Thursday 22 December 2011

Viongozi wanachochea uvunjaji sheria Zanzibar - Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema uvunjaji wa sheria unachochewa na baadhi ya viongozi kuwabeba wawekezaji kujenga vitenga uchumi katika maeneo yasiyoruhusiwa kimazingira.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya mwaka mmoja tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Novemba, mwaka jana.

Akitoa mfano Maalim Seif alisema Hoteli ya Zanzibar Ocean View, imejengwa katika eneo ambalo kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, haliruhusiwi kuanzishwa kwa ajili ya mradi huo.

Alisema anashangaa kwamba hata baada wataalamu kuzuia eneo hilo kwa mradi huo, hoteli hiyo ilijengwa baada ya wamiliki kubebwa na viongozi wazito serikalini.

Mfano mwingine wa uvunjaji wa sheria za mazingira alisema ni ujenzi wa hoteli ya kitalii ya Misali ambayo imejengwa kinyume na Sheria za Uhifadhi wa mazingira kisiwani Pemba.

Alisema hoteli hiyo imejengwa karibu na kituo cha kuhifadhi mafuta ya aina mbalimbali pia karibu na Kituo cha umeme cha Wesha ambacho hupokea nishati hiyo kutoka gridi ya taifa kupitia waya uliotandikwa chini ya bahari kuanzia mkoani Tanga.

Maalim Seif alisema hata wataalamu wa mazingira wanaposhauri miradi inayokiuka uhifadhi wa mazingira ivunjwe maamuzi yao yamekuwa hayazingatiwi kutokana na wawekezaji hao kulindwa na vigogo serikalini.

Alisema kitendo hicho ni cha hatari kwa sababu kina hatarisha usalama wa wananchi na mpango mzima wa uhifadhi wa mazingira pamoja na kwenda kinyume na misingi ya utawala wa sheria.

Alisema wapo wawekezaji ambao wamediriki kujenga ndani ya fukwe za bahari tofauti na maelekezo ya kisheria kwamba miradi kama hiyo ijengwe umbali wa mita 30 kutoka ufukwe wa bahari.

Alisema kitendo cha baadhi ya viongozi kuwaruhusu wawekezaji kuvunja sheria hatimaye kitakuwa na madhara katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema licha ya kuhatarisha uhifadhi wa mazingira, ujenzi vitenga uchumi fukweni pia umeibua migogoro mikubwa kati ya wavuvi wadogo wadogo na na wawekezaji walioanzisha miradi yao katika fukwe.

Aidham alisema wakati umefika kwa wananchi wa kuongeza uwajibikaji katika kulinda na kuhifadhi mazingira hasa kwa kujiepusha na vitendo vya ukataji miti ya mikoko, uchimbaji wa mchanga na matumizi mabaya ya fukwe za bahari.

Alisema katika kupambana na tatizo la uchafuzi wa mazingira ikiwemo kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki, serikali imeunda kamati maalum ya kuwasaka wanaoingiza mifuko hiyo kutoka nje ya nchi na wanauza kwa wananchi kwa rejareja.

Hata hivyo, alisema adhabu ya faini ya Sh. milioni 10 kwa mtu anayepatikana na kosa la kuwa na mfuko mmoja wa plastiki na Sh. milioni 10 kwa mtu anayetiwa hatiani kwa kuwa na shehena ya mifuko hiyo inahitaji kuangaliwa upya utekelezaji wake.

Alisema kwa msingi huo serikali imeamua kuiangalia upya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwakamata wananchi wanaotumia mifuko hiyo na kuwafikisha mahakamani kutokana na kuwa tayari imepigwa marufuku matumizi yake

Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment