Friday 26 July 2013

Muungano wa Tanzania au Tanganyika na Zanzibar?

KWA mujibu wa Mkataba wa Muungano, uliotiwa sahihi Aprili 22, 1964, kati ya Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, na kwa mujibu pia wa Sheria ya Muungano, Namba 22 ya 1964, iliiyoridhia Mkataba huo na kuupa nguvu ya Kisheria na kutumika nchini, jina sahihi la Muungano limetajwa kama:
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo, zitaungana kuwa Jamhuri moja kwa jina la Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar.
Kufikia hapo, wengi wanaweza kujiuliza; kama hapajawa na Muungano mwingine, jina hili la ‘Muungano wa Tanzania’ linatoka wapi? Na kama jina Tanzania limebuniwa baada ya Muungano, ina maana kwamba katika kipindi cha Muungano tangu ulipotiwa sahihi hadi kubuniwa kwa ‘Tanzania,’ hapakuwa na Muungano? Marekebisho yapi yalifanyika kufikia ‘Tanzania’ badala ya ‘Tanganyika na Zanzibar’? Na kwa nini?
Haya ni maswali mepesi, lakini yenye utata kwa Mtanzania yeyote yule. Yana utata kwa sababu historia ya Muungano, haijaandikwa itakiwavyo na kuwekwa wazi. 
Watanzania wamekuwa wakipewa tafsiri za kisiasa, nyepesi na za majukwaani. Na kwa kuwa ilikuwa ni dhambi kuu kuhoji juu ya Muungano wala kutoa maoni juu ya muundo na aina gani ya Muungano uliokusudiwa, Watanzania wameishi kwa kuuchukulia Muungano huo kama ‘fumbo la imani’ tu, huku kero za Muungano zikichipuka kama uyoga kwenye shamba lenye rutuba lililotelekezwa.
Jina la Muungano huu limetajwa kwenye Sheria ya Muungano Namba 22 ya mwaka 1964, kifungu cha 4, kuwa ni “Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar” (URTZ), kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo.
Wakati nchi mbili hizi zikiungana hapakuwa na Katiba iliyoandaliwa kusimamia Muungano. Kwa hiyo, ilikubaliwa kwamba katika kipindi cha mpito (wakati Muungano huo ukiandaliwa Katiba yake), Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika itumike (na ilitumika) pia kama Katiba ya Muungano kwa kufanyiwa marekebisho kuingiza yale mambo 11 yaliyopitishwa kushughulikiwa na Serikali ya Muungano na kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar (Sheria ya Muungano-Kifungu cha 5).
Mambo hayo ni Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mambo ya Nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya hali ya hatari na Uraia. Mengine ni Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo, Utumishi wa Jamhuri ya Muungano, Kodi na Ushuru wa Forodha, na mwisho, Bandari, ndege za kiraia, Posta na simu za maandishi (telegraph).
Itakumbukwa kwamba Zanzibar haikuwa na Katiba yake wakati Muungano unafanyika, hadi mwaka 1984. Lakini Zanzibar ilikuwa na Sheria zake zitokanazo na maagizo ya Rais (Decrees).
Kwa hiyo, kwa kutambua kwamba Serikali za Tanganyika na Zanzibar hazikufa baada ya Muungano, iliwekwa bayana kuwa Sheria za Tanganyika na zile za Zanzibar, zitaendelea kutumika katika nchi hizo (Kifungu 8 cha Sheria ya Muungano na Ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano), bila kuingilia au kuingiliwa na shughuli za Serikali ya Muungano.
Ndiyo kusema kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (URTZ), uliundwa kwa ajili ya, na ili kushughulikia mambo 11 tu ya kila nchi, wakati ule, ambapo Serikali za Tanganyika na Zanzibar zilibakia hai kuendelea kushughulikia mambo mengine yote yasiyo ya Muungano katika maeneo yake, huku Katiba ya Tanganyika ikiendelea kutumika kama Katiba ya Muungano pia.
Jamhuri ya Muungano ilitakiwa kuwa na Katiba yake katika muda wa miezi 12 iliyofuata kuanzia Aprili 26, 1964, yaani kufikia Machi 26, 1965, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano; lakini haikuwa hivyo.
Ilipofika Machi 24, 1965, Bunge lilipitisha Sheria Namba 18 ya mwaka 1965 kuongeza muda wa kuitisha Bunge la Katiba “hadi hapo itakapoonekana vyema kufanya hivyo.”
Kuongezwa kwa muda wa kuitisha Bunge la Katiba, kulimaanisha kuchelewa kupatikana kwa Katiba halali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba na Sheria ya Muungano ya 1964.
Ili kuokoa Muungano huo usiendelee kuchangia Katiba na Serikali ya Tanganyika, Julai 10, 1965, Bunge lilipitisha Katiba ya Muda (Sheria No. 43 ya 1965) ya Tanzania, iliyotambua kuwa “Tanzania ni Jamhuri ya Muungano” (Ibara ya 1) inayoundwa na Tanganyika na Zanzibar (Ibara ya 2), na kwamba kutakuwa na Chama kimoja cha siasa Tanzania (Ibara ya 3); lakini hadi hapo TANU na ASP vitakapoungana, Chama cha siasa kwa Tanganyika kitakuwa “The Tanganyika African National Union (TANU), na kwa Zanzibar, kitakuwa “Afro-Shirazi Party” (ASP).
Hapa, Katiba ilijikanganya. Kulikuwa na Chama kimoja vipi Tanzania wakati kulikuwa na TANU na ASP?
Hapo ndipo jina la “Tanzania” lilipoanza kuonekana katika ‘Katiba ya Muungano’ na kuleta mgongano kati yake na jina asilia la Muungano huo linalotambulika katika Mkataba wa Muungano, na katika Sheria ya Muungano ya 1964.
Ifahamike kwamba vyama vya siasa havikuwa na havijawa jambo la Muungano. Kwa hiyo, kwa kuingiza vyama vya siasa katika suala la Muungano, Katiba ya Muda ya 1965, ilikuwa imekiuka Mkataba/Sheria ya Muungano.
Utata huu unazua maswali pia juu ya uhalali wa Tume ya Vyama vya TANU na ASP, iliyoteuliwa kuandaa mapendekezo ya Katiba ya kudumu ya mwaka 1977. Ni kuingizwa kwa vyama vya siasa katika muundo wa Muungano kulikozua, na kunaendelea kuzua, mitafaruku na kero ndani ya Muungano hadi sasa.
Lakini kwanini haya yaliruhusiwa kuingia katika Katiba wakati kulikuwa na Wanasheria wenye elimu nzuri na uelewa wa juu katika kuutahadharisha Uongozi? Au ni kwa sababu ya wanasiasa wasioambilika?
Ni vyema nikumbushe pia kwamba Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, ndivyo msingi mkuu wa Katiba ya Muungano, vinginevyo hakuna Katiba ya Muungano wala ya Zanzibar, na hivyo, hakuna Muungano.
Wala Bunge la kawaida la Muungano halina mamlaka ya kurekebisha Mkataba/Sheria ya Muungano, au kuongeza ambacho hakikukusudiwa au kutajwa katika Mkataba wa Muungano. Hadi sasa, Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano vinasomeka kama vilivyopitishwa mwaka 1964, lakini Katiba imeendelea kugeuzwa na kurekebishwa kwa matashi ya wanasiasa.
Hapa maswali yafuatayo yanajitokeza. Jina ‘Tanzania’ lilitoka wapi, na liliingiaje katika msamiati wa Katiba ya Muungano? Je; kutumika kwa jina hilo kunabatilisha jina asilia la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?’ Kama halibatilishi, nini suluhisho la mgongano huu?
Ilikuwa hivi: Miezi mitatu baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, lilitangazwa shindano la kubuni jina litakalowakilisha hadhi na kuwapo kwa Muungano wa nchi hizi mbili. Mshindi aliahidiwa zawadi ya pauni 10 za Uingereza, sawa na Shilingi 20/= za wakati ule za Tanzania.
Kamati ndogo ya Baraza la Mawaziri iliteuliwa kupokea na kuchambua maoni ya washindani 1,534 yaliyopokelewa na kuwasilisha machache (idadi haifahamiki) kwenye Baraza la Mawaziri kwa uamuzi wa mwisho. Maoni yalipokelewa kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwamo Urusi, Uingereza, Sweden, Uchina, Ufaransa, Poland, Italia na Australia.
Katika mkutano na Waandishi wa Habari, Ikulu, Oktoba 29, mwaka 1964, Rais Julius Nyerere alitangaza kwamba Baraza la Mawaziri limechagua jina ‘Tanzania’ kuwakilisha Jamhuri ya Muungano, lakini hakutaja jina la mshindi ambaye hajajulikana hadi leo. 
Aliwafundisha pia namna ya kulitamka jina jipya, kwamba ni ‘Tan-Zan-ia,’ na si ‘Tanzania’ kama inavyotamkwa sasa. Tan-zan-ia ni kifupisho chenye kumaanisha Tan – Tanganyika na Zan – Zanzibar, ambapo herufi– ‘ia’ kukamilisha Tan-zan-ia, zimetoka Zanzibar (i) na Tanganyika (a). Kati ya majina manne yaliyochuana hadi mwisho na ‘Tan-Zan-ia,’ ni pamoja na ‘Tanzan,’  ‘Tangibar’ na ‘Zantan.’
Hapa ifahamike kwamba, jina hili ‘Tan-Zan-ia,’  mbali na kuzua mgongano na jina la Muungano (URTZ) kwa mujibu wa Mkataba na Sheria ya Muungano, lilikusudia kuwakilisha jina la ‘Muungano’ na mambo ya Muungano tu, lakini halikufuta, na hatudhani kwamba lilikusudia kufanya hivyo, muundo wa Muungano uliokusudiwa, wala kufuta Serikali ya Tanganyika na Zanzibar na mamlaka zake, kama tulivyoelezea hapo mwanzo.
Kuonyesha kwamba Tanganyika ilikuwa na hadi sasa ni hai, Katiba ya mwaka 1965 kwa mfano, Ibara ya 12, ilitambua Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa pia ndiye Rais wa Tanganyika, chini ya Katiba ya Muda.
Nayo Ibara ya 13 (1) ilitambua kuwa na Makamu wawili wa Rais, mmoja (wa pili) akiwa Msaidizi wa Rais kwa mambo ya Muungano nchini Tanganyika.
Ibara ya 20 ilimpa Rais mamlaka ya kuteua Mkuu wa Mkoa kwa kila Mkoa nchini Tanganyika, ambapo Ibara ya 25 ilizungumzia kuhusu Tanganyika kuwa na majimbo ya uchaguzi; na mifano mingine mingi.
Wataalamu wa mambo ya Sheria na Katiba bado wanahoji, kama Bunge la kawaida lililobadili jina la Muungano lilikuwa na mamlaka au uwezo wa kufanya hivyo kisheria.
Katiba ya Muda ya 1965 ilibainisha wazi kuwa Muungano wa ‘Tanzania’ unaundwa na Tanganyika na Zanzibar kwa maana ya kutambua kuwako kwa nchi hizi mbili.
Lakini Katiba ya 1977 inataja kuwa Muungano huo unaundwa na ‘Tanzania Bara’ na ‘Tanzania Zanzibar,’ kwa maana ya majina hayo kuchukua nafasi ya majina ya Tanganyika na Zanzibar.”
Kama lilivyo jina la ‘Tanzania,’ majina ya ‘Tanzania Bara’ na ‘Tanzania Zanzibar’ hayajulikani katika Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano ambayo haijabadilika hadi leo.
Nini athari ya mgongano huu na uhalali wa mabadiliko haya kwa Mkataba/Sheria ya Muungano? Je; Bunge la Katiba lililopitisha Katiba hiyo, ndilo lile la aina ya lililotakiwa chini ya Mkataba na Sheria ya Muungano? Je; Serikali ya Muungano ina mamlaka na uwezo wa kubadili (majina) yaliyomo katika Mkataba uliyoiunda? Je; yai laweza kumbadili kuku?
Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kufanya rejea kwa ufupi tu, mchakato mzima wa Katiba tatu za Muungano zilizopita ili kuona utata ulipo.
Hakuna ubishi kwamba Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964, na Katiba ya muda (Interim Constitution) ya 1964 na ile ya 1965, zilitambua kuwapo kwa Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar zikiwa na mamlaka kamili kuhusu mambo ya nchi yasiyo ya Muungano.
Ilikubaliwa pia kwamba iandaliwe Katiba ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa utaratibu uliowekwa, na ipatikane ndani ya mwaka mmoja tangu siku ya Muungano; na kwamba wakati hilo likifanyika, Katiba ya Tanganyika itumike pia kama Katiba ya Tanganyika, na hapo hapo kama Katiba ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanyiwa marekebisho kutambua kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar, kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Tatizo lilianza na Katiba ya Muda ya mwaka 1965, ambayo, chini ya Ibara ya 12 (1), ilibainisha kwamba “Mamlaka ya Utendaji (the Executive) kuhusu mambo yote ya Muungano, katika, na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na (pia) kwa (Serikali ya) Tanganyika, yatakuwa kwa Rais wa Serikali ya Muungano.”
Kwa maana hii, Rais wa Kwanza wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa wakati huo huo Rais wa Tanganyika pia.  Ingekuwa vivyo hivyo, kama Rais Abeid Karume wa Zanzibar angeteuliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Muungano, kwamba angesimamia Serikali ya Muungano na Serikali ya Tanganyika, kwanza kama Rais wa Muungano, na pia angesimamia Serikali ya Zanzibar kama Rais wa Zanzibar. 
Huu ulikuwa ni mpangilio wa muda kusubiri kuandikwa kwa Katiba ya Muungano ambapo madaraka na mamlaka hayo yangetenganishwa kwa kuzingatia Mkataba wa Muungano.
Utata huu ulizidishwa na Ibara ya 49 ya Katiba hiyo iliyoweka wazi kwamba mamlaka ya kutunga Sheria kuhusu mambo yote ya Muungano katika na kwa ajili ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kwa mambo yote katika na kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika, ni ya Bunge la Muungano.
Hii ilimaanisha sasa kwamba Rais wa Muungano ndiye aliyekuwa Rais wa Tanganyika, na Bunge la Muungano ndilo lililokuwa Bunge la Tanganyika pia.
Kama tunaweza kuufananisha Muungano huu na taasisi mbili zilizokubaliana kuunda ubia (Jamhuri) kwa njia ya hisa zilizo sawa (tuseme hisa 11 kila moja, kama yalivyokuwa mambo ya Muungano), basi Tanganyika imetoa kila ilicho nacho juu na zaidi ya hisa ilizopaswa kuchangia katika Muungano, tofauti na matakwa ya Mkataba.
Na kwa kuwa mchango huo wa ziada hautambuliki katika hati zote za kuanzisha Ubia huo, basi, inakuwa imetoa kwa hiari na haiwezi kuongezewa gawio wala kuwa na sauti na kauli katika Ubia huo kwa hicho cha ziada.  Kufanya hivyo ni kuhodhi mamlaka ya Muungano ambako Wazanzibari wanaita ‘kumezwa kwa Zanzibar.’
Lakini kwa upande wa Zanzibar, mamlaka ya utendaji kwa Serikali ya Zanzibar, kwa mambo yasiyo ya Muungano, yalibakia kwa Rais wa Zanzibar.  Vivyo hivyo, mamlaka ya kutunga Sheria kwa mambo yasiyo ya Muungano, yalibaki kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Hapo ndipo Bunge na jina la Tanganyika lilianza kupotea kimiujiza, wakati jina la mdau wa pili, Zanzibar, likaendelea kudumu, na wakati huo huo Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, ziliendelea, na zinaendelea kuutambua Muungano kwa jina la Tanganyika na Zanzibar.
Nyundo ya chuma ilipigiliwa kichwani mwa Tanganyika, pale Sheria Na. 24 ya mwaka 1967 ilipotungwa kumpa Rais uwezo wa kuweka neno ‘Tanzania’ badala ya neno ‘Tanganyika’ katika maandishi na nyaraka zote za kisheria, lakini haikubadili majina hayo katika Hati ya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano.
Mabadiliko yote haya, kwa kuanzia na Katiba ya Muda ya mwaka 1965, ndiyo yaliyorithiwa bila utafiti makini na kuingizwa katika Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Ni kutokana na mabadiliko hayo, yanayofanya watu wafikirie na kuamini kwamba Tanzania ndiyo Tanganyika, na Tanganyika ndiyo Tanzania; wakati si kweli.   Na hii ndiyo dhana potofu ya Serikali mbili – Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
Chanzo: Raia Mwema

Thursday 25 July 2013

Wanasiasa Z’bar na propaganda dhaifu

Leo nalazimika kuandika makala haya kwa mshangao mkubwa wa baadhi ya wanasiasa hapa Zanzibar kutengeneza taswira ambayo haikubaliki wala kuendana na wakati tulionao.
Kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia propaganda dhaifu kwamba wanaodai mabadiliko katika muundo wa Muungano wanataka kumrejesha Sultan!
Hii ni ajabu ya mwisho, pia ni aibu kusikia kauli kama hizo baada ya takriban miaka hamsini ya kujitawala.
Inafahamika vizuri kwamba Zanzibar ni nchi kamili na watu wake waliamua kujitawala wenyewe kupitia mapinduzi yaliyoung’oa utawala kisultan Januari 1964 na Aprili mwaka huu Jamhuri ya watu wa Zanzibar ikaungana  na Jamhuri ya Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Sultan wa mwisho kutawala Zanzibar ni Jamshid bin Abdullah Al Said ambaye kwa sasa anaishi Portsmouth, Uingereza akiwa na umri wa miaka 83.
Hakuna anayemtambua katika medani za kisiasa kwa Zanzibar ya leo zaidi ya kubaki katika vitabu vya kihistoria tu, lakini kizazi hiki kinachojali ni nchi yao iliyo huru ambayo ilikombolewa kutoka kwa wakoloni.
Umezuka mtindo kwa wasiokuwa na nguvu ya hoja kudai eti kuna watu vibaraka wa Sultan, ndiyo maana wanadai mabadiliko katika Muungano!
Huu ni uzushi na uongo usiokuwa na hata chembe ya ukweli, wananchi wa Zanzibari chini ya Afro Shiraz Party ndio waliompindua Sultan na kuirejesha nchi yao mikononi mwa wazalendo ambao ni wakwezi na wakulima; iweje leo miaka 49 tukijiandaa kuadhimisha jubilee ya miaka 50 ya Mapinduzi watamani kutawaliwa tena?
Kama leo itapigwa kura, kuulizwa nani kati ya Abeid Amani Karume na Sultan Jamshid anayefahamika, jawabu lisilokuwa na hata chembe ya shaka ni Karume. Sultan hana mlango wa kuingilia Zanzibar.
Kabla ya Mapinduzi, Zanzibar haikuwa Jamhuri, ilikuwa chini ya Sultan, lakini Mapinduzi ya umma ndio yaliyoifanya Zanzibar kuwa Jamhuri.
Umoja wa Mataifa uliyatambua Mapinduzi hayo kuwa ni halali na uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) uliyatambua pia.
Sheria na mikataba ya kimataifa haitoi nafasi kwa Sultan kujipenyeza Zanzibar na wala hicho kiti chake huko UN hakipo, kilibiruka mwaka 1964. Kwa hiyo msipoteze muda kwa propaganda mfu na zisizokuwa na mashiko.
Vuguvugu la mabadiliko lililoanzia na Mapinduzi ya kule Ufaransa yaliamsha ari na kuwatia shime wazalendo wa Zanzibar kufanya Mapinduzi yaliyosimamiwa na kuratibiwa na ASP.
Athari za Mapinduzi ya Ufaransa zilienea kote duniani na ilipofika Januari 12, 1964, Wazalendo wa Zanzibar chini ya Afro Shiraz Party walirejesha heshima na utu kwa wakulima na wakwezi.
Wazanzibari sasa wanataka mabadiliko, hawatafanya kama wale wa Ufaransa isipokuwa watatumia haki ya kutoa mawazo yao, iwe wanataka Serikali tatu au mbili ni haki yao.
Saa ya mabadiliko imefika, vijana wasiokuwa na ajira, uhakika wa chakula wala kulala wamefikia pahala wanataka kuona mabadiliko ya kweli yanatokea siyo tu katika siasa bali hata katika uchumi na ndiyo maana wengi wanaunga mkono pendekezo la tume ya Jaji Warioba la kuwa na shirikisho.
Ni lazima wanasiasa wetu wafahamu kuwa ulimwengu wa leo, vijana haukubali tena kuburuzwa na mara nyingi vijana wa kileo waliozaliwa katika Teknohama wanaunga mkono siasa yenye uchumi na wanazuoni wanaipima hoja hiyo katika  mizania miwili; mosi, msukumo binafsi wa kijana wa Zanzibar wa uhitaji wa mabadiliko na pili, ni mhemko wa majira.
Mhemko huu ni kama kilevi ambapo kama ukweli ulivyo idadi kubwa ya vijana ndio wanywaji ambao hawatapenda kunywa kilevi kama togwa kisichokuwa na ‘stim’ yoyote kwao.
Demokrasia ya kisasa inalazimisha kuheshimu mawazo ya wengine hata kama huyataki, ndiyo maana watu makini wanaamini kuwa uvumilivu mzuri ni ule unaojiepusha na chuki zisizo na msingi (prejudice).
Hata kama anayetoa maoni au kueleza ni yule msiyeafikiana, au kimaumbile si mzungumzaji mzuri jaribu kuuweka sawa ujumbe wake kwa misingi ya nguvu ya hoja huku ukizingatia alichokizungumza siyo namna alivyozungumza. Mara zote chuki isiyo na msingi huviza mabadiliko.
Ikiwa dhana ya ujana ndio nguvu ya mabadiliko katika jamii, wanaobeza msimamo wa wale wanaotaka Serikali tatu, tumeona namna watu wa Zanzibar na Tanganyika walivyotoa mawazo yao kutaka mabadiliko ya msingi katika muundo wa Muungano.
 Watu wasijadili suala la muundo wa Muungano kwa jazba wala chuki kama ilivyoanza kujitokeza hivi karibuni kwa upande wa Tanganyika ambao wanawachukulia Wazanzibari kama wakorofi.
Hawa wanaokejeli wenzao tunawafahamu ndio masalia ya wanasiasa waliochoka kimawazo, wengine wana joto lao la kushindwa maisha na kukosa vyeo walipokuwa Serikalini, ndio leo wanamalizia hasira zao kwa wale wanaotoa hoja za kudai Muungano wenye usawa baina ya nchi ya Zanzibar na Tanganyika .
Haitawezekana kwa hali yoyote ile wananchi wa Zanzibar walio huru waliokataa kutawaliwa eti baada ya miaka 49 ya Mapinduzi watamani kutawaliwa tena na ukoloni wa Sultan!
Hili ni jambo la kushangaza kuona kwamba katika Afrika hii kuna watu wanamuota Sultan, napenda kuwaeleza kwamba Sultan na watu wake hawana hata chembe ya nafasi katika Zanzibar mpya, wala ya zamani.
Itakumbukwa pia kuwa mara tu baada ya Mapinduzi mwaka 1964, Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere naye alichukia sana ubaguzi na ndio maana aliongoza kampeni ya ndoa za mchanganyiko wa rangi na makabila mbalimbali hapa Zanzibar.
Mzee Karume hakulazimisha watu kuoana bali aliwataka wazazi wawape watoto wao uhuru wa kuoa na kuolewa na wawapendao. Waarabu hawakutaka mabinti wao waolewe na Waafrika ilhali, na kinyume chake baadhi ya Waafrika walikataa watoto wao kuoa Waarabu.
Chanzo: Mwananchi