Friday 30 March 2012

Buriani Wolfango Dourado: Shujaa na mzalendo halisi

Ahmed Rajab
KUNA siku nikiwa London, Uingereza nilighadhibika nikawaambia niliokuwa nao: “Nikimuona Dourado nitamzaba kibao.”
Mapema siku hiyo Mahakama Kuu ya Zanzibar iliusikiliza ushahidi wa Amar Salim (Kuku), mmoja wa washtakiwa kwenye kesi ya uhaini iliyohusika na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Sheikh Abeid Amani Karume.
Takriban washitakiwa wote walikuwa ‘Makomredi’ kama wanavyojulikana wanachama au wafuasi wa chama cha zamani cha Umma Party.  Amar Salim, aliyekuwa ameteswa kama washitakiwa wengine, alikuwa mmoja wa vigogo wa chama hicho.
Shitaka lilikuwa kwamba washitakiwa walikula njama ya kuipindua serikali iliyopelekea kuuawa kwa Karume. Alipokuwa akitoa ushahidi wake Amar Salim alikiri kwamba mpango huo ulikuwako. Alipoambiwa na Dourado awataje waliohusika alianza kwa kuwataja makomredi raia wa kawaida na waliokuwa wanajeshi huko Visiwani na waliokuwako Bara. Kisha akanyamaza kuashiria kuwa amemaliza.
Dourado hakutosheka. Akamwambia: “Na kuna walio nje sio?”
Ndipo Amar Salim alipoanza kubwabwajika akitaja kila jina lililomjia kichwani akianza na langu nikifuatiwa na Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York, Mohamed Ali Foum, aliyekuwa ubalozi wa Tanzania, Ethiopia, Dakta Said Himidi aliyekuwa akifanya kazi katika hospitali moja nchini Denmark na mwandishi wa habari, Said Salim (Kiazi) aliyekuwa Beijing, China.
Baadhi ya maswali ya Dourado mahakamani yalikuwa ya dharau na ya kuwakashifu watuhumiwa waliokuwa kizimbani. Hata hivyo, aliwapata waliokuwa kiasi chake au waliomzidi kwa maarifa kama Maalim Nurbhai Issa ambaye kwa majibu yake aliithibitisha ile sifa ya Makomredi ya kutokubali kutishwa na kutoogopa kifo.
Miaka michache baadaye nikiwa nimeketi ndani ya treni chini ya ardhi ya Jiji la London, nilisadifu kumuona mtu mfupi aliyeshika kiko mkononi amenikalia mkabala nami.
Huku treni ikitikisika na kufanya kelele nilimsogelea na kusema: “Bwana Dourado?”
Nilimtambua kwa haraka kwa sababu utotoni mwangu nikimuona sana mtaani Vuga alipozaliwa na nilipozaliwa na kukulia. Nilipomuona nilikuwa na hakika kwamba hakuwa akinijua kwa sura. Hivyo, nikajijulisha.
“Aah, nilikuwa nikikufikiria kuwa wewe ni baba kubwa,” aliniambia huku akitabasamu. Siku hizo nilikuwa kijana mbichi na umbo langu lilikuwa jembamba, ingawa wembamba wangu haukuwa wa njaa.
Treni iliposimama kwenye kituo kimoja mtu aliyekuwa amekaa ubavuni mwake aliinukana kuondoka.  Haraka haraka nikenda kukaa mimi.
Nilishangaa na pengine nilivunjika moyo kidogo kuona kuwa zile ghadhabu zangu juu ya Dourado zilikuwa zimeyayushwa na wakati. Lakini moyoni mwangu nilifurahi kumwona kidogo akitaharak nilipokwenda kukaa ubavuni mwake. Nilimuuliza kwa upole nini kilichompa kunitaja kwenye kesi ya uhaini.
Alinifumba mdomo aliponijibu: “Siye miye niliyekutaja. Ilikuwa Komred mwenzako.” Tukaanza kuzungumza na kuanzisha usuhuba uliodumu hadi alipofariki saa nane za alasiri ya Jumatatu ya wiki iliyopita (tarehe 19 Machi) huko mtaani kwetu Vuga.
Alianzisha mazoea ya kila anapokuja London kunipigia simu ama mimi au mwenzangu Salim Rashid aliyewahi kufanya kazi naye wakati Salim alipokuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi.  Mara nyingi tukikutana kwa dada yake Yolanda huko Ealing, Magharibi mwa London, tukibugia sambusa na chai na tukimsikiliza akitueleza yaliyokuwa yakijiri nchini kwetu.
Akipenda soga lakini soga la maana na alikuwa mtu wa mizaha lakini dhihaka zake zilikuwa za kijiutu uzima. Na ukitaka kumchokoza ilikuwa rahisi. Ukimtajia jina la Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa kama umewasha kibiriti kwenye petroli.
Ingawa wote wawili walikuwa waumini wa dhati Wakikatoliki walikuwa wakichukiana.
Akiwa mpinzani asiyeweza kudhibitika, Dourado akipenda kumshambulia Nyerere.
Alikuwa akisema kwamba akikirihishwa na pengo aliloliona kati ya fikra za kimaadili za Nyerere na vitendo vyake. Ukiyataja hayo ilikuwa kama unamtia ufunguo. Alikuwa hawezi kujizuia, kama alikuwa amekaa basi husimama na kuanza kuzunguka huku na huku akimshambulia Nyerere.
Jingine lililokuwa likimuudhi Dourdo ilikuwa kumwita ‘Wolfgang’ ilhali jina lake halisi ni Wolfango.
Wolfango J Dourado alizaliwa miaka 84 iliyopita. Utotoni mwake alisomeshwa na Wakatoliki katika shule ya Saint Joseph Convent (siku hizi inaitwa Mtakuja) iliyo karibu na kwao. Alivutiwa sana na waalimu wake Wakikatoliki, hasa Rev. Sr. Josefrieda (aliyewahi baadaye kufundisha katika shule ya Riruta Convent jijini Nairobi) na Sr. M Sveglinda ambaye baadaye pia aliishia Kenya kwenye Kituo cha Bikira Maria huko Mbitiri.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi na ya sekondari huko Zanzibar, Dourado alifanya kazi ya ukarani kwa muda mfupi katika serikali ya ukoloni.  Alipata msaada wa kwenda Uingereza kwa masomo ya juu lakini alikataa kwenda kwa sababu baba yake alikuwa amefariki na alilazimika kufanya kazi kumuangalia mamake na nduguze.
Alipopata msaada mwingine wa masomo alikwenda London alikosomea sheria katika Middle Temple, moja ya jumuiya nne za mawakili Uingereza zenye haki pekee ya kuwafanya wanachama wake wawe mawakili. Dourado alifanywa wakili mwaka 1957.
Alipomaliza masomo na kurudi kwao Dourado aliteuliwa kuwa Msaidizi wa Msimamizi Mkuu wa shughuli za serikali wadhifa alioushika hadi mwaka 1960 alipoteuliwa kuwa Wakili Mwandamizi wa Serikali.  Mwaka 1963 aliteuliwa kuwa katibu mkuu katika wizara ya mambo ya nchi za nje; waziri wake kwa muda alikuwa Sheikh Ali Muhsin Barwani.
Aliushika wadhifa huo hata baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ambapo kwa muda pia waziri wake alikuwa Abdulrahman Babu. Baada ya hapo aliteuliwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali.  Aliendelea kuushika wadhifa huo mpaka mwaka 1977 alipofanywa Meneja Mkuu wa Shirika la Bima la Zanzibar. Mwaka 1983 alipewa uwenyekiti wa Tume ya Kuzipitia Sheria za Zanzibar.
Pengine utajiuliza: mtu huyu ana msimamo wowote? Daima amekuwa mtiifu akizitumikia tawala mbalimbali; ya kikoloni, ya kisultani na ya Mapinduzi (katika nyakati zake za ukarimu na pia katika nyakati zake za uhabithi).
Aliyatumikia Mapinduzi kwa kutunga sheria za kimapinduzi lakini pia aliendesha mashtaka dhidi ya Makomredi waliokuwa wafuasi wa siasa za kimapinduzi za Karl Marx.
Nililiuliza swali hilo na kuyasema hayo mingine kwenye makala ya wasifu wake niliyokuwa nimeandika katika jarida la Africa Events la mwezi Novemba mwaka 1985. Miezi miwili baadaye alijibu. Hakuwa mtu wa kubania bania. Na alijitetea vilivyo.
Muhimu ni kwamba alikana ya kuwa akitaka walio hatiani kwenye kesi ya uhaini wapewe hukumu ya kifo.  Alisema ilikuwa ni yeye aliyekuwa akiwaombea wapewe hukumu hafifu, msimamo ambao alidai uliwaudhi wale waliokuwa wakitaka kuona damu ya washitakiwa inamwagika. Na ni kweli kwamba ingawa washtakiwa kadhaa walihukumiwa kifo hakuna hata mmoja aliyeuawa.
Ukweli lakini ni kwamba wakati huo tulikuwa tukifanya kampeni kubwa ya kimataifa kuukashifu mfumo wa Mahakama na wa sheria wa Zanzibar. Katika mfumo huo wa siku hizo washitakiwa wakishitakiwa katika ‘mahakama za umma’ na majaji wale walikuwa watu wasio na ujuzi wa kisheria. Miongoni mwao alikuwamo mtu ambaye kazi yake zamani ilikuwa kuuza njugu mitaani. Mfumo huo pia uliharamisha mawakili wa kuwatetea wafungwa.
Mnamo mwaka 1983 wakati wa mjadala wa mwanzo kuhusu Muungano, Dourado aliibuka na kuwa shujaa wa Wazanzibari kwa kufanya kampeni kali ya kutaka funganisho baina ya Tanganyika na Zanzibar zilegezwe huku akidai kwamba Muungano haukuwa wa halali kwa vile Hati za Muungano hazikuidhinishwa na vyombo  viwili vya utungaji sheria vya nchi hizo mbili kama ilivyotakiwa.
Dourado alizidi kumkoroga kichwa Nyerere kwa kusisitiza kwamba Sheikh Karume alipoweka saini yake kwenye Hati za Muungano alikuwa akifikiria kuwa pataundwa aina ya shirikisho na sio Muungano kama ulivyo.
Ilikuwa kama Dourado alichokoza sega la nyuki.  Watu wa usalama wa taifa waliingilia nyumba yake wakaiparaganya kwa kuikagua juu chini na wakamshika Dourado na kwenda naye Bara walikomweka kizuizini.
Hiyo ilikuwa mara ya pili Dourado kutiwa ndani kwa sababu ya maoni yake.  Mara ya kwanza alitiwa ndani na Sheikh Karume alipopinga waheshimiwa kuwaoa kwa nguvu wasichana Wakizanzibari wenye asili ya Kiajemi. Karume alimtia ndani na akamtandika bakora.
Nyerere alimfungua baada ya kumweka kizuizini Bara kwa muda wa siku 103. Alipofunguliwa alilazimishwa ajiuzulu nyadhifa zake zote za serikali.
Dourado alijiuzulu lakini hakusalimu amri. Alitaka kupigania kiti cha uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi ili aweze kuendelea na kampeni yake dhidi ya Muungano. Hizo zilikuwa ni siku za mfumo wa chama kimoja cha CCM. Wakaazi wa Raha Leo wakamtaka agombee kwenye jimbo lao.
Bado watu wanakumbuka jinsi alivyojitetea kwenye kamati ya CCM ya Raha Leo iliyokuwa ikiyachuja majina ya wagombea. Wapinzani wake kwenye kamati hiyo hawakuweza kufua dafu, walikuwa dhaifu walipokabiliwa na Dourado.
Mmoja alimwambia Dourado: “Lakini huwezi kuzungumza Kiswahili.” 
“Na mimi nazungumza na wewe kwa lugha gani?”  Alijibu Dourado kwa Kiswahili ingawa kwa lafudhi ya matata matata.
Mpinzani wake mwingine akaruka na kumwambia: “Wewe unaupinga Ujamaa.”  Dourado akajibu: “Siyo. Umekosea. Miye napinga jamaa jamaa,” akiwa na maana ya jamaa kupendeleana kwa sababu ya uhusiano wao.
Mwengine akamshtumu kwa kusema kuwa aliichafua hali ya kisiasa wakati wa mjadala wa katiba. Naye Dourado akamjibu kwamba alikuwa akitumia haki zake za kikatiba kwa mujibu wa sheria za nchi.
Wajumbe wa kamati wakampigia makofi.  Dourado akaushambulia mfumo wa chama kimoja wa wakati huo na jinsi chama kilivyofanywa kiwe adhimu kushinda taasisi yoyote nyingine.  Wajumbe wakazidi kumshangilia na kupiga makofi.  Na wote walikuwa viongozi wa ngazi mbalimbali za CCM. 
Kura ilipopigwa asilimia 95 ya kura zilimpendelea yeye awe mgombea wa jimbo hilo la Raha Leo.
Hata hivyo, hakufanikiwa kuwa mgombea wa uchaguzi kwani jina lake lilipigwa mkasi lilipopelekwa Dodoma kwenye makao makuu ya CCM.
Dourado hakupumzika. Aliendelea kumuandikia barua Nyerere akimweleza jinsi mfumo wa chama ulivyokuwa ukimdhalilisha tangu Julai 1983 alipoanza kutoa maoni yake kuhusu mapendekezo ya kuzibadili katiba mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.  Nyerere hakumjibu.
Mwisho wa maisha yake Dourado alikuwa sana ndani nyumbani kwake na mkewe akiugua ugonjwa mbaya wa ngozi ambao husababishwa na hali ya wasiwasi ya kuishi na roho mkononi.
Wazanzibari wanamkumbuka kwa mema yake na wanasikitika zaidi kwamba amewatoka katika wakati huu wa mchakato wa kuizingatia upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Saturday 24 March 2012

MIAKA 48 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR, WAZANZIBAR NA MAONI YAO

 Na Suleiman Al Kindy
Utangulizi
Imetulazimu kutoa mawazo haya kwa kuzingatia ibara ya 18(1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 tolea la 2010, inayosema kama ifuatavyo-:
Bila ya kuathiri sheria ya nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote,bila ya kujali mipaka ya nchi,na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”
Katika miaka yote 48 ya umri wa muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru, (Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Tanganyika), hakuna shaka ya kwamba Zanzibar imekuwa ikiendelea kulalamika na kuonesha kwa vitendo juu ya kutoridhishwa kwake na muundo na mfumo wa muungano huo, pamoja na usimamiaji wake na utekelezaji wake.
Kwa msingi huo,hayo ndio yaliyozaa Muungano ambao ni kero kwa Wazanzibari walio wengi., ni wazi kwamba kuna kila dalili, kasoro na matendo yaliyowazi mengi yaliyojaa shaka inayotulazimu tuamini kuwa kuna dhamira ya makusudi ya kuifikisha Zanzibar pale pasipo takiwa na Wazanzibari walio wengi.
Miongoni mwa mambo yaliyo na athari mbaya na machungu sana na matendo yaliyowazi na yaliyojaa shaka kwa nchi ya Zanzibar na Wazanzibari wenyewe, ni pale siku chache tuu baada ya Muungano huo tumeiona Tanganyika ikihaulisha Mamlaka yake kwa serikali ya Jumhuri ya Muungano,na Zanzibar nayo ikisalimisha mamlaka yake kwa Jamuhuri ya Muungano hiyo hiyo ya Tanzania katika namna ambayo Wazanzibari tunaamini kuwa ni mbinu na hila za kuipokonya Zanzibar mamlaka yake (Soverenity), na hapo ndio ukawa mwanza wa safari ya kuvunjwa nguvu za kimamlaka kwa nchi ya Zanzibar.
Kitendo hicho cha Tanganyika kuhaulisha mamlaka yake kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kimezaa faida mbili kubwa kwa Tanganyika na kusababisha hasara nyingi kwa Zanzibar.
Faida ambazo Tanganyika imezipata ni kama zifuatazo ,Kwanza kuivunja nguvu Zanzibar za Mamlaka, Pili kujikweza na kujipatia maguvu ya kimamlaka ndani ya Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(a) Maamlaka ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kwa mfano katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Ibara ya 33(2) inasema kama ifuatavyo-:
Raisi atakuwa mkuu wa nchi , kiongozi wa Serikali na amiri jeshi Mkuu’
Ibara ya 34 (1) pia inasema kama ifuatavyo-:
Kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na Mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano,na pia juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara (Tanganyika)”
Ibara ya 34 (2) inasema kama ifuatavyo-:
Mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yatahusu utekelezaji na hifadhi ya katiba hii na pia mambo mengineyo yote ambayo Bunge lina mamlaka ya kuyatungia Sheria”
Pia ibara ya 34(3) inasema kama ifuatavyo-:
Mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano,na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara,yatakuwa mikononi mwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano”
Ndugu msomaji, ukiitizama ibara ya 33(2) utagundua kuwa maaana yake ni kwamba huyo Rais ndiye mwenye maamlaka mengineyo yote ya Tanzania Bara (Tanganyika), pia soma kwa makini ibara ya 34(1) (2) na (3), hapo ndipo utagundua kuwa Tanzania Bara (Tanganyika) ipo na ina maguvu kamili ya ndani ikiwemo kuiamulia Zanzibar juu ya mambo yake ya ndani, na nje ya nchi, kwa kumpata Rais aliye amiri jeshi Mkuu na ambaye atasimamia mambo yote ya Tanzania Bara (Tanganyika) kwa maana hiyo kwa nini tusiamini kuwa Tanzania Bara (Tanganyika ) ndio Jamhuri ya Muungano yenyewe?, tumekokotwa kwa mtindo huu kwa muda wa miaka isiyopungua 48.
Kwa upande wa Zanzibar kumezaliwa hasara nyingi kubwa zikiwemo Kupoteza mamlaka yake ya kutambulika duniani kama ni nchi, ambayo mamlaka hayo yamo mikononi mwa Tanzania Bara (Tanganyika), na kutokuwa na mamlaka ya kuhudhuria vikao vya Kimataifa mfano UN,AU,CW, East Africa Community nk.
Hasara nyengine ambayo Zanzibar inaipata ni kupoteza uwezo wake wa kufunga mikataba ya Kimataifa, pia kutokuwa na mamlaka ya kujiamulia ni nchi gani au Taasisi gani ingependa kuwa na mahusiano nayo au kutokuwa na mahusiano nayo ambapo mambo hayo ndio msingi mkuu na chachu ya mafanikio katika nchi yoyote duniani na ndiyo yanayopelekea kuifanya nchi kutambulika kuwa ni nchi kamili , kinyume chake ni kuwa na nchi dhaifu isiyotambua ulimwengu ukoje na unakwendaje.
Hapo ndipo utapoona kwa ubainifu wa mambo yalivyo kama tulivyonukuu maandiko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara tulizotangulia kizielekeza zinaonyesha wazi na kubainisha upamoja wa mamlaka hizo juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano na pia mambo yote yanayohusu Tanzania Bara( Tanganyika).
Ndugu msomaji, hivyo utaona kuwa upamoja wa mamlaka hizo ambazo ziko mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ni kwa kiwango gani Tanganyika inafaidika kupitia upamoja huo.
Kwa maaana hiyo Katiba hiyo moja ni ya Muungano na ndio yenye mamlaka ya Tanzania Bara (Tanganyika) ambayo Tanzania Bara (Tanganyika) ndio yenye mamlaka na Katiba hiyo.
(b) Mamlaka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika ibara ya 64(1) inasema kuwa:-
Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara (Tanganyika) yatakuwa mikononi mwa Bunge”
Ndugu msomaji tunatakiwa tufahamu ya kuwa mamlaka hizo mbili (Bunge na Rais) ndizo zinazosimamia na kutekeleza kuitendaji kwa wizara zote za Tanzania Bara ( Tanganyika).
Vile vile ikumbukwe kuwa mamlaka hizo ndizo zinazotambulika kuwa ni kiwakilishi cha nchi duniani, Rais ndio mamlaka pekee inayowakilisha vikao vyote vya juu vya kimataifa (rejea ukurasa no 3 hapo juu).
Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa-:
Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza-:
(e) “Kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa”
Mamlaka haya ya Bunge ni sawa na mamlaka aliyonayo Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (rejea ukurasa no 2-4 hapo juu).
Hizo ndizo mamlaka zinazosimamia na kutekeleza kiutendaji mambo mengineyo ya Tanzania Bara (Tanganyika).
Kwa uchanganuzi huu ni kwa nini tusiamini kuwa Tanzania Bara (Tanganyika) ni nchi ndani ya Tanzania na pia ni nchi nje ya Tanzania kwa sababu ina sifa za kisheria ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa fursa ya kuzipa mamlaka hizo mbili kuu (Bunge na Raisi) kusimamia mambo yake.
Kwa kigezo cha kukosa sifa hizo ndio kuliifikisha Zanzibar kubainishiwa hadharani kwamba “Zanzibar si nchi”, hili ndio tamko la mwanzo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, hivyo ukijiuliza ndugu msomaji unapoambiwa Zanzibar si nchi maaana yake ni nini kinyume chake? je inamaanisha ni Mkoa? au Jimbo? jawabu zuri unalo wewe ndugu msomaji.
Kisha ikafuatia kauli ya pili kuwa “Zanzibar ni nchi ndani ya Tanzania lakini si nchi nje ya Tanzania”, hivyo duniani kuna utaratibu wa kuwa na nchi ndani ya nchi? au Wazanzibari tumependelewa? Je tutamini vipi kuwa kauli hizo mbili kuwa hazina lengo na dhamira ya majibu ya masuala tuliyoyauliza hapo juu?
Viongozi hao wamejiamini na kukinai kwa uhakika juu ya matamshi yao hayo kwa kutokuwa na shaka wala wasiwasi na kauli hizo, kwa sababu Zanzibar zamani kabla ya leo ilishapotezewa vigezo na sifa hizo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku tukiiona Tanzania Bara (Tanganyika) ikikweya juu ya mabega ya Jamhuri ya Muungano kikatiba kutekeleza malengo yake yote ya kitaifa na kimataifa.
Ndugu msomaji mimi na wewe tutakubaliana ya kwamba Serikali ya Muungano haina utaratibu unaokubalika Kisheria wa kuwakutanisha katika vikao vya pamoja vya walioungana (Tanganyika na Zanzibar) vitakavyojiamulia kila upande kipi kiongezwe na kipi kipunguzwe kwa makubaliano ya nchi huru zilizoungana, hilo halijawahi kutokea katika historia ya Muungano huu kwa sababu halina miguu ya kusimama kisheria.
Sasa hapo ndipo yanapozuka masuala yafuatayo katika vichwa vya Wazanzibari;
  1. Je ni kwa vielelezo gani ambavyo vinaweza kutufanya sisi Wazanzibar kwamba tuamini kuwa kero za Muungano pamoja na utata uliojaa wingi wa matukio kwamba hivyo au hayo hayakupangwa kwa makusudi?
  2. Je ni hoja gani tunaweza kuelimishwa kwamba kero zote za Muungano ambazo ni mzigo mzito kwa Zanzibar zimetokea kwa bahati mbaya?
  3. Je tunatakiwa tuamini kuwa haya na mengineyo yote yanayolalamikiwa na Wazanzibar ni dhana potofu au ni hakika?
  4. Je kama ni bahati mbaya au ni kasoro za Kisheria au kuna dhamira njema juu ya hayo ni sababu gani iliyosababisha kukosa ufumbuzi na utatuzi au kudhihirika kwa nia njema kwa muda wa nusu karne sasa ?
  5. Kwa nini walamikaji wa kimaslahi wa Muungano huu iwe ni upande mmoja nayo ni Zanzibar tu?
Wazee wetu wa hikima wanasema “Mwanadamu humgeuza paka akawa chui pindipo tu atapoamua kumfanyia madhara paka huyo ndani ya eneo la chumba kilichofungwa milango”,
Pia Wataalamu wa Saikologia wanasema kuwa kadiri mwanadamu utakavyo mkosesha haki zake huku akiwa ametambua kuwa unamkosesha haki yake hiyo inayomuwajibikia elewa kwamba atabuni mbinu za kutegua kwa kila kilichotegwa hata kama uteguwaji wake utamletea madhara.
Huu ni wakati wa kuirejeshea Zanzibar Mamlaka yake ili viongozi waliotuelimisha kuwa Zanzibar si nchi wawe na kauli na tamko moja tu lisilo kuwa na upungufu wala ufafanuzi utakaogeuza maana , ya kwamba “Zanzibar ni nchi nje ya Tanzania”’
Hilo linawezekana tukiamuwa kwa Umoja wetu Wazanzibar.
Kwa kulitambua suala muhimu la umoja Katiba ya Zanzibar inathamini suala hilo la umoja na kutuongoza kama inavyojieleza katika ibara ya 23(3)-
Watu wote watatakiwa na Sheria kulinda vizuri mali ya Zanzibar na kwa pamoja kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchum wa Zanzibar kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadae ya Taifa lao”
Pia ibara 23(4) inasema kuwa:-
Kila Mzanzibar ana wajibu wa kulinda,kuihifadhikudumisha uhuru,mamlaka,ardhi na Umoja wa Zanzibar”.
Pia ibara 9(a) inasema kuwa:-
Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya Wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na katiba hii utatoka kwa wananchi wenyewe”
Kwa mantiki pamoja na maoni hayo tunapenda kuwahimiza Wazanzibar kuwa kuigomboa Zanzibar kutoka katika mfumo ulio na Kero ni jambo linalowezekana ikiwa patapatikana umoja miongoni mwetu pamoja na kuamini kuwa kulizungumzia suala la Muungano wa Zanzibar na Tanganyika na kutoa mawazo juu ya kutatua matatizo ya Muungano kwa nguvu za Hoja ni wajibu wa kila Mzanzibar na kufanya hivyo ni kukuza Demokrasia

Friday 23 March 2012

SMZ yatoa miche 200,000 ya karafuu, matunda

WIZARA ya Kilimo na Maliasili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema tayari imetoa miche ya mikarafuu na mazao ya matunda ipatayo 200,000 kwa ajili ya msimu wa kilimo wa mvua za masika Unguja na Pemba zinazotarajiwa kuanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Affan Othman Said alisema utoaji wa miche ya mikarafuu pamoja na mazao ya matunda ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein ambaye ameitaka wizara hiyo kutoa miche hiyo kwa wakulima.
“Tumeanza kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein la kutoa miche ya mikarafuu pamoja na ya matunda kwa wakulima katika matayarisho ya kilimo yanayotokana na mvua za masika,” alisema Affan.
Alisema wananchi wameitikia vizuri agizo la Rais la kuchukua miche ya mikarafuu kwa ajili ya kilimo hasa katika kisiwa cha Pemba ambako zao la karafuu linastawi vizuri.
Katibu Mkuu huyo alisema mikakati inayochukuliwa na wizara hiyo kwa sasa ni kuotesha miche ya mikarafuu na matunda mengine kwa wingi katika vitalu vinavyomilikiwa nayo.
“Tumeanza kuimarisha vitalu vya miche ya mazao mbalimbali ikiwemo mikarafuu pamoja na miti ya matunda....wakulima wameitikia vizuri na wanakuja kwa wingi kuchukua miche hiyo na kuotesha katika mashamba yao,” alisema Katibu Mkuu.
Affan alisema kazi kubwa inayofanywa na Wizara kwa sasa ni kutoa elimu juu ya kuotesha miche ya mikarafuu kwa mafanikio ili miche hiyo iendelee kukua vizuri.
Alisema wamechukua uamuzi huo kutokana na kuwepo kwa malalamiko kwa wakulima kwamba miche ya mikarafuu imekuwa na matatizo mengi yakiwamo ya ukuaji mgumu kwani ukipanda miche 50, inayokubali na kustawi vizuri ni 10 tu.
“Tumeanza kutoa elimu kwa mabwana shamba pamoja na mabibi shamba kwa wakulima juu ya mbinu za kisasa za kuotesha miche ya mikarafuu kwa mafanikio makubwa,” alisema Affan.
Wizara ya Kilimo na Maliasili imeweka lengo la kuotesha na kusambaza miche ya mikarafuu pamoja na ya matunda kwa wakulima ipatayo 200,000 Unguja na Pemba.
Chanzo: habari leo

Wenye kutukosesha miujiza ya Singapore

Na Ahmed Rajab
MARA kadha wa kadha nimekuwa nikigusia katika safu hii jinsi viongozi wetu wanavyokosa mwelekeo au dira ya kuongoza. Badala ya kuikwamua nchi kutoka umasikini wanajikwamua wenyewe na wanaiachia nchi iselelee na hali yake ya ufukara.
Ukiwaangalia utawaona kila uchao wamo mbioni kujipendekeza kwa wanaowaita wafadhili japokuwa fadhila ya hao wafadhili ni kama fadhila ya punda kwa vile mara nyingi huwa ina harufu mbovu. Inawafanya viongozi wetu wasiweze kufikiria mbinu za kuiendeleza nchi bila ya kushikilia uzi uleule wa ‘omba omba’.
Viongozi wetu hawana kazi ila kila mara kuwabembeleza wafadhili wawasaidie kutuletea maendeleo kana kwamba wao na wananchi wenzao hawana uwezo wa kuiendeleza nchi.
Viongozi wetu wana tabia ya kusahau kama miujiza hutokea duniani hata katika upande wa maendeleo ya nchi. Hapa ningependa kukumbusha miujiza iliyotokea Singapore hasa kwa vile Zanzibar inalingana mengi na Singapore huko ilikotoka.
Nchi hiyo ilijitangazia uhuru mwaka 1963 na ikajiunga na Malaysia pamoja na Sabah na Sarawak kuunda Shirikisho la Malaysia. Sababu zilizowafanya viongozi wa Singapore wajiunge na Malaysia zinaeleweka.
Kwanza wakihisi kwamba Uingereza isingeliipa uhuru nchi yao kwa sababu ingeiona kuwa ni ndogo isiyoweza kujitegemea. 
Pia wao wenyewe viongozi wa Singapore wakiamini kwamba nchi yao isingeweza kujikimu kwa vile haikuwa na eneo kubwa la ardhi, haikuwa na maji ya kutosha, haikuwa na masoko wala maliasili. Tena wakitaka kuwa chini ya mwavuli wa Malaysia kujikinga na joto la Wakomunisti waliokuwa wakiyarandia madaraka.
Kwa muda wa miaka miwili Singapore ilikuwa sehemu ya Malaysia. Lakini kama ulivyo Muungano wetu muungano wao nao ulikuwa na kero zake na Singapore na Malaysia zilikuwa hazishi kusuguana roho. Hatimaye Malaysia ikaitoa Singapore kutoka Shirikisho. Ndipo Uingereza ilipoipa Singapore uhuru rasmi mwaka 1965.
Wakati huo taifa hilo dogo lilikuwa limetumbukizwa kwenye gunia la nchi za Ulimwengu wa Tatu.  Miujiza ya mambo ni kwamba leo limo kwenye kaumu ya nchi za Ulimwengu wa Kwanza.
Singapore imeweza kujipatia ufanisi wake licha ya kwamba haina idadi kubwa ya wakaazi, haina eneo kubwa la ardhi (ni taifa dogo lenye visiwa 63) na kama nilivyokwishagusia ina ukosefu wa maliasili. Ilipopata uhuru si wengi waliofikiri kwamba kijinchi hicho kitaweza kuwa na uhai. 
Wakati wa uhuru jumla ya Pato la Taifa kwa kila mtu huko Singapore lilikuwa sawa na dola 400; hii leo ni zaidi ya dola 22,000. Pato hilo ni la nne kwa ukubwa duniani na linalipita lile la Uingereza iliyokuwa ikiitawala Singapore.
Hii leo Singapore ina moja ya bandari zenye shughuli nyingi duniani, ni kituo cha tatu kwa ukubwa duniani cha kusafishia mafuta na nchi hiyo imegeuka kuwa kituo kikuu duniani cha kuzalisha bidhaa viwandani na katika makarkhana.  Singapore imeweza kuchupa kutoka kwenye umasikini na kusimama kwenye utajiri katika muda wa kizazi kimoja tu.
Nini kinachoizuia Zanzibar au Tanzania Bara isipate miujiza kama hiyo? Labda niligeuze swali naniulize ilikuwaje hata Singapore ikapata miujiza hiyo?
Jibu ni rahisi kulipata. Tangu ipate uhuru Singapore imekuwa na uongozi bora.  Anayepongezwa kwa ufanisi huo ni Lee Kuan Yew aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa miongo mitatu tangu uhuru na aliyeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika uongozi wa serikali hadi hivi karibuni.
Ni yeye aliyekuwa akisisitiza kwamba maliasili pekee ya Singapore ni watu wake na jitihada yao ya kazi. Wengi nchini mwake wanamsema vyema kwa mvuto wa uongozi wake wakati wa uhuru na wa kujitenga na Malaysia.
Lazima nikumbushe kuwa Lee Kuan Yew si malaika. Alikuwa dikteta. Tena alikuwa jeuri; hakuwa akimsikiliza mtu; alitakalo ndilo. Utawala wake ukiingilia kila jambo.
Ingawa watu walikuwa na uhuru akisisitiza kuwa hawakuwa na uhuru wa kuwaudhi wengine. Kwa hivyo, si karaha tu bali ni kosa la jinai, kwa mfano, kutema mate njiani. Adhabu ya uhalifu huo ni faini ya dola 250 sawa na adhabu ya kuvuta sigara kwenye ofisi za serikali au kuvuka barabara hovyo hovyo bila ya kujali magari.
Wenye kutafuna ubani (chingamu) njiani nao pia hutozwa faini hiyo hiyo. Adhabu ya wanaopatikana na hatia ya kuingiza nchini mihadarati ni kifo.
Lee aliwalazimisha watu waweke akiba asilimia 25 ya pato lao ingawa kulikuwa na malalamiko kwamba serikali ilikuwa ikizitumia kwa ubadhirifu hizo fedha za akiba ya wananchi.
Hata hivyo, udikteta wake Lee ulikuwa na tofauti. Haukuwatia sana hofu wananchi. Lee alikuwa dikteta karimu.
Wakati wa zama za ‘vita baridi’ yaani zama za  michuano ya kisiasa baina ya nchi za kibepari na zile za kisoshalisti sisi tuliokuwa katika mrengo wa kushoto tukimponda Lee Kuan Yew kuwa alikuwa kibaraka wa nchi za Magharibi. Yeye mwenyewe akijinata kuwa alikuwa msoshalisti aliyeutumia ubepari kufikia lengo la kuunda jamii yenye haki na ustawi.
Ninaamini kwamba viongozi wetu wa Visiwani na wa Bara wana mengi wanayoweza kujifunza kutoka kwa kiongozi huyo wa Singapore. Nadhani kila mmojawao anapaswa asome kitabu alichokiandika kiitwacho ‘From Third World to First’ (Kutoka Ulimwengu wa Tatu hadi wa Kwanza).
Mengi aliyoyaandika yanataka utulivu na nafasi kubwa kuyajadili. Lakini naitoshe hapa tukiyapitia machache tu. Kati ya muhimu aliyoyataja ni kwamba utamaduni wa taifa, zaidi ya uchumi na siasa, ndio utaoamua mustakabali wa nchi.
Suala hili la nafasi ya utamaduni katika maendeleo ya nchi ni muhimu lakini mara nyingi hupuuzwa na viongozi wetu.  Nadhani ni kiongozi mmoja tu Wakiafrika, Amilcar Cabral wa Guinea-Bissau aliyelijadili kwa kina suala hilo ingawa kwa bahati mbaya hakupata kuongoza nchi kwani Wareno walimuua kabla ya nchi yake kuwa huru.
Kwa mujibu wa Lee walipoanza harakati za kisiasa katika miaka ya 1950 hawakujua namna ya kuendesha nchi au jinsi ya kuyatanzua matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii. Lakini walikuwa na raghba kubwa ya kuibadili jamii isiyokuwa na usawa na haki na kuifanya iwe jamii ya haki na usawa.
Anasema alilazimika kuhakikisha kuwa ana watu wenye uwezo ambao aliwapachika katika nyadhifa kubwa kwa kuwateua wawe mawaziri na watumishi wakuu wa serikali. Lengo lilikuwa kuwafanya waendeshe utawala wenye mfumo aminifu, ulio mnyofu na wenye kuyakidhi mahitaji ya wananchi. 
Lee ameendelea kusema kwamba alikuwa na kazi ngumu ya kuwafanya wafanya kazi wawe upande wa serikali wakati ambapo serikali ilikuwa inayashughulikia mahitaji ya wawekezaji ambao wakiwategemea kwa rasilmali zao za fedha, maarifa, uweledi  wa menejimenti na wa kuendesha mambo kwa jumla na masoko yao ya nje.
Kitu cha awali alichohakikisha alipokuwa waziri mkuu (wakati huo akiwa na umri wa miaka 34)  ni kwamba pawepo mawaziri kadhaa wenye kupenda mno kusoma na wanaovutiwa na fikra mpya lakini wasiofadhaishwa au kupigwa na bumbuwazi na fikra hizo.  
Lee ameeleza jinsi yeye na mawaziri wake walivyokuwa wakiazimana vitabu na makala mbalimbali za kuvutia.  Walipoingia serikalini walikuwa madubu, wajinga hawakujuwa namna ya kutawala. Lakini walikuwa waangalifu na wakizizingatia sera kwa makini kabla ya kuzitekeleza. 
Muhimu yeye na mawaziri wake wakiaminiana. Wakijuwana nini uwezo wa kila mmojawao na nini udhaifu wao kwa hivyo wakichukuliana.
Alibahatika kuwa na mawaziri waliokuwa na azma moja na malengo sawa. Mawaziri waliokuwa karibu naye walifanya kazi pamoja kwa zaidi ya miongo miwili na walikuwa wakubwa zake kwa umri na hawakuchelea kumpasulia walivyokuwa wakifikiri, hasa alipokuwa akikosa.
Amesisitiza  kwamba jambo lililowapelekea wakafanikiwa ni kwamba kila mara wakitalii na kuangalia namna ya kutanzua matatizo au namna ya kuyafanya mambo yawe bora zaidi. Hakuwa mfungwa wa nadharia yoyote.  Mantiki na hali halisi ilivyo ndiyo mambo yaliokuwa yakimuongoza.
Jambo jengine ni kwamba akijaribu kujifunza kutokana na makosa waliyoyafanya viongozi wengine katika nchi zao.
Aligundua mapema alipoanza kutawala kwamba hakukuwa na matatizo yaliyoikabili serikali yake ambayo serikali nyingine hazijayakabili na kuyatanzua. 
Kwa hivyo, alikuwa na desturi ya kuchunguza nani mwengine alikabiliwa na matatizo kama ya Singapore, na kutaka kujuwa namna alivyoyashughulikia, yawematatizo hayo kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege mpya au mitindo ya kusomeshea maskuli. Alifanya hima ya kuwatuma maofisa wake wende kwenye nchi zilizofanya mambo yao vyema ili wajifunze. 
Lee anakumbusha kwamba akipuuza lawama na nasaha kutoka kwa mabingwa au mabingwa uchwara, hasa wasomi wa sayansi za kijamii na kisiasa.
Tukiyatafakari maandishi ya Lee tunaona kwamba miongoni mwa kanuni zilizoifanya Singapore iendelee ni pamoja na ile ya kuwa na umoja wa kijamii, kuufyeka ufisadi serikalini, kugawana kwa usawa matunda ya maendeleo, kuwapa wananchi wote fursa sawa na kuwa na mfumo wa serikali unaoongozwa na wataalamu na weledi.
Hizi ni kanuni za kimaadili na tunastahili kuziiga. Angalau huko Zanzibar tayari tuna umoja wa kijamii; yanayokosekana ni maendeleo na hayo mingine yanayofuata maendeleo

Thursday 15 March 2012

Wakati umefika wa kuwa na ‘Mkataba wa Kijamii’ Zanzibar

Na Ahmed Rajab
MWANADAMU amezaliwa huru lakini kote duniani ametiwa minyonyoro,”  nimeyanukuu hayo kutoka katika maandishi ya Jean-Jacques Rousseau, mwanafalsafa na mwandishi mashuhuri aliyeishi nchini Ufaransa karne ya 18.
Rousseau aliwahi pia kuandika kwamba wenye mamlaka katika nchi ni umma na kwa vile umma hauna nguvu yoyote isipokuwa ya utungaji sheria, basi hutenda mambo kwa kutumia sheria.  Ameendelea kueleza kwamba sheria yoyote ile isiyoidhinishwa na umma huwa ni batili, kwa hakika huwa si sheria kamwe. Wenye nguvu ya kutunga sheria ni umma na ni umma tu wenye nguvu hiyo, kwa mujibu wa Rousseau.
Mwanafalsafa huyo ni maarufu kwa ile nadharia yake ya kutaka pawepo Mkataba wa Kijamii baina ya serikali na umma. Kitabu chake kuhusu ‘Mkataba wa Kijamii’ ni moja ya nguzo kuu za fikra za kisasa za kisiasa na za kijamii. Na ni moja ya misingi ya utawala wa kidemokrasi.
Maandishi ya Rousseau kuhusu siasa na elimu yalikuwa na athari kubwa kwa nadharia za kisiasa za karne mbili zilizopita. Maandishi hayo ndiyo yaliyowavutia na kuwaathiri wanamapinduzi waliokuwa wakiandaa Mapinduzi ya Ufaransa yaliyotokea baada ya kufariki kwake.
Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964 yaliwaahidi Wazanzibari mambo kadhaa ambayo hadi leo bado hayajatimizwa. Waliopindua waliiona jamii ya Visiwani kabla ya Mapinduzi kuwa ni jamii isiyokuwa na haki na iliyokuwa ya kibaguzi. Wanazungumzia hasa kuhusu haki za kimsingi za binadamu na fursa zilizokuwepo, fursa ambazo wanasema walikuwa wakipewa wachache na walio wengi wakinyimwa.
Hadi leo wenye kujiona kuwa ni warithi wa Mapinduzi hayo haweshi kuelezea kuhusu yale wanayoyaona kuwa ni maovu na madhambi ya utawala uliopinduliwa. 
Kama ilivyo kawaida ya wanaopindua wapinduzi wa Zanzibar muda wote huu wamekuwa wakidai kwamba wao ndio wenye utatuzi wa matatizo yote yanayoikabili nchi na hivyo wamekuwa wakiahidi kuwa watawapa wananchi wenziwao fursa sawa bila ya kujali hadhi zao katika jamii. Mtu hatoangaliwa ikiwa ni wa tabaka la wanaotawala au la matajiri wa juzi juzi au ikiwa ni mwana wa mkulima kutoka shamba. Wote watapewa fursa sawa.
Ahadi zilizotolewa na Mapinduzi zimevunjwa. Matokeo yake ni kwamba wengi wa watu wa mijini na wa mashambani wangali wanaishi katika mazingira magumu ya umasikini, magonjwa na uhaba wa chakula.
Hali hiyo haishangazi kwa sababu hii leo uchumi wa Zanzibar umeanguka. Mdororo huo wa uchumi unazidi huku wale wenye dhamana ya kuushughulikia, ingawa wanajaribu, bado hawakufanikiwa kuchukuwa hatua madhubuti za kuuzuia uchumi huo usizidi kuporomoka. 
Hali ya mambo inazidi kutatanika kwa vile sekta ya kilimo nayo imeanguka na wakati huo huo hakuna fedha nchini na hivyo kuna ukosefu mkubwa wa ajira (kama asilimia 70 ya watu wenye uwezo  wa kufanya kazi hawana ajira). Watu hawana fedha za kutumia na serikali haina mpango wa kutoa huduma za jamii bure.
Huo bila ya shaka sio urithi wa kujivunia wa wale walioyaasisi Mapinduzi. Na historia haiwaonei huruma inapowahukumu na kuangalia iwapo wameineemesha jamii au wameisakamiza kwa kuufisidi uchumi uliokuwa ukistawi kabla ya Mapinduzi.
Kuna swali ambalo Wazanzibari wana haki ya kuliuliza, nalo ni: nini matokeo ya miaka 50 ya serikali za awamu zote ya kuuimba na kuufatiliza ule wimbo wa ‘Mapinduzi Daima’? Hilo ni swali rahisi kulijibu kwani tukiiangalia hali ya mambo ilivyo hatuna budi ila kukubali kwamba sera zilizokuwa zikifuatwa na Serikali ya Mapinduzi kwa muda wa miaka 50 iliyopita ni sera zilizoshindwa kuleta tija na ufanisi. Na tunakuwa tunajidanganya tu tusemapo kwamba Wazanzibari wote au wengi wao wanaishi maisha stahifu yasiyo na unyonge.
Hii leo si uchumi tu bali hata sekta muhimu za elimu ya kijamii na afya zinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa. Jambo la kutia moyo ni kuona kwamba pamoja na jitihada za wachache serikalini za kujaribu kuibadili hali ya mambo pia kuna asasi za kiraia zinazotoa mchango wao.  Mojawapo ya asasi hizo na iliyo mbele katika haya ni taasisi ya ZIRPP ambayo hivi majuzi ilimkabidhi Rais Ali Mohamed Shein ripoti mbili, moja kuhusu upangaji wa miji na ya pili kuhusu uchumi.
Wanachopaswa serikali na wananchi kukumbuka ni kuwa Zanzibar ni ya Wazanzibari wote; ni kama shirika lao wote. Kila mmojawao ana hisa na pia dhamana katika shirika hilo. Kila mmojawao, si serikali pekee, ana wajibu wa kuibadili hali iliyopo.
Lazima hali iliyopo ibadilike. Na inaweza kubadilika. Duniani kuna mifano mingi ya nchi ambazo zamani zilikuwa nyuma kimaendeleo na ambazo sasa ziko katika safu za mbele miongoni mwa nchi zilizoweza kubadili mifumo yao ya kiuchumi na ya kijamii.
La awali kufanywa ni kwamba serikali itambue kwamba inapaswa iwe na mkataba na wananchi. Ili Zanzibar iweze kupiga hatua na kuendelea kuna mambo yanayohitaji kutekelezwa na serikali na hivyo kuutimiza ule mkataba wake wa kijamii na wananchi. Muhimu ni kuwa na sera zitazoweza kuvinyanyua viwango vya sekta mbalimbali zikiwa pamoja na za elimu, afya, kilimo, biashara na utalii.
Inatia moyo kuona kwamba Wizara ya Elimu ya Zanzibar imeanza kampeni ya kuvinyanyua viwango vya elimu nchini humo na kwamba wenye kuhusika katika wizara hiyo wana hisia ya kuikuza elimu. 
Changamoto kubwa inayoikabili serikali ni kufuata sera ya uchumi itayoigeuza Zanzibar iwe Visiwa visivyotoza ushuru na kodi za kibiashara.  Ikifanya hivyo itakuwa rahisi kuwavutia wawekezaji kutoka nje waingize rasilmali zao katika sekta zilizo muhimu za uchumi wa nchi hiyo. Rasilmali hizo zikiingia kuufufua uchumi pataweza kupatikana fursa nyingi za ajira.
Uwekezaji huo pia utaufanya uchumi ukue kila mwaka si kitakwimu tu bali kwa kuongezeka kwa mapato ya kila Mzanzibari na hivyo kuwapatia wananchi uwezo halisi wa kujikimu kimaishi. Kwa sasa wengi wao wanaishi kwa kasoro ya dola moja ya Marekani kwa siku.
Hatua nyingine zinazoweza kuchukuliwa na serikali ni kuwa na mkakati wa kuvigeuza visiwa vya Unguja na Pemba viwe ni kituo cha huduma za fedha na za shughuli za benki.
Sambamba na hatua hizo ni kuifanya tena Zanzibar iwe ni kitovu cha biashara na usafiri kwa eneo zima la Afrika ya Mashariki na ya Kati.  Hatua zote hizo zitachangia sana kutanzua matatizo ya kiuchumi ya Visiwa hivyo.
Linalotakiwa kufanywa ni kuchukuliwa hatua ambazo zitaweza kwa haraka kuirejeshea Zanzibar ile hadhi yake ya kale ya kuwa kituo madhubuti cha kiuchumi katika eneo la Afrika ya Mashariki na Kati. Kwa bahati mbaya kwa sasa Zanzibar haiwezi kujichukulia hatua zote hizo za kiuchumi kwa vile inahitaji ridhaa na ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Na hatua kama hizo zisipochukuliwa basi hali za kimaisha ya wengi wa Wazanzibari zitaendelea kuwa ngumu kwa muda mrefu ujao kwa sababu uchumi wa nchi yao haumudu kuwahudumia wananchi kwa kuyakidhi mahitaji yao ya kila siku.
Wazanzibari wana matumaini mema wakizingatia utajiri unaoweza kupatikana Zanzibarna zaidi wakiyafikiria mafuta yaliyo chini ya maji ya bahari ya Zanzibar.Wana matumaini na wana subira.
Wazanzibari wa ndani ya nchi na walio ughaibuni wote wana hamu ya kuendelezwa kwa hali iliyopo Visiwani ya amani, umoja na utulivu wa kisiasa. Na wote wanataka nchi yao ipate maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.
Kwa haya na kwa mahitaji ya baadaye ya uchumi, kuna haja muhimu ya kuukuza uwezo wa watendaji katika sekta za serikali na au za mashirika ya watu binafsi. Hii ina maana kwamba Zanzibar lazima iwe na uwezo wa kuzipokea fedha nyingi za rasilimali zitakazoingia nchini na pia iwe na uwezo wa kuhudumia uchumi utakaokuwa unatanuka kwa haraka.
Changamoto iliyopo hapo ni kwamba kwa sasa Zanzibar ina ukosefu wa watendaji wenye ujuzi au waliopata mafunzo yatayostahiki kwa uchumi wa aina hiyo.  Hivyo, serikali inawajibika kuchukuwa hatua za dharura ili kuiitayarisha Zanzibar kwa mustakabali huo.
Chanzo: Raia Mwema

Weiss: Zionism has created 'rivers of blood'


When Binyamin Netanyahu, Israel’s prime minister, visited Washington last week on the eve of the Purim holiday, he gave Barack Obama, the US president, what he considered a symbolic gift - a copy of the old testament book of Esther.

Netanyahu called it "background reading on Iran", since its story concerns relations with Jews in the Persian empire some 2,500 years ago.
It is considered by scholars to be mostly fiction, but for Netanyahu Esther represented justification for his stance against modern Iran.
”Israel must reserve the right to defend itself. And after all that’s the very purpose of the Jewish state. To restore to the Jewish people control over our destiny,” Netanyahu said.

But Netanyahu’s controversial reading of history, even his fight to preserve the state of Israel, are questioned by many of Judaism’s own religious authorities.

"This is against the will of the Almighty and this is not what it means to be a Jew," says Jewish religious scholar Rabbi Yisroel Dovid Weiss, a spokesman for "Jews against Zionism", who believes that Israel as a state is not legitimate. He says that Zionism has created "rivers of blood" and he opposes the occupation of Palestine.
On the threat from Iran and President Ahmadinejad he says: "He gives charity to Jewish communities and he says one thing: he has a problem with the oppression of the Palestinian people. And the words "wipe out" he constantly says that Iran doesn't have a history and he is not talking about harming anybody he says that God will not allow this crime to happen. We concur with him that Jews are in danger because there is Zionism because it says in the Tora if you rebel against God, it will not be successful and there will be catastrophic results and Zionism has brought catastrophic results and it could be much worse."
Today on Talk to Al Jazeera Weiss explains why Zionism and Judaism are not necessarily the same thing

Tuesday 13 March 2012

Wanaosaka ajira Oman wakwama Zanzibar

ZAIDI ya vijana 150 waliokuwa wasafirishwe kwenda Oman kwa ajili ya kupata ajira katika viwanda mbalimbali, wamekwama baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kushindwa kuitambua Kampuni ya Zam Agency yenye makao makuu yake Unguja, inayowasafirisha vijana hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Zainab Ramadhan Mohammed aliwaambia waandishi wa habari kwamba kampuni yake imekwama kusafirisha vijana hao ambao walikuwa waende Oman kufanya kazi katika viwanda mbalimbali, baada ya kukamilika kwa masharti mbalimbali ikiwemo mikataba halali ya ajira.
“Tunasikitika sana kusema tumeshindwa kusafirisha vijana 150 ambao walikuwa waende Oman kufanya kazi katika kampuni za viwanda ikiwemo vya kutengeneza maziwa kwa sababu Serikali haijakubaliana na sisi ikiwemo kutupa kibali cha kufanya kazi hiyo,” alisema Zainab.
Zainab alielekeza shutuma zake kwa Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Ushirika, Haroun Ali Suleiman ambaye alizungumza katika vyombo vya habari akisema kwamba kampuni yake haitambui.
Alisema alisikitishwa na kauli hiyo ya waziri kwa sababu kampuni yake imesajiliwa na kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo za kutoa misaada ya kibiashara.
Alisema kutokana na uamuzi wa SMZ kuchelewesha kutoa kibali kwa kampuni hiyo, tayari ajira 200 zimepotea na kuchukulia na Serikali ya Kenya iliyopeleka watu kufanya kazi katika kampuni na sehemu za viwandani.
Alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kumuona tena waziri ili kulipatia ufumbuzi suala hilo ikiwemo kutoa kibali cha ruhusa ya kusafirisha vijana nje ya nchi ili kupata ajira zenye kutambulika rasmi.
Zainab alionesha mkataba wa kusafirisha vijana kwenda Oman wa Kampuni ya Ilya Manpower ambao unatakiwa kujazwa na wizara husika ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hivi karibuni, Waziri Haroun alipozungumza na waandishi wa habari alizitaka kampuni ambazo hazina vibali, kuacha kusafirisha vijana nje ya nchi

Saturday 10 March 2012

Jee Tanganyika Imekufa

Nembo ya Tanganyika kabla ya Muungano
Nembo ya Tanzania baada ya muungano
Mimi hushangazwa sana na viongozi wetu wa smz kila moja husema subirini ukushanyaji wa maoni ya Katiba mutapata fursa ya kutocha kutowa maoni yenyu?, hii Wzanzibar nikurowekwa tu na viongozi wetu tulio wapa majukumu hutafuta mbinu za kuyakwepa.

Kifupi ikiwa Wzanzibar hatuto fanya kitu chochote hivi sasa kabla ya kuja hilo Jindamizi la Katiba na tukaskiliza kauli za wana siasa basi tutaangamia sisi na kizazi chetu chote kijacho, maana haingii akilini hata kidogo kuwa Wzanzibar tukae kitako tusubiri Azabu yenye kumiza? sisi maoni ya katiba yatatusaidia nini Zanzibar?.

Wallah ikiwa tutakaa na kusubiri tutowe michango yetu kuhusu vipi katiba ya Tanganyika iwe basi itakuwa sisi ni majuha na twachangia kitu kisicho tuhusu sisi na upande mwengine ni hasara na majonzi kutowa michango yetu tukifanya hivyo.

Nasema hivyo kutokana na dalili nyingi ambazo zimechajitokeza kuwa wenzetu siwo na hawana zamira ya kweli, kwanza utasemaje kuwa ktk kuchangia maoni swala la Muungano lisikuswe abooo? sasa ikiwa swala la Muungano ndio priority yamwanzo kwa Wzanzibar, kuna kipi tena chakuchangia kwa Zanzibar?

Au wamesha zowea ktk vigao vyao vya chama kuwa kwa upande wa viongozi wao Zanzibar siku zote ni hawala Bwana hata kama wanaiteketeza Zanzibar na kuitowa mlongo wa Nyuma? wakati ule umeshapitwa na hatutekeemei kurudi tena.

Wazanzibar wa sasa sio wakufanya Bind na kuibiwa kimacho macho na wajanja wanao jita Wtanzania kumbe ni Wtanganyika, hakuna asio juwa kuwa hivi sasa Muungano unanuka Zanzibar kama vile vidonda vya Muhimbili kutokana na ujambazi na ulahai muliotufanyia na munaendelea kufanya, ikiwa utamuona Mzanzibar kasimama hivi sasa kutetea Muungano awe kiongozi au mtu wa kawaida basi nilazima ufanye chaka itakuwa ama kachanganya na Tanganyika ana damu ya huko.

Mimi nasema hivi sasa sio wakati tena wakudai Serekali 3 hata tujalie Bara wakubali hivyo basi sisi Wzanzibar nikuvunja Muungano fake, tusikubali kudanganywa muda huu tulio nao, Sitta asema kurudi kwa Tanganyika ni uchindani, wewe Sitta unazani Wzanzibar wote Pumba?

Sisi tumechawashtukizia kuwa nimatapeli,majambazi mpaka ktk Serekali, Nimpumbavu gani alokuwa hajuwi kuwa Tanganyika ipo na haikupoteza kitu chochote cha Tanganyika ktk Muungano? Kuanzia Katiba, Bendera Mpaka nembo ya Taifa la Tanganyika ni ile ile inayo tumika hivi sasa kufanya nembo ya Tanzania, na Bendera ya Tanganyika ni ile ile ya Tanzania Bada ya mistari kukaa sawa imepanda kilima tu.

Kwa hio nisawa Mh Samuil Sitta useme Tanganyika isirudi ndio ? kwa sababu Tanganyika ipo na ndio hio Tanzania nisawa na Zaire Kuita Kongo hivi sasa, kwa hio wanao sema hawataki mfumo wa sasa wa Serekali mbili akina Mh Mansoor nazani wamejisahau au wameshindwa kujuwa mambo?

Kwani hivi sasa tujiulize tuka ktk mfumo wa Serekali ngapi? kifupi Serekali ni Moja yani Republic of Tanzanzia/Tanganyika, Zanzibar imecha mezwa ktk Tumbo la Tanzania ambayo ni Tanganyika kikatiba,Bendera,Nembo ya Taifa na hata Mambo ya Njee inajulikana Tanzania lakini ni kitega uchumi cha Tanganyika huvugwa vugwa tu Viongozi wa smz lakini Tanganyika haijaluzi kitu na iko imara kwa Mwezuli wa Tanzania.

Kwa hio Ndugu zangu kama tunasubiri kutowa michango yetu ya katiba ? basi tusubiri kuchangia bajeti ya Tanganyika kwa faida ya Wtanganyika sisi Zanzibar tumepotezwa hata jirani zetu Mourishz Wanatucheka kuto kujitambua na mpaka leo kuona viongozi wetu wanajuwa Muungano haupo tena lakini wao bado wamebaki tulinde na tuienzi Tanganyika izidi kumaliza.

SASA ANGALIENI JEE TANGANYIKA IMEKUFA?

Source: Jamii Forum

SMZ inacheza na Mishahara ya watu

 Salim Said Salim
UTAWALA wa kidemokrasia, haki na sheria una vigezo vingi vinavyohitaji kulindwa na kuheshimiwa siku zote na wakati wote.
Miongoni mwao ni kwa watawala kutumia sheria ziliopo na si kuzifumbia macho na kuachana na matumizi ya amri, maelekezo sambamba na mabavu.
Katika miaka ya mwanzo baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 amri zilizotolewa na wakubwa katika serikali, iwe kwa matamshi au maandishi, ndizo zilizotumika na watu hawakuwa na haki ya kukataa, kushauri, kukosoa au kutaka ufafanuzi wa jambo lile.
Aliyejaribu hata kunong’ona kulalamikia amri iliyotolewa na wakubwa alijikuta amejitafutia balaa isiyoelezeka na hata kujikuta amefunguliwa milango ya jela.
Waliojaaliwa kutoka hai (wengine hawakuonekana mpaka leo) baada ya kuwekwa gerezani, wengine wakiwa na majeraha mwilini kutokana na mijeledi waliochapwa au kupungukiwa nuru ya macho kutokana na kuwekwa vyumba vya kiza walibaki kumshukuru Mungu na hapakuwepo pahala pa kupeleka malalamiko.
Mtu aliyelalamika au kuikosoa serikali alipachikwa kila majina ya uovu yaliyomo katika msamiati wa Kiswahili … adui wa mapinduzi...kibaraka...msaliti..si mwenzetu au haini.
Wengine waliporwa mali zao na hata wake zao wakati wakiwa jela.
Miaka sasa imepita na watu wengi walianza kujenga dhana na kuamini kuwa dhuluma za aina ile zimepita na zitakuwa ni sehemu ya kusikitisha ya historia ya Zanzibar , lakini wapi?
Sasa mambo kama yale ya zamani, lakini kwa kiwango kidogo sana , yanaonekana kuchipua kidogo kidogo na kustawi ndani ya baadhi ya taasisi za serikali.
Miongoni mwa taasisi hizo ni vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar- Magereza (wenyewe wanaita Mafunzo), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM).
Ni lazima yaanze kudhibitiwa mapema kabla hayajastawi na kuwa kama kidonda ndugu…hakiponi.
Wananchi hivi sasa wanalamikia makato katika mishahara kama vile wao ni askari ambao hupaswa kutii kila amri wanayopewa kama walivyo askari kwenye gwaride wakati tu kama tunavyoona wakati wa sherehe za uhuru, mapinduzi na muungano.
Hali hii ilionekana katika taassi za serikali wakati timu za Zanzibar ziliposhiriki katika mashindano ya Shirikisho la Kandanda la Afrika (CAF).
Wafanyakazi katika baadhi ya taasisi walikatwa fedha za tiketi ya michezo hii iliyofanyika Zanzibar bila ya kushauriwa.
Hii sio haki na ni uonevu mkubwa. Mshahara ni mali ya mfanyakazi na ni yeye tu ndiye mwenye mamlaka kamili juu ya matumizi yake.
Anachoweza mtu mwingine au taasisi kufanya ni kumshauri mtu juu ya njia nzuri za kuutumia huo mshahara na si kumuamulia utumike vipi.
Akitaka kuutumia kidogo kujenga kibanda cha kuku, akitaka kuongezea mke au hata kuutoa sadaka ni shauri yake. Ni yeye ndiye aliyeutolea jasho na si mtu mwingine.
Hali hii ya kuchakua mishahara ya wafanyakazi iliwahi siku za nyuma kulalamikiwa hata ndani ya Baraza la Wawakilishi na wananchi wengi waliamini serikali imesikia kilio cha wafanyakazi na haitarudia mwenendo huu.
Sasa tena tunasikia malalamiko ya watu kukatwa mishahara yao bila ya ridhaa yao au kushauriwa, bali amri ndiyo iliyotumika.
Sina hakika kama hili ni agizo rasmi la serikali au ni baadhi ya wakubwa wanaoongoza taasisi za serikali ndio wamejifanyia wenyewe tu na kuamini hapana anayeweza kuhoji uamuzi wao huo.
Hili si suala dogo na halifai kupuuzwa. Ni vyema kwa serikali ikafanya uchunguzi wa kina na kutoa tamko la ufafanuzi.
Ufafanuzi utawafanya watu waelewe kama kwa Zanzibar mishahara ya watumishi wa serikali ni mali ya serikali na sio hao watumishi wanaoihudumia kwa uadilifu mchana na usiku na katika mazingira mbali mbali.
Hata kama palionekana kuwepo haja na busara ya kutoa mchango ili kusaidia watu au jamaa wa waliopata maafa kama yale ya kuzama kwa meli ya mv Spice Islanders mwaka jana iliyokuwa inatoka Unguja kwenda Pemba bado ridhaa ya wafanyakazi ilikuwa inahitajika.
Lakini kama hao wakubwa katika baadhi ya taasisi za serikali walijichukulia wenyewe tu hatua za kuwakata mshahara wafanyakazi wanaowaongoza basi wawajibishwe kinidhamu au kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wasifanye mchezo huu wa kuchezea mishahara ya watu.
Hatari ninayoiona hapa ni kuwepo uwezekano wa siku za mbele kurudia mtindo wa zamani wa wafanyakazi wa serikali kukatwa mshahara kuchangia mbio za mwenge na sherehe nyingine mbali mbali za kitaifa zisiokwisha.
Hapa inafaa tukumbuke kwamba hali ya maisha hivi sasa Zanzibar na Tanzania kwa jumla ni ngumu na viwango vya nishahara vya hivi sasa havikidhi hata robo ya mahitaji ya lazima ya wafanyakazi wengi wa serikali.
Kwahiyo, unapokata hicho kinachoitwa “kitu kidogo tu” kutoka katika mishahara kwa kweli si unajeruhi, bali unauwa.
Kama serikali kwa hivi sasa haina uwezo wa kiuchumi wa kuongeza viwango vya mishahara kwa watumishi wake basi ijizuie kuukata huo mkia wa mbuzi inaowapa watumishi wake.
Dhuluma nyingine inayoonekana kufanyiwa wafanyakazi wa Zanzibar katika baadhi ya taasisi za serikali na kampuni nyingi.
Binafsi ni kwa wafanyakazi kukatwa asilimia 5 ya mshahara, lakini feha hizo na mchango wa asilimia 10 wa muajiri kutowasilishwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF) kama sheria inavyoeleza.
Suala hili nalo pia linafaa kushughulikiwa haraka sana kwa sababu kwa kiasi fulani linawakatisha tamaa wafanyakazi wa Zanzibar .
Kwa muda mrefu wafanyakazi wamekuwa wakipigiwa kelele za kuwataka wawajibike makazini kwao, lakini hakuna anayewasimamia waajiri wao kuona nao wanawajibika na kuheshimu sheria za kazi ikiwa pamoja na kuwasilisha ZSSF michango ya hifadhi ya jamii.
Tuachane na mtindo wa kuendesha shughuli za serikali kwa mabavu na kutumia maagizo, maelekezo na amri na badala yake viongozi wawe mfano mzuri wa kuheshimu katiba, sheria za nchi na taratibu za utawala katika serikali.
Source: Tanzania Daima

Friday 9 March 2012

Na Ahmed Rajab
MENGI yameandikwa na mengi yataendelea kuandikwa kumhusu Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa mwanzo na wa pekee wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambaye Aprili, mwaka 1964 alikubali kuiunganisha nchi yake na ile ya Tanganyika.
Hadi sasa walioandika kumhusu Karume ni waandishi wa habari, wanahistoria na wataalamu wa fani ya sayansi ya siasa. Waandishi wa riwaya hata wa riwaya sahili na wa tamthilia bado hawajajitokeza uwanjani kumuandika Karume.  Sitoshangaa pakitokea magwiji watanzu hizi mbili za fasihi watakaoamua kumtoa ukumbini Sheikh Karume kwa kumjadili na kumzungumza ama katika riwaya za kisiasa au katika michezo ya kuigiza.
Pengine tutaweza kupata taswira iliyokamilika ya Sheikh Karume endapo atachambuliwa katika fani zote hizo mbili au mojawapo ya fani hizo kwani hutokea simulizi za kubuni zikaukaribia sana ukweli kushinda simulizi za kitaalamu, ziwe za wanahistoria au za wataalamu wa sayansi ya siasa.
Kwa upande mwingine, hutokea pia simulizi za wanahistoria au za wataalamu wa sayansi ya siasa zikawa sawa na za kubuni kwa vile huandikwa ama kwa kutouzingatia au kwa kuupotosha ukweli.
Waandishi wa riwaya au wa tamthilia watakuwa na uwanja mkubwa wa kuandika mengi kuhusu nyanja mbalimbali za Ukarume na Karume — namna alivyoishi yeye mwenyewe binafsi, jinsi alivyoitawala nchi na maingiliano yake na Mwalimu Julius Nyerere.
Baadhi yatawachekesha watu waumwe na mbavu; mengine yatawahuzunisha na kuwafanya watokwe na machozi.  Bila ya shaka, watakaoandika riwaya au tamthilia kumhusu Karume watakuwa na fursa ya kuyaanika mema na mabaya yake.
Fursa nyingine watayokuwa nayo ni ya kunukuu matamshi yake. Kati ya misemo maarufu ya Karume inayokumbukwa sana na Wazanzibari siku hizi ni ule usemi wake wa kuulinganisha Muungano wa Tanzania na koti.  “Muungano ni kama koti tu, likikubana unalivua,” aliwahi kusema.
Tunavyofahamu ni kwamba kabla ya mauti kumkuta Sheikh Karume alikuwa na azma ambazo lau angelizitimiza basi hii leo Muungano huo ungekuwa na sura nyingine kabisa. Miongoni mwa mipango aliyokuwa nayo ni kuifanya Zanzibar iwe na Benki Kuu yake yenyewe badala ya kuitegemea Benki Kuu ya Tanzania. Tena akitaka Zanzibar iwe na sarafu yake yenyewe kama ilivyokuwa nayo kwa karne kadhaa kabla — tangu ilipokuwa na sarafu ya riyali, rupia na hatimaye ya shilingi.
Karume alikuwa akiamini kwamba kwa kuchukua hatua hizo atakuwa anayatetea na kuyalinda maslahi ya Zanzibar. Zaidi akiamini kwamba kutimizwa kwa malengo hayo kutairejeshea Zanzibar uungwana wake wa kitaifa.
Hii kanuni ya kutetea na kulinda maslahi ya Zanzibar ni muhimu sana wakati huu wa mchakato wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Kwa hakika, miongoni mwa mambo ambayo Wazanzibari wanapaswa kuyazingatia wakati wa mchakato huo ni hili suala la maslahi ya jumla ya nchi yao na ile kanuni ya kimsingi ya kwamba taifa lao ni muhimu zaidi kushinda chochote kingine. Hivyo maslahi ya nchi yao ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya vyama vyao vya kisiasa kiwe cha CCM, CUF, CHADEMA ama chochote kile kingine.
Wazanzibari hawatoweza kuyatetea na kuyalinda maslahi ya nchi yao endapo watagawanyika hasa kwa vile hawana kiongozi mshupavu mithili ya Sheikh Karume. Kwa sababu hiyo basi lazima wawe waangalifu wasibabaishwe na kugawanywa kama walivyokuwa wakigawanywa zamani. Wakijiachia wakagawanywa itakuwa rahisi kwa wasioitakia kheri nchi yao kuunda mifumo ya utawala itakayoyadhuru maslahi yao.
Hali hiyo ikizuka na wakijikuta wamegawika tena basi wao wenyewe ndio watakaolaumiwa na vizazi vijavyo vya Wazanzibari kwa ‘kuiuza’ nchi yao.  Njia moja ya kuiuza nchi yao ni kukubali mfumo wa Muungano utakaoyadhuru matarajio ya kuleta mageuzi na maendeleo nchini Zanzibar.
Bahati waliyonayo Wazanzibari kwa sasa ni kwamba wananchi kwa jumla na viongozi wao si tu kuwa wana umoja lakini wanatambua kwamba lazima wawe na sauti moja na fikra moja.
Wanatambua kwamba lazima wawe na msimamo mmoja hasa pale utakapowadia wakati wa kutakiwa watoe maoni yao katika shehia zao kuhusu Katiba waitakayo na watapotakiwa  waiidhinishe au waikatae katiba mpya wakati wa kupiga kura ya maoni.
Kura hiyo itakuwa na lengo la kuihalalisha katiba mpya pamoja na Muungano ambao haujapata kamwe kukubaliwa rasmi na wananchi au na taasisi yoyote ya Kizanzibari.
Umoja huo walionao sasa Wazanzibari unawapa fursa nzuri ya kuyatimiza malengo yao ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii. Aidha, kwa vile ajenda yao inaungwa mkono na kanuni za kisheria na za kimaadili hawastahiki kuwa na hofu katika kuitetea ajenda hiyo ambayo inataka pawepo na uhusiano mpya na Tanganyika juu ya msingi wa mkataba au mikataba na sio juu ya msingi wa Katiba kama ilivyo sasa.
Pamoja na hayo Serikali ya Zanzibar na wawakilishi Wakizanzibari katika Tume ya Kuipitia Katiba na wale wataoiwakilisha Zanzibar katika Baraza (au Bunge) la Katiba lazima wawe wanashauriana kwa karibu sana na wawe kitu kimoja wanapofanya kazi zao.
Lililo muhimu ni kwamba wasipoteze fursa yoyote ya kuyawakilisha matakwa ya nchi yao, nchi ambayo inahitaji mageuzi makubwa katika sera zake za ndani na za nje hasa katika uhusiano wake na jirani zake.
Hivi sasa kuna mjadala mkubwa unaoendelea Zanzibar kuhusu mustakbali wa Visiwa hivyo. Kwa vile Zanzibar ni nchi yenye demokrasia changa ni muhimu kwamba wananchi wasiwekewe mipaka kwa yale ambayo wanastahili kuyajadili hata ikiwa watataka Muungano uyayushwe na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar isimamishwe tena.
Kuna baadhi ya watu Tanzania Bara wasikiapo matamshi kama haya huruka na kuanza kuwashutumu wenye fikra hizo kuwa ni wasaliti au wachochezi.  Ukweli ni kwamba wasaliti na wachochezi ni wale wenye kwenda kinyume cha matakwa ya Wazanzibari walio wengi wenye kutaka pafanywe mageuzi makubwa kwa namna nchi yao inavyoongozwa. Wao ndio wenye kuhatarisha usalama wa sehemu zote mbili za Muungano kwa kuwalazimisha watu waache kufikiri na wafuate amri za wenye nguvu.
Hata hivyo, haishangazi kuwaona baadhi ya ndugu zetu wa Bara wakitoa shutuma kama hizo kwani wakati tulio nao ni wakati nyeti.  Kwa upande wao Wazanzibari nao  wanapaswa wawe makini na wasitoe matamshi ya uchokozi. Wanachopaswa kufanya ni kutoa mwito wa kutaka pawepo uhusiano patanifu utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili katika mfumo mpya wa Muungano.
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni Muungano pekee uliobuniwa na nchi mbili zilizo huru — hakuna Muungano aina hiyo popote pengine duniani.  Ulibuniwa kwa kuungana nchi mbili zilizo huru na zilizo na haki sawa na wajibu sawa mbele ya sheria ya kimataifa na pia mbele ya sheria zisizoandikwa.
Dosari iliyokuwepo ni kwamba kwa muda wa takriban miaka 50 Muungano huo umegeuka na kuwa Muungano usio na usawa na umeipelekea Zanzibar inyang’anywe uhuru wake na madaraka yake ya utawala bila ya ridhaa yake. Nguvu hizo za utawala zikahamishiwa Tanzania Bara, yaani kwa Serikali ya Muungano ambayo kwa hakika ni Serikali ya Tanganyika.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na michakato ya kutunga katiba au ya kuipitia upya katiba ya nchi. Na hapa ninawajibika kukumbusha namna CCM ilivyoandika na kuishurutisha Katiba ya mwaka 1977 ambayo ndiyo inayotumika sasa.
CCM iliyafanya hayo kwa njia isiyo ya halali. Ninasema hivi kwa sababu Hati za Muungano za Aprili 1964 kati ya Tanganyika na Zanzibar zilikuwa bayana kwamba Bunge la Katiba litaundwa kabla ya mwezi Aprili mwaka 1965 likiwa na idadi sawa ya wawakilishi kutoka Zanzibar na Tanganyika kuzingatia mfumo wa kudumu wa Muungano na Katiba yake.
Kama tujuavyo hayo hayajatendeka. CCM iliweza kuishurutisha Katiba iliyopo sasa bila ya upinzani wowote kwa sababu taifa lilikuwa na mfumo wa chama kimoja tu cha kisiasa na chama ndicho kilichokuwa taasisi adhimu nchini kushinda taasisi yoyote nyingine. Kwa hivyo, pale muswada muhimu wa Katiba mpya ulipofikishwa bungeni mwaka 1977 muswada huo ulipitishwa bila ya mjadala kwani siku hizo Bunge likichukuliwa kuwa ni kama kamati ya chama.
Jengine lililotokea ni kwamba wawakilishi Wakizanzibari katika Bunge walipewa maamrisho na viongozi wao akina Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa Zanzibar wa wakati huo, wasiupinge muswada huo. Hivyo kimya kimya wabunge wa Zanzibar waliziridhia hatua kama vile ile ya kuongeza Mambo ya Muungano kutoka 11 hadi idadi ya sasa ya mambo 22.
Hatua hiyo iliidhuru Zanzibar kwa vile iliiondoshea serikali yake uwezo wa kupanga na kujiendeshea mambo yake ya kiuchumi na ya kijamii bila ya kuingiliwa. Matokeo yake ni hali hii iliyopo sasa ya Zanzibar kuwa nchi lakini isiyo na uhuru wala nguvu zozote.
Wazanzibari wametanabahi na wanapiga kelele kuipinga hali ilivyo na hawana tena hofu katika jaribio lao la kuirejeshea serikali yao mamlaka yake kamili. Wanayataka yale aliyokuwa akiyapanga Sheikh Karume katika siku za mwisho za uhai wake, yaani nchi yao iwe na sarafu yake yenyewe, iwe na Benki Kuu yake yenyewe, kwa jumla iwe na uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe bila ya kuingiliwa. Kadhalika wanataka nchi yao iwe na uhusiano na Tanganyika katika mfumo unaoshabihi uhusiano wa nchi zilizo katika Jumuiya ya Ulaya
Chanzo: Raia Mwema.

Sunday 4 March 2012

Canadian firm set to explore oil in Zanzibar

The Canadian oil firm-Antrim Energy is to start exploration of oil in the small Island of Zanzibar paving the way for resumption of exploration activities on the Production Sharing Agreement (PSA) for the Pemba which has been stalled for some years now.
Under the signed agreement with Ras Al Khaimah Gas Tanzania Limited (RAK Gas) and NOR Energy AS (NOR), will see Antrim Energy replacing its previous right to be carried through the pre-drilling exploration phase of the PSA with a 20 per cent carried interest through the pre-drilling phase and an additional 10 per cent right to participate in the PSA.
The agreement will also see the carried interests of up to 30 per cent to be repaid from future production.
Stephen Greer, President and Chief Executive Officer (CEO) of Antrim Energy, said that concurrent with this agreement, RAK Gas and NOR have entered into an agreement that provides RAK Gas with the option to acquire control of the Pemba-Zanzibar PSA.
“Mr. Greer said that as part of this agreement, RAK Gas has undertaken to re-negotiate the P-Z PSA exploration work programme with Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) and to secure access rights to the licence area from the relevant authorities.
“We are very encouraged by the entry of RAK Gas into this licence. The Pemba-Zanzibar block has enormous exploration potential, and the area has recently been attracting considerable interest from major petroleum companies,” he said.
The licence which covers 3.5 million acres is in highly prospective oil and gas region that has recently seen significant exploration activity and to the moment, the Licenses on trend are held by Shell, Exxon Mobil, Statoil, Petrobras, Ophir Energy, British Gas and Tullow Oil.
Antrim Energy expect the two agreements, and the participation of RAK Gas in particular, will lead to a resumption of exploration activity on the Pemba-Zanzibar block in the near future.
Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) expects up to ten offshore wells will be drilled in offsetting licenses in 2010 – 2011, including a three well programme by Ophir – British Gas, two of which were drilled in 2010, two wells planned by Petrobras, one by Statoil, and one by Dominion.
Antrim Energy’s previous option was acquired in 2006 as part of a sale of several assets to NOR, including its wholly owned subsidiary Antrim Resources (Tanzania) Limited.
The Pemba – Zanzibar block has a proven hydrocarbon system, as evidenced by the Tundaua oil seep on Pemba Island and oil shows in previous exploration wells.
Multiple source rocks and petroleum reservoirs are anticipated and numerous prospects mapped. Approximately 75 per cent of the licence lies in water depths of less than 200 metres, with the islands of Pemba and Zanzibar providing potential for on-shore directional drilling.
RAK Gas LLC is the state natural gas utility of the Emirate of Ras al Khaimah in the UAE. It was established in 1984, and in 2007 converted to a limited liability corporation incorporated under the laws of Ras al Khaimah.
The Company’s core business is to source natural gas and markets. In addition, the Company has gas processing facilities and a modest portfolio of E&P assets in East Africa mainly. The Company holds one majority and seven minority interests in exploration blocks in East Africa and in Egypt.

Friday 2 March 2012

Mradi Mkubwa Bandari Lamu wazinduliwa

Ujenzi wa mradi mkubwa wa bandari na utakaogharimu $23bilioni (£14.5bn) kusini mashariki mwa pwani yaKenyakatika mji wa Lamu karibu na mpaka wa Somalia umezinduliwa.
Bomba la mafuta, reli na barabara pia zitajengwa kuunganisha Lamu na Sudan Kusini na Ethiopia.
Nchi iliyopata uhuru wake hivi karibuni ya Sudan Kusini ina mipango ya kutumia Lamu kama njia kuu ya kusafirishia mafuta yake.
Mwandishi wa BBC anasema wasiwasi kuhusu usalama wa mradi huo unaweza kuelezea umhimu wa kuwepo kwa vikosi vyaEthiopianaKenyanchiniSomaliavikilenga kulipatia utulivu eneohilo.

'Mradi mkubwa zaidi Afrika'

Rais wa Kenya Mwai Kibaki alizindua mradi huo sambamba na Rais wa Sudan Kusini na Waziri Mkuu waEthiopiaMeles Zenawi.
"Sina mashaka kuwa siku hii itakumbukwa katika historia wakati tunapojaribu kuwaunganisha watu wetu na kupata fursa za muhimu za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maishayaoyajayo" Shirika la habari la AFP limemnukuu Rais Kibaki akisema wakati wa sherehe za uzinduzi.
Ikifahamika kama kama Bandari ya Lamu ya usafiri ukanda wa Sudan KusiniEthiopia(Lapsset), inatarajiwa kumalizika kwa miaka minne ikiwa na gharama za awali kutoka serikali hizo tatu huku mipango ya kuwaalika wawekezaji wa kimataifa ikiwekwa.
Steven Ikuwa, anayesimamia mradi huo aliiambia BBC kuwa mipango hiyo ni mikubwa.
"Nina furaha kusema kuwa huu ni mradi mkubwa kabisa ambao tunauanza barani Afrika."
Mwandishi wa BBC Noel Mwakugu akiwa Lamu anasema kuna wasiwasi kuhusu mazingira ya eneo la mradi huo ambalo ni sehemu zuri zaidi kimazingira Afrika Mashariki sambamba na bahari ya Hindi na utajiri wa urithi wa kimazingira katika kisiwa cha Lamu.
"Lamu ni urithi ulio hai. Tayari Unesco imetangaza Lamu kuwa Urithi wa Dunia na kuwa eneo lililo katika hatari ya kupotea," Mualimu Badi kutoka kundi la Save Lamu aliiambia BBC.
"Iwapo watu 500,000 watakuja hapa kama wafanyakazi nadhani tutapoteza hadhi hiyo. "
Bw Badi pia alisema wenyeji wana wasiwasi wa kukosa makazi kutokana na kutokuwa na uthibitisho kuwa ni wakazi halali wa eneo hilo.
Akijibu malalamiko hayo Rais Kibaki ametangaza kuwa wakazi wa eneo hilo watapewa hati za kumiliki ardhi na utawala wake utatoa mafunzo kwa vijana 1,000 kuwaandaa kwa fursa zitakazotokana na bandari hiyo.
Chanzo: BBC

Nyakati za dhiki na dhima aliyonayo Shein

RAIS Ali Mohamed Shein ana dhamana kubwa kushinda kiongozi yeyote mwengine wa Zanzibar, tangu nchi hiyo iungane na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dhamana yake ni kubwa hivyo kwa sababu Wazanzibari wenzake wanasubiri kwa hamu matokeo ya mchakato wa kuipatia Jamhuri ya Muungano Katiba mpya.
Imepangwa kwamba kazi hiyo imalizwe Aprili, mwaka 2014 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano. Miaka 50 ni muda mwingi, uhai wa mtu wa kuzaa na kujukuu ingawa kwa kipimo cha kihistoria huo ni muda mfupi sana kama wa kufumba na kufumbua macho.
Shein ana bahati. Bahati yake ni kwamba hakabiliwi na upinzani licha ya shida za kiuchumi na za kijamii zilizozagaa huko Visiwani. Kama wapo wenye kumpikia majungu chini kwa chini basi hawathubutu kujitokeza. Hali iliyopo Visiwani haiwaruhusu. Shein anaiongoza nchi wakati ambapo Wazanzibari wameungana baada ya kuziyayusha chuki zao za kisiasa na kukubaliana, Novemba mwaka 2010 kuwa na suluhu ya kitaifa kwa Maridhiano ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Maridhiano hayo ndiyo yaliyosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuibuka kwa ile iitwayo Ajenda ya Zanzibar. Na ni umoja huo uliosababisha pasiwepo upinzani dhidi ya Shein, si wa dhahiri si wa shahiri.
Hiyo ni bahati kubwa kwa Shein na inampa fursa adhimu ya kuongoza taifa lilioungana. Lakini pia ni changamoto kwake yeye na serikali yake. Ni changamoto kwa sababu Wazanzibari kwa pamoja wanataraji mengi kutoka kwake. Awali ya yote wanamtaka awe na  msimamo ulio imara wa kumwezesha kuyatetea vilivyo maslahi ya Zanzibar.
Ni matumaini yao kwamba hatoteteleka wala kuyumba-yumba atapohitajika kuwasilisha na kuyasimamia maoni yao kuhusu mustakbali wa nchi yao na hususan suala la iwapo Muungano uendelee kama ulivyo au la. Kwa ufupi, tegemeo lao ni kwamba hatowaendea kinyume kwa kutoyapigania matilaba yao.
Wengi wa Wazanzibari wanataraji kwamba mfumo wa Muungano utaochomoza baada ya kumalizika hiyo shughuli ya kutunga Katiba utakuwa tofauti kabisa na ule wa sasa wa serikali mbili zisizo na mamlaka sawa wala haki zilizo sawa.
Siku hizi Wazanzibari wana kiu cha kutamani ya kale wanapoukumbuka ufanisi waliokuwa nao wakati wa kupigania uhuru kutoka kwa Waingereza. Juu ya migawanyiko ya kisiasa ya zama hizo hali zao za maisha kwa jumla zilikuwa za juu na uchumi wa nchi yao haukuathiriwa na mchafuko wa kisiasa.
Hizo zilikuwa nyakati za maisha ya raha na furaha kinyume na sasa ambapo pameingia maisha ya dhiki.
Sisemi kwamba ufanisi huo ulikuwa timilifu au kwamba haukuwa na kasoro, la. Nisemacho ni kwamba licha ya taksiri zake — na zilikuwa nyingi —dosari hizo hazikuufanya uchumi wa Zanzibar uzorote. Nchi ilikuwa na neema, watu wakipata ajira, sekta ya kilimo ilistawi na pakipatikana vyakula vya kila aina tena kwa bei rahisi.
Siku hizo angalau kila Mzanzibari akimudu kula vyakula mbalimbali si kama sasa ambapo waliobahatika siku nenda siku rudi wanakula ugali na maharagwe mara tatu kwa siku. Huo ndio mlo wa wengi wa Wazanzibari siku hizi na wapo baadhi yao wasiobahatika hata kuumudu mlo huo.
Ingawa utawala wa ukoloni Wakiingereza ulikuwa wa kimabavu, ulikuwa hivyo dhidi ya wale waliokuwa wakiupinga na waliokuwa wakidai uhuru.  Wananchi kwa jumla walikuwa na uhuru wao wa kiraia ingawa hawakuwa na uwakilishi wa kisiasa.  Zanzibar ikitawaliwa moja kwa moja na Uingereza.
Kinyume na wanavyofikiri wengi tangu mwaka 1890 masultani walikalia kiti cha enzi huko Zanzibar lakini hawakuwa na nguvu za kutawala na kuendesha nchi.  Mabwana waliokuwa na amri walikuwa wakoloni Wakiingereza na si masultani. Wao walikuwa wanyenyekevu kwa Waingereza.
Hii leo Wazanzibari wana mapato ya kujikimu tu, wengi wao hususan vijana hawana ajira. Kuna mfumuko mkubwa wa bei na mapato, bei za vyakula ni za kuruka, huduma za lazima ni duni kama vile za afya, maji, umeme na kumekosekana mfumo wa kuchimba mitaro ya kuchukua maji machafu.
Zama hizo zilizopita, mfumo wa elimu Visiwani ulikuwa wa kupigiwa mfano. Mwaka 1961 Zanzibar ilikuwa na wahitimu wengi wa chuo kikuu waliopata digrii au shahada kulinganishwa na wale wa Tanganyika.
Huo ndio ukweli uliokuwepo. Siku hizo Zanzibar ikitajwa kuwa na nafasi ya pili baada ya Afrika ya Kusini katika mizani ya maendeleo miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.  Si leo.
Mfumo wa leo wa elimu hauwezi kamwe kufananishwa na ule wa kale. Kwa sababu ya mfumo wa elimu uliopo sasa ni muhali kupata wataalamu wataoiwezesha serikali ya Zanzibar iendeshwe kistadi na ipasavyo bila ya ulaji rushwa au kupendeleana wakati wa kuajiri watu katika kazi za serikalini.
Badala yake tunaona kwamba watu wasio na elimu ya kutosha au ujuzi na uzoefu unaohitajika wanapewa madaraka makubwa serikalini ama kwa sababu za kisiasa au za kupendeleana. Hawa ndio wenye kuhodhi nyadhifa nyeti serikalini na kushika kwao nyadhifa hizo kunaleta madhara makubwa kwa jamii kwani wanakuwa wanazitumia vibaya rasilmali za nchi na wanapoteza fursa ya kuziinua hali za maisha Visiwani kwa kuwapatia watoto elimu bora na kuwapatia wananchi kwa jumla huduma zote za lazima.
Ingawa hii leo Zanzibar kuna umoja wa kitaifa pamoja na suluhu na hali tulivu ya kisiasa uchumi wake si wa kuridhisha. Isitoshe huduma zake za kijamii hazikidhi mahitaji ya kila Mzanzibari hasa wale walio maskini na wasiojiweza ambao ndio walio wengi Visiwani.
Tumekumbushana kidogo hali ya mambo ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi na Muungano na Tanganyika na tukagusia hali ilivyo sasa. Na hatuna budi kusema kwamba hali iliyopo sasa hairidhishi hata kidogo na ni lazima ibadilishwe ili Zanzibar iweze tena kuwa nchi ya neema.
Kwa bahati nzuri, mchakato utaopelekea kupatikana kwa katiba mpya unawapa Wazanzibari na viongozi wao fursa ya kuweza kujipatia ukombozi na maendeleo kwa kuachana na hali ya sasa ilivyo.
Kwanza ili Zanzibar iweze kuendelea na kujipatia mamlaka yake ndani ya  Muungano na Tanganyika utaokuwa wa Mkataba na si wa Katiba, kuna mambo mawili yanayohitaji kuzingatiwa na kutanzuliwa. La kwanza linahusika na hali ya ndani Visiwani kwenyewe na la pili linahusika na uhusiano wa baadaye kati ya Zanzibar na jirani wake wa kidugu Tanganyika.
Hali ya ndani inatokana na kuzuka kwa utawala wa kisiasa wa kinasaba (political dynasty). Hali hiyo nayo ni chanzo cha kuwako utawala mbovu. Wanaonufaika katika mazingira hayo ni hao watawala wa kinasaba na walio wao pamoja na wafanyabiashara wachache walio matajiri sana na wakubwa wengine. Wao ndio wenye kustarehe ilhali wengi wa wananchi wanahangaika kila uchao kutafuta chakula na uwezo wa kulipia huduma za afya au wa kuwasomesha watoto wao.
Mustakbali wa Zanzibar, ndani au nje ya Muungano na jirani yake Tanganyika, utaamuliwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Inavyoonyesha ni kuwa Wazanzibari hawatokubali zoezi la utungwaji wa Katiba mpya lifanyiwe uzembe na kuachiwa lipindukie mwaka 2014 kwa sababu wana hamu kubwa ya kuona kwamba serikali yao  inarejeshewa mamlaka yake yote ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii kutoka serikali ya Muungano.
Wao wanaamini kwamba kurejeshewa mamlaka na madaraka hayo kutawawezesha kuufyeka au angalau kuupunguza kwa kiwango kikubwa umaskini uliopo sasa na kujipatia maendeleo na ufanisi.
Rais Shein na viongozi wenzake kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa wanayaelewa hayo kwa sababu kila siku Wazanzibari wa itikadi tofauti za kisiasa, kuanzia wananchi wa kawaida hadi viongozi wao, wanashauriana na kujadiliana kuhusu mustakbali wa nchi yao.
Suala kuu linalowashughulisha nilile la kuamua ni Zanzibar aina gani waitakayo. Ni muhimu kwamba Shein ahakikishe ya kuwa Wazanzibari wanaitumia kikamilifu haki yao ya kidemokrasi ya kushauriana na kulijadili vilivyo suala la Katiba bila ya kuwekewa mipaka na hususan haja ya kuujadili Muungano kwa ukamilifu bila ya woga.
Hilo ndilo jukumu kubwa alilonalo Shein na wenzake. Wazanzibari wenzao wameshikamana na hadi sasa wako nyuma yao lakini wanachotaka hasa ni kuwaona viongozi wao wakisema kwa kauli moja na kuitetea Ajenda ya Zanzibar. Wanasema kuwa Shein na wenzake ndio ambao ama watainusuru au wataitosa nchi yao. Hilo si jukumu dogo