SIKU moja baada ya wabunge wa Chadema, kutoka nje ya Bunge na
kutoshiriki mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa
mwaka 2011, wabunge wa CCM na CUF wamepinga hatua hiyo na kusema wenzao
hao wana kusudio la kuchochea vurugu na kuvunja Muungano.
Pia wengi wa wabunge hao waliochangia wamemnyooshea kidole Msemaji
wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, kuwa amewapotosha Watanzania na ni
mwanasheria na mwanaharakati anayepaswa kurudi shule kusoma na pia ni
mchochezi wa kutotaka Muungano na Wazanzibari.
Sambamba na hilo, wabunge hao waliochangia Muswada huo juzi na jana,
walitetea madaraka aliyonayo Rais wakisema si makubwa na anastahili
kuwa nayo kama kiongozi wa nchi.
Tofauti na wabunge hao wa CCM na CUF, Mbunge wa NCCR-Mageuzi wa
Kasulu Mjini, Moses Machali, alikuwa pekee aliyewatetea Chadema kwa
uamuzi wao wa kususia majadiliano hayo akisema wametekeleza matakwa ya
wananchi.
Miongoni mwa waliochangia mjadala huo ni Mbunge wa Wawi, Hamad
Rashid Mohammed (CUF) aliyesema “ni dhambi isiyosameheka kudharau
Wazanzibari waliopiga kura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa halafu
unajifanya wewe (Chadema) ni mkombozi wa watu, Lissu anasema Bunge la
kikatiba halitakuwa na haki kwa sababu wabunge wa Zanzibar watashiriki !
“Mna ajenda yenu (Chadema) ya siri, mnaleta ubaguzi ndani ya Bunge,
sisi (CUF) ndio tuliandamana kudai Katiba na tulipeleka rasimu ya
Katiba, Watanzania wenzangu tusishawishike, maoni ya mabadiliko ya
Muswada yametokana na wananchi, taasisi na Kamati ya Bunge, tuaminiane
na tupendane,” alisema na kupinga wananchi kuandamana nchi nzima kupinga
Muswada huo.
Alihoji kauli ya maoni ya Kambi ya Upinzani kuwa Rais ni dikteta
wakati Rais huyo ndiye aliyeleta Katiba hiyo na kufafanua kuwa tangu
mwaka 1977 hakuwahi kuona Muswada ulioshirikisha wananchi kama huo.
Alisema madaraka ya Rais yameshapunguzwa vya kutosha kama rasimu ya
Katiba kupelekwa kwa wananchi kujadiliwa kabla ya kupitishwa, pamoja na
hadidu za rejea kutotungwa na Rais isipokuwa zimeshawekwa kwenye Muswada
kitendo ambacho Rais amekikubali.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Ummy Mwalimu, alilalamikia wanasheria na wanaharakati bungeni kwamba
ndio wanapotosha ukweli kwa makusudi na kuwataka kuacha kupinga madaraka
ya Rais kwa kumwangalia kama Mwenyekiti wa CCM, bali kama taasisi yenye
madaraka na Katiba ya sasa na kuacha kumwita Rais dikteta.
“Mimi nimekuwa mwanaharakati, najua siasa za uanaharakati, waseme
huko nyuma kuna maslahi ya nani...wakasome tena wanasheria hawa, si
kuleta uchochezi katika nchi yetu,” alisema. Alisema Rais amefanya
uungwana kuwaheshimu na kuleta Muswada huo bungeni kwa ajili ya kuunda
Tume hiyo, vinginevyo Katiba iliyopo inamruhusu kuunda Tume bila hata
kushirikisha wabunge.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) pamoja na
kutaka mamlaka ya Rais yasiingiliwe, alimtaka Lissu anayejiita
mwanasheria na mwanaharakati kurudi darasani kuelimika kutokana na
kupotosha historia ya nchi kwamba Mwalimu Julius Nyerere alihusika
kumomonyoa Muungano kwa kutofuata haki za binadamu, wakati kipengele
hicho kiliingizwa kwenye Katiba wakati wa utawala wake na Zanzibar
kushirikishwa.
Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema Chadema
wakipata Dola hawatautaka Muungano wala Wazanzibari. Mbunge wa Viti
Maalumu, Angela Kairuki (CCM), alishauri wajumbe wa Tume itakayoundwa
walipwe kwa mujibu wa kanuni na malipo ya Serikali na si Waziri wa
Katiba apange.
Pia Mwenyekiti wa Tume awasilishe ripoti bungeni na si Waziri wa
Katiba na misingi na gharama za Bunge la Katiba ziainishwe kwa uwazi
kwenye sheria.
Mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage (CCM) alisema wasiokubaliana na
Muswada huo wanatafuta mwanya wa kuleta vurugu na kuongeza: “Wanaotaka
kuhoji madaraka ya Rais ni wahuni … nimekerwa na kauli ya wenzetu wa
Chadema, taarifa ya Lissu inalenga kuvunja Muungano”.
Hata hivyo, Mbunge Machali tofauti na wenzake, aliwatetea akisema
“watakaopitisha Muswada huu laana za Watanzania ziwe juu yenu kwa sababu
hamkutaka usomwe mara ya pili”.
Alisema wabunge kujikita katika malumbano kunazidi kujenga chuki na
aliwatetea Chadema kutoka ukumbi wa Bunge kutokana na kushindwa
kuvumilia na walifanya hivyo kupinga mwenendo mzima wa kuwasilishwa
Muswada huo.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi
(CCM), aliomba mwongozo wa Spika wa kitendo cha Chadema kutoka nje na
kama vyama vingine vitatoka nje, mjadala wa Bunge utaendeleaje. Spika,
Anne Makinda alijibu:
“Tumekubaliana mikutano yote ya vyama ifanyike saa 7 mchana na
watakaotoka katikati ya mjadala waombe ruhusa, Katibu wa Chadema
hajaniomba wakutane baada ya kipindi cha maswali, nami nilivyowaona
nimewachukulia kama wengine wanavyokwenda kunywa chai”.
Chanzo: Habari leo
No comments:
Post a Comment