinyume na mila
na utamaduni wa wananchi na imani zao za dini” alisema.
Sheikh Mohammed, alipongeza msimamo ulionyeshwa na viongozi
hao na kwamba unapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kwa sababu kuwatambua
mashoga ni kwenda kinyume dini, mila na utamaduni wa wananchi wa Zanzibar na
Tanzania kwa jumla.
Aidha, alisema wakati umefika kwa viongozi kuwa makini na
mikataba ya kimataifa ili kuepusha sheria zinazotungwa kwenda kinyume na mila
na utamaduni na kutoa mfano wa sheria ya haki za watoto iliyopitishwa mwaka huu
Zanzibar ilikuwa na kasoro kabla ya kurekebishwa baada ya mzazi kuzuiwa
kumchapa bakora mtoto wake.
Chanzo: Nipashe
ADB
No comments:
Post a Comment