Na Ahmed Rajab
MENGI yameandikwa na mengi yataendelea kuandikwa kumhusu Sheikh
Abeid Amani Karume, Rais wa mwanzo na wa pekee wa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar ambaye Aprili, mwaka 1964 alikubali kuiunganisha nchi yake na
ile ya Tanganyika.
Hadi sasa walioandika kumhusu Karume ni waandishi wa habari,
wanahistoria na wataalamu wa fani ya sayansi ya siasa. Waandishi wa
riwaya hata wa riwaya sahili na wa tamthilia bado hawajajitokeza
uwanjani kumuandika Karume. Sitoshangaa pakitokea magwiji watanzu
hizi mbili za fasihi watakaoamua kumtoa ukumbini Sheikh Karume kwa
kumjadili na kumzungumza ama katika riwaya za kisiasa au katika michezo
ya kuigiza.
Pengine tutaweza kupata taswira iliyokamilika ya Sheikh Karume endapo
atachambuliwa katika fani zote hizo mbili au mojawapo ya fani hizo
kwani hutokea simulizi za kubuni zikaukaribia sana ukweli kushinda
simulizi za kitaalamu, ziwe za wanahistoria au za wataalamu wa sayansi
ya siasa.
Kwa upande mwingine, hutokea pia simulizi za wanahistoria au za
wataalamu wa sayansi ya siasa zikawa sawa na za kubuni kwa vile
huandikwa ama kwa kutouzingatia au kwa kuupotosha ukweli.
Waandishi wa riwaya au wa tamthilia watakuwa na uwanja mkubwa wa
kuandika mengi kuhusu nyanja mbalimbali za Ukarume na Karume — namna
alivyoishi yeye mwenyewe binafsi, jinsi alivyoitawala nchi na
maingiliano yake na Mwalimu Julius Nyerere.
Baadhi yatawachekesha watu waumwe na mbavu; mengine yatawahuzunisha
na kuwafanya watokwe na machozi. Bila ya shaka, watakaoandika riwaya au
tamthilia kumhusu Karume watakuwa na fursa ya kuyaanika mema na mabaya
yake.
Fursa nyingine watayokuwa nayo ni ya kunukuu matamshi yake. Kati ya
misemo maarufu ya Karume inayokumbukwa sana na Wazanzibari siku hizi ni
ule usemi wake wa kuulinganisha Muungano wa Tanzania na koti.
“Muungano ni kama koti tu, likikubana unalivua,” aliwahi kusema.
Tunavyofahamu ni kwamba kabla ya mauti kumkuta Sheikh Karume alikuwa
na azma ambazo lau angelizitimiza basi hii leo Muungano huo ungekuwa na
sura nyingine kabisa. Miongoni mwa mipango aliyokuwa nayo ni kuifanya
Zanzibar iwe na Benki Kuu yake yenyewe badala ya kuitegemea Benki Kuu
ya Tanzania. Tena akitaka Zanzibar iwe na sarafu yake yenyewe kama
ilivyokuwa nayo kwa karne kadhaa kabla — tangu ilipokuwa na sarafu ya
riyali, rupia na hatimaye ya shilingi.
Karume alikuwa akiamini kwamba kwa kuchukua hatua hizo atakuwa
anayatetea na kuyalinda maslahi ya Zanzibar. Zaidi akiamini kwamba
kutimizwa kwa malengo hayo kutairejeshea Zanzibar uungwana wake wa
kitaifa.
Hii kanuni ya kutetea na kulinda maslahi ya Zanzibar ni muhimu sana
wakati huu wa mchakato wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ya Tanzania. Kwa hakika, miongoni mwa mambo ambayo Wazanzibari
wanapaswa kuyazingatia wakati wa mchakato huo ni hili suala la maslahi
ya jumla ya nchi yao na ile kanuni ya kimsingi ya kwamba taifa lao ni
muhimu zaidi kushinda chochote kingine. Hivyo maslahi ya nchi yao ni
muhimu zaidi kuliko maslahi ya vyama vyao vya kisiasa kiwe cha CCM,
CUF, CHADEMA ama chochote kile kingine.
Wazanzibari hawatoweza kuyatetea na kuyalinda maslahi ya nchi yao
endapo watagawanyika hasa kwa vile hawana kiongozi mshupavu mithili ya
Sheikh Karume. Kwa sababu hiyo basi lazima wawe waangalifu
wasibabaishwe na kugawanywa kama walivyokuwa wakigawanywa zamani.
Wakijiachia wakagawanywa itakuwa rahisi kwa wasioitakia kheri nchi yao
kuunda mifumo ya utawala itakayoyadhuru maslahi yao.
Hali hiyo ikizuka na wakijikuta wamegawika tena basi wao wenyewe ndio
watakaolaumiwa na vizazi vijavyo vya Wazanzibari kwa ‘kuiuza’ nchi
yao. Njia moja ya kuiuza nchi yao ni kukubali mfumo wa Muungano
utakaoyadhuru matarajio ya kuleta mageuzi na maendeleo nchini Zanzibar.
Bahati waliyonayo Wazanzibari kwa sasa ni kwamba wananchi kwa jumla
na viongozi wao si tu kuwa wana umoja lakini wanatambua kwamba lazima
wawe na sauti moja na fikra moja.
Wanatambua kwamba lazima wawe na msimamo mmoja hasa pale utakapowadia
wakati wa kutakiwa watoe maoni yao katika shehia zao kuhusu Katiba
waitakayo na watapotakiwa waiidhinishe au waikatae katiba mpya wakati
wa kupiga kura ya maoni.
Kura hiyo itakuwa na lengo la kuihalalisha katiba mpya pamoja na
Muungano ambao haujapata kamwe kukubaliwa rasmi na wananchi au na
taasisi yoyote ya Kizanzibari.
Umoja huo walionao sasa Wazanzibari unawapa fursa nzuri ya kuyatimiza
malengo yao ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii. Aidha, kwa vile ajenda
yao inaungwa mkono na kanuni za kisheria na za kimaadili hawastahiki
kuwa na hofu katika kuitetea ajenda hiyo ambayo inataka pawepo na
uhusiano mpya na Tanganyika juu ya msingi wa mkataba au mikataba na sio
juu ya msingi wa Katiba kama ilivyo sasa.
Pamoja na hayo Serikali ya Zanzibar na wawakilishi Wakizanzibari
katika Tume ya Kuipitia Katiba na wale wataoiwakilisha Zanzibar katika
Baraza (au Bunge) la Katiba lazima wawe wanashauriana kwa karibu sana
na wawe kitu kimoja wanapofanya kazi zao.
Lililo muhimu ni kwamba wasipoteze fursa yoyote ya kuyawakilisha
matakwa ya nchi yao, nchi ambayo inahitaji mageuzi makubwa katika sera
zake za ndani na za nje hasa katika uhusiano wake na jirani zake.
Hivi sasa kuna mjadala mkubwa unaoendelea Zanzibar kuhusu mustakbali
wa Visiwa hivyo. Kwa vile Zanzibar ni nchi yenye demokrasia changa ni
muhimu kwamba wananchi wasiwekewe mipaka kwa yale ambayo wanastahili
kuyajadili hata ikiwa watataka Muungano uyayushwe na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar isimamishwe tena.
Kuna baadhi ya watu Tanzania Bara wasikiapo matamshi kama haya huruka
na kuanza kuwashutumu wenye fikra hizo kuwa ni wasaliti au
wachochezi. Ukweli ni kwamba wasaliti na wachochezi ni wale wenye
kwenda kinyume cha matakwa ya Wazanzibari walio wengi wenye kutaka
pafanywe mageuzi makubwa kwa namna nchi yao inavyoongozwa. Wao ndio
wenye kuhatarisha usalama wa sehemu zote mbili za Muungano kwa
kuwalazimisha watu waache kufikiri na wafuate amri za wenye nguvu.
Hata hivyo, haishangazi kuwaona baadhi ya ndugu zetu wa Bara wakitoa
shutuma kama hizo kwani wakati tulio nao ni wakati nyeti. Kwa upande
wao Wazanzibari nao wanapaswa wawe makini na wasitoe matamshi ya
uchokozi. Wanachopaswa kufanya ni kutoa mwito wa kutaka pawepo uhusiano
patanifu utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili katika mfumo mpya
wa Muungano.
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni Muungano pekee uliobuniwa na nchi
mbili zilizo huru — hakuna Muungano aina hiyo popote pengine duniani.
Ulibuniwa kwa kuungana nchi mbili zilizo huru na zilizo na haki sawa na
wajibu sawa mbele ya sheria ya kimataifa na pia mbele ya sheria
zisizoandikwa.
Dosari iliyokuwepo ni kwamba kwa muda wa takriban miaka 50 Muungano
huo umegeuka na kuwa Muungano usio na usawa na umeipelekea Zanzibar
inyang’anywe uhuru wake na madaraka yake ya utawala bila ya ridhaa
yake. Nguvu hizo za utawala zikahamishiwa Tanzania Bara, yaani kwa
Serikali ya Muungano ambayo kwa hakika ni Serikali ya Tanganyika.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na michakato ya kutunga
katiba au ya kuipitia upya katiba ya nchi. Na hapa ninawajibika
kukumbusha namna CCM ilivyoandika na kuishurutisha Katiba ya mwaka 1977
ambayo ndiyo inayotumika sasa.
CCM iliyafanya hayo kwa njia isiyo ya halali. Ninasema hivi kwa
sababu Hati za Muungano za Aprili 1964 kati ya Tanganyika na Zanzibar
zilikuwa bayana kwamba Bunge la Katiba litaundwa kabla ya mwezi Aprili
mwaka 1965 likiwa na idadi sawa ya wawakilishi kutoka Zanzibar na
Tanganyika kuzingatia mfumo wa kudumu wa Muungano na Katiba yake.
Kama tujuavyo hayo hayajatendeka. CCM iliweza kuishurutisha Katiba
iliyopo sasa bila ya upinzani wowote kwa sababu taifa lilikuwa na mfumo
wa chama kimoja tu cha kisiasa na chama ndicho kilichokuwa taasisi
adhimu nchini kushinda taasisi yoyote nyingine. Kwa hivyo, pale muswada
muhimu wa Katiba mpya ulipofikishwa bungeni mwaka 1977 muswada huo
ulipitishwa bila ya mjadala kwani siku hizo Bunge likichukuliwa kuwa ni
kama kamati ya chama.
Jengine lililotokea ni kwamba wawakilishi Wakizanzibari katika Bunge
walipewa maamrisho na viongozi wao akina Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa
Zanzibar wa wakati huo, wasiupinge muswada huo. Hivyo kimya kimya
wabunge wa Zanzibar waliziridhia hatua kama vile ile ya kuongeza Mambo
ya Muungano kutoka 11 hadi idadi ya sasa ya mambo 22.
Hatua hiyo iliidhuru Zanzibar kwa vile iliiondoshea serikali yake
uwezo wa kupanga na kujiendeshea mambo yake ya kiuchumi na ya kijamii
bila ya kuingiliwa. Matokeo yake ni hali hii iliyopo sasa ya Zanzibar
kuwa nchi lakini isiyo na uhuru wala nguvu zozote.
Wazanzibari wametanabahi na wanapiga kelele kuipinga hali ilivyo na
hawana tena hofu katika jaribio lao la kuirejeshea serikali yao mamlaka
yake kamili. Wanayataka yale aliyokuwa akiyapanga Sheikh Karume katika
siku za mwisho za uhai wake, yaani nchi yao iwe na sarafu yake
yenyewe, iwe na Benki Kuu yake yenyewe, kwa jumla iwe na uhuru wa
kujiamulia mambo yake yenyewe bila ya kuingiliwa. Kadhalika wanataka
nchi yao iwe na uhusiano na Tanganyika katika mfumo unaoshabihi
uhusiano wa nchi zilizo katika Jumuiya ya Ulaya
Chanzo: Raia Mwema.
No comments:
Post a Comment