Pia pande mbili hizo zimekubaliana CUF
iwasilishe mapendekezo rasmi serikalini ya namna ya kurekebisha sheria
hiyo pamoja na mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Makubaliano hayo yalifikiwa na pande mbili
hizo katika kikao cha pamoja kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es
Salaam, Desemba 2, mwaka huu.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara,
Julius Mtatiro, alisema katika kikao hicho, walimkabidhi Rais Kikwete
mapendekezo na maoni, kuhusu namna bora ya utekelezaji wa sheria hiyo.
Maeneo hayo ni pamoja na uteuzi wa
Makamishna wa Tume ya Katiba pamoja na Sekretarieti yake; hadidu za
rejea za Tume ya Katiba; uhuru mpana usio na vikwazo wa wananchi katika
kutoa maoni na marekebisho ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na
sekretarieti yake. Alisema maeneo, ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika
kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuifanya kuwa bora zaidi, ni
pamoja na kifungu cha 6 (4) cha sheria hiyo.
Mtatiro alisema kifungu hicho kimeweka
sharti linalokataza kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi ya taifa, mkoa
au wilaya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba.
Hivyo, alisema wamependekeza marekebisho
ya kuondoa sharti hilo, kwa vile wanaamini kuwa katiba licha ya kuwa ni
waraka wa kisheria, pia ni waraka wa kisiasa unaobeba malengo na
matarajio ya taifa.
Pia wamependekeza watu watakaoteuliwa
katika tume hiyo wawe waadilifu, wanaoheshimika na kuaminika mbele ya
jamii, wawe na ujuzi na uzoefu wa kutosha katika masuala ya katiba
wakiwa na uelewa mpana wa mambo ya sheria, siasa, uchumi na maendeleo.
Alisema kuteuliwa kwa watu wa aina hiyo
kutajenga heshima na imani kubwa ya tume mbele ya jamii na hivyo kuondoa
wasiwasi na hofu zinazojengwa za kutokuwapo kwa nia ya dhati na ya
kweli ya kupata katiba ya kidemokrasia inayoyotokana na Watanzania
wenyewe.
Mapendekezo mengine, ni Hadidu za Rejea za
Tume ya Katiba kujulikana mapema na kufanywa sehemu ya sheria hiyo kama
jedwali na pia ziwe zinatoa uhuru mpana na zisizobana kwa namna yoyote
ili tume au wananchi watoe maoni yao kwa maeneo watakayoona yanapaswa
kuzingatiwa na kuwamo katika katiba mpya.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment