Tuesday 6 December 2011

HOTUBA YA JUMUIYA YA WAFANYA BIASHARA, WENYE VIWANDA NA WAKULIMA KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MLIPA KODI.

TAREHE 06/12/2011

Mheshimiwa, Mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Afisi Ya Rais Fedha Uchumi, na Mipango Ya Maendeleo.
Naibu Kamishna TRA,
Waheshimiwa, Wafanyabiashara wa Zanzibar,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Assalaamu Alaykum.


1)Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwingi wa Rehema kwa viumbe vyake vyote, kwa kutujaliia kuwa na afya njema katika siku hii adhimu ya Mlipa Kodi katika mwaka huu wa 2011.

2)Napenda vile vile kueleza shukurani zetu za dhati kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) Zanzibar kwa kutupatia nafasi ya kueleza mawazo ya wafanyabiashara katika hafla hii. Tutajaribu kueleza yale ambayo tunaamini yanaweza kuletea ufanisi katika kutekeleza jukumu kubwa walilopewa wenzetu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Zanzibar. Jukumu hilo ni lile la kukusanya kodi kwa lengo la kukuza uchumi wa Zanzibar na kuendeleza huduma za kijamii kwa wananchi wake. Kwa ujumla maudhui yangu ni kuwa kodi inayokusanywa Zanzibar ni kwa maendeleo ya huduma za kijamii na za kiuchumi za Zanzibar.


3)Kwa ujumla kodi ni makusanyo ya sehemu ya mapato yanayofanywa na utawala wa nchi kutoka wenye kipato kulingana na sheria ili mapato hayo yaweze kutumika kutoa huduma za jumla ambazo ni za lazima na haziwezi kutolewa na mtu mmoja mmoja, katika jamii nzima. Mfano wa hayo ni usalama wa raia, barabara, elimu na hata ulinzi wa nchi. Orodha wa yale ambayo yanaweza kuhudumiwa kwa kutumia kodi ni mrefu wala sina madhumuni ya kuelezea zaidi upande huo, isipokuwa tu kuongeza kuwa kwa ujumla madhumuni yake ni kuleta maendeleo ya nchi.

Zaidi ya yote hamasa na hiari ya ulipaji kodi usio wa kushurutishwa unachangiwa sana pale mlipa kodi anapoona kuwa kodi yake inatumika ipasavyo na kwa uangalifu na kwamba mwisho ya yote inamrudia mwenyewe kwa kupata huduma stahiki kama vile matibabu bora, elimu , huduma za maji nk. Hivyo ni jambo la msingi serikali iwe na uangalizi mkubwa katika suala la matumizi ili ipige vita aina zote za ubadhirifu ili mlipa kodi aone matunda ya kodi yake.

4)Kwa hapa Zanzibar vyombo vinavyokusanya kodi mbali na TRA, ni pamoja na Zanzibar Revenue Board, Mabaraza ya Manispaa, Halmashauri, na Vitengo vyengine vya Idara za serikali, ambavyo hukusanya “kodi” kwa majina mbalimbali.

5)Kwa upande wetu wafanyabiashara, tunahisi ingekuwa vyema kama shughuli hii ya leo ingelijumuisha pia na Bodi ya Mapato Zanzibar, na vyombo vyote vya ukusanyaji “mapato” kwani kwa mtazamo wetu Bodi hii, pamoja na vitengo vyengine vya serikali, vinawajibika moja kwa moja kwa Serkali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na muhimu zaidi vinakusanya kodi kutoka mlipa kodi mmoja huyo huyo. Mkusanyiko wa vyombo vya ukusanyaji hapa leo ungeipa serikali picha halisi ya mzigo wa kodi na mzigo wa kuwajibika kulipa kodi (cost of compliance) kwa mlipa kodi. Katika mipango yake ya kutaka kodi kutoka kwa wafanyabiashara tunaiomba serikali isisahau kwamba kuna gharama za kuwajibika na kulipa kodi, mbali na kodi yenyewe. Serikali ina wajibu wa kupunguza gharama hizo na ikiwezekana kuziondosha kabisa.

6)Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kitendo cha kuiweka siku maalum ya mlipa kodi ni kitendo cha kimaendeleo. Si mara nyingi watu, hata viongozi wanaoelewa yakua walipa kodi ndio “engine’ ya shughuli zote za Serikali. Mara nyingi watu huhisi yakua Serikali inazo tu fedha lakini hawajui zinatoka wapi. Kwa hivyo kitendo
cha kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kulipa kodi ni kitendo muwafaka kabisa. Ni katika kuiendeleza dhana hii ndio serikali inapata fursa ya kuanzisha ushirikiano na walipa kodi katika mfumo wa PPP wenye lengo la kuleta maendeleo ya wote kwa jumla.

7) Kitendo cha kuwapa tunzo walipaji kodi wazuri ni kitendo cha kiungwana na chenye kuleta faraja, kwani wahenga wanasema “mcheza kwao hutunzwa”, hata kama kitakuwa kidogo lakini hufarijika na kuwashajiisha wengine kuiga mfano mwema na hatimaye kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari. (Voluntary Tax Compliance). Haitakuwa vibaya kama katika hafla kama hii siku za mbele serikali au TRA ikavitambulisha vigezo vilivvyotumiwa kupata walipa kodi wazuri. Jambo hilo yumkin huenda likawashajiisha na wengine kujaribu kuvifikia. Kwani wafanyabiashara wakijaribu, hata kama hawakuvifikia watakua wamechangia katika makusanyo ya kodi.

8) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Labda tuulizane hii mbinu ya kuwazawadia walipa kodi wazuri inatosha kuongeza kodi kwa serikali? Sisi tunadhani mbinu hii inachangia sana lakini haitoshi pekee, na kwa hivyo mbinu nyengine kutoka upande wa sera itabidi ziangaliwe. Itabidi tuliangalie suala hili katika daraja ya sera na si ile daraja ya ukusanyaji pekee. Katika daraja ya sera kama tunataka kuongeza makusanyo hapana budi mbinu nyengine za ziada zitumiwe ili wigo utanuke, au biashara na uzalishaji utanuke zaidi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

9) Katika uwanja wa biashara ni vipi tutaweza kuongeza makusanyo wakati soko la Zanzibar la watu milioni moja ni lile lile? Sisi wafanyabiashara tunadhani biashara inaweza kutanuka kama Zanzibar itajipatia soko kubwa zaidi ya lile la visiwa hivi viwili. Uanzishwaji wa Jumuia ya Africa Mashariki, pamoja na Zanzibar kuwa ni sehemu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ni nafasi ambazo zinaweza kutumiwa kisera kuipatia Zanzibar soko kubwa la bidhaa ambalo litaweza kutoa kodi ya kutosha kwa maendeleo ya Zanzibar. Kwa mantiki hii mbinu za kulifikia soko la Jumuia ya Africa Mashariki ndio kazi kubwa ya kuangaliwa watunga sera wetu.

10) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Naomba kutoa mfano mdogo kihesabu na uzoefu kuhusu namna ya kuitumia kodi kama nyenzo ya kuongeza mapato. Mfano Zanzibar inatoza wastani wa kodi ya 30% kwa bidhaa fulani bandarini, na mizigo 1,000 ya bidhaa hizo ikaingizwa nchini kwa kipindi fulani. Zanzibar itapata kodi sawa na mizigo 300. Lakini ikiwa itapunguza kodi hadi 5% tu (badala ya 30%) na mizigo ikapungua bei na ikaingizwa 50,000 (badala ya 1,000) basi Zanzibar itapata kodi ya wastani wa mizigo (5%x50,000 = 2,500). Ongezeko la hapa ni kutoka Zanzibar kupata wastani wa kodi wa mizigo 300 hadi kufikia mizigo 2,500. Papo hapo ieleweke hakuna namna ya mizigo kuongezeka kutoka 1,000 hadi kufikia 50,000 bila ya kazi hiyo kuongeza ajira nchini. Na vile vile tujiulize, Jee ni lazima mizigo iongezeke hadi kufikia 50,000 kutoka 1,000. La, hasha. Hata kama mizigo ingeongezeka kufikia 7,000 (kutoka 3,000) tu basi tayari wastani wa mizigo 300 umeshapitwa. Ninalojaribu kusema ni kuwa uko uwezekano kuongeza mapato ya kodi na ajira hata katika kupunguza viwango. Tunavyoiona TRA sisi wafanyabiashara wa Zanzibar ni kuwa ina sera maalum ya kuidhibiti Zanzibar isitumie fursa zilizomo ndani ya Muungano huu, na mbaya zaidi inaonekana ina mamlaka makubwa ya kutojali maamuzi ya viongozi wa Jamhuri Ya Muungano. TRA inaonekana ina sera ya kuitumia kodi kama kidhibiti Zanzibar!
11) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Wafanya Biashara sote hatuwezi kuwa walipa kodi bora, lakini sote tunaweza kuwa walipa kodi wazuri na kukaribiana katika ulipaji kodi kwa mujibu wa biashara zetu zilivyo. Aidha mchango wa kodi katika makusanyo unaweza kuongezeka kutokana na sera tunazoziomba kuwapa mwanya zaidi wafanyabiashara wetu kupata uhuru wa kufanya biashara wakiwa hapa Zanzibar, na kulipa kodi zao hapa Zanzibar bila ya kushurutishwa kuhamishia biashara zao Tanzania Bara au sehemu nyengine za Africa Mahariki. Katika mkakati wa kuendeleza Tanzania TRA nao waelimishwe yakua Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri hii na maendeleo au mafanikio ya Zanzibar ni maendeleo ya Tanzania na wao wawe watekekezaji wa sera za kuendeleza Tanzania yote.

12) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, hivi sasa tunaona wafanyabiashara wetu wengi wakihamisha sehemu kubwa ya biashara zao na kuzipeleka Tanzania Bara na huku wakituambia yakua vikwazo vya kodi hasa ya bandarini vimewaondokea katika biashara zao za huko bara. Jee kuna sera mbili za kuendeleza Tanzania. Jee kuna manufaa yeyote kwa Tanzania kama upande wake mmoja utadumaa. Sisi wafanyabiashara wa Zanzibar na ambao tunalipa kodi hapa Zanzibar, tunadhani kuna upotofu katika muelekeo huu wa TRA kuhusu biashara za Zanzibar; na kwa vile kijiografia Dar-es-salaam ndio njia ya bidhaa za Zanzibar kuingia katika soko la Africa Mashariki kwenda Uganda, Rwanda Burundi na Kenya suala hili lina umuhimu wake na tunaomba lisidharauliwe.

13) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Hapa naomba kutoa mfano hai wa yanayofanywa na TRA kuhusu biashara za Zanzibar ziendazo bara na zipitiazo bara kwenda nchi za nje. Super Shine ni kiwanda kipo eneo la Viwando Vidovidogo Amani kwa sheria za ZIPA EPZ kama mwekezaji tokea 1996. Kinazalisha audio cassettes, video cassttes, CDs, DVDs na bidhaa za plastic kwa kuuza 20% ndani ya nchi na 80% nje ya nchi.
Kinyume na makubaliano ya nyuma na sheria za EPZ kuanzia Aug 2011 wameanza kulazimishwa kulipa VAT na Import Duty kwa bidhaa zinazoingizwa Tanzania bara. Kwa maana hii bidhaa zinazozalishwa Zanzibar ni bidhaa za kigeni zinapoingizwa Bara. Wakati huo huo bidhaa zote za viwanda vya bara km saruji hailipishwi kodi hizi zinapoingizwa Zanzibar.
14) Jengine ni kuwa kuanzia Aug 2011 wamelazimishwa kulipa VAT na Import Duty kwa zile bidhaa wanazosafirisha nje ya nchi. Haya ni maajabu, bidhaa zinapita tu Tanzania bara na zinatozwa VAT ambayo ni kodi ya mlaji (wa Zambia) na Import duty wakati bidha hizi ni Exports zinapita njia tu. (maelezo kamili yapo kwenye pamphlet ambayo tutaomba tukupe Mheshimiwa Mgeni Rasmi.), pamoja na hotuba yetu hii.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

15) Sisi wafanyabiashara tunashukuru kuwa mwaka 2009 tulipatiwa fursa ya kutoa maoni yetu ingawa ufumbuzi bado umekuwa hafifu, hata hivyo tunathamini umuhimu wa siku hii ya mlipa kodi, kwa matumaini yakua maoni yetu yatasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi na mengine kuendelea kufanyiwa kazi kwa manufaa ya Zanzibar. Wakati huo huo kuna masuala mengine yamejitokeza na tunahisi kuwa ni muhimu kuangaliwa ili kumfanya mlipa kodi wa Zanzibar awe na shauku ya kulipa kodi na vile vile kuwashawishi wafanyabiashara wetu waendeleze biashara zao Tanzania nzima pamoja na Africa Mashariki huku wakiishi na kulipa kodi Zanzibar. Hii ni kwa dhamira ya kuona yakua si lazima kwa wafanyabiashara wahamie bara ili waendeleze biashara zao huko. Sasa naomba nieleze, kwa muhtasari yale ambayo tuliyasema mwaka 2009 na ambayo hayakuchukuliwa hatua pamoja na mepya ambayo ni muhimu kushughulikiwa.

16) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ingawa ni vyema kwa walipa kodi kulipa kodi, ni vyema vilivile wapewe uhuru wa kupata mapato ili walipe kodi.

17) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, leo hii tunazungumzia walipa kodi na mchango wao katika maendeleo. Si vibaya tukazungumzia wakusanyaji kodi nao mchango wao katika kuhakikisha yakua kodi inakuwa nyingi hapa Zanzibar ili ikusanywe na kuwasilishwa serikalini.

18) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, hapo juu nilitoa mfano wa kimahesabu kuhusiana na kodi na mienendo yake. Mfano ulikuwa wa kuongeza makusanyo ya kodi kwa kupunguza viwango vya kodi. Sasa naomba kutoa uzoefu tuliouona hapa Zanzibar kutokana na bidhaa kuongezewa kodi. Itakumbukwa yakua kulikuwa na kodi hapa Zanzibar zilizowaruhusu wafanyabiashara kuuza kwa bei za chini kulingana na kwengineko Africa Mashariki katika miaka ya 1990s na mapema ya 2000s. Matokeo ya bei hizo ni kuwa wafanya biashara wengi kutoka nje kama vile Comoro, Malawi, Burundi, Rwanda, Zambia, Kenya n.k walikuja kwa wingi kununua bidhaa, na kuzichukua makwao. Mbali na kukuza mfuko wa kodi walikuwa wakiishi kwenye mahoteli na kutumia huduma za mikahawa, taxi, mikokoteni nk. Yote hayo yalipotezwa kwa uamuzi wa TRA kuwatoza kodi za ziada bandarini Dsm hata kama wikuwa wakipita tu njia Dar es salaam. Katika hili Zanzibar imekosa kila kitu na wafanyabiashara pia wamekosa kila kitu. Hakuna tena wafanyabiashara kutoka nchi za jirani wanaokuja Zanzibar kununua bidhaa zao. Bila shaka kodi kwa Zanzibar nayo imepotea.

19) Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Ipo haja ya kujiuliza kama matokeo ya aina hii yanasaidia kujenga moyo wa ulipaji kodi katika wafanyabiashara wetu. Ni jambo la uhakika kwamba kila mlipa kodi atalipa kodi kwa furaha bila kinyongo kwa kiwango chochote pindipo tu akiona kwamba kodi anayoilipa inarudi kwake kwa jinsi inavyotumika kweli kweli katika kuleta maendeleo na kutoa huduma za jamii – afya ,elimu, miundombini n.k. Mifano hii inaonekana wazi katika nchi za wenzetu zilizoendelea.

20) Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Naomba kueleza kidogo kuhusu ukubwa wa kodi za Zanzibar kulingana na zile za bara. Ingawa Corporate tax hapa ni 30% kwa Tanzania yote kodi halisi yaani “effective tax rate”ni 40% hapa Zanzibar kulingana na uchambuzi uliofanywa na “Doing Business in Zanzibar. Viwango vya walipa kodi binafsi (Individual tax rates) pia vile vya Zanzibar ni vikubwa sana kulinganisha na vya Tanzania bara ingawaje hali ya kipato cha Wanzanzibari ni kidogo zaidi. Kodi ya Ujuzi wa Maendeleo – Skills Development Levy (SDL) abayo ni asilimia tano (5%) ya mapato ya mishahara ya wafanyakazi pia ni kubwa mno na tuna wasi wasi kwamba haitumiki kwa malengo khasa yaliyokusudiwa. Kulingana na ukubwa wa uchumi wa Zanzibar viwango hivi vya kodi ni vikubwa na vinadumaza juhudi ya kujipatia kipato na vivyo hivyo juhudi za kuongeza makusanyo ya kodi. Kwa upande wa sera naomba ieleweke kua kodi iliyo kubwa ina punguza shauku ya wawekezaji kuweka mitaji yao katika uchumi husika. Katika hali ya Zanzibar kodi kubwa na soko dogo ni mchanganyiko maalum wa kuwatisha wawekezaji na hivyo kupunguza mapato ya kodi, ajira na mengineyo. Kama washauri tunaomba viwango vya kodi viangaliwe ili vyenyewe viwe ni vivutio kwa wawekezaji

21) Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Muundo wa uongozi wa TRA Zanzibar (Organization Structure) bado hautoi mamlaka ya maamuzi kwa mujibu wa taratibu za TRA, hivyo tunaishauri Serikali iliangalie suala hili kwa undani zaidi ili maamuzi yanayotolewa na TRA Zanzibar yaheshimike na yaonekane kuwa ni maamuzi sahihi kama yalivyo kwa maamuzi ya TRA ya Tanzania Bara. Atawezaje kuisaidia Zanzibar kupata kodi zaidi ikiwa maamuzi yake hayathaminiwi. Jambo hili nalo linahitaji ufumbuzi.

22. Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mwisho, kwa vile leo ni siku yetu walipa kodi tunapenda kutoa kilio chetu juu ya haki yetu ya msingi tunayonyimwa ndani ya sheria ya Rufaa za Kodi (Zanzibar Tax Appeals Act (2006). Sheria hii ilianzishwa kwa misingi ya kutoa haki kwa mlipa kodi pindi asiporidhika na maamuzi ya vyombo vinavyokusanya kodi. Tuna hakika kwamba toka ilipoanzishwa bodi hiyo ya rufaa mwaka 2006 hakuna kesi hata moja waliyoipokea na sisi kama walipa kodi hatutegemei kupeleka kesi yoyote huko kutokana na ukandamizaji wa sheria hiyo na jinsi isivyompa haki mlipa kodi. Sheria ina masharti mawili makubwa kwanza- ni Lazima ikiwa mlipa kodi hakuridhika na kodi aliyoamriwa kulipa na Kamishna, basi afanye Objection kwa Kamishna wa chombo cha kodi kinachohusika (TRA/ZRB). Tatizo hapa ni kwamba kama tokea mwanzo mlipa kodi na Kamishna wameshindwa kukubaliana vipi mlipa kodi anatakiwa arudi tena kukata rufaa ya awali kwa huyo huyo kamishna waliyekwisha kukosana na atendewe haki? Pili, sheria inamtaka mlipa kodi alipe kwanza kodi aliyoamriwa na kamishna kiwango cha asilimia hamsini (50%), ili kesi yake iweze kusikilizwa. Yupo mlipa kodi ambae tayari amekisiwa na ameamriwa kulipa jumla ya kodi ya Tshs bilioni sita, maana yake ni kwamba anatakiwa alipe kwanza bilioni tatu ili asikilizwe, jambo ambalo milele haliwezekani. Mambo haya mawili yanamnyima uhuru na haki mlipa kodi, na tunapendekeza yaondolewe mara moja katika sheria ikiwa kweli tunataka ulipaji kodi wa hiari, (Voluntary compliance) wenye uwajibikaji (accountability) na usafi (transparency).
23) Umuhimu wa elimu ya kodi kwa walipaji na wakusanyaji hauhitaji kusisitizwa zaidi. Lililo muhimu ni uadilifu katika utendaji wa kazi zetu.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
ZNCCIA
Siku ya Mlipa Kodi
Zanzibar.
06/12/2011
Chanzo: Zanzinews

1 comment:

  1. Hizi ndizo hoja za nguvu, hakuna Kiongoza hata mmoja wa Tanganyika anaeweza kujibu, then huu ndio muungano na faida zake , mmoja mkubwa kumnyonya mdogo, ni choyo tu,

    ReplyDelete