Na Suleiman Al Kindy
Utangulizi
Imetulazimu kutoa
mawazo haya kwa kuzingatia ibara ya 18(1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984 tolea la 2010, inayosema kama ifuatavyo-:
“Bila
ya kuathiri sheria ya nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na
kutoa nje mawazo yake, na kutafuta kupokea na kutoa habari na dhana
kupitia chombo chochote,bila ya kujali mipaka ya nchi,na pia ana uhuru
wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”
Katika miaka yote
48 ya umri wa muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru, (Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar na Tanganyika), hakuna shaka ya kwamba Zanzibar imekuwa
ikiendelea kulalamika na kuonesha kwa vitendo juu ya kutoridhishwa kwake
na muundo na mfumo wa muungano huo, pamoja na usimamiaji wake na
utekelezaji wake.
Kwa msingi huo,hayo
ndio yaliyozaa Muungano ambao ni kero kwa Wazanzibari walio wengi., ni
wazi kwamba kuna kila dalili, kasoro na matendo yaliyowazi mengi
yaliyojaa shaka inayotulazimu tuamini kuwa kuna dhamira ya makusudi ya
kuifikisha Zanzibar pale pasipo takiwa na Wazanzibari walio wengi.
Miongoni mwa
mambo yaliyo na athari mbaya na machungu sana na matendo yaliyowazi na
yaliyojaa shaka kwa nchi ya Zanzibar na Wazanzibari wenyewe, ni pale
siku chache tuu baada ya Muungano huo tumeiona Tanganyika ikihaulisha
Mamlaka yake kwa serikali ya Jumhuri ya Muungano,na Zanzibar nayo
ikisalimisha mamlaka yake kwa Jamuhuri ya Muungano hiyo hiyo ya Tanzania
katika namna ambayo Wazanzibari tunaamini kuwa ni mbinu na hila za
kuipokonya Zanzibar mamlaka yake (Soverenity), na hapo ndio ukawa mwanza
wa safari ya kuvunjwa nguvu za kimamlaka kwa nchi ya Zanzibar.
Kitendo hicho cha
Tanganyika kuhaulisha mamlaka yake kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kimezaa faida mbili kubwa kwa Tanganyika na kusababisha hasara nyingi kwa Zanzibar.
Faida ambazo
Tanganyika imezipata ni kama zifuatazo ,Kwanza kuivunja nguvu Zanzibar
za Mamlaka, Pili kujikweza na kujipatia maguvu ya kimamlaka ndani ya
Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(a) Maamlaka ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kwa mfano katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Ibara ya 33(2) inasema kama ifuatavyo-:
“Raisi atakuwa mkuu wa nchi , kiongozi wa Serikali na amiri jeshi Mkuu’
Ibara ya 34 (1) pia inasema kama ifuatavyo-:
“Kutakuwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na Mamlaka juu ya
mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano,na pia juu ya mambo
mengine yote yahusuyo Tanzania Bara (Tanganyika)”
Ibara ya 34 (2) inasema kama ifuatavyo-:
“Mamlaka
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yatahusu utekelezaji na hifadhi ya
katiba hii na pia mambo mengineyo yote ambayo Bunge lina mamlaka ya
kuyatungia Sheria”
Pia ibara ya 34(3) inasema kama ifuatavyo-:
“Mamlaka
yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano
katika Jamhuri ya Muungano,na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo
Tanzania Bara,yatakuwa mikononi mwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano”
Ndugu msomaji,
ukiitizama ibara ya 33(2) utagundua kuwa maaana yake ni kwamba huyo
Rais ndiye mwenye maamlaka mengineyo yote ya Tanzania Bara (Tanganyika),
pia soma kwa makini ibara ya 34(1) (2) na (3), hapo ndipo utagundua
kuwa Tanzania Bara (Tanganyika) ipo na ina maguvu kamili ya ndani
ikiwemo kuiamulia Zanzibar juu ya mambo yake ya ndani, na nje ya nchi,
kwa kumpata Rais aliye amiri jeshi Mkuu na ambaye atasimamia mambo yote
ya Tanzania Bara (Tanganyika) kwa maana hiyo kwa nini tusiamini kuwa
Tanzania Bara (Tanganyika ) ndio Jamhuri ya Muungano yenyewe?,
tumekokotwa kwa mtindo huu kwa muda wa miaka isiyopungua 48.
Kwa upande wa
Zanzibar kumezaliwa hasara nyingi kubwa zikiwemo Kupoteza mamlaka yake
ya kutambulika duniani kama ni nchi, ambayo mamlaka hayo yamo mikononi
mwa Tanzania Bara (Tanganyika), na kutokuwa na mamlaka ya kuhudhuria
vikao vya Kimataifa mfano UN,AU,CW, East Africa Community nk.
Hasara nyengine
ambayo Zanzibar inaipata ni kupoteza uwezo wake wa kufunga mikataba ya
Kimataifa, pia kutokuwa na mamlaka ya kujiamulia ni nchi gani au Taasisi
gani ingependa kuwa na mahusiano nayo au kutokuwa na mahusiano nayo
ambapo mambo hayo ndio msingi mkuu na chachu ya mafanikio katika nchi
yoyote duniani na ndiyo yanayopelekea kuifanya nchi kutambulika kuwa ni
nchi kamili , kinyume chake ni kuwa na nchi dhaifu isiyotambua ulimwengu
ukoje na unakwendaje.
Hapo ndipo utapoona
kwa ubainifu wa mambo yalivyo kama tulivyonukuu maandiko ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano, ibara tulizotangulia kizielekeza zinaonyesha wazi
na kubainisha upamoja wa mamlaka hizo juu ya mambo yote ya Muungano
katika Jamhuri ya Muungano na pia mambo yote yanayohusu Tanzania Bara(
Tanganyika).
Ndugu msomaji,
hivyo utaona kuwa upamoja wa mamlaka hizo ambazo ziko mikononi mwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano ni kwa kiwango gani Tanganyika inafaidika
kupitia upamoja huo.
Kwa
maaana hiyo Katiba hiyo moja ni ya Muungano na ndio yenye mamlaka ya
Tanzania Bara (Tanganyika) ambayo Tanzania Bara (Tanganyika) ndio yenye
mamlaka na Katiba hiyo.
(b) Mamlaka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika ibara ya 64(1) inasema kuwa:-
“Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara (Tanganyika) yatakuwa mikononi mwa Bunge”
Ndugu msomaji
tunatakiwa tufahamu ya kuwa mamlaka hizo mbili (Bunge na Rais) ndizo
zinazosimamia na kutekeleza kuitendaji kwa wizara zote za Tanzania Bara (
Tanganyika).
Vile vile ikumbukwe
kuwa mamlaka hizo ndizo zinazotambulika kuwa ni kiwakilishi cha nchi
duniani, Rais ndio mamlaka pekee inayowakilisha vikao vyote vya juu vya
kimataifa (rejea ukurasa no 3 hapo juu).
Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa-:
Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza-:
(e) “Kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa”
Mamlaka haya ya Bunge ni sawa na mamlaka aliyonayo Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (rejea ukurasa no 2-4 hapo juu).
Hizo ndizo mamlaka zinazosimamia na kutekeleza kiutendaji mambo mengineyo ya Tanzania Bara (Tanganyika).
Kwa uchanganuzi huu
ni kwa nini tusiamini kuwa Tanzania Bara (Tanganyika) ni nchi ndani ya
Tanzania na pia ni nchi nje ya Tanzania kwa sababu ina sifa za kisheria
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa fursa ya
kuzipa mamlaka hizo mbili kuu (Bunge na Raisi) kusimamia mambo yake.
Kwa kigezo cha kukosa sifa hizo ndio kuliifikisha Zanzibar kubainishiwa hadharani kwamba “Zanzibar si nchi”, hili ndio tamko la mwanzo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, hivyo ukijiuliza ndugu msomaji
unapoambiwa Zanzibar si nchi maaana yake ni nini kinyume chake? je
inamaanisha ni Mkoa? au Jimbo? jawabu zuri unalo wewe ndugu msomaji.
Kisha ikafuatia kauli ya pili kuwa “Zanzibar ni nchi ndani ya Tanzania lakini si nchi nje ya Tanzania”, hivyo
duniani kuna utaratibu wa kuwa na nchi ndani ya nchi? au Wazanzibari
tumependelewa? Je tutamini vipi kuwa kauli hizo mbili kuwa hazina lengo
na dhamira ya majibu ya masuala tuliyoyauliza hapo juu?
Viongozi hao
wamejiamini na kukinai kwa uhakika juu ya matamshi yao hayo kwa kutokuwa
na shaka wala wasiwasi na kauli hizo, kwa sababu Zanzibar zamani kabla
ya leo ilishapotezewa vigezo na sifa hizo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, huku tukiiona Tanzania Bara (Tanganyika) ikikweya
juu ya mabega ya Jamhuri ya Muungano kikatiba kutekeleza malengo yake
yote ya kitaifa na kimataifa.
Ndugu msomaji
mimi na wewe tutakubaliana ya kwamba Serikali ya Muungano haina
utaratibu unaokubalika Kisheria wa kuwakutanisha katika vikao vya pamoja
vya walioungana (Tanganyika na Zanzibar) vitakavyojiamulia kila upande
kipi kiongezwe na kipi kipunguzwe kwa makubaliano ya nchi huru
zilizoungana, hilo halijawahi kutokea katika historia ya Muungano huu
kwa sababu halina miguu ya kusimama kisheria.
Sasa hapo ndipo yanapozuka masuala yafuatayo katika vichwa vya Wazanzibari;
-
Je ni kwa vielelezo gani ambavyo vinaweza kutufanya sisi Wazanzibar kwamba tuamini kuwa kero za Muungano pamoja na utata uliojaa wingi wa matukio kwamba hivyo au hayo hayakupangwa kwa makusudi?
-
Je ni hoja gani tunaweza kuelimishwa kwamba kero zote za Muungano ambazo ni mzigo mzito kwa Zanzibar zimetokea kwa bahati mbaya?
-
Je tunatakiwa tuamini kuwa haya na mengineyo yote yanayolalamikiwa na Wazanzibar ni dhana potofu au ni hakika?
-
Je kama ni bahati mbaya au ni kasoro za Kisheria au kuna dhamira njema juu ya hayo ni sababu gani iliyosababisha kukosa ufumbuzi na utatuzi au kudhihirika kwa nia njema kwa muda wa nusu karne sasa ?
-
Kwa nini walamikaji wa kimaslahi wa Muungano huu iwe ni upande mmoja nayo ni Zanzibar tu?
Wazee wetu wa hikima wanasema “Mwanadamu
humgeuza paka akawa chui pindipo tu atapoamua kumfanyia madhara paka
huyo ndani ya eneo la chumba kilichofungwa milango”,
Pia Wataalamu
wa Saikologia wanasema kuwa kadiri mwanadamu utakavyo mkosesha haki
zake huku akiwa ametambua kuwa unamkosesha haki yake hiyo
inayomuwajibikia elewa kwamba atabuni mbinu za kutegua kwa kila
kilichotegwa hata kama uteguwaji wake utamletea madhara.
Huu ni wakati wa
kuirejeshea Zanzibar Mamlaka yake ili viongozi waliotuelimisha kuwa
Zanzibar si nchi wawe na kauli na tamko moja tu lisilo kuwa na upungufu
wala ufafanuzi utakaogeuza maana , ya kwamba “Zanzibar ni nchi nje ya Tanzania”’
Hilo linawezekana tukiamuwa kwa Umoja wetu Wazanzibar.
Kwa kulitambua suala
muhimu la umoja Katiba ya Zanzibar inathamini suala hilo la umoja na
kutuongoza kama inavyojieleza katika ibara ya 23(3)-
“Watu
wote watatakiwa na Sheria kulinda vizuri mali ya Zanzibar na kwa pamoja
kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchum wa
Zanzibar kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadae ya
Taifa lao”
Pia ibara 23(4) inasema kuwa:-
“Kila Mzanzibar ana wajibu wa kulinda,kuihifadhikudumisha uhuru,mamlaka,ardhi na Umoja wa Zanzibar”.
Pia ibara 9(a) inasema kuwa:-
“Mamlaka
ya kuendesha nchi ni ya Wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa
Serikali kufuatana na katiba hii utatoka kwa wananchi wenyewe”
Kwa mantiki pamoja na maoni hayo tunapenda kuwahimiza Wazanzibar kuwa kuigomboa Zanzibar kutoka katika mfumo ulio na Kero
ni jambo linalowezekana ikiwa patapatikana umoja miongoni mwetu pamoja
na kuamini kuwa kulizungumzia suala la Muungano wa Zanzibar na
Tanganyika na kutoa mawazo juu ya kutatua matatizo ya Muungano kwa nguvu
za Hoja ni wajibu wa kila Mzanzibar na kufanya hivyo ni kukuza
Demokrasia
No comments:
Post a Comment