Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akizungumza katika viwanja vya Kibandamaiti
mjini hapa juzi alisema kuendelea kutegemea Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
kunainyima Zanzibar kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa ufanisi.
Aliuambia umati mkubwa uliojaa kwenye
viwanja hivyo kuwa wananchi visiwani humo wanaweza kudai haki ya
Zanzibar kuwa na benki kuu kwa njia ya kutoa maoni kupitia hatua
mbalimbali za mchakato unaoendelea juu ya Katiba mpya ya Tanzania.
Akizungumzia huduma za BoT kwa Zanzibar,
Maalim Seif alisema uwiano mbaya wa wafanyakazi kutoka pande mbili za
Muungano unasababisha upungufu wa wataalam wa kuishauri benki hiyo juu
ya mahitaji ya Zanzibar.
“Ikiwa kwa mfano BoT ina wafanyakazi 80
na wanne tu wanatoka Zanzibar, bila shaka uwiano huo ni mbaya katika
suala la utoaji vipaumbele kwa maendeleo ya visiwani,” alisema Maalim
Seif.
Alisema umuhimu kwa Zanzibar kuwa na
benki kuu yake sio jambo jipya, kwani hata awamu ya kwanza ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar iliweka wazi madai ya aina hiyo ikitaka kila
upande uwe na mambo yake katika masuala ya kibalozi, shughuli za polisi,
uraia na sarafu.
Alisema wakati wa kutoa maoni juu ya
Katiba mpya, pamoja na kudai haki ya kuwa na benki kuu, wananchi
waungane ili maoni yao yaweze kusaidia upatikanaji wa katiba
itakayoondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya
muungano.
Maalim Seif alisema ukosefu wa umoja
miongoni mwa wananchi katika suala la kudai maslahi ya Zanzibar ndani ya
Katiba mpya ni hatari kwa utaifa wao.
“Utakapofika wakati wa kutoa maoni
tusahau itikadi zetu, tuungane kulinda maslahi ya Zanzibar, vyama vya
siasa ni taasisi za kupita, ASP haipo, Tanu haipo na ZNP haipo, lakini
Zanzibar itaendelea kuwepo,” alisema.
Maalim Seif pia alisisitiza msimamo wa
kutaka Katiba mpya itakayoundwa iweke utaratibu unaoruhusu mzunguko wa
madaraka ya nafasi ya rais wa muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika.
“Mwandishi mmoja wa habari juzi alitaka
nieleze maslahi ya Zanzibar ninayowahimiza wananchi kudai yawekwe ndani
ya Katiba mpya, nikamwambia mfumo wa sasa wa uchaguzi umesbabisha nafasi
ya rais wa muungano kubaki bara kwa muda mrefu,” alisema Maalim Seif
akiwa anarejea jibu alilotoa katika mkutano wake na waandishi wa habari
baaya kuulizwa swali hilo na Muhibu Said, Mwandishi wa habari mwandamizi
wa NIPASHE.
Akifafanua zaidi haja ya kuwepo utaratibu
wa kikatiba unaoruhusu nafasi hiyo kutolewa kwa mzunguko, Maalim Seif
alisema chini ya mfumo wa uchaguzi uliopo Zanzibar imeshika nafasi hiyo
kwa miaka 10 tu wakati Tanzania bara imehodhi wadhifa huo kwa miaka 35.
Alisema hiyo ni kasoro katika uendeshaji wa serikali ya muungano iliyoundwa na mataifa mawili ambayo ni nchi.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment