Sunday 13 November 2011

Muswada wa Katiba moto

13th November 2011
 Wanasiasa, wanazuoni wakataa usisomwe mara ya pili

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amehoji juu ya madaraka makubwa aliyopewa Rais katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Kafulila alihoji hayo jana katika semina ya wabunge juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba 2011, iliyofanyika katika Ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma.
Alisema kuwa amepata wasiwasi baada ya kumsikiliza Profesa Issa Shivji, wakati akitoa uzoefu wake kwa wajumbe wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala kuhusiana Muswada huo.
Kafulila ni miongoni mwa wajumbe walioongezwa katika kamati hiyo na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kupitia kabla ya kusomwa mara ya pili kesho (Jumatatu).
Alisema Profesa Shivji alibainisha madaraka makubwa aliyopewa Rais katika uundaji wa Tume ya Katiba.
Alisema ameshangaa kuona Mkuu wa Shule ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi, akisema kuwa hakuna wasiwasi na jambo hilo kwa kuwa la msingi ni kuaminiana.
Kafulila alisema ni lazima kutazamwa kwa ukubwa wa madaraka ya Rais. “Huwezi kutenganisha siasa na utawala kwa kufanya hivyo utakuwa na dola na sio umma,” alisema.
Profesa Kabudi na Profesa Romwald Haule kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), walikuwa wakitoa kwa wabunge kuhusiana na muswada huo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema kwamba suala la mchakato wa Katiba Mpya halikueleweka vizuri kutokana na kuwepo kwa maoni tofauti .
Alisema awali ilipendekezwa kuundwa Tume ya watalaam na baadaye ikaja uamuzi wa kwenda bungeni na kwamba hiyo inaonyesha hakuna kuelewana.
Alisema huko mbele huenda kukawepo na kutosikilizana na kuwa kutokana na utata huo akatoa mfano kwamba kura ya maoni itakapopigwa ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ndiyo itakayoratibu zoezi hilo.
Hata hivyo, alisema Nec bado haikubaliki miongoni mwa wananchi.
Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Anne Kilango, aliwataka wabunge wenzake kumuunga mkono kwa kuto uchambua muswada huo ili wasiharibu ladha.
Alisema wataalamu hao wa mambo ya Katiba wamewatoa somo kwa kiwango kikubwa cha uelewa kuhusiana na Katiba.
Alitaka muswada huo kurushwa na telivesheni za nchini ili kuwawezesha wananchi wengi nchini kutazama na kupata elimu waliyoipata wabunge.
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema michakato ya kuandika katiba mpya ipo katika nchi nyingi barani Afrika, akahoji vipi katika nchi za Ulaya.
Alisema baadhi ya mambo yamezuiwa kujadiliwa katika Ibara ya Tano ya Katiba na kutaka kupata mawazo kutoka kwake wataalamu hao kuhusu tatizo lililopo kwenye jambo hilo.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, aliwataka wabunge kuzingatia elimu waliyoipata katika semina hiyo ili wasije kukwamisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugola, alisema wanaharakati wamekuwa wakiwapotosha wananchi kuhusiana na muswada huo na kwamba mambo wanayoyazungumza hayaendani na usomi wao.
Alihoji ni nini kinachowaharibu wanaharakati hao wanapokuwa katika shughuli zao za uanaharakati.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Chiku Abwao, alisema wanaharakati wametoa mchango mkubwa kuhusiana na kupatikana na Katiba Mpya kwa kuwa ndio waliokuwa wa kwanza kuidai.
Akiwasilisha mada hiyo, Profesa Kabudi, alisema pamoja na kwamba Katiba Mpya itapatikana lakini haitakuwa ya kudumu.
Alitoa mfano kwa nchi ya Kenya ambayo ilipata Katiba Mpya mwaka jana, lakini hivi sasa wameandaa muswada wa mabadiliko ya Katiba hiyo.
Kwa upande wake, Profesa Haule, alisema kinachofanyika hivi sasa ni kuundwa kwa Tume ya Katiba na sio Katiba yenyewe.
Awali akifungua semina hiyo, Mwenyekiti wa semina hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipongeza Kamati hiyo kwa kupokea maoni ya wananchi na kuyachambua.

WATAKA MUSWADA USISOMWE MARA YA PILI
Na Romana Mallya
Wanasiasa, wanasheria, mawakili wanafunzi pamoja na wananchi wameitaka serikali kuhakikisha kuwa muswada wa Katiba mpya unaotarajia kupelekwa bungeni mwezi ujao usisomwe kwa mara ya pili bali kwa mara kwanza lengo likiwa ni kuiwezesha Kamati ya Bunge kukusanya maoni ya wananchi kwa mara ya kwanza, Mwandishi Romana Malya anaripoti.
Maoni hayo yalitolewa jana jijini Dar es Salaam katika mazungumzo yaliyoandaliwa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kwa kushirikiana na vyama vya siasa lengo kuendeleza mchakato wa maoni ya kuandikwa kwa katiba mpya.
Akichangia katika mazungumzo hayo, kama raia wa kawaida, mwanazuoni na mtaalam wa sheria nchini, Profesa Issa Shivji, alisema kuwa, muswada wa katiba hiyo endapo utasomwa kama wa pili utainyima kamati hiyo kukusanya maoni na kuwanyima haki wananchi kutoa maoni yao.
Pia alisema ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya utasaidia kurudisha muafaka mshikamano katika taifa ambalo kwa sasa limegawanyika kwa kuwa na mipasuko na ufa.
“Tusipoteze nafasi hii ya kurudisha muafaka na mshikamano katika taifa letu ambalo hatuna budi kukiri limegawanyika kuna mipasuko, kuna ufa, kushirikisha wananchi ndio kurudisha muafaka, tusipoteze nafasi hii kwani itatusaidia kuleta malengo makuu,” alisema.
Kadhalika, Shivji alisema kuwa, wakati wa mchakato wa kuandaa katiba mpya serikali inatakiwa kuzingatia mambo makubwa matatu.
Aliyabainisha kuwa tume ya katiba ndicho chombo cha kuwawezesha wananchi kutoa maoni yao na kuyaratibu na kuyafanyia uchambuzi wa kisayansi bila kubagua.
Pia alisema chombo hicho sio cha uwakilishi bali cha kitaalamu ambacho kitafanya kazi bila kuingiliwa na mtu yeyote.
Profesa Shivji alisema jambo la pili ni Bunge la Katiba ambacho ni chombo cha uwakilishi kinachotengenezwa na wananchi wenyewe bila kuangalia misingi ya chama, elimu au hadhi ya anayewakilishwa.
Kadhalika alisema bunge hilo linatakiwa kutokuwa na madaraja na wawakilishi wake wawe na haki sawa.
Alibainisha jambo la tatu kuwa ni kura za maoni za wananchi ambazo zinahitaji demokrasia ya moja kwa moja.
“Kwenye hili naomba nitoe angalizo, wananchi wasistukizwe, wapewe muda wa kutosha na waridhike na kitu hicho, lakini pia suala la tume ya katiba ya kukusanya maoni ambayo Rais ndiye anayeichagua kunakipengele kinachosema Rais atakavyoona, mfumo huu hautatuwezesha kupata haki,” alisema.
Profesa Shivji katika mazungumzo hayo alipendekeza idadi ya jopo la wataalam lipunguzwe lifikie angalau wasiozidi watu 20 na wajumbe wachaguliwe kutoka katika fani tofauti.
“Nakumbuka tume ya Rais Mwinyi iliyoundwa kwa masuala ya ardhi mimi nilikuwa miongoni mwao tulikuwa watu 11 tu,” alisema.
Pendekezo lingine alilolitoa ni vyuo vikuu na vyama vya kitaalam wapewe nafasi ya kupendekeza majina ya wataalam ambayo yatapelekwa wa Rais.
Kadhalika alisema malipo na marupurupu yatajwe kisheria na taraifa na rasimu ya katiba ipelekwe kwa marais wote sambamba na kutangazwa hadharani.
“Lazima tukubali kuwa mpaka tulipofikia vipo vitu ambavyo wananchi inaonyesha wamekubaliana navyo kama katiba ni mali yao na sio viongozi au serikali, “ alisema na kuongeza:
“Nawaomba wananchi watumie nafasi kutoa maoni dukuduku na matumaini yao kwa wazi bila hofu wala wasiruhusu mtu yeyote awaendeshe, pia wananchi wasifunge eti katiba iwe na ibara ngapi, India katiba yao ina ibara zaidi ya 500, hivyo hili mlitambue,” alisema.
Mwenyekiti wa mjadala huo, James Mbatia, kwa upande wake alionyesha wasiwasi kupitia ibara ya 98 ya katiba ya sasa ambayo inafunga wananchi kujadili masuala hayo.
Katika mazungumzo hayo asilimia kubwa ya wawakilishi wa vyama vya siasa tofauti nchini na wananchi, wameunga mkono suala la bunge kutosoma muswada huo kama wa pili huku baadhi yao wakionyesha wasiwasi wao na serikali kwa madai kuwa haitaki katiba mpya na inatumia ujanja.
Mwakilishi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fred Hatari, ambaye ni mwanyekiti wa Umoja wa wanafunzi wanachama wa chama hicho, Chuo Kikuu Dar es Salaam, alisema kuwa serikali inatakiwa kuwa na msimamo wa hoja toshelezi kama ina nia madhubiti juu ya suala hilo.
Wakati mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), akizungumzia kuhusu migogoro na maandamano inayoendelea maeneo tofauti nchini kuwa hayataisha bila kuwa na katiba mpya iliyoandikwa na wananchi wenyewe, TLP kimesema kuwa katiba iliyopo imewagawa walionacho na wasionacho.
Chama cha NRA kwa upande wake kimepinga Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia suala hilo badala yake isihusishwe kabisa wakati mwenyekiti wa chama cha Tadea, John Chipaka, alisema kuwa, kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Anne Makinda, maoni ya wananchi yaliyotolewa awali yanaendelea kufanyiwa kazi.
 Haya jamani Wazanzibari mupooo???????????

CHANZO: NIPASHE 

No comments:

Post a Comment