Sunday 11 December 2011

Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Z`bar yapora mamlaka ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania

Jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini, January Msoffe amesema marekebisho ya 10 ya katiba ya Zanzibar yemepora Mamlaka ya kikatiba ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ya kusikiliza kesi za haki za binadamu nchini.

Tamko hilo alilitoa jana alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya haki za binadamu Duniani katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Alisema kwa mujibu wa marekebisho hayo ya katiba wananchi wa Zanzibar sasa hawana haki tena ya kikatiba ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania dhidi ya kesi za uvunjwaji wa haki za binadamu zitakazokuwa zikifunguliwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Jaji Msoffe, alisema katika mabadiliko hayo kuna tatizo kutokana na kifungu cha 24(3) cha katiba ya Zanzibar kufuta mamlaka ya kikatiba ya Mahakama ya rufaa Tanzania kupokea na kusikiliza rufaa za kesi za haki za binadamu zilizofunguliwa Zanzibar na kutolewa uamuzi na Mahakama Kuu ya Zanzibar.

“Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imenyang’anywa uwezo wa kusikiliza kesi za haki za binadamu kutoka Mahakama kuu ya Zanzibar,” Alisema Jaji Msoffe.

Alisema kwamba kifungu hicho kinahitaji kuangaliwa upya kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa sababu kina wanyima haki ya kikatiba wananchi ya kutumia Mahakama ya rufaa Tanzania iwapo watakuwa hawakuridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Jaji Msoffe, alisema kwamba katiba ya Zanzibar na marekebisho yake yamebadilisha yaliyomo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 ambayo ilikuwa ikitoa fursa kwa kila mwananchi wa Zanzibar kufuatilia haki zake Mahakama ya rufaa kama ikitokea hakuridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Alisema kwamba marekebisho hayo ya katiba yamempa uwezo Jaji Mkuu wa Zanzibar kuteua majaji watatu wa kusikiliza rufaa na uamuzi wao utakuwa wa mwisho kama mlalamikaji hatakuwa hakuridhika na uamuzi wa awali wa Mahakama hiyo.

Kuhusu katiba mpya ya Tanzania, Jaji Msoffe alisema mambo ya haki za binadamu lazima yaangaliwe upya katika katiba ya Muungano na ya Zanzibar ili yaendane na wakati katika mabadiliko hayo.

Alisema kwamba mabadiliko hayo ya katiba juu ya haki za binadamu vizuri kuangalia mifano ya Katiba za Kenya, Afrika Kusini na Uganda kwa vile katiba za mataifa hayo zimezingatia kwa kiwango kikubwa juu ya masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

Jaji Msoffe alisema mabadiliko ya katiba ya Tanzania lazima yazingatie haki za binadamu za kiraia, kisiasa haki za kiuchumi na kiutamaduni katika pande zote mbili za muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema kwamba wakati umefika kwa wananchi na viongozi kufundishwa juu ya haki za binadamu kwa sababu wapo ambao hawafahamu juu ya haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Siyo viongozi wengi wanaofahamu haki za binadamu. Huu ni mtihani mkubwa kwa sababu wanatakiwa watende haki na haki zenyewe hawazijui,”alisema Jaji Msoffe huku akipingwa makofi na washiriki wa Kongamano hilo.

Alisema kutokana na tatizo hilo wananchi wengi Tanzania wamejigeuza wao kuwa Polisi na Mahakama kwa kuwakamata watu na kuwaadhibu na wakati mwingine kukatisha maisha yao jambo ambalo ni kinyume na misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria. Alisema kwamba tatizo la wananchi kuchukua sheria mkononi lilianzia huko Tanzania bara na sasa limeingia kwa kishindo Zanzibar.

Alisema kwamba katika kuadhimisha miaka 63 ya tamko la umoja wa mataifa juu ya haki za binadamu duniani ni vizuri kwa serikali kutoa elimu ya uraia kwa wananchi wake ili wafahamu haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao na kujiepusha kuchukua sheria mkononi.

Kongamano hilo limetayarishwa na Kituo cha huduma za sheria (ZLSC) chini ya Mwenyekiti wake Profesa Chris Maina Peter, ambapo Mwanasheria mwanadamizi kutoka Ofisi ya Mwendesha mashitaka Safia Masoud Khamis, aliwasilisha katika kongamano hilo mada juu ya serikali katika kuheshimu haki za Binadamu Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment