Sunday 8 January 2012

Kafulila atimiza ahadi ya kusomesha wanafunzi 300

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ametimiza ahadi yake ya kusomesha wanafunzi 300 wanaotoka katika familia masikini katika jimbo lake, kwa kuwalipia ada na michango mingine katika sekondari mbalimbali walikopangiwa baada ya kufauli mitihani ya darasa la saba mwaka jana.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ilagala, katika wilaya ya Kigoma, Kafulila, alisema mwaka uliopita aliwalipia ada na michango mingine wanafunzi 100 waliofaulu mitihani ya darasa la saba, na wote wanatoka katika familia duni kiuchumi.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu niliahidi kuwasomesha wanafunzi 300 katika kipindi changu cha Ubunge, na mwaka jana nilianza na wanafunzi 100, mwaka huu licha ya matatizo niliyonayo na chama changu cha NCCR- Mageuzi nitahakikisha nawalipia ada na michangi mingine wanafunzi 300 wanaotoka katika familia masikini kama mimi,” alisema Kafulila.
Alieleza kuwa, yeye hajihusishi na mchakato wa kuwapata wanafunzi hao, kwani mambo yote huanzia kwenye kamati za shule, mikutano mikuu ya mijiji na hatimaye kamati za maendeleo za kata (WDC), hivyo wanafunzi wanaofanikiwa kupenya katika mchakato huo ni wale wenye sifa zinazokubalika.
Kafulila alisema, ameamua kuchukua wanafunzi 300 kutokana na hali halisi kwani wanafunzi hao watamaliza kidato cha nne mwaka 2014 na 2015, ambapo na yeye atakuwa anamaliza kipindi chake cha Ubunge kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alisema ili kuhakikisha wanafunzi wa Kigoma wanapata elimu na ujuzi kama wengine nchini, amenunua maabara tano za sayansi mwaka huu, kati ya kumi na nne zinazohitajika jimboni kwake, ambapo fedha za kugharamia zinatoka kwenye Mfuko wa Jimbo.
Aliahidi kukamilisha maabara tisa zilizosalia katika bajeti ya mwaka ujao wa 2013, ili kila sekondari katika jimbo iwe na maabara zitakazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na hivyo kuwa hodari katika masomo ya sayansi.
Kuhusu uhaba wa walimu na vitabu katika shule nyingi za msingi na sekondari katika wilaya ya Kigoma, Kafulila, alieleza kuwa kwa sasa taifa linakabiliwa na uhaba wa walimu katika maeneo mbalimbali, ingawa wanaoathirika zaidi na kadhia hiyo ni watoto wa masikini.
Pia, alisema atahakikisha zahanati zote zinapata umeme wa mfumo wa jua ili ziweze kutoa huduma bora ya kutibu kwa wagonjwa na kuhifadhi dawa kwenye majokofu, jambo litakalosaidia huduma kutolewa kwa ufanisi zaidi.
Chanzo: Nipashe



Nyongeza
Hapa nataka niwaulize hawa Wabunge wetu wa Zaznibar, jee wao pesa za majimbo wanapewa kidoga kuliko wenzao, nimekuwa nikifuatilia wabunge wa Tanganyika jinsi wanavofanya mambo makubwa kupitia pesa za mfuko wa jimbo lakini kwa bahati mbaya sana hawa wabunge wetu hawafanyi chochote kwenye majimbo yao hii inaonesha aidha hawapewi pesa au kama wanapewa huwa zinaishia wapi?
Inatokezea mbunge unamwambia changia laki tatu anashindwa na akitowa hiyo shilingi kumi analalamika kama anaitowa kwenye mfuko wake.
Na hii ndiyo sababu wabunge wetu wanafanya biashara kichaa kama ile wanayofanya wale wamachinga pale Darajani yaani wanamuhitaji mteja mara moja tu wanakuibia au wanakupandishia bei ili siku ya pili usende tena na hawa wabunge wetu wengi wao baada ya miaka mitano wananchi wanawaweka pembeni

No comments:

Post a Comment