NCHI yetu inaingia kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya. Tayari Bunge limepitisha muswada wa kuanzisha mchakato huo.
Moja ya mambo yanayoyumbisha nchi ni suala la Muungano usioeleweka.
Je, Katiba mpya itaweza kutatua kero hizo? Na ni zipi kero hizo?
Kama Wahenga walivyosema kwamba, “Kwa nahodha asiyejua bandari
aendayo, hakuna upepo ulio muafaka kwake”, ndiyo hali tulimo Watanzania
kwa sasa ya kutojua hatima ya Muungano wetu.
Na kwa sababu tumeibeza ramani ya Muungano, mambo mengi yanakwenda
kinyume kwa kishindo kikubwa. Baadhi ya hayo ambayo hapo kale
yalionekana kama dhambi kwa Muungano, sasa yanaonekana na kukubalika
kuwa si dhambi tena kutokana na uelewa wa abiria, baada ya kufichwa
ukweli kwa muda mrefu.
Kwa mfano, hapo kale, nani angekubali au kuamini kwamba Zanzibar
inaweza kuwa na wimbo wake wa Taifa, ngao ya Taifa, bendera ya Taifa na
Jeshi la Taifa?
Hapo kale, nani angeamini au kukubali kwamba Wazanzibari wanaweza
kuhoji muundo wa Muungano bila kutiwa kizuizini; au Rais wa Zanzibar
kukataa kauli za chama tawala (CCM) kwa mambo yanayogusa Katiba ya
Zanzibar, kama vile suala la Serikali ya Mseto, kama alivyofanya hivi
karibuni, Rais Abeid Amani Karume, kwa kubeza mapendekezo ya Tume ya
Halmashauri Kuu ya CCM, ikiongozwa na Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba,
na msimamo wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyoketi kijijini Butiama
mwaka jana?
Kama hapo kale, Rais wa Serikali ya awamu ya Pili Visiwani, Mzee
Aboud Jumbe Mwinyi, alivuliwa wadhifa huo na nyadhifa zote za Chama kwa
kutumia haki yake ya Kikatiba kuhoji muundo wa Muungano akidai kwamba
unapashwa kuwa Shirikisho, iweje leo Rais wa sasa, Amani Abeid Karume
na Wazanzibari kwa ujumla, wakiwamo kina Seif Sharif Hamad, wanaweza
kufanya hivyo bila ya kuadabishwa, wakati Katiba ya Muungano ni ile ile
iliyomng’oa Jumbe?
Hapo kale, nani angefikiria inawezekana, kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano kuteua wapinzani (kutoka CUF), kuingia katika Bunge la
Muungano; na kwa Rais wa Zanzibar vivyo hivyo?
Watanzania wamenyimwa fursa ya kuuona Mkataba, na hata Sheria ya
Muungano, ili kujua nini hasa kinasemwa au kinatakiwa kufuatwa chini ya
Mkataba huo.
Matokeo yake, tafsiri ya Muungano na kwa yale yanayotakiwa na
Muungano huo, wameachiwa wanasiasa kutafsiri wanavyotaka kwa manufaa
yao binafsi kama tabaka la Watawala, kama tutakavyoona katika makala
haya.
Rais Jumbe alitaka kutumia ibara hiyo hiyo ya Katiba kuhoji
Muungano, lakini ‘akatunguliwa’ kwa kishindo kikubwa; na hakuna
mwingine aliyethubutu kufanya hivyo baadaye. Ilikuwa dhambi hapo kale,
lakini si dhambi leo, chini ya Mkataba wa Muungano huo huo! Lazima
kuna mtu au watu waliojiona yeye au wao ndio Muungano, na Muungano
ndiye yeye au wao, lakini mambo sasa hayawezi kuwa hivyo tena kutokana
na uelewa wa umma juu ya kinachotakiwa chini ya Muungano.
Watanzania na Wazanzibari katika ujumla wao wanazidi na wataendelea
kuhoji tafsiri sahihi ya Muungano wao, hata kama watawala wataendelea
kuuficha Mkataba wa Muungano huo katika zama hizi za uelewa, demokrasia
na haki za binadamu; hasa wanapoona mambo kadha wa kadha ambayo
hayakutarajiwa, yakitendeka kwa mshangao wa wengi, kama nilivyoeleza
hapo mwanzo. Niharakishe kutamka hapa kwamba, kero za Muungano si za
kisiasa bali ni za kikatiba.
Wengi tunaamini kwa makosa kwamba Tanganyika na Zanzibar
zilipoungana, Aprili 26, 1964, ziliunda Muungano wa nchi inayoitwa
Tanzania. Ukweli ni kwamba, Muungano huo unajulikana kama “Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar”, na sio Tanzania. Hili ndilo jina la Muungano
linaloonekana katika Mkataba (Hati) wa Muungano huo wa Kimataifa wa
Aprili 22, 1964; na Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, ya kuridhia
Muungano kwa mabunge ya nchi hizo mbili. Je, jina “Tanzania” linatoka
wapi?
Miezi mitatu baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, lilitangazwa
shindano la kubuni jina lenye kuwakilisha hadhi ya Muungano na zawadi
ya pauni 10 za Uingereza kwa mshindi. Maombi yalipokelewa kutoka ndani
na nje ya nchi, zikiwamo Urusi, Uingereza, Sweden, China, Ufaransa,
Poland, Italia na Australia, ambapo jumla ya majina 1,534 yalipokelewa
na kushindanishwa.
Kati ya majina manne yaliyochuana hadi mwisho, ni pamoja na “Tanzania”, Tanzan, Tangibar na Zantan.
Akitangaza jina jipya Ikulu, mbele ya waandishi wa habari na namna
ya kulitamka, Oktoba 29, mwaka 1964, Rais Julius Kambarage Nyerere
alisema, jina hilo lilipitishwa na Baraza la Mawaziri Oktoba 28, 1964,
na litamkwe “Tan-zan-ia”, si “Tanzania”.
Ni kusema kwamba, hadi Oktoba 28,1968 hapakuwa na nchi iliyoitwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali kulikuwa na Jamhuri ya Tanganyika
na Zanzibar kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano. Wala hadi sasa hakuna
nchi au sehemu ya Tanzania iliyosajiliwa kuitwa “Tanzania Bara” au
“Tanzania Visiwani” kikatiba, bali kuna Tanzania na Zanzibar tu.
Tutaona baadaye chimbuko la ubatili huu.
Wakati nchi mbili hizi zikiungana, hapakuwa na Katiba kwa ajili ya
Jamhuri ya Muungano huo iliyoandaliwa. Kwa hiyo, ilikubaliwa chini ya
Mkataba wa Muungano kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika (ambayo
haikuuawa na Muungano) itumike pia kama Katiba ya mpito ya Muungano kwa
kufanyiwa marekebisho kuingiza mambo yote 11 ya Muungano (Angalia
Sheria ya Muungano ya 1964, kifungu cha 5).
Na kwa nini tunasema Tanganyika haikufa kufuatia Muungano? Katiba
ilikuwa wazi kwa hilo, kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 8, Sheria ya
Muungano; na ibara ya 5, Mkataba (Hati) wa Muungano, “Kuanzia siku na
baada ya siku ya Muungano, sheria za Tanganyika na zile za Zanzibar
zitaendelea kuwa Sheria za Tanganyika na za Zanzibar katika nchi hizo,
…”.
Maana yake ni kwamba, Sheria za Tanganyika na zile za Zanzibar kwa
mambo yasiyo ya Muungano ziliendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo,
pia kwamba, Tanganyika na Zanzibar hazikuuawa na Muungano, bali
zilibaki kama nchi ndani ya Serikali ya Muungano.
Chini ya ibara ya 8 ya Mkataba wa Muungano, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa makubaliano na Rais wa
Zanzibar, alitakiwa kuteua Tume ya kupendekeza Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, na hatimaye kuitisha “Bunge la Katiba”, likijumuisha
wawakilishi kutoka Tanganyika (sio Tanzania wala Tanzania Bara) na
kutoka Zanzibar, ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku ya Muungano, ili
kujadili na kupitisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, jambo ambalo
halikufanyika hadi mwaka 1977 ilipoteuliwa Tume ya kupendekeza
kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM ambapo, Tume hiyo, baada ya
kukamilisha kazi hiyo, ilijigeuza kuwa Tume ya kupendekeza Katiba ya
Jamhuri ya Muungano.
Kwa hili, ninawasilisha kwamba, Tume hiyo ilikuwa batili, kwa sababu
uteuzi wake haukuzingatia matakwa ya Mkataba wa Muungano, licha ya
kwamba muda wa mwaka mmoja wa Tume kama hiyo chini ya Mkataba wa
Muungano ulikuwa umepita. Wala Bunge halikuwa na mamlaka kutunga sheria
(Machi 24, 1965) Namba 18 ya 1965, kuongeza muda wa kuteuliwa kwa Tume
na kuitishwa kwa Bunge la Katiba “hadi hapo itakapoonekana inafaa na
vyema kufanya hivyo”.
Hilo ndilo lililokuwa kosa hatari la kwanza na ukiukaji wa Mkataba
wa Muungano uliofungua mlango kwa ukiukaji mwingine wa Mkataba kwa
miaka iliyofuata.
Kuongezwa kwa muda wa kuitisha Bunge la Katiba, kulimaanisha
kuchelewa kupatikana kwa Katiba halali ya Jamhuri ya Muungano; na kwa
sababu hiyo, Muungano uliondoshwa kwa vitimbwi na udikteta wa wanasiasa
walivyoona inafaa, na kwa njia ya Amri (Decrees) za Rais.
Hapo ndipo kuyumba kwa meli ya Muungano kulipoanzia na kwa manahodha
kulewa madaraka, wakidai Muungano hauwezi kuhojiwa na kufanya hivyo
ilikuwa sawa na uhaini.
Kutoteuliwa kwa tume na kutoitishwa kwa Bunge la Katiba kwa mujibu
wa Mkataba na Sheria ya Muungano, kulitokana na mifarakano ya dhahiri,
kati ya manahodha wa meli ya Muungano, Mwalimu Nyerere na Abeid Aman
Karume, baada ya kugunduana kwamba wasingeweza kupikwa chungu kimoja
wakaiva. Kuna wakati Karume alitamka wazi kwamba alikuwa amedanganywa
juu ya muundo wa Muungano; na katika hali ya kukata tamaa alidai kuwa
Muungano huo si kitu, akaufananisha na koti ambalo mtu likimbana aweza
kulivua wakati wowote.
Julai 10, 1965, Bunge lilipitisha Katiba ya Muda (Sheria Na 43 ya
1965) ya Tanzania, iliyotambua kwa mara ya kwanza kuwa “Tanzania ni
Jamhuri ya Muungano” (ibara ya 1) inayoundwa na Tanganyika na Zanzibar
(ibara ya 2), na kwamba, kutakuwa na chama kimoja cha siasa Tanzania
(ibara ya 3); “lakini, hadi hapo TANU na ASP vitakapoungana, chama cha
siasa kwa Tanganyika kitaendelea kuwa TANU, na kwa Zanzibar kitakuwa
ASP.
Katiba hii, kama tunavyosoma, bado iliendelea kutambua kuwapo kwa Tanganyika na Zanzibar kama nchi wabia wa Muungano.
Hata hivyo, Katiba hii ilivuka mipaka kwa kuingiza mambo ya vyama
vya siasa ambayo hayakuwa moja au sehemu ya mambo ya Muungano katika
Mkataba wa Muungano. Na kuanzia hapo, siasa ilichukua kiti cha mbele
badala ya Katiba katika kuongoza Muungano; na kwamba, badala ya kero za
Muungano kutatuliwa kwa mujibu wa Katiba, suluhisho lilitafutwa na
kufanyika kwa hisia za kisiasa chini ya dhana ya “chama kushika hatamu”
za uongozi.
Ninawasilisha kwamba, hatua ya kuingiza mamlaka ya vyama vya siasa
katika Muungano ilikuwa ya ukiukaji wa Mkataba wa Muungano wa Sheria ya
Muungano, kwa sababu vyama vya siasa halikuwa jambo au suala la
Muungano tangu mwanzo.
Ikumbukwe pia kwamba, wakati wakitia sahihi Mkataba wa Muungano na
Sheria za Muungano, waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere (Tanganyika) na Rais Abeid Amani Karume (Zanzibar), walifanya
hivyo kama marais wa Tanganyika na Zanzibar huru, na si kwa niaba ya
vyama vyao vya siasa, TANU na ASP.
Wasingeweza kutia sahihi Mkataba wa Muungano kwa niaba ya vyama vya
siasa kwa sababu hawakuwa na mamlaka (mandate) hayo, isipokuwa kama
marais pekee wa nchi zao.
Katiba ya muda ya 1965, iliandaliwa na Mwanasheria Mkuu (wa
Tanganyika), ikapitishwa na Baraza la Mawaziri la Muungano, kisha Bunge
la kawaida la Muungano na kutiwa sahihi na Rais wa Muungano, yote hayo
kinyume cha matakwa ya (hati) Mkataba wa Muungano, na pia sheria za
Muungano.
Haukupita muda, mara Serikali ya Muungano ilianza kunyemelea mambo
mengine yasiyo ya Muungano na kuongeza idadi ya mambo ya Muungano na
kuendelea kuyapunguza yasiyo ya Muungano hadi Tanganyika ikajikuta
imekuwa ndiyo Tanzania, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Ni hisia hizi za kisiasa zilizozaa Katiba inayoweza kuhojiwa mwaka
1977 na ambayo imeshindwa kutatua kero za Muungano na mtafaruku wa
kisiasa huko Zanzibar.
Katiba ya nchi haipashwi kutawaliwa na hisia za kisiasa, kwa sababu
si kila mwananchi ni mpenzi wa siasa. Katiba ya kweli lazima ilenge
kukidhi matakwa ya kila raia, bila kujali itikadi ya mtu; wala mtu
asiwekewe mipaka ya ushiriki wake katika mambo ya nchi na uongozi, kwa
maana huo ni ubaguzi kinyume na haki za raia. Katiba yetu ya sasa
imejikita katika hayo.
Lakini, kwa nini upungudu huo uliruhusiwa kuingia katika Katiba yetu? Au ni kwa sababu ya wanasiasa wasioambilika?
Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano ndiyo misingi mikuu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano, bila hivyo hakuna Katiba, Muungano wala
Zanzibar. Aidha, Bunge la kawaida la Muungano halina mamlaka ya
kurekebisha, kupunguza au kuongeza mambo ya Muungano yaliyofikiwa
kwenye Mkataba wa Muungano ambao hadi sasa unasomeka kama ulivyotiwa
sahihi na waasisi wake hapo Aprili 22, 1964.
Awali, Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, iliundwa
kushughulikia mambo 11 tu ya Muungano, na kuacha mambo mengine
yashughulikiwe na serikali huru za Tanganyika na Zanzibar, kila moja
kwa eneo lake. Hivi leo, mambo ya Muungano yamefikia 23 kwa njia ya
Amri za Rais (Decrees). Je, Rais, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, ana
mamlaka ya kuongeza au kupunguza mambo ya Muungano? Jibu ni “Hapana”.
Hakuna ubishi kwamba Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964
na Katiba ya mpito (Interim Constitution) ya 1964, zilitambua mwanzo
kuwapo kwa Serikali ya Muungano, Serikali hai ya Tanganyika na Serikali
hai ya Zanzibar; kila moja ikiwa na mamlaka kamili kwa mambo yasiyo ya
Muungano. Na hilo ndilo lilikuwa kusudio la Muungano chini ya mfumo
ulivyoundwa. Kama hivyo ndivyo, Tanganyika ilifia wapi na Zanzibar
ikasalimika?
Tatizo lilianza na Katiba ya muda ya 1965, ambayo, chini ya ibara ya
12 (1), ilibainishwa kinyemela kwamba, “Mamlaka ya utendaji (the
executive) kuhusu mambo yote ya Muungano katika, na kwa ajili ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na (pia) kwa Tanganyika,
yatakuwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano”.
Hii ni kusema kwamba, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu
Julius K. Nyerere, alifanywa kuwa Rais wa Serikali mbili - Serikali ya
Muungano na Serikali ya Tanganyika. Lakini isingekuwa hivyo, kama
Karume angekuwa Rais wa kwanza wa Muungano; yeye angekuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano na hapo hapo Rais wa Zanzibar na Nyerere kubakia
Rais wa Tanganyika.
Tunaamini kwamba, huu ulikuwa ni mpangilio wa muda tu kusubiri
Katiba ya Muungano; na pia kwamba Nyerere alikuwa hakwepeki kuhodhi
madaraka hayo kwa sababu Katiba ya Tanganyika ndiyo iliyokuwa pia
Katiba ya Muungano wakati akisubiri Katiba yake, kama nilivyoeleza
mwanzo.
Lakini utata huo ulizidi kuota mizizi pale, ibara ya 49 ya Katiba
hiyo ilipotamka kuwa, “Mamlaka ya kutunga Sheria kuhusu mambo yote ya
Muungano katika, na kwa ajili ya Muungano; na kwa mambo yote katika, na
kwa ajili ya Tanganyika, ni ya Bunge la Muungano”.
Hii ilimaanisha kwamba, Rais wa Muungano, sasa ndiye aliyekuwa pia
Rais wa Tanganyika; na Bunge la Muungano, ndilo lililokuwa Bunge la
Tanganyika na kinyume chake.
Kwa jinsi hii, Tanganyika, kwa ukarimu usio kifani, ilikuwa imetoa
kila kitu kilichokuwa chake juu na zaidi ya hisa ilizopashwa kuchangia
katika Muungano, tofauti na Zanzibar iliyotoa hisa 11, tu na kubakiza
mengine yote ndani ya mipaka yake, lakini ikaruhusiwa kutumbua vinono
vyote vya Tanganyika kwa mtaji mdogo wa hisa 11 tu.
Lakini kwa ukarimu huo, Tanganyika ilikiuka masharti ya Mkataba wa
Muungano, ambao uliitaka itoe/ichangie mambo 11 tu katika kapu la
Muungano, ili kutoifanya Zanzibar ijione kama mshiriki duni asiye na
sauti katika Muungano; au kama mgeni aliyekaribishwa tu kutumbua vinono
vingi vya mwenyeji wake. Huku ndiko Wazanzibari wanalalamikia
“kumezwa” na Tanganyika.
Lakini tofauti na Tanganyika, ambayo mamlaka yake yaligeuka kuwa ya
Kimuungano, mamlaka ya utendaji kwa Serikali ya Zanzibar yalibakia kwa
Rais wa Zanzibar, na yale ya kutunga Sheria kwa mambo yasiyo ya
Muungano, yalibakia kwa Baraza la Wawakilishi.
Tanzania ni jina lililosajiliwa kuwakilisha Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar, lakini jina halisia chini ya Mkataba na Sheria ya Muungano
linabakia kuwa “Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, bila kubadilika.
Ndiyo kusema kwamba, Tanzania ni kifupisho tu cha “Tanganyika na
Zanzibar”, kama vile Mwalimu Nyerere alivyowafundisha Watanzania
kulitamka kama “Tan-Zan-ia”, ili kutopoteza uwapo wa hadhi ya kila nchi
hizo katika Muungano. Lakini kwa nini jina “Tanganyika” lilipotea
miaka mitatu baada ya Muungano, wakati haikuwa hivyo tangu Muungano?
Kwa nini haikuwa dhambi kuwapo kwa Tanganyika hadi miaka mitatu
baadaye?
Tutatoa mfano: Katiba ya muda (ibara ya 2) ilitambua kwamba, “Eneo la Tanzania, linajumuisha Tanganyika na Zanzibar”.
Na kuhusu majimbo ya uchaguzi, ibara ya 25 ya Katiba hiyo, ilitamka
wazi kuwa, “Tanganyika itagawanywa katika majimbo mengi kadri ya idadi
ya wakazi wapiga kura, na kila jimbo litakuwa na Mbunge mmoja”.
Kuhusu wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, ibara ya 24 (1) (c),
ilitambua kuwamo kwa “Wakuu wa mikoa 17 wa kuteuliwa kwa mikoa 17
(wakati huo) ya Tanganyika, na watatu wa mikoa ya Zanzibar”, kuonyesha
kwamba Tanganyika na Zanzibar zilikuwa na mfumo wake wa utawala kwa
mambo yasiyo ya Muungano.
Kama Katiba hiyo ilitambua kuwapo kwa Tanganyika, nchi hiyo
iliyeyukia wapi, lini na kwa nini? Kwa nini kuyeyuka kwa Tanganyika
kusitafsiriwe kumaanisha mmoja wa wabia wa Muungano, Zanzibar, kukosa
mshirika katika Muungano kufuatia hatua hiyo? Je, Zanzibar imeungana na
nani - Tanganyika au Tanzania ambayo haimo katika Mkataba wa Muungano?
Kwa nini hatua hiyo isitafsiriwe kuwa ni kitendo cha kukatisha tamaa
(frustrate) au kuvuruga Muungano? Ni nani chanzo cha vurugu hii?
Msumari wa chuma ulipigiliwa kwenye kichwa cha Tanganyika kutokana
na kutungwa kwa Sheria Namba 27 ya 1967 na Bunge la kawaida, iliyompa
Rais uwezo wa kuweka neno “Tanzania” badala ya “Tanganyika” katika
Sheria zote, na mahali popote “Tanganyika” ilipoonekana, lakini bila
kugusa wala kubadili jina hilo katika Hati ya Mkataba wa Muungano na
Sheria ya Muungano, ambazo hata hivyo Rais hakuwa na mamlaka ya
kuzibadili kwa sababu, kwanza, Mkataba wa Muungano una hadhi ya
kimataifa usioweza kuguswa na Sheria za nchi; na pili, Sheria ya
Muungano ni tunda la Mkataba huo wa Kimataifa, ambapo kazi pekee ya
mabunge ya nchi hizo mbili huru ilikuwa ni kuridhia tu yaliyomo katika
Mkataba ili yapate nguvu ya kisheria kwa utekelezaji wa mambo yale 11
tu ya Muungano; na yasiyo ya Muungano yaendelee kushughulikiwa na
Serikali za nchi husika.
Mabadiliko yote haya, kuanzia na Rais kuahirisha kuteua tume ya
kupendekeza Katiba na kutoitisha Bunge la kupitisha Katiba kufikia
Machi 26, 1964; kutungwa kwa Katiba ya muda ya 1965, na sheria Na 24 ya
1967 iliyofuta kwa nguvu jina la Tanganyika; ndiyo yaliyoridhiwa bila
utafiti makini wa kisheria na kuingizwa katika Katiba ya kudumu ya
Jamhuri ya Muungano ya 1977, ambayo nayo hata hivyo, misingi na uhalali
wa kutungwa kwake inazua utata miongoni mwa wanasheria wa mambo ya
Katiba. Katiba hiyo ilikwenda mbali zaidi kwa kutoa “ubatizo” kwa
Tanganyika na kupewa jina la “Tanzania Bara”, na wakati huo huo mambo
yake yasiyo ya Muungano kuhamishiwa kwenye Muungano.
Ukweli ni kwamba, kuanzia hapo, Tanganyika ilifanywa kuwa ndiyo
Tanzania, na Tanzania kuwa ndiyo Tanganyika kwa jina jipya la “Tanzania
Bara”.
Mkanganyiko huu unathibitishwa pia na sheria ya tafsiri ya sheria na
vifungu vikuu (Interpretation of Laws and General Clauses Act) Namba
30 ya 1972, kifungu cha 3, ambapo neno “Jamhuri” limetafsiriwa kuwa na
maana ya “Jamhuri ya Tanganyika na inajumuisha Jamhuri ya Muungano”.
Tafsiri hii si tu kwamba inaifanya Tanganyika kuwa ndiyo “Jamhuri ya
Tanzania”, bali pia inafifisha jina la Tanganyika kwa upendeleo wa
jina kubwa la “Tanzania”. Ni kwa sababu hii sasa hakuna
“Watanganyika” ila kuna “Wazanzibari”; kuna Watanzania kwa maana ya
wakazi wa Bara.
Ndiyo maana sasa inavumilika kuona Zanzibar ina Rais wake, bendera
na wimbo wa Taifa; ngao ya Taifa na Jeshi ndani ya Muungano; lakini
Tanganyika haiwezi kuwa na hivyo vyote, ila kwa jina la Tanzania kwa
sababu imekuwa ndiyo “Tan-Zan-ia”.
Hili ndilo wanalolalamikia Wazanzibari, kwamba kitendo cha
Tanganyika kuingiza mambo yake yote yasiyo ya Muungano kuwa mambo ya
Muungano; kwanza ni cha ukiukaji wa Mkataba wa Muungano, na hivyo kilio
chao kwamba Zanzibar inamezwa na Tanganyika kinapata nguvu na
kusikika.
Kwa wasioyafahamu yaliyomo katika Mkataba wa Muungano, wanaweza
kushangaa kuona viongozi wa Zanzibar sasa wakijichukulia uamuzi wowote
bila hofu ya kuwajibishwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Uamuzi kama
vile Zanzibar kuwa na wimbo na bendera ya taifa; suala la mafuta; au
Rais wa Zanzibar kubeza baadhi ya uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM, ni
mambo yasiyokiuka Muungano, si kama tulivyoaminishwa siku za nyuma.
Wanafanya hivyo kwa sababu, wana uhakika kwamba hawavunji wala
kukiuka matakwa asilia ya mkataba na Sheria ya Muungano dhidi yale
yaliyoingizwa kwa ubabe.
Na kama kweli hatutapata akili na busara, tukakubali kupitia upya
msingi na matakwa ya Muungano, Zanzibar itaendelea “kusumbua” Muungano,
kero hazitakwisha hadi mwisho wa dahari.
Ni bahati mbaya kwamba viongozi wa nchi wamekuwa wazito na waoga
kuelezea historia sahihi ya Muungano, pengine kwa hofu ya kumwamsha
aliyelala, wasije wakalala wao. Lakini ni rahisi kuongoza au kutawala
watu wenye uelewa kuliko “waliolala”, kwani hao waliolala wakiamka,
wakafahamu kwamba wamedanganywa au wamehadaiwa au kupumbazwa kwa hila;
wanaweza kujeruhi, amani itatoweka.
Matarajio ya wengi sasa ni kwamba, Katiba mpya inayokusudiwa
kuandikwa kabla ya 2015, itaondoa utata na mkanganyiko huu ili Muungano
wetu uondokane na kero likuki zinazosumbua
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment