Thursday 29 December 2011

Zanzibar iwe na Benki kuu yake: Maalim Seif

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema ni muhimu kwa sasa Zanzibar kuwa na benki kuu yake ikiwa inataka kutumia kikamilifu rasilimali zake kujenga uchumi wake.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akizungumza katika viwanja vya Kibandamaiti mjini hapa juzi alisema kuendelea kutegemea Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kunainyima Zanzibar kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa ufanisi.  

Aliuambia umati mkubwa uliojaa kwenye viwanja hivyo kuwa wananchi visiwani humo wanaweza kudai haki ya Zanzibar kuwa na benki kuu kwa njia ya kutoa maoni kupitia hatua mbalimbali za mchakato unaoendelea juu ya Katiba mpya ya Tanzania.  

Akizungumzia huduma za BoT kwa Zanzibar, Maalim Seif alisema uwiano mbaya wa wafanyakazi kutoka pande mbili za Muungano unasababisha upungufu wa wataalam wa kuishauri benki hiyo juu ya mahitaji ya Zanzibar.  

“Ikiwa kwa mfano BoT ina wafanyakazi 80 na wanne tu wanatoka Zanzibar, bila shaka uwiano huo ni mbaya katika suala la utoaji vipaumbele kwa maendeleo ya visiwani,” alisema Maalim Seif.  

Alisema umuhimu kwa Zanzibar kuwa na benki kuu yake sio jambo jipya, kwani hata awamu ya kwanza ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliweka wazi madai ya aina hiyo ikitaka kila upande uwe na mambo yake katika masuala ya kibalozi, shughuli za polisi, uraia na sarafu.  

Alisema wakati wa kutoa maoni juu ya Katiba mpya, pamoja na kudai haki ya kuwa na benki kuu, wananchi waungane ili maoni yao yaweze kusaidia upatikanaji wa katiba itakayoondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya muungano.  

Maalim Seif alisema ukosefu wa umoja miongoni mwa wananchi katika suala la kudai maslahi ya Zanzibar ndani ya Katiba mpya ni hatari kwa utaifa wao.  

“Utakapofika wakati wa kutoa maoni tusahau itikadi zetu, tuungane kulinda maslahi ya Zanzibar, vyama vya siasa ni taasisi za kupita, ASP haipo, Tanu haipo na ZNP haipo, lakini Zanzibar itaendelea kuwepo,” alisema.  

Maalim Seif pia alisisitiza msimamo wa kutaka Katiba mpya itakayoundwa iweke utaratibu unaoruhusu mzunguko wa madaraka ya nafasi ya rais wa muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika.  

“Mwandishi mmoja wa habari juzi alitaka nieleze maslahi ya Zanzibar ninayowahimiza wananchi kudai yawekwe ndani ya Katiba mpya, nikamwambia mfumo wa sasa wa uchaguzi umesbabisha nafasi ya rais wa muungano kubaki bara kwa muda mrefu,” alisema Maalim Seif akiwa anarejea jibu alilotoa katika mkutano wake na waandishi wa habari baaya kuulizwa swali hilo na Muhibu Said, Mwandishi wa habari mwandamizi wa NIPASHE.  

Akifafanua zaidi haja ya kuwepo utaratibu wa kikatiba unaoruhusu nafasi hiyo kutolewa kwa mzunguko, Maalim Seif alisema chini ya mfumo wa uchaguzi uliopo Zanzibar imeshika nafasi hiyo kwa miaka 10 tu wakati Tanzania bara imehodhi wadhifa huo kwa miaka 35. 

Alisema hiyo ni kasoro katika uendeshaji wa serikali ya muungano iliyoundwa na mataifa mawili ambayo ni nchi.
Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment