Friday 23 March 2012

SMZ yatoa miche 200,000 ya karafuu, matunda

WIZARA ya Kilimo na Maliasili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema tayari imetoa miche ya mikarafuu na mazao ya matunda ipatayo 200,000 kwa ajili ya msimu wa kilimo wa mvua za masika Unguja na Pemba zinazotarajiwa kuanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Affan Othman Said alisema utoaji wa miche ya mikarafuu pamoja na mazao ya matunda ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein ambaye ameitaka wizara hiyo kutoa miche hiyo kwa wakulima.
“Tumeanza kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein la kutoa miche ya mikarafuu pamoja na ya matunda kwa wakulima katika matayarisho ya kilimo yanayotokana na mvua za masika,” alisema Affan.
Alisema wananchi wameitikia vizuri agizo la Rais la kuchukua miche ya mikarafuu kwa ajili ya kilimo hasa katika kisiwa cha Pemba ambako zao la karafuu linastawi vizuri.
Katibu Mkuu huyo alisema mikakati inayochukuliwa na wizara hiyo kwa sasa ni kuotesha miche ya mikarafuu na matunda mengine kwa wingi katika vitalu vinavyomilikiwa nayo.
“Tumeanza kuimarisha vitalu vya miche ya mazao mbalimbali ikiwemo mikarafuu pamoja na miti ya matunda....wakulima wameitikia vizuri na wanakuja kwa wingi kuchukua miche hiyo na kuotesha katika mashamba yao,” alisema Katibu Mkuu.
Affan alisema kazi kubwa inayofanywa na Wizara kwa sasa ni kutoa elimu juu ya kuotesha miche ya mikarafuu kwa mafanikio ili miche hiyo iendelee kukua vizuri.
Alisema wamechukua uamuzi huo kutokana na kuwepo kwa malalamiko kwa wakulima kwamba miche ya mikarafuu imekuwa na matatizo mengi yakiwamo ya ukuaji mgumu kwani ukipanda miche 50, inayokubali na kustawi vizuri ni 10 tu.
“Tumeanza kutoa elimu kwa mabwana shamba pamoja na mabibi shamba kwa wakulima juu ya mbinu za kisasa za kuotesha miche ya mikarafuu kwa mafanikio makubwa,” alisema Affan.
Wizara ya Kilimo na Maliasili imeweka lengo la kuotesha na kusambaza miche ya mikarafuu pamoja na ya matunda kwa wakulima ipatayo 200,000 Unguja na Pemba.
Chanzo: habari leo

No comments:

Post a Comment