WAKUTANA NA OFISI YA SPIKA, UPINZANI BUNGENI DODOMA
MVUTANO
baina ya wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kwa upande mmoja dhidi ya
Serikali na wabunge wa CCM kwa upande mwingine, umevuta nchi wahisani
ambao wametuma maofisa wake mjini Dodoma kuchunguza kiini cha mvutano
uliopo. Ujumbe wa maofisa watano ukiongozwa na Balozi wa Sweden nchini,
Lennart Hjelmaker ulifika katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda
na baadaye kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, Pindi Chana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu
na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila.
Imeelezwa
kwamba ujumbe huo wa nchi ambazo ni wafadhili wa Tanzania, umehoji
masuala mbalimbali kuhusu mchakato unaoanza sasa wa kuiwezesha Tanzania
kupata Katiba Mpya.
Taarifa hizo zinasema, maofisa hao wengi
wakiwa ni wale wanaohusika na ushauri wa masuala ya siasa katika balozi
hizo, wamekuwa wakihoji hatima ya msimamo wa upinzani ambao waliamua
kususia Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
Chana
akizungumza na kwa simu jana alikiri kukutana na ujumbe huo ambao pia
uliwajumuisha maofisa kutoka balozi zilizopo kwenye mabano, Logan
Wheeler (Marekani), Veslemoy Lothe Salvessen (Norway), Mark Polatjko
(Uingereza) na Dk Carol McQueen (Canada).
Maofisa hao wakiambatana
na wengine kadhaa, jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu
Bungeni, walitambulishwa na mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Janister
Mhagama wakiwa kwenye Ukumbi wa Spika.
Chana jana alisema:
“Ndiyo nilikutana nao na walichotaka kufahamu tu ni jinsi mchakato mzima
wa sheria hii ulivyokwenda na hatua zote tulizopitia kama kamati hadi
kufikishwa kwake bungeni.
Alipoulizwa iwapo walihoji suala la
Wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kususia mjadala wa muswada huo,
Mwenyekiti huyo alijibu kwa kifupi tu: “Ndiyo, hata hilo walitaka
kufahamu lilivyokuwa.”
Imeelezwa pia kwamba ujumbe huo ulifika
Ofisini kwa Spika Makinda, lakini haikufahamika mara moja kama walipata
nafasi ya kuzungumza na kiongozi huyo wa Bunge, kutokana na jana
kutokuwepo ofisini.
Wabunge wa upinzani
Juzi usiku, ujumbe
huo ukiongozwa na Balozi Hjelmaker ulikutana na Lissu pamoja na mambo
mengine ukihoji sababu za kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
Ujumbe
huo pia ulihoji hatua ambazo wapinzani hao wanakusudia kuchukua ikiwa
Bunge litatumia wingi wa wabunge wa chama tawala kupitisha muswada huo,
kisha kupata baraka za Rais na kuwa sheria ya nchi.
Pia walihoji
iwapo kuna dalili zozote za kufanya mazungumzo ya kuwezesha pande husika
kufikia mwafaka wa pamoja, ili wote waweze kushiriki katika mchakato wa
kuwezesha nchi kupata Katiba Mpya.
Akizungumzia kukutana ujumbe
huo Lissu alisema: “Ndiyo, nimekutana nao na wamehoji mambo mengi
kwelikweli lakini niseme kwamba inavyoonekana wana hofu kuhusu
investiment (uwekezaji) ikiwa hakutakuwa na makubaliano.”
“Nimewaambia
kwamba sisi msimamo wetu ni kwenda kwenye mahakama ya wananchi,
kuwaambia kwamba tumekataa kuhalalisha mchakato haramu wa upatikanaji wa
Sheria maana tangu mwanzo kanuni na sheria za nchi zilikiukwa.”
Kwa
upande wake, Kafulila pia alikiri kukutana na ujumbe huo jana, bila
kuwapo kwa Balozi wa Sweden ambaye aliondoka Dodoma kurejea Dar es
Salaam, baada ya kipindi cha maswali na majibu.
“Kwangu ni kama
walitaka kufahamu kuhusu mambo matatu, kwanza kwa nini tuliamua kutoka
nje, nilivyotumia nafasi yangu ndani ya Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala nilipoteuliwa na Spika kuingia kwenye kamati hiyo na nini
kinafuata ikiwa muswada huo utapitishwa na baadaye kuwa Sheria,” alisema
Kafulila na kuongeza:
“Kwa kifupi nimewaambia kwamba sababu za
kuondoka ziko wazi na tumezisema mara nyingi, lakini kubwa nimewaambia
kwamba mimi mawazo yangu ni kuwahamasisha wanaharakati na hata wabunge
wenzangu wa Chadema kuona kama tunakuwa na mchakato wetu, sambamba na
ule unaofanywa na Serikali.”
Kafulila alisema mchakato huo
utawawezesha wanaopinga wa Serikali kuwa na mfano wa bora na kwamba
matokeo ya kazi hiyo, yatatumika kuushawishi umma wa Watanzania kupiga
kura ya hapana dhidi ya Katiba ‘haramu’, inayokusudiwa kutungwa kutokana
na mfumo ‘haramu’.
Siku za mjadala zaongezwa
Mjadala kuhusu
muswada huo uliendelea jana na umeongezewa siku hadi leo
utakapohitimishwa majira ya mchana.Habari zilizopatikana zinasema
kuongezwa kwa muda wa majadiliano kunaweza kuathiri ratiba ya Bunge na
kwamba upo uwezekano wa kuongezwa kwa siku moja ili Bunge liahirishwe
Jumamosi.
Mkutano wa Tano wa Bunge, bado unakabiliwa na kazi ya
kujadili muswada mmoja wa sheria na kupokea taarifa mbili za kamati
ambazo kimsingi zinaweza kuhitaji kujadiliwa.
Taarifa hizo ni
ile ya Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa akichunguza tuhuma za Wizara za
Serikali kuchangisha fedha kutoka katika taasisi zilizoko chini yake kwa
lengo la kupitisha bajeti bungeni na ile ya Kamati ya Nishati na Madini
kuhusu sekta ya gesi nchini.
Mashambulizi kwa upinzani
Jana,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira
aliungana na Mawaziri Profesa Anna Tibaijuka wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, Ummy Mwalimu kuchangia muswada huo na kutuhumu kauli
zilizotolewa na Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Tundu Lissu akisema
ni mpotoshaji.
Wassira alisema anakishangaa Chadema kwani wakati
wanagombea Urais mwaka 2010, walisema “Wakichukua tu madaraka nchi hii
watahakikisha wanatubadilishia katiba ndani ya siku 100 lakini sasa hivi
wanabadilika tena wanasema haraka ya nini.”
Alisema hata wasomi
na wanaharakati nao pia wanawapotosha wananchi kwa kusema mambo yasiyo
ya kweli kuhusu mchakato huo. Alisema wasomi wanadai kwamba Bunge
linatunga Katiba wakati wanajua halina mamlaka hayo, badala yake
wanatakiwa kupelekewa wananchi waipitie na kutoa maoni yao.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alisema
kuna kundi la watu linapotosha wananchi kwa kujiona wao wanachokitaka
lazima kiwe hivyo hivyo. Chenge ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alisema kundi hilo linashinikiza wananchi kufuata maoni yao kwa
sababu limejiaminisha kwamba wao pekee ndiyo wanaoweza kutoa maoni yao
yakasikilizwa na zaidi ya Watanzania 40.
Naye Agripina Buyogela
Kasulu Vijijini (NCCR), alisema mchakato wa huo ufuate haki kwa kufuata
hekima za Mwalimu Julius Nyerere wakati wa mchakato wa kura za maoni
kuhusu vyama vingi. Alisema asilimia 80 ilikataa vyama vingi lakini
asilimia 20 ilikubali lakini kutokana na hekima za Mwalimu ilibidi
akubali kura za watu wachache, ndiyo maana mpaka leo kuna vyama vingi.
Muswada huo umekuwa ikipingwa na wasomi kupelekwa bungeni kujadiliwa badala yake wakitaka urejeshwe kwa wananchi.
Mwenyekiti
wa Kigoda cha Taaluma ya Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji alisema
unatakiwa kusomwa kwa mara ya kwanza. Alipendekeza Tume ya Katiba kuwa
na wataalamu wasiozidi 20 badala ya 30, kwani idadi hiyo ni kubwa mno
akitaka pia majina ya wanaotakiwa kuiunda wapendekezwe na vyuo vikuu na
vyama vya kitaaluma na Rais ateue majina kutokana na mapendekezo hayo.
Nahodha aonya
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amelitaka Jeshi la Polisi
kuwakamata wote wanaotishia hali ya amani kwa kutangaza kuitisha
maandamano bila kikomo.
Nahodha alisema jeshi hilo linatakiwa
kuchukua hatua hiyo ya kuwakamata wanaotishia usalama wa raia kwa kutoa
maneno ya uchochezi kwa wananchi ya kuandamana kuhusu katiba kwani ni
kosa.
Wakati Nahodha akisema hayo, Baraza la Vijana la Taifa la
Chadema (Bavicha), kupitia kwa Mwenyekiti wake, John Heche limetangaza
kufanya maandamano katika majimbo ya wabunge wote watakaounga mkono
muswada huo.Habari hii imeandaliwa na Neville Meena, Dodoma Keneth
Goliama, Hussein Issa na Geofrey Nyang'oro, Dar
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment