Friday 30 March 2012

Buriani Wolfango Dourado: Shujaa na mzalendo halisi

Ahmed Rajab
KUNA siku nikiwa London, Uingereza nilighadhibika nikawaambia niliokuwa nao: “Nikimuona Dourado nitamzaba kibao.”
Mapema siku hiyo Mahakama Kuu ya Zanzibar iliusikiliza ushahidi wa Amar Salim (Kuku), mmoja wa washtakiwa kwenye kesi ya uhaini iliyohusika na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Sheikh Abeid Amani Karume.
Takriban washitakiwa wote walikuwa ‘Makomredi’ kama wanavyojulikana wanachama au wafuasi wa chama cha zamani cha Umma Party.  Amar Salim, aliyekuwa ameteswa kama washitakiwa wengine, alikuwa mmoja wa vigogo wa chama hicho.
Shitaka lilikuwa kwamba washitakiwa walikula njama ya kuipindua serikali iliyopelekea kuuawa kwa Karume. Alipokuwa akitoa ushahidi wake Amar Salim alikiri kwamba mpango huo ulikuwako. Alipoambiwa na Dourado awataje waliohusika alianza kwa kuwataja makomredi raia wa kawaida na waliokuwa wanajeshi huko Visiwani na waliokuwako Bara. Kisha akanyamaza kuashiria kuwa amemaliza.
Dourado hakutosheka. Akamwambia: “Na kuna walio nje sio?”
Ndipo Amar Salim alipoanza kubwabwajika akitaja kila jina lililomjia kichwani akianza na langu nikifuatiwa na Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York, Mohamed Ali Foum, aliyekuwa ubalozi wa Tanzania, Ethiopia, Dakta Said Himidi aliyekuwa akifanya kazi katika hospitali moja nchini Denmark na mwandishi wa habari, Said Salim (Kiazi) aliyekuwa Beijing, China.
Baadhi ya maswali ya Dourado mahakamani yalikuwa ya dharau na ya kuwakashifu watuhumiwa waliokuwa kizimbani. Hata hivyo, aliwapata waliokuwa kiasi chake au waliomzidi kwa maarifa kama Maalim Nurbhai Issa ambaye kwa majibu yake aliithibitisha ile sifa ya Makomredi ya kutokubali kutishwa na kutoogopa kifo.
Miaka michache baadaye nikiwa nimeketi ndani ya treni chini ya ardhi ya Jiji la London, nilisadifu kumuona mtu mfupi aliyeshika kiko mkononi amenikalia mkabala nami.
Huku treni ikitikisika na kufanya kelele nilimsogelea na kusema: “Bwana Dourado?”
Nilimtambua kwa haraka kwa sababu utotoni mwangu nikimuona sana mtaani Vuga alipozaliwa na nilipozaliwa na kukulia. Nilipomuona nilikuwa na hakika kwamba hakuwa akinijua kwa sura. Hivyo, nikajijulisha.
“Aah, nilikuwa nikikufikiria kuwa wewe ni baba kubwa,” aliniambia huku akitabasamu. Siku hizo nilikuwa kijana mbichi na umbo langu lilikuwa jembamba, ingawa wembamba wangu haukuwa wa njaa.
Treni iliposimama kwenye kituo kimoja mtu aliyekuwa amekaa ubavuni mwake aliinukana kuondoka.  Haraka haraka nikenda kukaa mimi.
Nilishangaa na pengine nilivunjika moyo kidogo kuona kuwa zile ghadhabu zangu juu ya Dourado zilikuwa zimeyayushwa na wakati. Lakini moyoni mwangu nilifurahi kumwona kidogo akitaharak nilipokwenda kukaa ubavuni mwake. Nilimuuliza kwa upole nini kilichompa kunitaja kwenye kesi ya uhaini.
Alinifumba mdomo aliponijibu: “Siye miye niliyekutaja. Ilikuwa Komred mwenzako.” Tukaanza kuzungumza na kuanzisha usuhuba uliodumu hadi alipofariki saa nane za alasiri ya Jumatatu ya wiki iliyopita (tarehe 19 Machi) huko mtaani kwetu Vuga.
Alianzisha mazoea ya kila anapokuja London kunipigia simu ama mimi au mwenzangu Salim Rashid aliyewahi kufanya kazi naye wakati Salim alipokuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi.  Mara nyingi tukikutana kwa dada yake Yolanda huko Ealing, Magharibi mwa London, tukibugia sambusa na chai na tukimsikiliza akitueleza yaliyokuwa yakijiri nchini kwetu.
Akipenda soga lakini soga la maana na alikuwa mtu wa mizaha lakini dhihaka zake zilikuwa za kijiutu uzima. Na ukitaka kumchokoza ilikuwa rahisi. Ukimtajia jina la Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa kama umewasha kibiriti kwenye petroli.
Ingawa wote wawili walikuwa waumini wa dhati Wakikatoliki walikuwa wakichukiana.
Akiwa mpinzani asiyeweza kudhibitika, Dourado akipenda kumshambulia Nyerere.
Alikuwa akisema kwamba akikirihishwa na pengo aliloliona kati ya fikra za kimaadili za Nyerere na vitendo vyake. Ukiyataja hayo ilikuwa kama unamtia ufunguo. Alikuwa hawezi kujizuia, kama alikuwa amekaa basi husimama na kuanza kuzunguka huku na huku akimshambulia Nyerere.
Jingine lililokuwa likimuudhi Dourdo ilikuwa kumwita ‘Wolfgang’ ilhali jina lake halisi ni Wolfango.
Wolfango J Dourado alizaliwa miaka 84 iliyopita. Utotoni mwake alisomeshwa na Wakatoliki katika shule ya Saint Joseph Convent (siku hizi inaitwa Mtakuja) iliyo karibu na kwao. Alivutiwa sana na waalimu wake Wakikatoliki, hasa Rev. Sr. Josefrieda (aliyewahi baadaye kufundisha katika shule ya Riruta Convent jijini Nairobi) na Sr. M Sveglinda ambaye baadaye pia aliishia Kenya kwenye Kituo cha Bikira Maria huko Mbitiri.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi na ya sekondari huko Zanzibar, Dourado alifanya kazi ya ukarani kwa muda mfupi katika serikali ya ukoloni.  Alipata msaada wa kwenda Uingereza kwa masomo ya juu lakini alikataa kwenda kwa sababu baba yake alikuwa amefariki na alilazimika kufanya kazi kumuangalia mamake na nduguze.
Alipopata msaada mwingine wa masomo alikwenda London alikosomea sheria katika Middle Temple, moja ya jumuiya nne za mawakili Uingereza zenye haki pekee ya kuwafanya wanachama wake wawe mawakili. Dourado alifanywa wakili mwaka 1957.
Alipomaliza masomo na kurudi kwao Dourado aliteuliwa kuwa Msaidizi wa Msimamizi Mkuu wa shughuli za serikali wadhifa alioushika hadi mwaka 1960 alipoteuliwa kuwa Wakili Mwandamizi wa Serikali.  Mwaka 1963 aliteuliwa kuwa katibu mkuu katika wizara ya mambo ya nchi za nje; waziri wake kwa muda alikuwa Sheikh Ali Muhsin Barwani.
Aliushika wadhifa huo hata baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ambapo kwa muda pia waziri wake alikuwa Abdulrahman Babu. Baada ya hapo aliteuliwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali.  Aliendelea kuushika wadhifa huo mpaka mwaka 1977 alipofanywa Meneja Mkuu wa Shirika la Bima la Zanzibar. Mwaka 1983 alipewa uwenyekiti wa Tume ya Kuzipitia Sheria za Zanzibar.
Pengine utajiuliza: mtu huyu ana msimamo wowote? Daima amekuwa mtiifu akizitumikia tawala mbalimbali; ya kikoloni, ya kisultani na ya Mapinduzi (katika nyakati zake za ukarimu na pia katika nyakati zake za uhabithi).
Aliyatumikia Mapinduzi kwa kutunga sheria za kimapinduzi lakini pia aliendesha mashtaka dhidi ya Makomredi waliokuwa wafuasi wa siasa za kimapinduzi za Karl Marx.
Nililiuliza swali hilo na kuyasema hayo mingine kwenye makala ya wasifu wake niliyokuwa nimeandika katika jarida la Africa Events la mwezi Novemba mwaka 1985. Miezi miwili baadaye alijibu. Hakuwa mtu wa kubania bania. Na alijitetea vilivyo.
Muhimu ni kwamba alikana ya kuwa akitaka walio hatiani kwenye kesi ya uhaini wapewe hukumu ya kifo.  Alisema ilikuwa ni yeye aliyekuwa akiwaombea wapewe hukumu hafifu, msimamo ambao alidai uliwaudhi wale waliokuwa wakitaka kuona damu ya washitakiwa inamwagika. Na ni kweli kwamba ingawa washtakiwa kadhaa walihukumiwa kifo hakuna hata mmoja aliyeuawa.
Ukweli lakini ni kwamba wakati huo tulikuwa tukifanya kampeni kubwa ya kimataifa kuukashifu mfumo wa Mahakama na wa sheria wa Zanzibar. Katika mfumo huo wa siku hizo washitakiwa wakishitakiwa katika ‘mahakama za umma’ na majaji wale walikuwa watu wasio na ujuzi wa kisheria. Miongoni mwao alikuwamo mtu ambaye kazi yake zamani ilikuwa kuuza njugu mitaani. Mfumo huo pia uliharamisha mawakili wa kuwatetea wafungwa.
Mnamo mwaka 1983 wakati wa mjadala wa mwanzo kuhusu Muungano, Dourado aliibuka na kuwa shujaa wa Wazanzibari kwa kufanya kampeni kali ya kutaka funganisho baina ya Tanganyika na Zanzibar zilegezwe huku akidai kwamba Muungano haukuwa wa halali kwa vile Hati za Muungano hazikuidhinishwa na vyombo  viwili vya utungaji sheria vya nchi hizo mbili kama ilivyotakiwa.
Dourado alizidi kumkoroga kichwa Nyerere kwa kusisitiza kwamba Sheikh Karume alipoweka saini yake kwenye Hati za Muungano alikuwa akifikiria kuwa pataundwa aina ya shirikisho na sio Muungano kama ulivyo.
Ilikuwa kama Dourado alichokoza sega la nyuki.  Watu wa usalama wa taifa waliingilia nyumba yake wakaiparaganya kwa kuikagua juu chini na wakamshika Dourado na kwenda naye Bara walikomweka kizuizini.
Hiyo ilikuwa mara ya pili Dourado kutiwa ndani kwa sababu ya maoni yake.  Mara ya kwanza alitiwa ndani na Sheikh Karume alipopinga waheshimiwa kuwaoa kwa nguvu wasichana Wakizanzibari wenye asili ya Kiajemi. Karume alimtia ndani na akamtandika bakora.
Nyerere alimfungua baada ya kumweka kizuizini Bara kwa muda wa siku 103. Alipofunguliwa alilazimishwa ajiuzulu nyadhifa zake zote za serikali.
Dourado alijiuzulu lakini hakusalimu amri. Alitaka kupigania kiti cha uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi ili aweze kuendelea na kampeni yake dhidi ya Muungano. Hizo zilikuwa ni siku za mfumo wa chama kimoja cha CCM. Wakaazi wa Raha Leo wakamtaka agombee kwenye jimbo lao.
Bado watu wanakumbuka jinsi alivyojitetea kwenye kamati ya CCM ya Raha Leo iliyokuwa ikiyachuja majina ya wagombea. Wapinzani wake kwenye kamati hiyo hawakuweza kufua dafu, walikuwa dhaifu walipokabiliwa na Dourado.
Mmoja alimwambia Dourado: “Lakini huwezi kuzungumza Kiswahili.” 
“Na mimi nazungumza na wewe kwa lugha gani?”  Alijibu Dourado kwa Kiswahili ingawa kwa lafudhi ya matata matata.
Mpinzani wake mwingine akaruka na kumwambia: “Wewe unaupinga Ujamaa.”  Dourado akajibu: “Siyo. Umekosea. Miye napinga jamaa jamaa,” akiwa na maana ya jamaa kupendeleana kwa sababu ya uhusiano wao.
Mwengine akamshtumu kwa kusema kuwa aliichafua hali ya kisiasa wakati wa mjadala wa katiba. Naye Dourado akamjibu kwamba alikuwa akitumia haki zake za kikatiba kwa mujibu wa sheria za nchi.
Wajumbe wa kamati wakampigia makofi.  Dourado akaushambulia mfumo wa chama kimoja wa wakati huo na jinsi chama kilivyofanywa kiwe adhimu kushinda taasisi yoyote nyingine.  Wajumbe wakazidi kumshangilia na kupiga makofi.  Na wote walikuwa viongozi wa ngazi mbalimbali za CCM. 
Kura ilipopigwa asilimia 95 ya kura zilimpendelea yeye awe mgombea wa jimbo hilo la Raha Leo.
Hata hivyo, hakufanikiwa kuwa mgombea wa uchaguzi kwani jina lake lilipigwa mkasi lilipopelekwa Dodoma kwenye makao makuu ya CCM.
Dourado hakupumzika. Aliendelea kumuandikia barua Nyerere akimweleza jinsi mfumo wa chama ulivyokuwa ukimdhalilisha tangu Julai 1983 alipoanza kutoa maoni yake kuhusu mapendekezo ya kuzibadili katiba mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.  Nyerere hakumjibu.
Mwisho wa maisha yake Dourado alikuwa sana ndani nyumbani kwake na mkewe akiugua ugonjwa mbaya wa ngozi ambao husababishwa na hali ya wasiwasi ya kuishi na roho mkononi.
Wazanzibari wanamkumbuka kwa mema yake na wanasikitika zaidi kwamba amewatoka katika wakati huu wa mchakato wa kuizingatia upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment