Friday 25 November 2011

SMZ yaitupia Serikali ya Muungano gharama za Katiba Mpya

Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary, amesema Zanzibar haitachagia gharama za kufanikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania.
Abubakary alisema hayo wakati anafunga mjadala kuhusu katiba mpya katika kongamano lililofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo mjini hapa jana.
Alisema gharama zote za kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya zitabebwa na Serikali ya Muungano ikiwemo vifaa, malipo ya makamishina wa Tume, Wajumbe wa Bunge la Katiba na watendaji wa tume.
“Mfuko wa Fedha wa Muungano ndiyo utatumika kufanikisha kazi zote na sie Zanzibar ndio tumenufaika zaidi katika hilo,” alisema.
Hata hivyo, hakutaja kiasi cha fedha ambacho kinatarajiwa kutumika kama gharama za kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya ambayo inatakiwa kuwa imekamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Waziri Abubakary alisema wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watakuwa sehemu ya Bunge la Katiba pamoja wajumbe 116 ambao watatoka katika asasi za kiraia Tanzania Bara na Zanzibar.
Kuhusu kero za Muungano, Waziri huyo alisema wananchi watumie fursa hiyo kutoa maoni yao juu ya mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika mabadiliko ya Muungano.
Alisema zipo kero za Muungano na kutoa mfano kwamba wapo mabalozi wa Tanzania nje ya nchi 30, lakini Wazanzibari ni watatu tu.
Waziri huyo alisema katiba ni mali ya wananchi na itajengwa na wananchi wenyewe na ndiyo maana serikali imeamua kuwapa nafasi wananchi ya kutoa maoni kabla ya kuandikwa upya kwa katiba hiyo.
Kuhusu urasimu wa upatikanaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, alisema wapo watendaji wa SMZ wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa makusudi kwa malengo ya kutaka kuchafua hali ya kisiasa ya Zanzibar
Hata hivyo alisema Serikali ya Umoja wa kitaifa ipo macho na haitokubali kuona Wazanzibari wananyimwa haki ya kupinga kura ya maoni kwa kukosa Vitambulisho hivyo.
Viongozi wengine waliyoshiriki katika mjadala huo ni Waziri wa Afya, Juma Duni Haji; Waziri Asiye na Wizara Maalum, Haji Faki Shaari; Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Mrajisi Mkuu wa Serikali, Abdallah Waziri na viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment