Monday 14 November 2011

Makubaliano SMZ na Ras el Khaiman kuinufaisha Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar na Ras Al Khaiman zimesaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano katika uimarishaji wa sekta za maendeleo ambapo miongoni mwa makubaliano hayo, ni pamoja na ushirikiano katika kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kiuchumi na kuendeleza ajira.

Utiaji saini huo ulishuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein pamoja na mwenyeji wake, Kiongozi wa Ras Al Khaimah, Shehe Saud Bin Saqr Al Qasimi na viongozi wengine wa pande mbili hizo katika Kasri ya kiongozi huyo iliyopo mjini Ras Al Khaimah.

Kwa upande wa Zanzibar, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman alisaini ambapo kwa upande wa Ras-Al-Khaimah aliyetia saini ni Shehe Abdalla Bin Humaid Al Qasimi.

Miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na kuendeleza Maeneo Huru ya Uchumi, Bandari Huru ambapo itaifanya Zanzibar kuwa Kituo Kikuu cha Biashara, ushirikiano wa kitaalamu, kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu katika nyanja za afya, nishati, huduma za afya, ufundi.

Aidha, utafiti juu ya vianzio vya maji, ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuendeleza ajira.

Mapema, Dk. Shein alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Kiongozi wa Ras-Al-Khaimah, Shehe Saud Bin Saqr Al Qasimi yaliyolenga kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Katika mazungumzo hayo kwenye Kasri ya kiongozi huyo, viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya kukuza uhusiano na kuimarisha ushirikiano katika kuinua seka za maendeleo ikiwemo uwekezaji, biashara, viwanda, elimu, maeneo huru ya uchumi, afya na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Aidha, viongozi hao walizungumza juu ya sekta za maendeleo na katika kuimarisha ushirikiano kwenye sekta nzima ya maeneo huru na uwekezaji sanjari na bandari huru.


Katika maelezo yake, Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na mwaliko wake na kusisitiza kupongeza mafanikio yaliyopatikana nchini humo kwa kipindi kifupi. Alimueleza kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras-Al-Khaimah.

Naye kiongozi huyo alieleza kuwa Ras-AlKhaimah itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Ras-el-Khaimah zina historia kubwa katika nyanja ya kibiashara hivyo hatua zaidi zitaimarishwa kwa pamoja katika kukuza sekta hiyo pamoja na sekta ya uwekezaji.

Pia, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ras-Al-Khaimah na kueleza kuwa muendelezo wa biashara kati ya Zanzibar na Ras-Al-Khaimah ndio msingi mkubwa wa uhusiano uliopo.

Dk. Shein akiwa na ujumbe wake katika ziara hii ya nchi za Falme za Kiarabu (UAE), alitembelea Chuo Kikuu cha Sayansi cha Ras-Al-Khaimah, Hospitali ya Rufaa ya Ras-Al-Khaimah na kiwanda cha dawa cha Julphar. Alitembelea maeneo huru ya uwekezaji Rakia ambako hutengeneza bidhaa mbalimbali.

Source: Habari Leo

No comments:

Post a Comment