MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema
anaridhishwa na mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Amesema kutokana na hali hiyo, hafikirii kwamba Zanzibar inapaswa
kurejea katika mfumo tenganishi ambao ulisababisha mgawanyiko mkubwa
visiwani.
Maalim Seif aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa
habari kwenye Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi kuzungumzia
mafanikio na changamoto za mwaka mmoja wa Serikali hiyo inayoundwa na
vyama vya CCM na CUF.
“Naam, ninaridhika sana na mafanikio yaliyopatikana katika Serikali
hii, sio mafanikio madogo, ni ya kuridhisha,” alisema Seif na kuongeza
kuwa kila jambo lina changamoto zake.
Alisema kutokana na hilo, changamoto zilizopo hazina budi
kurekebishwa ili kuiwezesha Serikali hiyo iliyoundwa baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana, kupata mafanikio makubwa zaidi.
Alisema ukilinganisha na Serikali kama hizo zilizopo Zimbabwe na
Kenya, ya Zanzibar imeonesha kwenda vizuri licha ya kuwepo kwa upungufu
kadhaa.
Alisema katika kuendesha Serikali hiyo wanatumia sera za chama
anachotoka Rais, lakini kwa busara za Rais Dk. Ali Mohammed Shein,
Serikali hiyo inatekeleza sera zote zenye manufaa wa ustawi wa Zanzibar
hata kama zinatoka kwa chama kingine.
Alisema licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mwaka mmoja
wa Serikali hiyo, yapo mafanikio katika uboreshaji wa kilimo katika
mazao ya chakula na biashara, kuimarisha sekta ya uvuvi, kuboresha hali
za maisha za wafanyakazi na kukuza teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Katika kilimo, alisema zao la karafuu limepanda ambapo mwaka huu,
kilo moja inanunuliwa kwa Sh 15,000, na inatarajiwa kuwa ifikapo Mei
mwakani, kwa kisiwa cha Pemba pekee, wakulima watapata Sh bilioni 50
kutokana na mauzo ya karafuu.
Katika uvuvi, Maalim Seif alisema Serikali imechukua hatua kuifanya
rasilimali ya bahari kuwanufaisha wananchi, na hivi sasa wawekezaji
wengi wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo.
“Katika kuendeleza sekta ya uvuvi, tayari Serikali imewapeleka
wananchi 30 huko China kujifunza mbinu za kufuga samaki,” alieleza
Maalim Seif.
Maalim Seif alisema mbali ya mafanikio hayo, zipo changamoto kadhaa
zikiwemo za baadhi ya watendaji wa Serikali kutofahamu malengo ya
kuanzishwa kwa mfumo wa Serikali shirikishi, badala yake kuendelea na
mfumo tenganishi.
“Badala yake wanaendesha shughuli za umma kwa taratibu zile zile
ambazo hazisaidii sana kuimarisha umoja wetu,” alieleza Seif na kuongeza
kuwa baadhi ya watendaji hao wanafanya kazi kwa mazoea.
Alisema pia yapo malalamiko mengi kuhusu suala la ardhi, ambayo hata
hivyo, alibainisha kuwa Serikali inayafanyia kazi na tayari inapitia
upya sera ya ardhi na sheria zote zinazohusu masuala ya ardhi.
“Kuna malalamiko makubwa ya kuwa wanafunzi wengi hawajafaidika na
mikopo ya kuwawezesha kupata elimu ya juu. Hili linatokana na uwezo
mdogo wa Serikali,” alisema na kuongeza: “Wanafunzi wanaohitaji mikopo
ni zaidi ya 1,500.
Uwezo uliopo kwa mwaka huu wa fedha ni kuwapatia huduma hii muhimu
wanafunzi 191 tu. Serikali itakuwa ikiongeza fungu la mikopo hii kila
mwaka ili wanafunzi wanaofaidika waweze kuongezeka kila mwaka.”
Aidha, alisema baadhi ya wananchi wanalalamikia kuwa wananyimwa
vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, na kuona kuwa hiyo ni haki ya kila
mtu na Rais Shein alishatoa maelezo kwamba kila mtu apatiwe, hivyo ofisa
asiyetekeleza hivyo, anafanya utovu wa nidhamu.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
aliwataka Wazanzibari kushirikiana kwa pamoja kuinua ustawi wa nchi yao.
Chanzo: Habari leo
Maalim kuhusu muungano jee munatumia sera gani
ReplyDeleteCCM (mbili kuelekea moja) au CUF (Tatu kuelekea kila mtu yake)
Hebu tuwekeeni wazi hii kwani ndio muhimu kwetu wazanzibari kwa wakati huu