Monday 14 November 2011

Mwaka mmoja wa ubia matumbo yanawaka moto

Ahmed Rajab
 
HAKUNA tukio lililokuwa muhimu sana katika historia ya karibuni ya Zanzibar kama lile lililojiri miezi 12 iliyopita palipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani humo.  Serikali hiyo iliundwa kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010 na kura ya maoni iliyopigwa kabla ya uchaguzi huo na iliyoidhinisha mageuzi ya kikatiba yaliyowezesha kuundwa hiyo serikali ya ubia.
Hivyo, tunaweza kusema kwamba maridhiano yaliyofikiwa baina ya vyama vya Civic United Front (CUF) na Chama cha Mapinduzi (CCM) kukomesha uhasama wa kisiasa kati yao huko Visiwani ni tuko liso kifani tangu uchaguzi wa mwanzo mnamo mwaka 1957. 
Ule mgogoro wa kisiasa uliosababisha kuzuka kwa Mapinduzi ya Januari 1964 na halafu Muungano na Tanganyika mwezi Aprili mwaka huohuo umeleta madhara makubwa sana kwa ustawi wa vizazi vya Wazanzibari ambao wengi wao, hii leo, wanaishi maisha duni kabisa.  
Hawawezi kumudu hata vijisenti vya kusukumia maisha ya kila siku, hasa wakati huu ambapo watu wasio na ajira Zanzibar wanakadiriwa kuwa si chini ya asilimia 80 ya wakazi wa huko wenye kuweza kufanya kazi. Wengi wao ni vijana, wa kiume na wa kike, wanaoonyesha kwamba wamekata tamaa kuhusu mustakbali wao.  Wanajiona wamekwisha, hawana lao, wako hohehahe.
Kwa hakika, tukiangalia hali za maisha ya wananchi wa Zanzibar tunaona kwamba asimilia 95 ya wakazi wa Zanzibar, si vijana tu, wanaishi maisha magumu.  Maisha hayo yanazidi kuwakaba roho si tu kwa sababu ya ukosefu wa ajira au ya mfumuko wa bei na mapato lakini pia kwa vile viwango vya elimu na vya huduma za afya ni vya chini. 
Umati huo wa watu unaishi tu bila ya kuwa na matumaini na maisha.
Kushangilia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa si kusema kwamba serikali hiyo imeweza kuyatanzua matatizo yote ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii yanayoikabili Zanzibar ya leo.
Suala hili la kisiasa lenye umuhimu mkubwa, lina pande mbili.  Upande mmoja unahusika na mambo ya ndani kwenyewe Zanzibar na wa pili unahusika na Muungano. 
Serikali ya Umoja wa Kitaifa inastahili kupongezwa kwa namna ilivyosimama imara kutetea maslahi ya Zanzibar mwanzoni mwa mchakato wa sasa wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunajua kwamba katika majadiliano na mashauriano na wenzao wa Bara kuhusu suala hili lenye kuhusika na Muswada wa Kuipitia Katiba, wakuu wa Zanzibar waliyang’ang’ania na waliyapata mengi ya makusudio yao.
Mengi ya makusudio hayo yalikuwa na lengo la kuiwekea kinga Zanzibar pamoja na kuweka usawa kati ya Zanzibar na Tanganyika katika huu mchakato wenye dhamira ya kuitunga katiba mpya ya Muungano.  Lau pasingalikuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa ingekuwa muhali kwa Zanzibar kuweza  kupata tahafifu yoyote kutoka Bara.  Isingeweza kamwe kufua dafu. 
Hii ni kwa sababu Serikali ya Muungano imezoea kuitawala Zanzibar iliyogawika kisiasa — hali iliyozusha uhasama kati ya viongozi wa kisiasa na wafuasi wao na iliyoiondosha Ajenda ya Zanzibar kutoka kwenye mlinganyo wa siasa za Tanzania.
Nafikiri kwamba hili, pamoja na Wazanzibari kuanza kuwa na sauti moja ya kisiasa kuhusu Muungano, ni kati ya mafanikio makubwa yaliyopatikana Zanzibar katika medani yake ya kisiasa kwa muda wa zaidi ya nusu karne.
Bila ya shaka, ni kweli kabisa kwamba tukija kwenye misingi ya uchumi wa Zanzibar na tukiangalia muundombinu wake wa kijamii, tutaona kwamba badala ya kutengenea hali imezidi kuwa mbaya katika kipindi cha miezi kumi na mbili iliyopita. 
Si tu kwamba bei za vyakula zimezidi kuruka lakini sarafu ya nchi kila uchao imekuwa ikipoteza thamani yake — tena kwa mporomoko wa harakaharaka — ikilinganishwa na thamani ya sarafu ya dola ya Marekani. 
Hiyo sarafu ya dola ndiyo sarafu inayotumiwa katika biashara za kimataifa na ndiyo pia inayotumiwa na Serikali pamoja na wafanya biashara wa Zanzibar.  Watu wanahiari kufanya biashara kutumia sarafu hiyo badala ya ile ya shilingi ya Tanzania.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo inashughulikia mambo yasiyo ya Muungano kama vile kilimo, huduma za afya na baadhi ya mambo ya elimu haina mamlaka ya kuyashughulikia mambo ya Muungano.  Na hayo mambo ya Muungano ndiyo yaliyo ya lazima katika kuupanga, kuujadhibisha na kuusarifu uchumi wa Zanzibar, uchumi ambao daima umekuwa umetangana na Bara.
Ijapokuwa inatazamiwa kwamba Katiba mpya ya Muungano itakuwa tafauti kabisa na hii iliyopo sasa, na huenda ikawa na mambo yanayodaiwa na Zanzibar, kuna wenye kuuliza iwapo wananchi wa Zanzibar wataweza kuvumilia miaka minne ya utungwaji wa katiba bila ya kupata mageuzi ya kimsingi katika hali zao za kiuchumi na kijamii. Mageuzi hayo, kwa mfano, ni kama yale yatayoweza kupunguza bei za kuruka za vyakula na za mahitaji mingine ya maisha.
Watu hao wanaendelea kuuliza ni jambo gani linaloizuia Serikali ya Zanzibar isianze kufanya mashauriano na serikali ya Muungano ili pawepo na mpango, ingawa wa muda, wa kuuokoa uchumi wa Zanzibar usizidi kudidimia?  Kinyume na Zanzibar ambako bei za vyakula na bidhaa nyingine ni za juu sana, huko Bara kuna uchumi ulio imara zaidi na kuna maliasili za madini na gesi.
Kuna haja ya dharura ya kuuzuia uchumi wa Zanzibar usizidi kuporomoka kwani endapo hapatochukuliwa hatua yoyote kila mwaka, uchumi wa Zanzibar hautokua.  Wala Zanzibar haitoweza kuyatanzua matatizo yake ya muda mfupi, ya muda wa wastani au ya muda mrefu.
Bila ya shaka tatizo muhimu la muda mfupi linahusika na bei za vyakula.  Kuna haja ya dharura kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuzingatia hatua zote inazoweza kuchukua hata ikiwa pamoja na kuondoa ushuru na aina nyingine za kodi zinazotozwa vyakula muhimu au mafuta ya petroli.
Katika hiki kipindi cha mageuzi,   Zanzibar inapaswa kushauriana na Serikali ya Muungano ili iipatie misaada ya kiuchumi na kijamii.  Hali kadhalika, katika kipindi hikihiki Zanzibar inawajibika kufikiria namna ya kupunguza, tena kwa kiwango kikubwa, matumizi ya Serikali. 
Serikali ya Zanzibar lazima ichukue hatua hiyo ili iweze kugharamia miradi ya kutoa huduma za bure kwa jamii, huduma ambazo zikiendelea kukosekana wananchi watazidi kuteseka.
Aidha kuna umuhimu kwa Zanzibar kuwa na Mfuko wake wa Utajiri, si tu kwa sababu ya  kulipia madeni yake ya nchi, lakini pia kutumia utajiri huo kuzalisha utajiri wa ziada utaoweza kutumika kugharamia mahitaji ya muda mfupi na miradi ya muda mrefu.  Mfuko huo unafaa uchangiwe kimataifa — kwanza na nchi za wafadhili zenye kuonyesha ihsani kwa Zanzibar na zilizo tayari kugharamia mahitaji yake ya sasa na ya baadaye.
Ni vigumu sana kuwa na mizania ya mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja. Hii ni kwa sababu miradi mingi kama vile ile inayohusika na umeme na maji imo bado ikifanyiwa kazi pamoja na miradi mingine ambayo huenda ikawapatia wananchi wengi ajira.
Hata hivyo, bila ya Serikali ya Zanzibar kuchukua hatua ya haraka ya kuurekebisha uchumi wa Visiwani tunaweza kusema kwamba mafanikio pekee ya maridhiano ni kupatikana umoja, amani na utulivu. 
Hayo matatu pamoja na upatanifu katika jamii na ulinganifu wa sauti za Wazanzibari kuhusu mustakbali wao ndio silaha kubwa walizo nazo katika juhudi zao za kujipatia muradi wao wa kitaifa. Muradi huo ni wa kuwa na uhuru zaidi na uwezo wa kuyatanzua wenyewe matatizo yao bila ya kuirejea dola ya kigeni.  Hayo nayo si mafanikio madogo.

Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment