Ahmed Rajab
“JITAYARISHE kunyanyaswa na kudhalilishwa,” ndivyo alivyoniambia
sahibu yangu mmoja mwenye asili ya Kipalestina kama miaka miwili
iliyopita. Alikuwa akiniaga baada ya kunikirimu kwa chakula cha usiku
nyumbani kwake mjini Amman, Jordan. Alihisi lazima anionywe hivyo kwa
vile siku ya pili alfajiri nilikuwa ninaelekea Israeli kwa mara yangu ya
mwanzo.
Nilipanga kuingia Israeli kwa kuivuka Daraja ya Allenby au kama
inavyoitwa siku hizi Daraja ya Mfalme Hussein, niweke maskani mjini
Jerusalem kwa wiki nzima ili niweza kuizuru miji mingine ya Israeli na
halafu nivuke mpaka wa Eratz na kuingia Ukanda wa Gaza kwa ziara ya siku
mbili.
Sikutaka kukaa sana Gaza kwa sababu kulikuwa moto. Wiki sita kabla,
mabomu ya Israeli yaliitwanga Gaza, yakazifanya shule na majumba yawe
vifusi na kuwaua Wapalestina chungu nzima. Na rafiki yangu wa Amman
aliponiambia nijitayarishe kunyanyaswa alikusudia kunyanyaswa na
‘vijijanajeshi’ vya Kiyahudi kwenye kivuko cha mpakani cha Eratz cha
kuingilia Gaza. Hayo yalinikuta.
La kuudhi zaidi ni kwamba wanyanyasaji ni vitoto vidogo unaweza
ukafikiri kama vina umri wa miaka 16. Lakini wana silaha nzito na
ufedhuli umewajaa kwenye ndimi zao. Kwa hivyo wao wanakuwa mabwana —
ingawa wengine ni wasichana — na wewe unakuwa mtoto.
Kwa hakika, niliyaona mengi Israeli. Nilizifuata nyayo za Yesu
Kristo, nikatembea kwenye Mji Mkongwe wa Quds, yaani Jerusalem,
nikaswali Ijumaa mbili kwenye msikiti wake wa Al Aqsa. Kiguu na njia
nikaizuru miji ya Tel Aviv, Jaffa, Sderot na Be’er Sheva ambao ni mji
mkubwa katika Jangwa la Negev.
Niliiona Israeli kuwa ni nchi ya kuta, vizuizi, vikwazo, vipingamizi
na vikaratasi vya ruhusa na vibali vya kila aina wanavyotakiwa
Wapalestina wawe navyo. Daima wanadhalilishwa kwa kila namna ya
idhilali. Nyumba zao zinabomolewa, wanafukuzwa makwao na lengo la
Wazayoni mjini Jerusalem ni kuufanya mji mzima uwe na sura ya Kiyahudi.
Wapalestina hawaruhusiwi kujenga Jerusalem ya Magharibi kwa Wayahudi
lakini Wayahudi wanaruhusiwa kujenga Jerusalem ya Mashariki kwa
Wapalestina. Ajabu ni kwamba juu ya yote hayo Wapalestina wanaendelea
kucheka, kutabasamu na wanaweza kufanya dhihaka.
Siku moja nilialikwa kwenye Bunge la Israel, Knesset, na Dakta Dov
Khenin, Mbunge wa chama cha Hadash, chama pekee cha Wayahudi na Waarabu
na ambacho ni cha mrengo wa kushoto na chenye wabunge wanne. Khenin
hali kadhalika ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha Kikomunisti cha
Israel, Maki.
Ofisini mwake bungeni Khenin ametundika picha ya Che Guevara.
Nilipomwambia kwamba tathmini yake ya mustakbali wa mzozo wa Israel na
Wapalestina inakosa rajua, ikiyaona mambo yote kuwa hayana mbele wala
nyuma, yamejaa misiba na mashakil alinijibu kwa kumnukuu mwanafalsafa wa
Kitaliana, Antonio Gramsci.
Alinikumbusha kwamba Gramsci akitaka pawepo na ‘pessimism of the
intellect, optimism of the will’ yaani pawepo na ukosefu wa rajua ya
akili, (lakini) pawepo na msimamo wa kutegemea mazuri katika dhamira.’
Gramsci akitaka hivyo ili ukosefu wa rajua uwe ni kichocheo cha
kuchukuwa hatua, na msimamo wa kutegemea mazuri uwe ni ukakamavu wa
kuamini kwamba hatua hiyo italeta mageuzi ya maana hata pakiwa na
nakama.
Mbunge huyo alinisikitikia kwamba ubovu wa Israeli ni kuwa hakuna
mlingano wa aina yoyote kati ya Waarabu na Wayahudi. Jamii hizo mbili
zimegawika vibaya. Hajakusudia Wapalestina na Wayahudi lakini Waarabu wa
Israel na Wayahudi wao.
Si tu kwamba Waarabu na Wayahudi wanazungumza lugha tofauti lakini
hata misamiati wanayoitumia ni tofauti, dhana (concepts) zao pia ni
tofauti katika siasa hata katika utamaduni na katika maingiliano yao ya
kijamii ambayo ni madogo mno na pia kwa namna wanavyoangaliana.
Kwa ufupi, pande zote mbili zina hofu. Wayahudi wanatishwa na
Waarabu; Waarabu nao wanawaogopa Wayahudi. Lakini aliniambia alitaka
nitambuwe kwamba 'Israeli sio tu pahala pa kukutania matatizo lakini pia
ni pahala penye uwezekano mwingi,’ yaani kuna mengi yanayoweza
kutendeka.
‘Je, Israeli ni dola la ubaguzi wa kikabila?’ Swali hilo nilimuuliza
mwandishi habari maarufu Gideon Spiro kwenye mgahawa wa Bookworm Café
mjini Tel Aviv. Bookworm, kwa hakika, ni duka la vitabu lakini lina
mgahawa na ni mahali ambapo Waisraeli wa mrengo wa kushoto hupenda
kukutana.
Sijui nini kiliniandisi nimuulize Gideon swali hilo kwa vile jibu
nilikuwa nalo. Labda nikitaka kushangazwa, kumsikia Mwisraeli mwenye
siasa za mrengo wa kushoto akiutetea msimamo wa Serikali yake kuhusu
suala hilo kwa kukana kwamba dola lao si la kibaguzi.
Siku chache kabla nilimuuliza mwandishi mwingine Wakiisraeli mwenye
mawazo ya wastani na jibu alilonipa halikuwa na shaka yoyote. Alisema
kwamba Israel ni dola la kibaguzi.
Lakini Gideon, mzee wa miaka 77, akiwa na tabasamu iliyokunjika
ikichezacheza kwenye ndimi zake na macho yake yakimetameta, alilipima
jibu lake: ‘Ni mfumo wa utawala wa kimbari (ethnocracy)’. Akasita,
akapiga fundo la kahawa aipendayo aina ya Cappuccino iliyojaa povu la
maziwa na akaendelea kunieleza hivi:
‘Kwa Wayahudi ni utawala wa demokrasia yenye mipaka, kwa Wapalestina
walio kwenye maeneo yanayokaliwa na Israeli ni utawala wa udikteta wa
kijeshi na kwa Waarabu wa Israeli ni utawala wa demokrasia yenye
ubaguzi. Lakini kwa Wayahudi na Waarabu pamoja utawala huo si wa
demokrasia,’ alisema.
Gideon Spiro aliongeza kunena kwamba hata miongoni mwa wenyewe kwa
wenyewe Wayahudi wanabaguana. Wayahudi wenye asili za kizungu ndio
walio tabaka la juu lenye kutawala na Wayahudi waliosalia, hasa walio
weusi, wako chini, wa mwisho, fungu la Mungu.
Nilipoingia Ukanda wa Gaza sikuona kitu ila maangamizi na maafa na
mji uliovunjwavunjwa na kuangushwa kwa mabomu ya Waisraeli. Ijapokuwa
umasikini umezagaa na watu wengi wanaishi chini ya ule uitwao mstari wa
ufukara, hata hivyo niliwasikia wakiangua vicheko na niliziona nyuso zao
zikiwa na bashasha.
Nilipata wasaa wa kwenda Ramallah, kwenye Ufukwe wa Magharibi, kwa
siku moja. Nililizuru kaburi la Yasser Arafat na niliona ushahidi wa
jinsi Wapalestina walio ughaibuni wanavyomimina fedha kwao na kukujenga.
Hilo ni funzo moja kwetu sisi.
Jingine lililonivutia Ramallah ni namna watu wenye dhamana katika
utawala wa huko walivyobobea katika fani zao mbalimbali. Nina hakika
kwamba watapopata uhuru wao na kuondoshewa bughdha za 'kukaliwa' na
Waisraeli basi watapiga hatua kubwa mbele kuishinda Israeli katika muda
wa miaka 20 tu ijayo, juu ya rushwa iliyosambaa.
Katika kutafakari kwangu baada ya kuyazuru maeneo ya Wapalestina
yanayokaliwa na Israeli niliona kwamba kuna mingine tunayoweza kujifunza
kutoka kwa Wapalestina na yapo ambayo Wapalestina wanayoweza kujifunza
kutoka kwetu.
Kwa upande wetu ni kuwa umma unaposema kwa sauti moja kuwa umechoshwa
watawala huwa hawana budi ila kuridhia. Hivyo, umma unapovinjari
unakuwa na nguvu ya kuleta mabadiliko.
Pili, ni kwamba mabavu au ubabe hauwezi kudumu milele. Huu ni ukweli
wa kihistoria. Utawala wa Arafat uliandamwa na kashfa za rushwa na
ubadhirifu. Hata mkewe Arafat, Suha, aliingizwa kundini kuwa miongoni
mwa waliokuwa wakiramba asali.
Hatimaye umma ulivinjari na wakuu wa Mamlaka ya Palestina akiwemo
Waziri Mkuu, Ahmed Qurei walijiuzulu. Lilipoingia wimbi la kujivua gamba
waliingia walokuwemo na wasiokuwemo, kila mmojawao akibeba dhamana ya
kuwa ndani ya Serikali iliyoshindwa kutekeleza matarajio ya wananchi.
Huko ndiko kuwajibika.
Tatu, tunaweza kujifunza kutokana na maendeleo ya kijamii, hasa
Ukanda wa Gaza ambako pamoja na vikwazo na hali ngumu inayotokana na
ukandamizaji unaoendelea wa dola ya Kiyahudi, utawala wa chama cha Hamas
bado unaungwa mkono kwa vile unawajali na kuwafaraji walalahoi.
Lile ambalo Wapalestina wanaweza kujifunza kutoka kwetu ni haja ya
kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama iliyoko Zanzibar. Serikali
kama hiyo haikupatikana Palestina tangu chama cha Hamas kilipokishinda
chama cha Fatah katika uchaguzi wa mwaka 2006 huko Gaza na kukilazimisha
chama cha Fatah kuhodhi mamlaka ya utawala katika Ufukwe wa Magharibi
pekee.
Licha ya makubaliano yaliyofikiwa mwishoni mwa mwaka jana jijini
Cairo kati ya pande hizo mbili serikali aina hiyo bado haijapatikana.
Hivyo panakosekana msimamo mmoja wa Wapalestina dhidi ya Israeli.
Kufanikiwa kwa Palestina mwaka jana kujiunga na Shirika la Elimu,
Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) 2011, kunaibua swali
la kwa nini iwe ni vigumu kwa Zanzibar, licha ya kuhudhuria
vikao mbalimbali vya shirika hilo mjini Paris?
Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikipigania kuwa na uwakilishi
katika jumuiya kadhaa za kimataifa kama Jumuiya ya Nchi Za Kiislamu na
hata Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la dunia FIFA. Juhudi hizo
zimekwama hadi sasa. Pengine serikali imeshindwa kulivalia njuga vya
kutosha suala hilo.
Kuna usemi kwamba katika siasa kila kitu kinawezekana. Ikiwa Misri
imefikia amani na Israeli, kwa nini pasiwe na uwezekano wa Hamas kukaa
pamoja na Israeli kuendeleza mchakato wa kupatikana amani?
Na kwa Tanzania, kwa nini tusiweze siku moja kushuhudia Tanganyika na
Zanzibar zikiingia katika enzi mpya na kuwa na uhusiano mpya
uliojengeka juu ya msingi wa haki na usawa kati ya nchi mbili zilizo
huru? Yote hayo yanawezekana kwani uamuzi wa haki na wenye nguvu ni ule
wa umma na sio wa viongozi.
Raia Mwema
No comments:
Post a Comment