Na Ahmed Rajab
MARA kadha wa kadha nimekuwa nikigusia katika safu hii jinsi
viongozi wetu wanavyokosa mwelekeo au dira ya kuongoza. Badala ya
kuikwamua nchi kutoka umasikini wanajikwamua wenyewe na wanaiachia nchi
iselelee na hali yake ya ufukara.
Ukiwaangalia utawaona kila uchao wamo mbioni kujipendekeza kwa
wanaowaita wafadhili japokuwa fadhila ya hao wafadhili ni kama fadhila
ya punda kwa vile mara nyingi huwa ina harufu mbovu. Inawafanya viongozi
wetu wasiweze kufikiria mbinu za kuiendeleza nchi bila ya kushikilia
uzi uleule wa ‘omba omba’.
Viongozi wetu hawana kazi ila kila mara kuwabembeleza wafadhili
wawasaidie kutuletea maendeleo kana kwamba wao na wananchi wenzao
hawana uwezo wa kuiendeleza nchi.
Viongozi wetu wana tabia ya kusahau kama miujiza hutokea duniani
hata katika upande wa maendeleo ya nchi. Hapa ningependa kukumbusha
miujiza iliyotokea Singapore hasa kwa vile Zanzibar inalingana mengi na
Singapore huko ilikotoka.
Nchi hiyo ilijitangazia uhuru mwaka 1963 na ikajiunga na Malaysia
pamoja na Sabah na Sarawak kuunda Shirikisho la Malaysia. Sababu
zilizowafanya viongozi wa Singapore wajiunge na Malaysia zinaeleweka.
Kwanza wakihisi kwamba Uingereza isingeliipa uhuru nchi yao kwa sababu ingeiona kuwa ni ndogo isiyoweza kujitegemea.
Pia wao wenyewe viongozi wa Singapore wakiamini kwamba nchi yao
isingeweza kujikimu kwa vile haikuwa na eneo kubwa la ardhi, haikuwa na
maji ya kutosha, haikuwa na masoko wala maliasili. Tena wakitaka kuwa
chini ya mwavuli wa Malaysia kujikinga na joto la Wakomunisti waliokuwa
wakiyarandia madaraka.
Kwa muda wa miaka miwili Singapore ilikuwa sehemu ya Malaysia.
Lakini kama ulivyo Muungano wetu muungano wao nao ulikuwa na kero zake
na Singapore na Malaysia zilikuwa hazishi kusuguana roho. Hatimaye
Malaysia ikaitoa Singapore kutoka Shirikisho. Ndipo Uingereza ilipoipa
Singapore uhuru rasmi mwaka 1965.
Wakati huo taifa hilo dogo lilikuwa limetumbukizwa kwenye gunia la
nchi za Ulimwengu wa Tatu. Miujiza ya mambo ni kwamba leo limo kwenye
kaumu ya nchi za Ulimwengu wa Kwanza.
Singapore imeweza kujipatia ufanisi wake licha ya kwamba haina idadi
kubwa ya wakaazi, haina eneo kubwa la ardhi (ni taifa dogo lenye
visiwa 63) na kama nilivyokwishagusia ina ukosefu wa maliasili.
Ilipopata uhuru si wengi waliofikiri kwamba kijinchi hicho kitaweza kuwa
na uhai.
Wakati wa uhuru jumla ya Pato la Taifa kwa kila mtu huko Singapore
lilikuwa sawa na dola 400; hii leo ni zaidi ya dola 22,000. Pato hilo
ni la nne kwa ukubwa duniani na linalipita lile la Uingereza iliyokuwa
ikiitawala Singapore.
Hii leo Singapore ina moja ya bandari zenye shughuli nyingi duniani,
ni kituo cha tatu kwa ukubwa duniani cha kusafishia mafuta na nchi
hiyo imegeuka kuwa kituo kikuu duniani cha kuzalisha bidhaa viwandani
na katika makarkhana. Singapore imeweza kuchupa kutoka kwenye
umasikini na kusimama kwenye utajiri katika muda wa kizazi kimoja tu.
Nini kinachoizuia Zanzibar au Tanzania Bara isipate miujiza kama
hiyo? Labda niligeuze swali naniulize ilikuwaje hata Singapore ikapata
miujiza hiyo?
Jibu ni rahisi kulipata. Tangu ipate uhuru Singapore imekuwa na
uongozi bora. Anayepongezwa kwa ufanisi huo ni Lee Kuan Yew aliyekuwa
waziri mkuu wa nchi hiyo kwa miongo mitatu tangu uhuru na aliyeendelea
kuwa na ushawishi mkubwa katika uongozi wa serikali hadi hivi karibuni.
Ni yeye aliyekuwa akisisitiza kwamba maliasili pekee ya Singapore ni
watu wake na jitihada yao ya kazi. Wengi nchini mwake wanamsema vyema
kwa mvuto wa uongozi wake wakati wa uhuru na wa kujitenga na Malaysia.
Lazima nikumbushe kuwa Lee Kuan Yew si malaika. Alikuwa dikteta.
Tena alikuwa jeuri; hakuwa akimsikiliza mtu; alitakalo ndilo. Utawala
wake ukiingilia kila jambo.
Ingawa watu walikuwa na uhuru akisisitiza kuwa hawakuwa na uhuru wa
kuwaudhi wengine. Kwa hivyo, si karaha tu bali ni kosa la jinai, kwa
mfano, kutema mate njiani. Adhabu ya uhalifu huo ni faini ya dola 250
sawa na adhabu ya kuvuta sigara kwenye ofisi za serikali au kuvuka
barabara hovyo hovyo bila ya kujali magari.
Wenye kutafuna ubani (chingamu) njiani nao pia hutozwa faini hiyo
hiyo. Adhabu ya wanaopatikana na hatia ya kuingiza nchini mihadarati ni
kifo.
Lee aliwalazimisha watu waweke akiba asilimia 25 ya pato lao ingawa
kulikuwa na malalamiko kwamba serikali ilikuwa ikizitumia kwa
ubadhirifu hizo fedha za akiba ya wananchi.
Hata hivyo, udikteta wake Lee ulikuwa na tofauti. Haukuwatia sana hofu wananchi. Lee alikuwa dikteta karimu.
Wakati wa zama za ‘vita baridi’ yaani zama za michuano ya kisiasa
baina ya nchi za kibepari na zile za kisoshalisti sisi tuliokuwa katika
mrengo wa kushoto tukimponda Lee Kuan Yew kuwa alikuwa kibaraka wa
nchi za Magharibi. Yeye mwenyewe akijinata kuwa alikuwa msoshalisti
aliyeutumia ubepari kufikia lengo la kuunda jamii yenye haki na ustawi.
Ninaamini kwamba viongozi wetu wa Visiwani na wa Bara wana mengi
wanayoweza kujifunza kutoka kwa kiongozi huyo wa Singapore. Nadhani
kila mmojawao anapaswa asome kitabu alichokiandika kiitwacho ‘From
Third World to First’ (Kutoka Ulimwengu wa Tatu hadi wa Kwanza).
Mengi aliyoyaandika yanataka utulivu na nafasi kubwa kuyajadili.
Lakini naitoshe hapa tukiyapitia machache tu. Kati ya muhimu
aliyoyataja ni kwamba utamaduni wa taifa, zaidi ya uchumi na siasa, ndio
utaoamua mustakabali wa nchi.
Suala hili la nafasi ya utamaduni katika maendeleo ya nchi ni muhimu
lakini mara nyingi hupuuzwa na viongozi wetu. Nadhani ni kiongozi
mmoja tu Wakiafrika, Amilcar Cabral wa Guinea-Bissau aliyelijadili kwa
kina suala hilo ingawa kwa bahati mbaya hakupata kuongoza nchi kwani
Wareno walimuua kabla ya nchi yake kuwa huru.
Kwa mujibu wa Lee walipoanza harakati za kisiasa katika miaka ya
1950 hawakujua namna ya kuendesha nchi au jinsi ya kuyatanzua matatizo
mengi ya kiuchumi na kijamii. Lakini walikuwa na raghba kubwa ya
kuibadili jamii isiyokuwa na usawa na haki na kuifanya iwe jamii ya
haki na usawa.
Anasema alilazimika kuhakikisha kuwa ana watu wenye uwezo ambao
aliwapachika katika nyadhifa kubwa kwa kuwateua wawe mawaziri na
watumishi wakuu wa serikali. Lengo lilikuwa kuwafanya waendeshe utawala
wenye mfumo aminifu, ulio mnyofu na wenye kuyakidhi mahitaji ya
wananchi.
Lee ameendelea kusema kwamba alikuwa na kazi ngumu ya kuwafanya
wafanya kazi wawe upande wa serikali wakati ambapo serikali ilikuwa
inayashughulikia mahitaji ya wawekezaji ambao wakiwategemea kwa
rasilmali zao za fedha, maarifa, uweledi wa menejimenti na wa
kuendesha mambo kwa jumla na masoko yao ya nje.
Kitu cha awali alichohakikisha alipokuwa waziri mkuu (wakati huo
akiwa na umri wa miaka 34) ni kwamba pawepo mawaziri kadhaa wenye
kupenda mno kusoma na wanaovutiwa na fikra mpya lakini wasiofadhaishwa
au kupigwa na bumbuwazi na fikra hizo.
Lee ameeleza jinsi yeye na mawaziri wake walivyokuwa wakiazimana
vitabu na makala mbalimbali za kuvutia. Walipoingia serikalini walikuwa
madubu, wajinga hawakujuwa namna ya kutawala. Lakini walikuwa
waangalifu na wakizizingatia sera kwa makini kabla ya kuzitekeleza.
Muhimu yeye na mawaziri wake wakiaminiana. Wakijuwana nini uwezo wa
kila mmojawao na nini udhaifu wao kwa hivyo wakichukuliana.
Alibahatika kuwa na mawaziri waliokuwa na azma moja na malengo sawa.
Mawaziri waliokuwa karibu naye walifanya kazi pamoja kwa zaidi ya
miongo miwili na walikuwa wakubwa zake kwa umri na hawakuchelea
kumpasulia walivyokuwa wakifikiri, hasa alipokuwa akikosa.
Amesisitiza kwamba jambo lililowapelekea wakafanikiwa ni kwamba
kila mara wakitalii na kuangalia namna ya kutanzua matatizo au namna ya
kuyafanya mambo yawe bora zaidi. Hakuwa mfungwa wa nadharia yoyote.
Mantiki na hali halisi ilivyo ndiyo mambo yaliokuwa yakimuongoza.
Jambo jengine ni kwamba akijaribu kujifunza kutokana na makosa waliyoyafanya viongozi wengine katika nchi zao.
Aligundua mapema alipoanza kutawala kwamba hakukuwa na matatizo
yaliyoikabili serikali yake ambayo serikali nyingine hazijayakabili na
kuyatanzua.
Kwa hivyo, alikuwa na desturi ya kuchunguza nani mwengine
alikabiliwa na matatizo kama ya Singapore, na kutaka kujuwa namna
alivyoyashughulikia, yawematatizo hayo kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege
mpya au mitindo ya kusomeshea maskuli. Alifanya hima ya kuwatuma
maofisa wake wende kwenye nchi zilizofanya mambo yao vyema ili
wajifunze.
Lee anakumbusha kwamba akipuuza lawama na nasaha kutoka kwa mabingwa
au mabingwa uchwara, hasa wasomi wa sayansi za kijamii na kisiasa.
Tukiyatafakari maandishi ya Lee tunaona kwamba miongoni mwa kanuni
zilizoifanya Singapore iendelee ni pamoja na ile ya kuwa na umoja wa
kijamii, kuufyeka ufisadi serikalini, kugawana kwa usawa matunda ya
maendeleo, kuwapa wananchi wote fursa sawa na kuwa na mfumo wa serikali
unaoongozwa na wataalamu na weledi.
Hizi ni kanuni za kimaadili na tunastahili kuziiga. Angalau huko
Zanzibar tayari tuna umoja wa kijamii; yanayokosekana ni maendeleo na
hayo mingine yanayofuata maendeleo
No comments:
Post a Comment