Saturday 24 December 2011

Dr Shein asifu invyofua walimu

DHAMIRA ya kuwa na walimu waliofuzu katika kiwango cha Shahada katika shule za sekondari
hapa Zanzibar itafikiwa kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali kwa sasa.

Hayo yalisema na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika Mahafali ya saba ya chuo hicho yaliyofanyika Kampasi ya Vuga.

Chuo hicho kilianzishwa miaka 10 iliyopita kwa lengo la kuinua taaluma ya ualimu.

Katika mahafali hayo ambapo pia, aliwatunukia Shahada za Heshima za Uzamivu za Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Salmin Amour Juma na Dk. Amani Abeid Karume kutokana na juhudi zao katika uanzishwaji wa chuo hicho pamoja na juhudi zao katika kuiletea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa Zanzibar.

Dk.Shein katika hotuba yake wakati akiwapa wahitimu 139 Shahada zao za Sanaa na Elimu
na 63 Shahada ya Sayansi na Elimu, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake katika
kuhakikisha chuo hicho kinatoa fani nyinginezo kama vile utalii, kilimo na udaktari na kueleza furaha yake kwa chuo kuanza kutoa wataalamu wa Fani ya Teknohama (IT).

Katika maelezo yake, Dk. Shein pia alishauri kwamba Shule ya Kiswahili na Lugha za Kigeni katika chuo kikuu hicho ikuzwe ili iwe mashuhuri kwa lugha hiyo duniani kama ilivyo kwa chuo kikuu cha Oxford, Uingereza kilivyo mashuhuri kwa lugha ya Kiingereza.

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Idrisa Ahmada Rai alieleza kuwa dhamira kuu ya chuo wakati kinaanzishwa ilikuwa ni kutayarisha walimu wenye sifa ili kukuza elimu ya msingi na sekondari Zanzibar, na baadaye kukitanua na kusomesha masomo mengine tofauti chuoni hapo.

Alisema kuwa ndani ya miaka 10 ya SUZA hilo limefanikiwa asilimia 100.

Chanzo: Habari leo

No comments:

Post a Comment