Monday 5 December 2011

UZALENDO UWE MBELE MJADALA KATIBA MPYA - JAJI MKUU MAKUNGU

Na Mwantanga Ame

WAKATI watanzania wakisubiri kuanza kwa mjadala wa kuandikwa kwa katiba mpya, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amewetaka wananchi kuweka mbele mjadala wa uwazi kwa kuzingatia hoja zenye kujenga uzalendo wataposhiriki kutoa maoni yao wakijadili kupatikana katiba mpya.

Jaji Makungu, aliyasema hayo jana wakati akitoa hotuba yake katika kumbukumbu ya Profesa Haroub Othman Miraji iliyoandaliwa na kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, iliyofanyika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mkunazini Mjini Zanzibar.


Jaji Makungu alisema Profesa Haroub Othman Miraji katika uhai wake alikuwa ni miongoni mwa alieanzisha wazo la kupatikana kwa katiba mpya na ili kuweza kumuenzi vyema mawazo yake hayo Wazanzibari watapaswa kuona wanaweka mbele mjadala wa uwazi kwa kuzingatia kutoa hoja zenye kujenga uzalendo.

Alisema hivi sasa serikali imeanzisha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya kwa dhamira njema na lazima wananchi wataposhiriki kutoa maoni wahakikishe wanatumia vyema fursa hiyo kwani ndio mustakbali wa taifa kwa kuchagua mambo yepi wanayoyataka.

“Naomba tujadili kwa kina, uwazi na kuweka uzalendo mbele kuliko chengine chochote kwani mjadala wa katiba mpya ni fursa muhimu kwetu hasa Wazanzibari kwani ndio itayotuletea mustakbali mzuri ule tunaoutaka” Alisema Jaji Makungu.

Alisema jambo la msingi kwa wanajamii kuona wanajiandaa zaidi kuwa na hoja zitazokuwa na majibu badala ya mtindo wa sasa wa baadhi ya watu kutoa hoja zinazokataa mambo lakini wanashindwa kuelekeza namna vipi wanavyotaka liwe.

Akiendelea Jaji Makungu, alisema wakati wakiwa na kumbukumbu ya Profesa haroub Serikali bado inathamini mchango wake alioutoa katika uhai wake, kwani ameiwezesha taasisi ya Mahakama kukabiliana na changamoto mbali mbali katika kusimamia haki na sheria.

Alisema moja ya mchango huo ni pale alipoiomba ofisi ya Katiba na Sheria kuanzisha siku ya sheria Zanzibar, ambayo ikiwa na lengo la kuwakutanisha wadau wa sheria waweze kutathmini kazi zao na kufahamu mabadiliko na changamoto zilizomo katika sekta hiyo.

Alisema kutokana na wazo hilo tayari Wizara ya sheria imeamua kuiweka Mwezi Febuari kuwa siku ya sheria Zanzibar ambapo mwakani itaanza kuadhimishwa rasmi.

Alisema mawazo ya Profesa Haroub yalikuwa ni mengi katika kuimarisha utawala wa sheria likiwemo suala la haki za binadamu na ndio maana aliamua kuanzisha kituo kwa ajili kuwasaidia watu wenye matatizo ya kisheria ambao hawakuwa na uwezo wa kuajiri wakili kwa ajili ya kesi zao.

Alisema kuwepo kwa kituo hicho kutaweza kutoa msaada mkubwa kwa Wazanzibari wasiokuwa na uwezo wa kuajiri wanasheria katika kesi zao.

Hata hivyo alikiomba kituo hicho kuendeleza kumbukumbu hiyo kwa kuhakikisha wanakiendeleza kituo hicho ili jamii ya wazanzibari iweze kufaidika nacho jambo ambalo litaweza kumuenzi kwa vitendo muasisi huyo.

Mapema mmoja wa wanafamilia ya marehemu huyo Adalla Miraji, akitoa salamu za familia alisema wamefarajika kuona serikali ya Tanzania kulikubali wazo la kiongozi huyo wa familia yao kwani imethamini mchango wake katika kuliimarisha Taifa la Tanzania.

Alisema kuwepo kwa mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ni wazo zuri lakini watanzania watapaswa kutambua kuja kwa mchakato huo bado hakuondoi amani ya Tanzania kwa kuanzisha mijadala itayokuwa inaanzisha jazba zitazochafua amani.

Alisema dhamira ya viongozi hao kuomba katiba ya Tanzania kuandikwa upya haina nia mbaya kwa watanzania na wataoendesha mijadala hiyo kwa dhamira ya kuchafua amani watakuwa hawakuwatendea haki waasisi wa wazo hilo.

“Katiba ni kitu muhimu inahitajika tutumie busara zaidi na sio jazba kwani inaweza kusababisha lengo lisifikiwe tusijenge mazingira ya kuwagawa watu mshikamano uliopo tuuendeleze na sio tunyosheane vidole wakati tutapokuwa tukiotoa maoni kwa kumuona mtu hafai hili tutakuwa hatuwatendei haki walioanzisha wazo hili” alisema Miraji.

Akiendelea alisema jambo la msingi ambalo jamii watapaswa kuona wanajiandaa nalo ni kuona wanajenga mshikamano kwa kuandaa hoja ambazo zitaiwezesha Zanzibar kukaa sehemu nzuri katika mazingatio bora ya Katiba mpya.

Hata hivyo mwanafamilia huyo, aliiomba taasisi hiyo kuona inajiandaa kwa kuweka mazingira bora ya utoaji wa elimu ya uraia kuhusu Katiba iliyopo kutokana na hivi sasa bado kuna watu ambao hawaifahamu.

Na Mwenyekiti wa Kituo hicho, Profesa Chris Peter Maina, akitoa maelezo yake alisema ingawa ameteuliwa kufanya kazi katika shirika la kimataifa, bado mchango wake utaendelea kuwepo katika kukuza kituo hicho ikiwa ni hatua ya kumuenzi mwanzilishi wa taasisi hiyo.

Alisema taasisi ya huduma za Sheria imekuwa ni yenye mchango mkubwa kwa wazanzibari ambapo hivi sasa wameanzisha utoaji wa huduma za sheria katika majimbo 50 ya Zanzibar pamoja na vikosi Maalum vya SMZ ambapo watu 65 wanaifanya kazi hiyo.

Alisema hivi sasa wanajiandaa kuutekeleza mradi mkubwa wa kituo hicho hapo mwakani utaokuwa unahusu uandishi wa kitabu ambacho kitakuwa kikionesha kesi zote zitazokuwa zimefikishwa mahakamani, zilizotolewa uamuzi na sheria zote zitazokuwa zimepitisha na serikali.

Wakati wa mjadala wa katiba wanahitaji kuzingatia kuwa na nia njema kwa kuhakikisha hawajadili suala hilo kwa kuangaliana na mchango mtu anayoyatoa.

Jumla ya mada tatu zilijadiliwa katika kumbukumbu hiyo ikiwemo inayohusu uhuru wa Mahakama na Katiba mpya iliyotolewa na Mwanasheria Yahya Hamad, ambapo alisema inaonekana bado haijatulia kutokana na baadhi ya wakati kuingiliwa maamuzi yake.

Mada nyengine ilihusu ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ya Tanzania iliyowasilishwa na Marcus Albani, ambaye alisema kutambua katiba ndio nyenzo ya kuendesha nchi na viongozi wazuri lazima waifuate katiba.

Nae Rais wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Said, akitoa mada juu ya Katiba mpya ya Tanzania maeneo ya migongano na makubaliano baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, alisema migogoro katika Muungano sio jambo jipya kwani imeanza tangu Muungano ulipoanza lakini kinachotakiwa kufanyika ni kuona kunakuwa na majadiliano kila pale wanapoona inafaa kufanywa hivyo

No comments:

Post a Comment