Saturday 10 March 2012

SMZ inacheza na Mishahara ya watu

 Salim Said Salim
UTAWALA wa kidemokrasia, haki na sheria una vigezo vingi vinavyohitaji kulindwa na kuheshimiwa siku zote na wakati wote.
Miongoni mwao ni kwa watawala kutumia sheria ziliopo na si kuzifumbia macho na kuachana na matumizi ya amri, maelekezo sambamba na mabavu.
Katika miaka ya mwanzo baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 amri zilizotolewa na wakubwa katika serikali, iwe kwa matamshi au maandishi, ndizo zilizotumika na watu hawakuwa na haki ya kukataa, kushauri, kukosoa au kutaka ufafanuzi wa jambo lile.
Aliyejaribu hata kunong’ona kulalamikia amri iliyotolewa na wakubwa alijikuta amejitafutia balaa isiyoelezeka na hata kujikuta amefunguliwa milango ya jela.
Waliojaaliwa kutoka hai (wengine hawakuonekana mpaka leo) baada ya kuwekwa gerezani, wengine wakiwa na majeraha mwilini kutokana na mijeledi waliochapwa au kupungukiwa nuru ya macho kutokana na kuwekwa vyumba vya kiza walibaki kumshukuru Mungu na hapakuwepo pahala pa kupeleka malalamiko.
Mtu aliyelalamika au kuikosoa serikali alipachikwa kila majina ya uovu yaliyomo katika msamiati wa Kiswahili … adui wa mapinduzi...kibaraka...msaliti..si mwenzetu au haini.
Wengine waliporwa mali zao na hata wake zao wakati wakiwa jela.
Miaka sasa imepita na watu wengi walianza kujenga dhana na kuamini kuwa dhuluma za aina ile zimepita na zitakuwa ni sehemu ya kusikitisha ya historia ya Zanzibar , lakini wapi?
Sasa mambo kama yale ya zamani, lakini kwa kiwango kidogo sana , yanaonekana kuchipua kidogo kidogo na kustawi ndani ya baadhi ya taasisi za serikali.
Miongoni mwa taasisi hizo ni vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar- Magereza (wenyewe wanaita Mafunzo), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM).
Ni lazima yaanze kudhibitiwa mapema kabla hayajastawi na kuwa kama kidonda ndugu…hakiponi.
Wananchi hivi sasa wanalamikia makato katika mishahara kama vile wao ni askari ambao hupaswa kutii kila amri wanayopewa kama walivyo askari kwenye gwaride wakati tu kama tunavyoona wakati wa sherehe za uhuru, mapinduzi na muungano.
Hali hii ilionekana katika taassi za serikali wakati timu za Zanzibar ziliposhiriki katika mashindano ya Shirikisho la Kandanda la Afrika (CAF).
Wafanyakazi katika baadhi ya taasisi walikatwa fedha za tiketi ya michezo hii iliyofanyika Zanzibar bila ya kushauriwa.
Hii sio haki na ni uonevu mkubwa. Mshahara ni mali ya mfanyakazi na ni yeye tu ndiye mwenye mamlaka kamili juu ya matumizi yake.
Anachoweza mtu mwingine au taasisi kufanya ni kumshauri mtu juu ya njia nzuri za kuutumia huo mshahara na si kumuamulia utumike vipi.
Akitaka kuutumia kidogo kujenga kibanda cha kuku, akitaka kuongezea mke au hata kuutoa sadaka ni shauri yake. Ni yeye ndiye aliyeutolea jasho na si mtu mwingine.
Hali hii ya kuchakua mishahara ya wafanyakazi iliwahi siku za nyuma kulalamikiwa hata ndani ya Baraza la Wawakilishi na wananchi wengi waliamini serikali imesikia kilio cha wafanyakazi na haitarudia mwenendo huu.
Sasa tena tunasikia malalamiko ya watu kukatwa mishahara yao bila ya ridhaa yao au kushauriwa, bali amri ndiyo iliyotumika.
Sina hakika kama hili ni agizo rasmi la serikali au ni baadhi ya wakubwa wanaoongoza taasisi za serikali ndio wamejifanyia wenyewe tu na kuamini hapana anayeweza kuhoji uamuzi wao huo.
Hili si suala dogo na halifai kupuuzwa. Ni vyema kwa serikali ikafanya uchunguzi wa kina na kutoa tamko la ufafanuzi.
Ufafanuzi utawafanya watu waelewe kama kwa Zanzibar mishahara ya watumishi wa serikali ni mali ya serikali na sio hao watumishi wanaoihudumia kwa uadilifu mchana na usiku na katika mazingira mbali mbali.
Hata kama palionekana kuwepo haja na busara ya kutoa mchango ili kusaidia watu au jamaa wa waliopata maafa kama yale ya kuzama kwa meli ya mv Spice Islanders mwaka jana iliyokuwa inatoka Unguja kwenda Pemba bado ridhaa ya wafanyakazi ilikuwa inahitajika.
Lakini kama hao wakubwa katika baadhi ya taasisi za serikali walijichukulia wenyewe tu hatua za kuwakata mshahara wafanyakazi wanaowaongoza basi wawajibishwe kinidhamu au kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wasifanye mchezo huu wa kuchezea mishahara ya watu.
Hatari ninayoiona hapa ni kuwepo uwezekano wa siku za mbele kurudia mtindo wa zamani wa wafanyakazi wa serikali kukatwa mshahara kuchangia mbio za mwenge na sherehe nyingine mbali mbali za kitaifa zisiokwisha.
Hapa inafaa tukumbuke kwamba hali ya maisha hivi sasa Zanzibar na Tanzania kwa jumla ni ngumu na viwango vya nishahara vya hivi sasa havikidhi hata robo ya mahitaji ya lazima ya wafanyakazi wengi wa serikali.
Kwahiyo, unapokata hicho kinachoitwa “kitu kidogo tu” kutoka katika mishahara kwa kweli si unajeruhi, bali unauwa.
Kama serikali kwa hivi sasa haina uwezo wa kiuchumi wa kuongeza viwango vya mishahara kwa watumishi wake basi ijizuie kuukata huo mkia wa mbuzi inaowapa watumishi wake.
Dhuluma nyingine inayoonekana kufanyiwa wafanyakazi wa Zanzibar katika baadhi ya taasisi za serikali na kampuni nyingi.
Binafsi ni kwa wafanyakazi kukatwa asilimia 5 ya mshahara, lakini feha hizo na mchango wa asilimia 10 wa muajiri kutowasilishwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF) kama sheria inavyoeleza.
Suala hili nalo pia linafaa kushughulikiwa haraka sana kwa sababu kwa kiasi fulani linawakatisha tamaa wafanyakazi wa Zanzibar .
Kwa muda mrefu wafanyakazi wamekuwa wakipigiwa kelele za kuwataka wawajibike makazini kwao, lakini hakuna anayewasimamia waajiri wao kuona nao wanawajibika na kuheshimu sheria za kazi ikiwa pamoja na kuwasilisha ZSSF michango ya hifadhi ya jamii.
Tuachane na mtindo wa kuendesha shughuli za serikali kwa mabavu na kutumia maagizo, maelekezo na amri na badala yake viongozi wawe mfano mzuri wa kuheshimu katiba, sheria za nchi na taratibu za utawala katika serikali.
Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment