TATIZO la wanafunzi wengi wa kidato cha nne Zanzibar kufutiwa matokeo ya
mitihani yao limeisikitisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na sasa
imeanza kufanya uchunguzi kutafuta kiini chake.
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo jana
wakati alipozungumza na waandishi wa habari nje kidogo ya mji wa
Unguja.
“Serikali imesikitishwa sana na tatizo la kufutiwa kwa mitihani ya
wanafunzi wengi wa Zanzibar...kwa sasa tunafanya uchunguzi zaidi kujua
kiini cha tatizo hilo kwa ajili ya kulifanyia kazi,” alisema Balozi
Seif.
Alisema tatizo hilo limezusha malalamiko na majonzi makubwa kwa
wananchi na wazazi kwa kuwa kitendo cha kufutiwa mitihani kwa wanafunzi,
kinatishia maendeleo na mustakabali wa elimu.
Awali Kamati ya Wazee iliyoundwa kuangalia suala hilo, walilitaka
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutengua uamuzi wa kuwafutia
wanafunzi mitihani ya kidato cha nne.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Hassan alisema si kitendo cha
kiungwana kuwafutia wanafunzi mitihani wakati hawahusiki na tatizo hilo
na kupendekeza kiini cha tatizo hilo kitafutwe na kuchukuliwa hatua za
kinidhamu wahusika.
“Sisi kamati ya wazee tunalitaka Baraza la Taifa la Mitihani
kubadilisha uamuzi wake wa kuwafutia wanafunzi mtihani wa taifa kwa
sababu makosa si ya wanafunzi waliovujisha mitihani hiyo,” alisema
Hassan.
Kamati hiyo imepinga adhabu ya miaka mitatu ya wanafunzi kutofanya
mitihani baada ya kubainika kufanya udanganyifu wa mitihani hiyo na
kusema hayo si makosa yao.
Imedai kuwa wanafunzi 1,045 wameathirika baada ya kufutiwa mitihani
hiyo kwa upande wa Unguja na Pemba ambapo shule 30 zilihusika na mpango
huo
No comments:
Post a Comment