Thursday 14 March 2013

WATANZANIA WAASWA KUNYWA MAJI KWA WINGI

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewahimiza Watanzania kuwa na tabia ya kunywa maji mengi kila siku ili kujikinga na matatizo ya figo ambayo yanazidi kuongezeka kila siku. Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Machi 14, 2013) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mji wa Arusha waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya Siku ya Afya ya Figo Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya AICC jijini humo. Kaulimbiu ya Siku ya Afya ya Figo Duniani mwaka huu ni “Figo Salama kwa Maisha yako: Epusha Madhara Makubwa kwa Figo” au “Kidneys for Life: Stop Acute Kidney Injury”. Waziri Mkuu
alisema mtoto wa miaka 10 hadi mtu mzima wanatakiwa wanywe maji kiasi kisichopungua lita moja na nusu kwa siku wakati mtoto mwenye mwaka mmoja anatakiwa anywe maji yasiyopungua nusu kikombe (sawa na mililita 100) na kwamba kiasi hicho huongezeka kadri umri wa mtoto unavyoengezeka. “Hii itasaidia kuhakikisha hawaishiwi maji mwilini,” aliongeza.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, imekadiriwa kuwa watu milioni mbili hupoteza maisha kila mwaka kutokana na maradhi ya ghafla ya figo wakati asilimia 20 ya vifo vya wagonjwa waliolazwa hospitalini husababishwa na maradhi hayo.
“Wataalam wanasema maambukizi ya magonjwa hayo husababisha madhara makubwa ya figo (Acute Kidney Injuries) ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa utendaji kazi wa figo. Hali hiyo husababisha watu kupata ugonjwa wa ghafla wa figo (mshtuko wa figo) na pia kusababisha athari kubwa kwenye figo na kuzifanya zishindwe kufanya kazi ipasavyo,” alisema.
Alisema maradhi yanayoweza kujitokeza ghafla na kuharibu figo hayajatiliwa mkazo ipasavyo, hasa katika nyanja za utoaji mafunzo ya tiba, utafiti na elimu ya afya ya figo kwa umma. “Hali hii husababisha kutotumika kikamilifu kwa fursa za kubaini maradhi yanayojitokeza ghafla na kuharibu figo; pia inaathiri utoaji huduma za afya ya figo usiokidhi, na hivyo wagonjwa kulazwa kwa muda mrefu hospitalini,” alisititiza.
Chanzo: MjengwaBlog

Saturday 9 March 2013

Sympathy ya wakenya yamnyanyuwa Kenyatta

Rais Kenyatta akipiga kura
Inavyoonekana katika uchaguzi wa Kenya ni jinsi gani wananchi wa Africa wasivokuwa na imani na mahakama ya kimataifa, duru nyingi zilimpa nafasi Odinga kuwa angeshinda kirahisi hasa ukitizamia kuwa Kenyata anakabiliwa na mashitaka kwnye mahakama ya ICC. Lakini wananchi wa Kenya wamemchaguwa mtuhumiwa kama vile ni kuionesha mahakama hiyo kuwa huyu munaemshitaki kwetu sisi ni lulu. Na tunasubiri tuone jee nchi za kiafrica zitamuunga mkno Kenyata au Marekani na mataifa mengine ya ulaya ambayo yalionesha wazi kumuunga mkono Raila Odinga? Nawapongeza wakenya kwa uzalendo halisi wa kujali utu wao na kutokuburuzwa na mataifa yasiyowapendelea mema. Tungojee tuone.Mungu ibariki Africa

Sunday 3 March 2013

Tukiri Muungano Unazidi Kudhoofika

KWA muda mrefu sasa watu wengi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamika kimya kimya kwamba pamekuwa pakifanyika kile wanachokiona kama mizengwe ya kuwalazimisha kukubali kuongozwa na watu ambao ndugu zao wa Tanzania Bara wanawaona wanaofaa kushika hatamu za uongozi visiwani.
Tafsiri iliyokuwa inapatikana miongoni mwa watu hawa ni kuwa watu wa visiwani hawajui kutenganisha kizuri na kibaya, kile chenye manufaa na maslahi na wao na kile ambacho hakina faida kwao na nchi.
Kwa kiwango kikubwa unaweza kusema watu hawa wamekuwa wanahisi wanaonekana kuwa hawajui tofauti iliyopo ya mbichi na mbivu.
Kwahivyo, njia nzuri ya kuwasaidia ni kuwafanyia uamuzi badala ya wao wenyewe kujiamulia wanataka nini.
Kwa bahati mbaya sana, wale ambao wamekuwa wakilalamikia mwenendo huu, wamekuwa wakipachikwa kila aina ya majina ambayo ni ya kejeli na kumfanya mtu aonekane si mzalendo na hata kupachikwa majina kama vile; “Huyo sio mwenzetu’, ‘Ametumwa’, ‘Hana nia njema’, ‘Anakwenda kinyume na utaratibu tuliojiwekea’ na kadhalika.
Lakini hivi sasa hali inaonekana kubadika, kwani hata baadhi ya wale walioweka chama chao cha siasa mbele kuliko nchi na kudharau uamuzi wa wengi, wameanza kuamka kutoka katika usingizi mzito waliokuwa nao.
Usingizi huu ulijengwa na utamaduni wa kuitikia ‘hewalla bwana’ au ‘hewalla bibi’ na kupiga makofi, hata pakiwa hapana sababu ya kufanya hivyo.
Yote haya yametokana na kutokuwa na ubavu wa kutamka “hapana” au kutoa maoni ya kupinga baadhi ya mwenendo unaotumika katika chama chao kwa kisingizio cha kile walichokuwa wanakiita “jeuri ya chama”. Sijui jeuri hii ni ya maana au vinginevyo.
Lakini sasa wingu la kiza linaonekana kutoweka na mwanga umeanza kuonekana.
Hivi karibuni pameanza kusikika sauti za baadhi ya hao wanaotaka mambo ya chama chao yasiingiliwe, wakielezea hadharani kutaka mabadiliko ili watu wa Zanzibar waachiwe kuchagua wale wanaowaona wao ndio wanaofaa kuwaongoza.
Miongoni mwa sauti zilizosikika zikitaka mabadiliko ya kutaka Zanzibar kuachiwa mamlaka ya kumchagua mgombea urais wa CCM wa visiwa vya Unguja na Pemba, badala ya utaratibu wa sasa unaoshirikisha wenzao wa Tanzania Bara ni ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Vuai anasema suala hilo linajadiliwa, na kwamba ana matumaini kuwa litapatiwa ufumbuzi muafaka.
Anasema ndani ya CCM upo utaratibu ambao chama hicho umejiwekea wa kupata viongozi, lakini suala la kuchaguliwa mgombea urais wa Zanzibar kutoka kwenye vikao vya Dodoma linawagusa, na sasa wapo kwenye mchakato wa kulijadili ili upatikane ufumbuzi.
Hakuelezea mchakato huo umefikia wapi. Hata hivyo, Vuai alikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa hata suala la kupokezana urais kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano na jinsi ya kupata viongozi wengine kama wabunge na wawakilishi, linajadiliwa ndani ya CCM (hakueleza wapi) kwa kina.
Ama kweli zama zimebadilika kwa sababu kwa muda mrefu yeyote yule aliyeweza kujitokeza hadharani kutoa kauli kama hiyo, angelisakamwa na viongozi wenzake wa CCM na angelielezwa kuwa “sio mwenzetu” na “amekwenda kinyume na utaratibu tuliojiwekea”.
Hapa tunachojifunza ni kwamba, kero (au malalamiko) juu ya Muungano hayapo tu katika mfumo na uendeshaji wa shughuli za Serikali ya Muungano, bali hata ndani ya chama tawala cha CCM.
Kutokana na hali hii, tunajifunza kwamba upo umuhimu mkubwa kwa mfumo wa Muungano ukaangaliwa upya na kwa upana na urefu kwa sababu kila kukicha malalamiko yanazidi na kuyafumbia macho sio suluhu.
Ukweli ni kwamba kuyafumbia macho kunaudhoofisha Muungano ijapokuwa tunajaribu kujidanganya kwamba kila siku zikienda mbele unazidi kuimarika, badala ya kukiri kwamba unadhoofika.
Hivi sasa mchakato wa kupata katiba mpya umepamba moto nchini kwetu, na kwa upande wa Zanzibar
suala lililochukua nafasi kubwa ya mjadala na watu wengi hata kuonekana kutojali mengine yote yanayohusu katiba ni hili la Muungano.
Mmoja wa wajumbe wa tume anakiri kwamba Wazanzibari wanatofautiana kwa mengi kisiasa, lakini linapokuja suala la Muungano sauti yao ni moja na unakuwa hujui ni nani CCM , CUF au chama kingine.
Kwa bahati mbaya wapo watu waliotaka Watanzania wanapojadili na kutoa maoni juu ya katiba mpya wasiuguse Muungano kama vile suala hilo limejaa utukufu kama maneno yaliyokuwemo kwenye Kuran au Biblia, na kwahivyo halipaswi kuguswa kwa lengo la kufanya mabadiliko yoyote.
Huu sio mwendo sahihi, na kulipuuza suala la Muungano katika kutenegeneza katiba mpya hakutawasaidia Watanzania waliopo Bara wala Visiwani.
Tunawajibika kuwa wakweli na kuukubali ukweli kwa maslahi yetu binafsi na nchi yetu, hata huo ukweli ukiwa na ladha ya uchungu au maumivu.
Suala la Muungano kwa watu wengi wa Zanzibar, sasa linaonesha kuwa hata ndani ya nyoyo za makada na viongozi wa juu wa CCM, lina matatizo yanayohitaji kushughulikiwa kitaifa na sio kichama.
Kama CCM wanahisi chama chao kinayo haki ya kuendelea kuwachagulia wagombea wa uchaguzi Dodoma, hilo ni suala la wanachama wenyewe kuamua, na wanaweza kuendelea kufanya hivyo kama katiba yao inawaruhusu.
Lakini ni vema ieleweke wazi kwamba hao wanaochaguliwa na baadaye kuitumikia Zanzibar, huwa watumishi wa umma sio wa CCM peke yake.
Suala la kuwepo zamu ya urais kati ya Bara na Visiwani (hizi ni nchi mbili zilizoungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) nalo lisipuuzwe kwa kisingizio cha kwamba Zanzibar ni ndogo kama baadhi ya watu Bara, wakiwemo wabunge walivyojaribu kueleza katika kutaka malalamiko ya watu wa Visiwani yasitiliwe maanani.
Hili ni suala nyeti, na ni lazima hekima na busara itumike na ukweli wa kwamba Zanzibar na Tanganyika ni washirika sawa katika Muungano ionekane kwa vitendo.
Sio vibaya, kama kiongozi wa awamu mbili au tatu akatoka upande mmoja wa Muungano, lakini hii ifanyike kwa ridhaa, na pande zote mbili za Muungano kuwa hazina kinyongo.
Katika miaka ya nyuma mwenendo huu wa uamuzi wa watu wa Zanzibar kuwekwa pembeni na yale ya Dodoma kutawala umezusha hisia mbaya Visiwani.
Wapo watu ambao hadi leo wanahisi wenzao wa Bara hawawatendei haki na kwamba Muungano wa vyama vya ASP na TANU na kuunda CCM na wa serikali mbili (Zanzibar na Tanganyika) umekuwa ukisababisha watu wa Visiwani kuburuzwa na kulazimishwa mbichi kuiita mbivu.
Kwa upande mwingine wapo wanaofanya jeuri ya kuwaambia wenzao wa Visiwani kama hawatamchagua yeye hashituki kwa sababu atapigwa jeki na kura za watu kutoka Bara wanapokutana Dodoma.
Katika mchakato wa katiba mpya, sauti za Wazanzibari juu ya mfumo wa Muungano zimesikika na itakuwa vizuri kama Tume ya Jaji Warioba itaziheshimu na kutozibana katika majumuisho yake kabla ya kuandikwa katiba mpya.
Kinachotakiwa hapa ni nini wananchi wanataka na sio wanasiasa.
Vinginevyo malalamiko juu ya Muungano yataendelea kusikika kila upande na kuwalaumu hao wanaopiga kelele bila ya hoja za msingi.
Hatimaye kitachotokea ni kuzidi kuudhoofisha Muungano ambao Watanzania wengi wanautaka na kuuthamini, lakini wanaonekana kutofautiana juu ya mfumo wake na namna ambavyo baadhi ya shughuli za Serikali ya Muungano zinavyoendeshwa.
Si ajabu watu hao watakaotoa maoni tofauti wakaitwa “Uamsho” kwani huu ndiyo mwenendo wa siasa za hapa nchini.
Hali hii ya kupuuza sauti za wananchi ndiyo iliyosababisha kuonekana baadhi ya watu kuona Bara inaionea na kuisakama Zanzibar, hasa kiuchumi, na wapo wanaohisi na kuamini kuwa Zanzibar inadekezwa ndani ya Muungano, na kwa kweli inafaidika zaidi kuliko upande wa pili wa Muungano.
Yote haya yatakwisha kama dosari za Muungano zilizopo zitashughulikiwa vyema kwa manufaa ya watu wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano.
Chanzo: Tanzania Daima

Friday 1 March 2013

Kama Muungano wetu ni Zimbabwe na Pemba, tutarajie nini kidato cha nne?

MIONGONI mwa habari ambazo zinatawala kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini mwetu, ni matokeo ya kutisha ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa wamefeli.
Ingawa matokeo hayo yamewashitua wengi, lakini kimsingi halikuwa jambo lisilotarajiwa. Kwa muda mrefu, sekta ya elimu imekuwa ikipewa kipaumbele kwa kauli zaidi kuliko vitendo vya dhati. Wakati chama tawala, CCM, ambacho kwa vyovyote vile hakiwezi kukwepa lawama kuhusu matokeo hayo mabovu, kimekuwa mahiri kuonyesha kuwa kinathamini sana umuhimu wa elimu, na hivyo kuipigia mstari katika kila manifesto zake za chaguzi kuu zilizopita, ukweli unabaki kuwa sekta ya elimu imekuwa ikipuuzwa.
Pengine, huwezi kuelewa mazingira mabovu yanayozikabili shule mbalimbaliza msingi na sekondari mpaka utoke nje ya miji. Kimsingi, wanafunzi wengi katika maeneo ya vijijini wanasoma katika mazingira magumu sana, na kitu pekee kinachowasukuma wazazi kupeleka watoto wao shuleni ni ukweli kuwa bado wanaamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, hata kama ufunguo huo umepotea au haupo kabisa!
Binafsi, nadhani moja ya sababu kubwa za matokeo hayo mabaya ni mgogoro wa muda mrefu kati ya Serikali na walimu. Kilio kikubwa cha walimu kimekuwa ni kuitaka Serikali iboreshe mazingira ya utoaji na upatikanaji wa elimu, hususan kwenye maeneo ya mishahara na makazi ya walimu, pamoja na vitendea kazi vyao, sambamba na nyenzo muhimu kwa wanafunzi kama vile madarasa na madawati.
Hata hivyo, kama ilivyozoeleka kila inapojitokeza migogoro kati ya Serikali na watumishi wake, ubabe ulitawala kuliko busara. Pasi kujali busara kuwa ‘unaweza kumpeleka punda mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji,’ walimu walipoonyesha dalili ya kuchoshwa na ‘kupuuzwa kwao’ na kufanya migomo ya hapa na pale, walishurutishwa kurejea mashuleni kufundisha.
Pengine walimu wanaweza kulaumiwa kwa matokeo hayo mabaya, na tayari kuna taarifa kuwa watachunguzwa na Serikali, lakini ni muhimu kabla ya kuwalaumu tukaelewa kwa undani mazingira ya kazi ya walimu wetu.
Binafsi, ni mhanga wa kumomonyoka kwa mfumo wetu wa elimu, ingawa si kwa kiasi kikubwa. Nilikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza wa shule ya sekondari ya Kilombero, kule Ifakara, mkoani Morogoro, ilipoanzishwa mwaka 1986.
Pamoja na kufanikiwa kuwa mmoja wa wanafunzi wanne waliopata daraja la kwanza miaka minne baadaye, lakini ukiachilia mbali masomo ya sanaa (arts), tulisoma masomo ya sayansi kama vile Kemia, Fizikia na Baiolojia kwa nadharia tu kwani maabara yetu ilikuwa ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Nilipokwenda kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Wavulana Tabora (Tabora Boys’), nikakumbana na tatizo la ukosefu wa mwalimu wa somo la Jiografia, ambapo ilitulazimu kwenda shule ya jirani ya Sekondari ya Wasichana Tabora (Tabora Girls’) kumfuata mwalimu wa somo hilo. Na japo nilifanya vizuri kwenye mitihani ya kuhitimu kidato cha sita, uzoefu niliopata unanikumbusha mengi kuhusu sekta ya elimu huko nyumbani.
Lakini angalau wakati huo nilipokuwa mwanafunzi kulikuwa hakuna vitu vinavyoweza ‘kumpa faraja feki mwanafunzi.’ Hapa ninazungumzia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ambapo tunakutana na vitu kama Facebook,YoutTube, BBM na kadhalika.
Ingawa kwa maeneo ya vijijini upatikanaji wa teknolojia hiyo bado ni wa kubahatisha, ni rahisi kwa wanafunzi wa mijini ‘kumalizia hasira zao za shuleni’ kwa ku-chat kwenye Facebook, kutumiana meseji kupitia BBM au kuangalia video huko YouTube!
Na ni wazi kuwa mwanafunzi anayetumia muda mwingi kwenye vitu kama hivyo, anajinyima nafasi ya kujisomea na hivyo kujitengenezea mazingira mazuri ya kufeli. Lakini wakati ni rahisi kukilaumu ‘kizazi cha Facebook’ ni vema tukatambua pia ili mwanafunzi aweze kujisomea, sharti awe na kitu cha kusoma.
Ukichanganya ufundishaji wa walimu ‘wanaofunika kombe ili mwanaharamu apite’ (wanatimiza tu wajibu wao) na uhaba wa vitabu vya kiada, hata mwanafunzi mwenye kiu ya kujisomea binafsi anakuwa na wakati mgumu kufanya hivyo.
Tukiweka kando lawama, ni vigumu japo kufikiria jinsi taifa letu linavyoweza kuirejesha elimu kwenye viwango kama vile vya zama za Ujamaa. Ninasema ni vigumu kwa vile kinachohitajika zaidi si kauli za porojo, bali uwekezaji wa kutosha katika sekta ya elimu.
Na ili uwekezaji huo uwezekano, inalazimu kuwapo na fedha. Sasa wakati Tanzania yetu inakabiliwa na deni la ndani na nje lenye thamani ya matrilioni ya Shilingi, na huku watawala wakigoma kuelewa kuwa sisi ni masikini na tunapaswa kupunguza matumizi ya anasa zisizo za lazima, tutakuwa tunajidanganya tukidhani kuwa uwekezaji huo katika sekta ya elimu utawezekana.
Vipaumbele vya watawala wetu vipo katika kuboresha maslahi ya wabunge badala ya kuboresha walau mazingira tu ya shule zetu, achilia mbali maslahi ya walimu. Ni busara gani iliyotumika kuongeza posho na mishahara ya wabunge wetu hadi kufikia zaidi ya Shilingi milioni 10 kwa kila mmoja ilhali shule kadhaa hazina madawati na majengo yake ni ya ‘mbavu za mbwa?’
Kuwaruhusu wanafunzi waliofeli warudie mitihani ilhali watajiandaa na mitihani hiyo katika mazingira yaleyale yaliyowafelisha mwanzoni, ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Kuwachunguza walimu ilhali sababu zilizopelekea matokeo mabaya zinajulikana, ni kutafuta mchawi asiyekuwapo.
Lakini tunaweza kwenda mbali zaidi na kuihoji Serikali kama kweli inathamini sekta ya elimu. Hivi kama Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, anaamini kuwa Muungano wa Tanzania ni matokeo ya Muungano wa visiwa vya Zimbabwe na Pemba, tutarajie nini kwa mwanafunzi wa kawaida?
Na Waziri Mulugo anataka Serikali isilaumiwe, bali wadau wote wa elimu waangalie uwajibikaji katika nafasi zao. Kwanini asionyeshe mfano kwa kuwajibika yeye kwanza, kisha adai wengine waige mfano wake? Kimsingi, huyu mtu hakustahili kuendelea kushika wadhifa huo baada ya ‘mchemsho’ wake wa Muungano. ‘He is a pretty bad influence.’
Nimalizie makala haya kwa kuikumbusha Serikali kuwa mpango wake kabambe wa maendeleo ambao unaojumuisha hatua kama kuwawajibisha mawaziri walioshindwa kazi, hauwezi kufanikiwa kwa stahili hii inayoonekana katika picha hii. Badala ya kusubiri mawaziri waboronge, ingekuwa vema mpango huo ukaanza kwa mifano hai na kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, ambaye ameshatamka kuwa hatojiuzulu, na Naibu wake Mulugo, ambaye ameshaliaibisha taifa vya kutosha.

Chanzo: Raia Mwema

Tusikipuuze kitisho cha ugaidi, tusikikuze pia

SITI binti Saad, malkia wa waimbaji wa kike Wakizanzibari, aliwahi kuimba nyimbo iliyokuwa na maneno: “Unguja ni njema, atakaye naje.”
Siti aliyaghani maneno hayo kwa madaha na maringo zaidi ya miaka 60 iliyopita lakini majisifu yake ya kuiringia nchi yake bado yanasibu.
Unguja na Pemba yake zote ni njema. Atakaye naje. Lakini aje kwa udhu na heshima. Aje akitambua kwamba Zanzibar ina maadili yake.
Visiwa hivyo vinaendelea kuwa visiwa vya amani na utulivu. Utulivu huo ndio moja ya sababu zinazowavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuizuru Zanzibar licha ya shida ilizo nazo za miundombinu.
Jengine lenye kuwavutia wageni ni ukarimu wa watu wake na upendo wao wa kuishi kwa amani. Kadhalika wenyeji wake wana moyo mkunjufu kwa wageni na ndio maana Wazanzibari wakawa hivi walivyo na michanganyiko yao ya damu.
Tena ni watu wavumilivu. Nchi yao iliyo ya Kiislamu ndiyo chimbuko la Ukristo katika Afrika ya Mashariki. Kutoka huko Ukristo ulivuka bahari na kuenea katika eneo zima la Maziwa Makuu na bara ya Afrika ya Mashariki.
Hatusemi kwamba kwa kuwa na taswira hiyo Zanzibar ya leo ni pepo. Wala hatusemi kama hakuna vitendo vya uhalifu vinavyotokea.
Uhalifu upo. Mfano mmoja ni tukio la Februari 17 la kuuawa Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki. Hicho kilikuwa ni kitendo cha uhalifu wa kinyama.
Binadamu yeyote yule anayedhulumiwa maisha yake akiwa padri asiwe padri anastahiki kuliliwa. Na aliyemuua anastahili kulaaniwa na kuapizwa kwa maapizo yote tuyajuayo. Tena asakwe mpaka apatikane ili atiwe adabu kama inavyostahiki.
Hadi sasa hakuna aliyejitokeza kudai kwamba alihusika na mauaji hayo na sababu gani zilizoyasababisha.
Serikali ya Zanzibar nayo hadi sasa haijatwambia mauaji hayo yalitekelezwa na akina nani. Haijatwambia kwa sababu ingali inaendelea na upelelezi na bado haijui wahusika ni nani na sababu gani zilizowafanya wamuue Padri Mushi.
Inasikitishakuona kwamba badala ya kusubiri matokeo ya upelelezi unaofanywa baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Muungano pamoja na baadhi ya viongozi wa Kikristo na vyombo vya habari wameyarukia mauaji hayo na wanayatumia kama fimbo ya kuwapigia Wazanzibari.
Mmoja wa viongozi walioshangaza ni Waziri wa Mambo ya ndani wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye mara baada ya Padri Mushi kuuawa aliruka na kuanza kutoa matamshi yasio na ithibati yoyote kwamba walioua ni ‘magaidi’.
Hivi karibuni aliuawa mchungaji Mathayo Kachila wa Kanisa la Pentekoste la Assemblies of God huko Geita lakini hatukumsikia Nchimbi akishutumu kwamba Kachila aliuliwa na magaidi. Wala hatukumsikia akitoa shutuma kama hizo Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga alipomwagiwa tindikali au alipopigwa mapanga imamu wa msikiti Sheikh Ali Khamis Ali na kuuawa.
Kwa vile Nchimbi hana ushahidi matamshi yake yanakua matamshi ya uchochezi wenye kutia fitina. Dhamira yake ni kuipaka tope Zanzibar na kuufanya ulimwengu uamini kwamba kuna mtandao wa kigaidi Visiwani wenye lengo la kuwaua Wakristo.
Nchimbi akijua vilivyo kwamba vyombo vya dola vinavyohusika vilikua vikiendeleana upelelezi na kwamba serikali yake imeiomba Idara ya Upelelezi ya Marekani (FBI) iisaidie.
Inavyosemekana ni kuwa mashirika kadhaa ya kigeni ya upelelezi na ya kijasusi yameombwa yaisaidie serikali katika upelelezi huo. Nimedokezwa na chanzo kimoja nje ya Tanzania kwamba Shirika la Ujasusi la Israel, Mossad, ni mojawapo ya mashirika hayo.
Mwaka juzi Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliizuru Kenya. Baada ya ziara yake ofisi ya waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga ilisema kwamba Netanyahu aliahidi kusaidia kuunda ‘muungano dhidi ya itikadi kali ya kidini (ya Kiislamu)’ utaoziunganisha nchi za Kenya, Ethiopia, Sudan ya Kusini na Tanzania.
Mwaka jana nilitahadharisha kwenye gazeti hili kwamba kuna watu nchini wasioridhika na Maridhiano yaliopatikana Zanzibar. Niliandika kwamba wakitakacho watu hao ni kuzusha fujo Zanzibar zitazoweza kuisambaratisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hata kuzusha hali zitazosababisha mchakato wa Katiba usimamishwe.
Mkakati wao ni kuwatumia vijana wachochee fujo kwa kuwatomeza wenye jazba wachome moto makanisa ili ulimwengu uamini kuwa kwa Wakristo na Wabara Zanzibar hapakaliki.
Watasema kwamba wenye kuleta fujo hizo ni wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho. Halafu watawahusisha viongozi wa Jumuiya hiyo na mtandao wa kigaidi wa al-Qa’eda na kwa mpigo mmoja watawahusisha viongozi wa CUF na Uamsho na harakati zao.
Tangu nitoe indhari hiyo shutuma zote hizo zimetolewa hata kabla ya kuuliwa Padri Mushi. Na sasa zinazidi kushadidiwa.
Wenye kutoa shutuma hizo wanatumai kwamba wataweza kuwafanya wakubwa wa dunia hii waiangalie Zanzibar kwa jicho jingine. Wanachotaka hasa ni kuzizima harakati za kuujadili Muungano na kuudhoofisha mshikamano wa Wazanzibari.
Wengine wenye kushtusha ni waandishi wa habari walioamua bila ya kufanya utafiti wowote kwamba magaidi wenye funganisho za kimataifa ndio waliomuua Padri Mushi, kwamba magaidi hao wanahusika na Uamsho. Na kuna waliosihi jumuiya hiyo ipigwe marufuku.
Ukweli ni kwamba kwa muda unaokaribia miezi sita viongozi wote wa Uamsho wameshikwa na wako jela wakisubiri kesi walizoshitakiwa. Muda wote huo wafuasi wao hawakufanya fujo. Wameusikiza (wametii) wito wa viongozi wa kisiasa Visiwani wakiwataka wawe watulivu.
Waandishi wengine wakafika hata kudai kwamba hao ‘magaidi’ wana wenzao ndani ya Serikali ya Zanzibar.
Huo ni uzushi na uzandiki usiofaa kuandikwa na mwandishi yoyote wa maana. Ukweli tuujuavyo ni kwamba hakuna ushahidi wowote wenye kuonyesha kwamba kuna mtandao wa kigaidi Zanzibar wenye kuwalenga Wakristo.
Kitisho cha ugaidi kipo Tanzania nzima na kinatokana na magaidi wa Al-Shabaab wenye kutishia amani ya kanda ya Afrika ya Mashariki.Lazima taifa liwe macho kukikabili lakini tusikikuze kuliko kilivyo.
Ukweli mwingine ni kwamba Waislamu wa Zanzibar, ambao takriban ni asilimia 98 ya wakaazi wa visiwa hivyo, wataendelea kuishi kwa amani na ndugu zao wachache Wakikristo na Wakihindu.
Ikiwa nia ya maadui wa Zanzibar ilikuwa kuyatumia mauaji ya Padri Mushi kwa kuliharibu jina la Zanzibar na kuyadanganya mataifa ya nje kuhusu ugaidi basi hawakufanikiwa.
Madola ya Magharibi hayakushtushwa na matamshi ya Nchimbi na ndio maana hayakutoa taarifa za kuwazuia au hata kuwatahadharisha wananchi wao wasiizuru Zanzibar.
Chanzo: Tanzania Daima