Tuesday 6 December 2011

Waziri ang`aka

Na Muhibu Said    

Ahoji Uingereza wameshitaki wangapi kwao
Ni kwa wabunge wake kutaka washitakiwe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe
Serikali haijaonyesha nia ya kuwashtaki watuhumiwa walioko nchini wanaohusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi licha ya kundi la wabunge wa Uingereza kutaka wahusika wa kashfa hiyo washtakiwe.
Msimamo huo wa serikali ya Tanzania, umedhihirika baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, kuwajia juu wabunge hao wa Uingereza kwa kuwataka waeleze idadi ya
wahusika wa kashfa hiyo walioko nchini mwao waliokwisha kufikishwa mahakamani, kabla ya kuwanyooshea kidole watuhumiwa walioko Tanzania.
Chikawe alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE, kueleza msimamo wa serikali ya Tanzania kuhusiana na wito wa wabunge hao kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini Uingereza, kutaka wahusika wa kashfa hiyo washtakiwe.
Kabla ya Chikawe kujibu swali hilo, alihoji rada hiyo ilinunuliwa na nani na kwa fedha za nani.
Alipojibiwa kuwa ilinunuliwa na serikali ya Tanzania na kwa fedha zake, Chikawe alisema: “Wapigie (simu) hao wabunge wa Uingereza uwaulize ni wangapi kwao wamewapeleka mahakamani?”
Chikawe alisema anasema hivyo kwa vile kashfa ya ununuzi wa rada inagusa orodha ya watu wengi nchini humo.
“Wao wanajua Tanzania tu. Achana nao,” alisema Waziri Chikawe kisha akakata simu.
Wito wa kutaka kufunguliwa mashtaka dhidi ya mtu yeyote aliyehusika katika kashfa ya ufisadi na rushwa kuhusiana na mauzo ya rada hiyo kwa Serikali ya Tanzania yaliyofanywa na kampuni ya vifaa vya ulinzi ya BAE Systems ya Uingereza mwaka 2002, ulitolewa na wabunge hao, Desemba Mosi, mwaka huu.
Wabunge hao walisema wako tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika mahakama zake kuendesha mashtaka dhidi ya watu wanaohusika na ulaghai huo.
Miongoni mwa wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa hiyo, ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Chenge anatuhumiwa kumiliki Dola za Marekani milioni 1 (Sh. bilioni 1.2) kwenye akaunti yake iliyoko katika Kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.
Alikutwa na kiasi hicho cha fedha mwaka 2008, kufuatia uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO).
Chenge amekanusha fedha hizo kuwa na uhusiano wowote na fedha za rada, ameweka wazi kuwa ni jasho lake kwa kazi za uwakili na urithi wa familia yake.
Chenge, ambaye wakati wa ununuzi wa rada hiyo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), anatuhumiwa kuwa kiungo muhimu katika ununuzi wa rada kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya BAE Systems.
Baada ya kukutwa na kiasi hicho kikubwa cha fedha zenye utata alichokiita “vijisenti”, kuliibuka shinikizo kubwa kutoka kwa watu wa kada tofauti nchini wakitaka akamatwe na kushitakiwa.
Julai 21, mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, alitangaza hadharani mjini Arusha kwamba, Chenge atashtakiwa chini ya kifungu cha 27 Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007.
Sehemu ya kifungu hicho cha sheria, inaainisha kuwa mtu akiwa na mali, ambazo hazilingani na kipato chake alichokipata akiwa madarakani au baada ya kuondoka, ni kosa kisheria.
Dk. Hoseah, alisema kama Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) atalipitisha jalada la Chenge, mbunge huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote.
Kashfa ya kuwa na fedha hizo katika akaunti ya nje, ndiyo ilimwondoa Chenge katika wadhifa wa Uwaziri wa Miundombinu mwaka 2008, baada ya gazeti la Guardian la Uingereza kufichua kuwa alikuwa akimiliki kiasi hicho cha fedha.
Dk. Hoseah akifafanua zaidi mchakato huo mzito wa kisheria, alisema ni Watanzania wachache mno wanaoweza kuwa na akiba ya fedha kiasi kama hicho nje ya nchi au mahali kokote.
Alisema jambo hilo ndilo lililowasukuma kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo za Chenge.
Kuhusu kuhusika kwa Chenge katika kashfa ya rada baada ya Mahakama Kuu Uingereza kuamuru BAE Systems kurejesha sehemu ya fedha kwa Tanzania kutokana na kubaini kutokuwekwa kwa rekodi za kiuhasibu sawasawa hasa katika fungu la kamisheni kwa waliofanikisha biashara hiyo, Dk. Hoseah, alisema Chenge hahusiki na kwamba, hakuna ushahidi wowote wa kumtia hatiani.
Kwa mujibu wa Dk. Hoseah, waliohusika na kashfa hiyo tayari wameshatajwa na hata washiriki wao wanajulikana, wakiwamo raia wa Uingereza.
Kutokana na kashfa hiyo, Chenge, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja watuhumiwa wa ufisadi, ambao wanatakiwa kujivua gamba.
Kampuni ya BAE Systems tayari imekubali kulipa takriban dola za Marekani milioni 46 kama fidia kwa Tanzania kwa kukosa kuweka kumbukumbu zake za mahesabu sawa kuhusiana na mauzo hayo ya rada yenye utata.
UINGEREZA YAIWEKEA MASHARTI TANZANIA
Katika hatua nyingine, Uingereza imeiwekea masharti serikali ya Tanzania kabla ya kuipatia fedha zilizozidi “chenji” kwenye ununuzi wa rada kwa kuitaka kupeleka kiasi hicho cha fedha kwenye sekta, ambayo itawanufaisha wananchi wote.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alithibitisha kuwapo kwa masharti hayo na kuongeza kuwa baada ya serikali kuyapata iliamua fedha hizo zitakapolipwa zipelekwe kwenye sekta ya elimu.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkulo, alisema mazungumzo kuhusiana na urejeshwaji wa “chenji” hiyo yamekamilika na kinachosubiriwa ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuainisha maeneo, ambayo yanahitaji kusaidiwa katika sekta ya elimu.
“Serikali ya Uingereza inatusubiri sisi kila kitu kipo tayari na sisi tukimaliza kuainisha maeneo tunayohitaji kuyasaidia kwenye sekta ya elimu watatuletea fedha hizo,” alisema Mkulo.
Alisema serikali ya Uingereza imeihakikishia Tanzania kwa maandishi kwamba, italipwa fedha hizo na zitakapoingia nchini zitatumika kwa ajili ya elimu pekee.
“Tumeshapata barua kutoka Serikali ya Uingereza kwamba, serikali ya Tanzania italipwa Paund milioni 29.50,” alisema.
Waziri Mkulo alisema utaratibu huo unafanywa kati ya serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Fedha hizo zinarejeshwa nchini baada ya BAE iliyouzia Tanzania rada hiyo kwa bei kubwa kuliko bei halisi na baada ya kukiri mahakamani Uingereza kosa la kuzembea katika uwekaji kumbumbu za kiuhasibu na amri ya kulipa kiasi hicho kama faini kuridhiwa.
BAE iliiuzia Tanzania rada hiyo kwa dola za Marekani milioni 40 hatua iliyopingwa na watu wengi, wakiwamo wanaharakati.
Mbali na Chenge, raia mwingine wa Tanzania ambaye anatuhumiwa katika kashfa hiyo ni Sailesh Vithlanmbali ambaye alikuwa mtu wa kati katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. Haya jamani hawa ndio viongozi ambao tunaambiwa wana imani na wananchi wao, Uingereza wao ndio ambao wamefaidika na mradi huu na kwa imani yao tu wametushtuwa kuwa tumeibiwa na waliosababisha wapo hapa petu leo waziri anamwambia mtu ambae katuonesha mwizi kuwa mbona wewe nawe unaibiwa na huwakamati, kamata wako kwanza ndipo uje uniambie niwakamate wezi wangu
    Hichi kichekesho

    ReplyDelete