Na Ahmed Rajab
MWANADAMU amezaliwa huru lakini kote duniani ametiwa minyonyoro,”
nimeyanukuu hayo kutoka katika maandishi ya Jean-Jacques Rousseau,
mwanafalsafa na mwandishi mashuhuri aliyeishi nchini Ufaransa karne ya
18.
Rousseau aliwahi pia kuandika kwamba wenye mamlaka katika nchi ni
umma na kwa vile umma hauna nguvu yoyote isipokuwa ya utungaji sheria,
basi hutenda mambo kwa kutumia sheria. Ameendelea kueleza kwamba
sheria yoyote ile isiyoidhinishwa na umma huwa ni batili, kwa hakika
huwa si sheria kamwe. Wenye nguvu ya kutunga sheria ni umma na ni umma
tu wenye nguvu hiyo, kwa mujibu wa Rousseau.
Mwanafalsafa huyo ni maarufu kwa ile nadharia yake ya kutaka pawepo
Mkataba wa Kijamii baina ya serikali na umma. Kitabu chake kuhusu
‘Mkataba wa Kijamii’ ni moja ya nguzo kuu za fikra za kisasa za kisiasa
na za kijamii. Na ni moja ya misingi ya utawala wa kidemokrasi.
Maandishi ya Rousseau kuhusu siasa na elimu yalikuwa na athari kubwa
kwa nadharia za kisiasa za karne mbili zilizopita. Maandishi hayo
ndiyo yaliyowavutia na kuwaathiri wanamapinduzi waliokuwa wakiandaa
Mapinduzi ya Ufaransa yaliyotokea baada ya kufariki kwake.
Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964 yaliwaahidi Wazanzibari mambo
kadhaa ambayo hadi leo bado hayajatimizwa. Waliopindua waliiona jamii
ya Visiwani kabla ya Mapinduzi kuwa ni jamii isiyokuwa na haki na
iliyokuwa ya kibaguzi. Wanazungumzia hasa kuhusu haki za kimsingi za
binadamu na fursa zilizokuwepo, fursa ambazo wanasema walikuwa wakipewa
wachache na walio wengi wakinyimwa.
Hadi leo wenye kujiona kuwa ni warithi wa Mapinduzi hayo haweshi
kuelezea kuhusu yale wanayoyaona kuwa ni maovu na madhambi ya utawala
uliopinduliwa.
Kama ilivyo kawaida ya wanaopindua wapinduzi wa Zanzibar muda wote
huu wamekuwa wakidai kwamba wao ndio wenye utatuzi wa matatizo yote
yanayoikabili nchi na hivyo wamekuwa wakiahidi kuwa watawapa wananchi
wenziwao fursa sawa bila ya kujali hadhi zao katika jamii. Mtu
hatoangaliwa ikiwa ni wa tabaka la wanaotawala au la matajiri wa juzi
juzi au ikiwa ni mwana wa mkulima kutoka shamba. Wote watapewa fursa
sawa.
Ahadi zilizotolewa na Mapinduzi zimevunjwa. Matokeo yake ni kwamba
wengi wa watu wa mijini na wa mashambani wangali wanaishi katika
mazingira magumu ya umasikini, magonjwa na uhaba wa chakula.
Hali hiyo haishangazi kwa sababu hii leo uchumi wa Zanzibar
umeanguka. Mdororo huo wa uchumi unazidi huku wale wenye dhamana ya
kuushughulikia, ingawa wanajaribu, bado hawakufanikiwa kuchukuwa hatua
madhubuti za kuuzuia uchumi huo usizidi kuporomoka.
Hali ya mambo inazidi kutatanika kwa vile sekta ya kilimo nayo
imeanguka na wakati huo huo hakuna fedha nchini na hivyo kuna ukosefu
mkubwa wa ajira (kama asilimia 70 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi
hawana ajira). Watu hawana fedha za kutumia na serikali haina mpango wa
kutoa huduma za jamii bure.
Huo bila ya shaka sio urithi wa kujivunia wa wale walioyaasisi
Mapinduzi. Na historia haiwaonei huruma inapowahukumu na kuangalia
iwapo wameineemesha jamii au wameisakamiza kwa kuufisidi uchumi
uliokuwa ukistawi kabla ya Mapinduzi.
Kuna swali ambalo Wazanzibari wana haki ya kuliuliza, nalo ni: nini
matokeo ya miaka 50 ya serikali za awamu zote ya kuuimba na kuufatiliza
ule wimbo wa ‘Mapinduzi Daima’? Hilo ni swali rahisi kulijibu kwani
tukiiangalia hali ya mambo ilivyo hatuna budi ila kukubali kwamba sera
zilizokuwa zikifuatwa na Serikali ya Mapinduzi kwa muda wa miaka 50
iliyopita ni sera zilizoshindwa kuleta tija na ufanisi. Na tunakuwa
tunajidanganya tu tusemapo kwamba Wazanzibari wote au wengi wao
wanaishi maisha stahifu yasiyo na unyonge.
Hii leo si uchumi tu bali hata sekta muhimu za elimu ya kijamii na
afya zinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa. Jambo la kutia moyo ni
kuona kwamba pamoja na jitihada za wachache serikalini za kujaribu
kuibadili hali ya mambo pia kuna asasi za kiraia zinazotoa mchango
wao. Mojawapo ya asasi hizo na iliyo mbele katika haya ni taasisi ya
ZIRPP ambayo hivi majuzi ilimkabidhi Rais Ali Mohamed Shein ripoti
mbili, moja kuhusu upangaji wa miji na ya pili kuhusu uchumi.
Wanachopaswa serikali na wananchi kukumbuka ni kuwa Zanzibar ni ya
Wazanzibari wote; ni kama shirika lao wote. Kila mmojawao ana hisa na
pia dhamana katika shirika hilo. Kila mmojawao, si serikali pekee, ana
wajibu wa kuibadili hali iliyopo.
Lazima hali iliyopo ibadilike. Na inaweza kubadilika. Duniani kuna
mifano mingi ya nchi ambazo zamani zilikuwa nyuma kimaendeleo na ambazo
sasa ziko katika safu za mbele miongoni mwa nchi zilizoweza kubadili
mifumo yao ya kiuchumi na ya kijamii.
La awali kufanywa ni kwamba serikali itambue kwamba inapaswa iwe na
mkataba na wananchi. Ili Zanzibar iweze kupiga hatua na kuendelea kuna
mambo yanayohitaji kutekelezwa na serikali na hivyo kuutimiza ule
mkataba wake wa kijamii na wananchi. Muhimu ni kuwa na sera zitazoweza
kuvinyanyua viwango vya sekta mbalimbali zikiwa pamoja na za elimu,
afya, kilimo, biashara na utalii.
Inatia moyo kuona kwamba Wizara ya Elimu ya Zanzibar imeanza kampeni
ya kuvinyanyua viwango vya elimu nchini humo na kwamba wenye kuhusika
katika wizara hiyo wana hisia ya kuikuza elimu.
Changamoto kubwa inayoikabili serikali ni kufuata sera ya uchumi
itayoigeuza Zanzibar iwe Visiwa visivyotoza ushuru na kodi za
kibiashara. Ikifanya hivyo itakuwa rahisi kuwavutia wawekezaji kutoka
nje waingize rasilmali zao katika sekta zilizo muhimu za uchumi wa nchi
hiyo. Rasilmali hizo zikiingia kuufufua uchumi pataweza kupatikana
fursa nyingi za ajira.
Uwekezaji huo pia utaufanya uchumi ukue kila mwaka si kitakwimu tu
bali kwa kuongezeka kwa mapato ya kila Mzanzibari na hivyo kuwapatia
wananchi uwezo halisi wa kujikimu kimaishi. Kwa sasa wengi wao wanaishi
kwa kasoro ya dola moja ya Marekani kwa siku.
Hatua nyingine zinazoweza kuchukuliwa na serikali ni kuwa na mkakati
wa kuvigeuza visiwa vya Unguja na Pemba viwe ni kituo cha huduma za
fedha na za shughuli za benki.
Sambamba na hatua hizo ni kuifanya tena Zanzibar iwe ni kitovu cha
biashara na usafiri kwa eneo zima la Afrika ya Mashariki na ya Kati.
Hatua zote hizo zitachangia sana kutanzua matatizo ya kiuchumi ya
Visiwa hivyo.
Linalotakiwa kufanywa ni kuchukuliwa hatua ambazo zitaweza kwa
haraka kuirejeshea Zanzibar ile hadhi yake ya kale ya kuwa kituo
madhubuti cha kiuchumi katika eneo la Afrika ya Mashariki na Kati. Kwa
bahati mbaya kwa sasa Zanzibar haiwezi kujichukulia hatua zote hizo za
kiuchumi kwa vile inahitaji ridhaa na ushirikiano wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Na hatua kama hizo zisipochukuliwa basi hali za kimaisha ya wengi wa
Wazanzibari zitaendelea kuwa ngumu kwa muda mrefu ujao kwa sababu
uchumi wa nchi yao haumudu kuwahudumia wananchi kwa kuyakidhi mahitaji
yao ya kila siku.
Wazanzibari wana matumaini mema wakizingatia utajiri unaoweza
kupatikana Zanzibarna zaidi wakiyafikiria mafuta yaliyo chini ya maji
ya bahari ya Zanzibar.Wana matumaini na wana subira.
Wazanzibari wa ndani ya nchi na walio ughaibuni wote wana hamu ya
kuendelezwa kwa hali iliyopo Visiwani ya amani, umoja na utulivu wa
kisiasa. Na wote wanataka nchi yao ipate maendeleo ya kiuchumi na ya
kijamii.
Kwa haya na kwa mahitaji ya baadaye ya uchumi, kuna haja muhimu ya
kuukuza uwezo wa watendaji katika sekta za serikali na au za mashirika
ya watu binafsi. Hii ina maana kwamba Zanzibar lazima iwe na uwezo wa
kuzipokea fedha nyingi za rasilimali zitakazoingia nchini na pia iwe na
uwezo wa kuhudumia uchumi utakaokuwa unatanuka kwa haraka.
Changamoto iliyopo hapo ni kwamba kwa sasa Zanzibar ina ukosefu wa
watendaji wenye ujuzi au waliopata mafunzo yatayostahiki kwa uchumi wa
aina hiyo. Hivyo, serikali inawajibika kuchukuwa hatua za dharura ili
kuiitayarisha Zanzibar kwa mustakabali huo.
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment