Keneth Goliama
TANZANIA imekataa Shirikisho la Ulinzi, Siasa
pamoja na Kinga za Viongozi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kutaka mambo hayo kujadiliwa kwa upana zaidi kuhusu uundwaji wake
ili wananchi waweze kushirikishwa kutoa maoni yao.
Hata hivyo
Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki, wamekubaliana kwa pamoja kuunda
Sekretarieti maalum ya Watalaam wa kufuatilia mchakato mzima wa maoni
ya watu ili waweze kuyawasilisha katika mkutano ujao.
Katika
mkutano huo pia kumependekezwa kuanzishwa kwa Benki Kuu Umoja wa
Jumuiya ya fedha, Bunge la Jumuiya lenye uwakilishi wa Kisiasa ,
Mamlaka ya Uangalizi, mahakama ya Jumuiya Afrika mashariki
itakayosimamia na kuhakiki mikataba .
Akizungumza na waandishi
wa habari , Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki , Dk
Stergomena Tax alisema Tanzania haijakubaliana na Uundwaji wa
Shirikisho la kisiasa , Ulinzi na Ardhi kwa madai kuwa masuala hayo
yanahitaji muda zaidi wa kujadiliwa na wadau husika wa Jumuiya.
Aliyataja
mambo mengine yaliyokubaliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Baraza la Mawaziri kuwa ni pamoja na Sera ya mkakati wa uendelezaji wa
viwanda, Kuimarisha Huduma ya Forodha, Itifaki ya kuzuia na kupambana
Rushwa sambamba na Itifaki ya kinga na hadhi ya jumuiya zilizopo chini
ya Jumuiya.
Dk .Tax Alisema suala la Ulinzi Shirikishi na siasa
katika mkutano huo liliibua mjadala mzito na kuonekana kuwa changamoto
inayohitaji kufikiriwa kwa makini ili kuepusha nchi husika kuingia
katika migogoro baina ya nchi na nchi pale zitakapo pingana .
“Nikitolea
mfano mambo ya vita katika kushirikiana na kusaidiana na nchi
inayopigwa ndani ya Jumuia ya Afrika mashariki linatakiwa kujadiliwa
kwa kina na kufanyiwa marekebisho ili kujua mambo gani muhimu
yatakayohusika katika Ulinzi ili kuweza kujulikana na kukubaliana”
alisema Dk Tax.
Katika Mkutano huo Tanzania imeteuliwa kuwa
Mwenyeji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika mashariki ambaye Makao
Makuu yake yatakuwa Zanzibar huku Rwanda ikichaguliwa kuongoza Kamisheni
ya Sayansi naTeknolojia na Burundi ikiongoza Kamisheni ya Utafiti wa
Afya.
Alisema upataji wa wenyeji huo unatokana na Tanzania kuwa
mwombaji pekee sambamba na kuomba nafasi zingine za Afya na Sayansi na
Teknolojia ambazo haikufanikiwa badala yake ilionekana kuwa na sifa
katika Kamisheni ya Kiswahili.
Alisema kwa kupata nafasi hiyo
Tanzania itanufaika kwa kiasi kikubwa katika kuinua Uchumi wake kutokana
na kuwepo kwa soko huria katika sekta za biashara ,viwanda na
uwekezaji katika kupunguza vikwazo vya uchumi.
Katika kongamano
la Jumuia ya Afrika mashariki kuhusu Maendeleo ya Bonde la ziwa
Tanganyika, Katibu huyo alisema , walijadili nchi wanachama kuvutia
biashara na kuongeza uwekezaji katika nchi wanachama ili kutumia
maliasili nyingi zilizopo kwaajili ya kuinua uchumi.
Dk Tax
alisisitiza kuwa Tanzania haina budi kulipeleka Suala la Ardhi, Ulinzi,
Siasa kwa wananchi ili walijadili zaidi kwani matokeo ya awali
yalionyesha kuwa asilimia 75 ya Watanzania walikataa uharakishwaji wa
uundwaji Shirikisho hilo .
Dk Tax alisema nchi wanachama
zinatakiwa kupima Ardhi na kuanzisha vyombo vya msingi vinavyotoa haki
ya umiliki wa ardhi kwa wananchi , Kusimamia mgawo wa faida, na
gharama za mali asili kuwa sehemu ya majadiliano katika mkataba wa
uundwaji wa shirikisho la kisiasa.
Kuhusu maombi ya uanachama wa
Nchi za Sudan Kusini na Sudan Kaskazini , alisema majadiliano hayo
yalifanyika na kwamba Sudan Kaskazini ilikosa vigezo vya kujiunga
kutokana na umbali uliopo katika mipaka na nchi wanachama .
Alisema
Sudan Kusini ilikidhi katika ibara ya tatu ya vigezo vya kujiunga
lakini majadiliano zaidi yanaendelea ili kuhakikisha wanapata mwafaka
zaidi katika kuweza kujiunga
Chanzo: Mwananchi
Jee Wazanzibari tunashirikishwa kwenye haya maamuzi ya East African community, kwani sisi ndio victim wakubwa hivi sasa hoteli zote zimejaa wafanyakazi wa kikenya na kiganda na watanganyika tunahitaji kuwa na sera maalum za uhamiaji kwanza kutokana kwamba visiwa vina ukomo, watanganyika wana ardhi mamilioni ya ekas lakini bado wanakuwa wagumu kuingia kwenye ushirika wa ardhi wazanzibari vipi?
ReplyDelete