Tuesday 29 November 2011

Kikwete amwaga wino Muswada wa Katiba

Tume ya Katiba kuundwa wakati wowote
  Wengi wapongeza maafikiano na Chadema
Siku 11 bada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete, ameutia saini ili uwe sheria ya kuruhusu kuundwa kwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya.
Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete aliusaini muswada huo jana na kuongeza kuwa hatua hiyo ya Rais itafutiwa na kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuupitisha baada ya kuwasilishwa na Serikali katika Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni.
"Kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua muhimu ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, pamoja na kutiwa saini hiyo, bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo.
WADAU WAMPONGEZA JK, CHADEMA
Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali wamepongeza uamuzi uliofikiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kutaka kujua ni mambo gani yaliyokubaliwa kufanyiwa marekebisho kabla ya kusainiwa kwa muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
DK. BANA: JK AMEONYESHA BUSARA
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mhadhiri Mwandamizi wa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alipongeza mwafaka huo akieleza kwamba Rais Kikwete ameonyesha busara na hekima ya hali ya juu kwa kusikiliza maoni ya Chadema kama kundi mojawapo katika jamii.
Alisema kwa kufanya hivyo Rais Kikwete ameonyesha uungwana na uvumilivu wa kuweza kuyasikiliza makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo Chadema.
Kadhalika, Dk. Bana alisema Chadema wametumia busara kufuata njia ya mazungumzo kuwasilisha mawazo yao badala ya kutumia ‘nguvu ya umma’ kama ambavyo walikuwa wameazimia.
“Tunaipongeza Chadema kwa kuona milango ya kutoa maoni hata baada ya Bunge kupitisha sheria ile, Chadema wanahoja kwa sababu Katiba ilikuwa ajenda yao kwenye kampeni za mwaka jana…nawapongeza kwa kutotumia nguvu ya umma kwa sababu ina mshindo mkubwa kwa taifa, ina madhara makubwa,” alisema.
Alisema hoja ya Katiba iliipandisha Chadema chati na kwamba kwa kuwa serikali imekubali kuitekeleza ni vyema ikaibeba hoja hiyo bila kuvunja Katiba iliyopo.
Alisema kimsingi, mwafaka uliofikiwa baina ya pande hizo mbili haupo kwenye sheria yoyote hivyo hayawezi kuathiri upande wowote ulioonyesha dhamira ya kushughulikia kilichokubaliwa.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk. Donath Olomi, alisema maamuzi ambayo ameyafanya Rais Kikwete ni mazuri kwa sababu amesikiliza maoni ya jamii ambayo walikuwa wanasema mchakato haukuwa mzuri.
Alisema inaonekana kuwa muswada huo una mapungufu na ndio maana jamii ilikuwa inataka ufanyiwe marekebisho hivyo ilikuwa vizuri kukubaliana na kufanya marekebisho katika suala hilo.
Dk. Olomi ambaye pia ni Mwenyekiti na Mkuu wa Taasisi ya mafunzo ya uongozi na ujasiriamali, alisema maamuzi hayo ni mazuri kwani amekubali kusikiliza yale mapungufu na kukubali kuyafanyia marekebisho.
KAULI YA MUFTI SIMBA
Naye Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Issa bin Shaaban Simba, alihoji kuwa maboresho hayo yanasaidia masuala ya dini? na kama ni ndio basi anayapongeza
“Hayo maboresho ambayo unanieleza yanasaidia mambo ya dini nijibu kama ni ndio basi nayapongeza,” alisema Sheikh Simba.
MAONI YA TEC
Katibu Mtendaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Anthony Makunde, alipongeza na kueleza kuwa suala la Katiba linawahusu Watanzania wote.
“Jambo lolote linaloelekea katika kujenga amani na mustakabali wa nchi linastahili kupongezwa...tushirikiane Watanzania wote tuweze kutengeneza Katiba inayofaa kwa vizazi vya leo na vizazi vijavyo,” alisema Padri Makunde.
JUKWA LA KATIBA
Mjumbe wa kamati ya uongozi ya Jukwa la Katiba, Hebron Mwakagenda, aliponda makubaliano hayo akieleza kwamba hayajakidhi kiu ya wananchi kwa kuwa haijaelezwa bayana kilichokubaliwa na utekelezaji wake utaanza lini.
Alisema suala la Katiba si la Chadema na Serikali bali ni la Watanzania wote hivyo kitendo cha pande hizo mbili kufikia makubaliano hakitakidhi matarajio ya wengi.
Alisema msimamo wa jukwaa hilo uko pale pale kwamba wanamtaka Rais asiusaini muswada huo hadi hapo maoni ya wananchi yatakaposikilizwa na kuingizwa kwenye maboresho hayo.
“Walichokubaliana ni kama kilichotokea Zanzibar kati ya Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif ambacho hadi leo haijulikani nini kiliafikiwa kwa hakika kabisa, kwa hiyo msimamo wetu ni kutokubali Rais asisaini ule muswada,” alisema Mwakagenda.
KAFULILA: HAKUNA JIPYA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema mwafaka huo hauna jambo lolote jipya kwa kuwa kilichoafikiwa sicho kilichokuwa kilio cha wananchi wengi.
“Tulitoka nje ya Bunge kwa kupinga muswada ule usisomwe mara ya pili tukitaka usomwe mara ya kwanza, kwa sababu kanuni zilikiukwa, matumaini yangu yalikuwa kwamba Rais angekubali kuurudisha bungeni ili ukajadiliwe upya,” alisema Kafulila.
Aliongeza: “Sioni mantiki yoyote ya makubaliano na sijui kwa nini Chadema wamekubali kusaini makubaliano hayo, kilichofanywa na CCM kupitisha muswada ule kinadhihirisha wazi kwamba serikali yake haina dhamira ya kutunga Katiba.”
Kafulila alisema makubaliano hayo hayatakuwa na manufaa makubwa kwa sababu hayaonyeshi kuwasilisha kilio cha wananchi waliokuwa wanataka muswada usomwe mara ya kwanza.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment