Tibaijuka amepotoka
Nimeona kuna haja ya kutoa maelezo mafupi kuhusiana na Hoja ya
Kujadili Jambo la Dharura niliyoiwasilisha Baraza la Wawakilishi na
kupitishwa na Baraza hilo tarehe 23 Januari, 2012 baada ya kuona kuna
njama za makusudi za kujaribu kuipotosha kutoka upande wa Tanzania Bara,
zikiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi, Prof.
Anna Tibaijuka.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari ambao anaonekana
alikurupuka (au sijui alikurupushwa) kuufanya tarehe 25 Januari, 2012,
siku mbili baada ya Baraza la Wawakilishi kujadili na kupitisha hoja
niliyoiwasilisha, alikuja na maelezo marefu ya kuthibitisha kwamba
Zanzibar ilishiriki kikamilifu katika mchakato wote wa kutayarisha na
hatimaye kuwasilisha Andiko Rasmi la kuomba Umoja wa Mataifa kuiongezea
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukanda wa bahari kuu (Exclusive Economic
Zone) kwa ziada ya maili za baharini (nautical miles) 150 baada ya
kuongezewa maili 200 za awali, eneo ambalo ni sawa na kilomita za mraba
61,000.
Inasikitisha kuona mtu mwenye dhamana ya Uwaziri tena akiwa Profesa
anashindwa hata kujiridhisha juu ya undani na uhalisia wa lile analotaka
kulitolea taarifa kwa umma. Kama angelifanya juhudi ndogo tu za
kuwasiliana na Ofisi za Baraza la Wawakilishi na kuomba kupatiwa nakala
ya Hoja niliyoiwasilisha, Prof. Tibaijuka asingepotoka kiasi ambacho
alipotoka.
Hoja yangu haikugusia suala la kushirikishwa au kutoshirikishwa
Zanzibar katika mchakato huo. Mimi si mjinga wa kiasi cha wale
wanaokurupuka kuzungumzia mambo wasiyoyajua hata nishindwe kuona picha
inayomuonesha ofisa wa Zanzibar akiwa na ujumbe wa Tanzania Bara
uliokwenda kuwasilisha andiko hilo. Isitoshe, hata katika maelezo ya
hoja yangu nilinukuu habari iliyochapishwa na gazeti la Nipashe la
tarehe 17 Januari, 2012 ambalo liliripoti maelezo yake Prof. Tibaijuka
akitaja ushiriki wa maofisa na wataalamu wa Zanzibar katika matayarisho
ya andiko hilo. Ndiyo kusema, nilikuwa najua ninachokizungumzia kwa
sababu mimi sina tabia wala mwenendo kama wa Prof. Tibaijuka wa
kukurupuka kuzungumzia nisichokijua.
Kama angejipa nafasi ya kuitafuta na kuisoma Hoja yangu ambayo sasa
si yangu tena maana imeshapitishwa na Baraza la Wawakilishi na hivyo ni
Hoja ya Baraza la Wawakilishi angejua kwamba miongoni mwa mambo
niliyoyahoji ni hilo la kwa nini Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati, Mhe. Ali Juma Shamuhuna, na maofisa wa Wizara yake walishiriki
katika mchakato huo huku wakijua kwamba Baraza la Wawakilishi
lishapitisha maamuzi tarehe 08 Aprili, 2009 ya kukataa ushirikiano
katika suala la EEZ na kutaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imiliki
na kusimamia wenyewe ukanda wake wa EEZ. Uamuzi huo unajulikana hata na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutokana na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Waziri Kiongozi wa wakati ule, Mhe. Shamsi Vuai
Nahodha, kumuandikia Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kumueleza maamuzi
ya Zanzibar yaliyofanywa na Baraza la Wawakilishi.
Kwa upande mwengine, mimi na Wajumbe wengine saba (7) waliochangia
hoja hiyo tulikosoa kitendo cha Waziri Shamuhuna kushiriki katika suala
hilo bila ya kulitaarifu Baraza la Mapinduzi (ambalo kwa Zanzibar ndiyo
Baraza la Mawaziri) ikiwa ni kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar, Ibara
ya 43 (5) inayozungumzia uwajibikaji wa pamoja (collective
responsibility).
Kitendo cha Prof. Tibaijuka kukurupuka na kujibu hoja isiyokuwepo ya
ushiriki wa Zanzibar kinaonesha jinsi asivyo makini katika kazi zake na
ndiyo maana akashindwa kupembua na kutofautisha mambo madogo kama haya.
Nadhani Rais Jakaya Kikwete anapaswa kufikiria tena uteuzi wake kwa mama
huyu ambaye ameonesha dhahiri hana uwezo wa kuchambua mambo.
Kwa upande mwengine, namuonea huruma Prof. Tibaijuka kwa kufanya
jaribio la jambo lisilowezekana tena katika Zanzibar ya leo. Kitendo
chake cha kuihusisha hoja niliyoiwasilisha na CUF kilikuwa na lengo la
kuchochea mgawanyiko wa itikadi za kisiasa katika suala kubwa linalogusa
maslahi ya Zanzibar kama hili. Bahati nzuri, angejipa nafasi ya
kuwasikiliza Mhe. Hamza Hassan Juma, Mhe. Asha Bakari Makame, na Mhe.
Ali Mzee Ali, wote wakiwa Wawakilishi wanaotoka CCM, angejua kuwa zama
za kuwagawa Wazanzibari zimepiwa na wakati kwani wote walitahadharisha
juu ya uwezekano wa upotoshaji kama ule aliokuja kuufanya Prof.
Tibaijuka.
Mwisho, niseme nimesikitishwa na kitendo cha Mhariri wa gazeti la
Mwananchi kupitia Tahriri ya gazeti lake la tarehe 26 Januari, 2012,
kupotosha kile kilichopitishwa na Baraza la Wawakilishi hadi kufikia
kusema kuwa kimetokana na ‘maneno ya mitaani’ huku akijaribu kukionesha
kama ni jambo langu binafsi. Kutokana na upotoshaji huo, nimemuandikia
Spika wa Baraza la Wawakilishi barua ambayo nitaifikisha Jumatatu ya
tarehe 30 Januari, 2012 kumuomba atumie Kanuni ya 116 (2) (a) kumuita
Mhariri huyo mbele ya Kamati ya Maadili na Kinga za Wajumbe na kumtaka
ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua kwa kutenda kosa la jinai chini ya
Sheria ya Kinga, Haki na Fursa za Baraza la Wawakilishi (Sheria Nam. 4
ya 2007), kifungu cha 32 (1) (a).
Ismail Jussa
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment