MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema
Zanzibar inataka kuwepo kwa muundo ambao utagawa zamu ya nafasi ya Urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika katiba.
Maalim alisema Zanzibar haifurahishwi na mfumo wa sasa ambapo Rais anatoka sehemu moja tu ya muungano ambayo ni Tanzania Bara.
“Kipaumbele chetu katika marekebisho ya katiba tunataka kuwepo kwa
muundo utakaoonesha na kutamka wazi wazi muda wa zamu ya urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...Zanzibar ni sehemu inayounda muungano
huo,” alisema.
Seif alisema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari hapo
katika ukumbi wa baraza la wawakilishi la zamani ambapo alizungumzia
mafanikio ya serikali ya umoja wa kitaifa tangu kuundwa mwaka jana.
Alisema kuwepo kwa utaratibu unaotambuliwa kisheria kwa kiasi
kikubwa utasaidia kujua kipindi hichi rais anatoka kutoka katika upande
upi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maalim alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa
haifurahishwi na utaratibu uliopo sasa ambapo rais wa Jamhuri ya
Muungano anatoka Tanzania Bara tu na Zanzibar kubaki na nafasi ya Makamu
wa Rais.
Kwa mara ya mwisho, Zanzibar ilitoa Rais wa serikali ya Muungano,
Mzee Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985 aliyekaa madarakani hadi mwaka 1995
alipompisha Benjamin Mkapa.
Hata hivyo, Maalim aliwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa
wingi wakati muda utakapofika wa kutoa maoni ya marekebisho ya katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa ujumla alisema Zanzibar imejizatiti katika marekebisho hayo
kuona kwamba maslahi ya Zanzibar katika mchakato huo yanazingatiwa kwa
umakini mkubwa.
Alitoa mfano wa visiwa vya Comoro ambapo katika katiba yake vimeweka
bayana kwamba mwaka huu raia anatoka kisiwa kimoja na katika uchaguzi
unaofuata, raia anatoka kisiwa kingine.
“Utaratibu kama huo ndiyo unaokubalika ambao unataja wazi wazi mwaka
huu rais anatoka wapi hatua ambayo ni nzuri kwani inasaidia kuondosha
malalamiko ya muungano,” alisema Maalim.
Chanzo: Habari leo
Mara hii ni zamu yetu jamani urais, hao akina lowasa na wenzake wanaojikomba kwa makanisa waache mtindo huo
ReplyDelete