Na Muhibu Said
Ahoji Uingereza wameshitaki wangapi kwao
Ni kwa wabunge wake kutaka washitakiwe
Ni kwa wabunge wake kutaka washitakiwe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe
Serikali haijaonyesha nia ya kuwashtaki watuhumiwa
walioko nchini wanaohusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi
licha ya kundi la wabunge wa Uingereza kutaka wahusika wa kashfa hiyo
washtakiwe.
Msimamo huo wa serikali ya Tanzania,
umedhihirika baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora),
Mathias Chikawe, kuwajia juu wabunge hao wa Uingereza kwa kuwataka
waeleze idadi ya
wahusika wa kashfa hiyo walioko nchini
mwao waliokwisha kufikishwa mahakamani, kabla ya kuwanyooshea kidole
watuhumiwa walioko Tanzania.
Chikawe alisema hayo alipotakiwa na
NIPASHE, kueleza msimamo wa serikali ya Tanzania kuhusiana na wito wa
wabunge hao kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini Uingereza, kutaka
wahusika wa kashfa hiyo washtakiwe.
Kabla ya Chikawe kujibu swali hilo, alihoji rada hiyo ilinunuliwa na nani na kwa fedha za nani.
Alipojibiwa kuwa ilinunuliwa na serikali
ya Tanzania na kwa fedha zake, Chikawe alisema: “Wapigie (simu) hao
wabunge wa Uingereza uwaulize ni wangapi kwao wamewapeleka mahakamani?”
Chikawe alisema anasema hivyo kwa vile kashfa ya ununuzi wa rada inagusa orodha ya watu wengi nchini humo.
“Wao wanajua Tanzania tu. Achana nao,” alisema Waziri Chikawe kisha akakata simu.
Wito wa kutaka kufunguliwa mashtaka dhidi
ya mtu yeyote aliyehusika katika kashfa ya ufisadi na rushwa kuhusiana
na mauzo ya rada hiyo kwa Serikali ya Tanzania yaliyofanywa na kampuni
ya vifaa vya ulinzi ya BAE Systems ya Uingereza mwaka 2002, ulitolewa na
wabunge hao, Desemba Mosi, mwaka huu.
Wabunge hao walisema wako tayari
kushirikiana na serikali ya Tanzania katika mahakama zake kuendesha
mashtaka dhidi ya watu wanaohusika na ulaghai huo.
Miongoni mwa wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa hiyo, ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Chenge anatuhumiwa kumiliki Dola za
Marekani milioni 1 (Sh. bilioni 1.2) kwenye akaunti yake iliyoko katika
Kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.
Alikutwa na kiasi hicho cha fedha mwaka
2008, kufuatia uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na
Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO).
Chenge amekanusha fedha hizo kuwa na
uhusiano wowote na fedha za rada, ameweka wazi kuwa ni jasho lake kwa
kazi za uwakili na urithi wa familia yake.
Chenge, ambaye wakati wa ununuzi wa rada
hiyo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), anatuhumiwa kuwa kiungo
muhimu katika ununuzi wa rada kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya
BAE Systems.
Baada ya kukutwa na kiasi hicho kikubwa
cha fedha zenye utata alichokiita “vijisenti”, kuliibuka shinikizo kubwa
kutoka kwa watu wa kada tofauti nchini wakitaka akamatwe na
kushitakiwa.
Julai 21, mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward
Hoseah, alitangaza hadharani mjini Arusha kwamba, Chenge atashtakiwa
chini ya kifungu cha 27 Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007.
Sehemu ya kifungu hicho cha sheria,
inaainisha kuwa mtu akiwa na mali, ambazo hazilingani na kipato chake
alichokipata akiwa madarakani au baada ya kuondoka, ni kosa kisheria.
Dk. Hoseah, alisema kama Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) atalipitisha jalada la Chenge, mbunge huyo atafikishwa
mahakamani wakati wowote.
Kashfa ya kuwa na fedha hizo katika
akaunti ya nje, ndiyo ilimwondoa Chenge katika wadhifa wa Uwaziri wa
Miundombinu mwaka 2008, baada ya gazeti la Guardian la Uingereza
kufichua kuwa alikuwa akimiliki kiasi hicho cha fedha.
Dk. Hoseah akifafanua zaidi mchakato huo
mzito wa kisheria, alisema ni Watanzania wachache mno wanaoweza kuwa na
akiba ya fedha kiasi kama hicho nje ya nchi au mahali kokote.
Alisema jambo hilo ndilo lililowasukuma kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo za Chenge.
Kuhusu kuhusika kwa Chenge katika kashfa
ya rada baada ya Mahakama Kuu Uingereza kuamuru BAE Systems kurejesha
sehemu ya fedha kwa Tanzania kutokana na kubaini kutokuwekwa kwa rekodi
za kiuhasibu sawasawa hasa katika fungu la kamisheni kwa waliofanikisha
biashara hiyo, Dk. Hoseah, alisema Chenge hahusiki na kwamba, hakuna
ushahidi wowote wa kumtia hatiani.
Kwa mujibu wa Dk. Hoseah, waliohusika na
kashfa hiyo tayari wameshatajwa na hata washiriki wao wanajulikana,
wakiwamo raia wa Uingereza.
Kutokana na kashfa hiyo, Chenge, ambaye
pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja watuhumiwa wa ufisadi, ambao
wanatakiwa kujivua gamba.
Kampuni ya BAE Systems tayari imekubali
kulipa takriban dola za Marekani milioni 46 kama fidia kwa Tanzania kwa
kukosa kuweka kumbukumbu zake za mahesabu sawa kuhusiana na mauzo hayo
ya rada yenye utata.
UINGEREZA YAIWEKEA MASHARTI TANZANIA
Katika hatua nyingine, Uingereza imeiwekea
masharti serikali ya Tanzania kabla ya kuipatia fedha zilizozidi
“chenji” kwenye ununuzi wa rada kwa kuitaka kupeleka kiasi hicho cha
fedha kwenye sekta, ambayo itawanufaisha wananchi wote.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo,
alithibitisha kuwapo kwa masharti hayo na kuongeza kuwa baada ya
serikali kuyapata iliamua fedha hizo zitakapolipwa zipelekwe kwenye
sekta ya elimu.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkulo,
alisema mazungumzo kuhusiana na urejeshwaji wa “chenji” hiyo
yamekamilika na kinachosubiriwa ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
kuainisha maeneo, ambayo yanahitaji kusaidiwa katika sekta ya elimu.
“Serikali ya Uingereza inatusubiri sisi
kila kitu kipo tayari na sisi tukimaliza kuainisha maeneo tunayohitaji
kuyasaidia kwenye sekta ya elimu watatuletea fedha hizo,” alisema Mkulo.
Alisema serikali ya Uingereza
imeihakikishia Tanzania kwa maandishi kwamba, italipwa fedha hizo na
zitakapoingia nchini zitatumika kwa ajili ya elimu pekee.
“Tumeshapata barua kutoka Serikali ya Uingereza kwamba, serikali ya Tanzania italipwa Paund milioni 29.50,” alisema.
Waziri Mkulo alisema utaratibu huo
unafanywa kati ya serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Fedha hizo zinarejeshwa nchini baada ya
BAE iliyouzia Tanzania rada hiyo kwa bei kubwa kuliko bei halisi na
baada ya kukiri mahakamani Uingereza kosa la kuzembea katika uwekaji
kumbumbu za kiuhasibu na amri ya kulipa kiasi hicho kama faini
kuridhiwa.
BAE iliiuzia Tanzania rada hiyo kwa dola za Marekani milioni 40 hatua iliyopingwa na watu wengi, wakiwamo wanaharakati.
Mbali na Chenge, raia mwingine wa Tanzania
ambaye anatuhumiwa katika kashfa hiyo ni Sailesh Vithlanmbali ambaye
alikuwa mtu wa kati katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
Haya jamani hawa ndio viongozi ambao tunaambiwa wana imani na wananchi wao, Uingereza wao ndio ambao wamefaidika na mradi huu na kwa imani yao tu wametushtuwa kuwa tumeibiwa na waliosababisha wapo hapa petu leo waziri anamwambia mtu ambae katuonesha mwizi kuwa mbona wewe nawe unaibiwa na huwakamati, kamata wako kwanza ndipo uje uniambie niwakamate wezi wangu
ReplyDeleteHichi kichekesho