SINA muda wa kupoteza leo isipokuwa naomba tujivue unafiki na kisha
kila mmoja wetu ajihoji Desemba 9, mwaka huu, tunasherehekea Uhuru wa
miaka 50 ya taifa lipi? Nahitaji jibu la moja kwa moja si siasa za
upotoshaji, anayejibu swali hili anapaswa kujiweka katika nafasi ya
mtoto mdogo anayepaswa kujua jambo fulani kiundani.
Desemba 9, mwaka 1961, kulikuwa nchi yetu inaitwa Tanganyika ambayo
ilipata uhuru wake. Ilipofika mwaka 1964 Rais wa Tanganyika Julius
Nyerere na mwenzake wa Zanzibar Abeid Amani Karume, waliona ipo haja ya
mataifa hayo kuunga.
Muungano ni kuunda umoja na ushirika wa pamoja lakini nje ya hapo kila
mtu anabakia kuwa kama alivyokuwa awali. Hii kwa bahati mbaya sivyo
ilivyokuwa kwa huu muungano wetu.
Baada ya Muungano kufanikiwa na kuundwa Tanzania, nchi moja ya
Tanganyika ilinyongwa na ikabakia Zanzibar. Na ndani yake zikaletwa
siasa za Tanzania Bara na Tanzania Visiawani.
Hivi mtoto wa kizazi cha leo anapohoji kujua ilipo Tanganyika
tunaweza kumweleza nini mbali na siasa? Zanzibar ipo Tanganyika ilikufa
ikazaliwa Tanzania Bara ambayo kimsingi ndiyo hiyo hiyo Tanzania.
Hii ndiyo historia ya nchi yetu, na tunathubutu kutembea kifua mbele
tukijiaminisha kuwa tumekomaa kifikra vya kutosha wakati tunapotosha
ukweli kuhusu Taifa letu?
Leo watoto, vijana, watu wazima na mbaya zaidi viongozi kila mmoja
anaimba kuwa Desemba 9, mwaka huu, tunasherehekea miaka 50 ya Uhuru wa
Tanzania Bara ( Hii ni nchi ipi?).
Zanzibar wana vielelezo vya utambulisho wao kama taifa, wana wimbo wa
taifa, bendera, katiba yao, Bunge lao na mengineyo. Nchi inayoitwa
Tanzania Bara haina bendera, wimbo wa taifa, Bunge badala yake wanatumia
vielelezo vya taifa la Tanzania lililotokana na muungano wa (Tanganyika
na Zanzibar).
Hivyo, hata Desema 9 mwaka huu, kinachosherehekewa si miaka 50 ya Uhuru
wa Tanganyika. Maana siku hiyo utaimbwa wimbo wa taifa wa Tanzania,
itapeperushwa bendara ya Tanzania, Rais atakuwa wa Muungano, sasa hapa
tutasemaje ni uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara kama
tunavyojidanganya)?
Hivi ndivyo tumeendelea kujidanganya kwa miaka yote. Tumekuwa na
Bunge la Muungano ambalo linawashirikisha wabunge kutoka Zanzibar,
kimsingi linapaswa kujadili mambo yale yanayohusu muungano tu.
Lakini kutokana na udhaifu wa muundo wa muungano wetu hata kwenye
mijadala ya mambo yasiyo ya Muungano wabunge wa Zanzibar wanaendelea
kuwemo wanashiriki kutuamulia wakati kule kwao wana Baraza la
Wawakilishi ambalo linajadili mambo yao pekee.
Huu mfumo wa muungano wetu lazima tukubaliane kuwa una kasoro hata kama
hatutaki kuambiwa ukweli. Ni bora kujitathmini kuanzia hapa ili itafutwe
suluhu ya kuondosha upotoshwaji wa historia ya nchi yetu ya Tanganyika
badala ya kuendelea kuzika vichwa mchangani kama kanga tukidhani
tumejificha hakuna shida.
Mfano mdogo wa mkorogano huu unajitokeza kwenye michezo hasa kwenye
mashirikisho yanayotutambua kama nchi mbili. Kwa sasa hapa Tanzania
yanaendelea mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la Shirikisho la Mpira
wa Miguu la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Katika michuano hiyo Zanzibar wameingia kama nchi, wanatambulika kwa
timu yao ya Zanzibar Heroes wakiwa na bendera ya taifa lao na wimbo wao
wa taifa halafu eti sisi tumejibadilisha kutoka Taifa Stars tunajiita
Kilimanjaro Stars.
Lakini kinachofanyika kwenye timu ya Kilimanjaro Stars ni kile kile
cha Taifa Stars, kwani wimbo na bendera wanavyotumia ni vile vile vya
Tanzania. Na hata kocha kabadilishwa tu mwaka huu baada ya Wazanzibari
kuhoji maana huyo huyo wa Taifa Stars ndiye alikuwa anafanywa wa
Kilimanjaro Stars.
Mimi ni mmoja wa waumini nisiyeona aibu kusema kuwa tunaadhimisha miaka
50 ya Uhuru wa Tanganyika, lakini siku hiyo ya Desemba 9 mwaka huu,
sitasherehekea maana hakutakuwa na bendera ya Tanganyika wala wimbo wa
Tanganyika ili kuniletea hisia za kumbukumbu ya kuachana na ukoloni.
Naogopa sana unafiki na uongo wa kujidanganya kushiriki kuimba wimbo
wa Mungu ibariki Tanzania wakati huo bendera ya rangi nne ya Tanzania
ikipeperuka halafu nijiaminishe kuwa nimesherehekea miaka 50 ya Uhuru wa
Tanganyika.
No comments:
Post a Comment