Ally Saleh
Nimesoma makala ambayo inaelekea kua imechapishwa katika gazeti
kuhusu matamshi ya Waziri wa Muungano wa Ardhi na Makazi, Professa Anna
Tibaijuka na kufadhaishwa na udhaifu wa ufahamu wake katika suala
linalohusu Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Ismail Jussa.
Kama Profesa Ana Tibaijuka angefahamu Hoja Binafsi ya Jussa basi
asingetamka kabisa kuwa Jussa aombe radhi, wala asingetamka kabisa kuwa
Serikali ya Zanzibar ilirishirikishwa.
Alichosema Jussa na anachokisema Professa Tibaijuka ni vitu viwili
tofauti, na kama Professa Tibaijuka alipita baina ya mstari kwa mstari
wa Tamko la Jussa basi kwa hakika yeye alipaswa kuilaumu Serikali ya
Zanzibar na sio Jussa.
Lakini hata hilo la kuilamumu Serikali ya Zanzibar halipo, kama ambavyo nitaeleza.
Anavyodai Profesa Tibaijuka ni kuwa mchakato si wa leo na jana na
kwamba ulianza tokea mwaka 2007 na wakati wote kulikuwa na ushiriki
kamili wa maafisa wa Serikali ya Zanzibar na hata kushiriki katika
safari ya kwenda New York kukabidhi andiko hilo.
Tukubali hilo la ushiriki wa SMZ, lakini ndio linalifanya jambo hilo kwa ukubwa na upana wake liwe halali? La.
Kwanza ni haramu kwa kuwa mwaka 2009 Baraza la Wawakilihsi
lilipitisha Azimio la Baraza kwamba mambo yote kuhusu mafuta na suala la
bahari na mipaka yake litoke au litolewe na kusimamiwa na Zanzibar
wenyewe.
Kwa hivyo kuanzia 2009 mtu yoyote aliyefanya chochote kinyume na
Azimio la Baraza alikuwa anakwenda kinyume na sheria na kinyume na
Katiba.
Pili, kuanzia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka jana kuwa
Zanzibar inarudisha mipaka yake yote ilikuwa yake kabla ya kuja kwa
Jamhuri ya Muungano, inakifanya kila kitu kinachohusu mipaka kikifanywa
na Serikali ya Muungano bila ya ridhaa ya Zanzibar ni haramu na batili.
Najua hapa kunaweza kuwa hoja kwamba Katiba ya Muungano ni Katiba
mama na kwa hivyo mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar hayawezi kukiuka
matakwa ya Katiba ya Muungano, lakini hilo ni kosa kuamini hivyo kwa
sababu katiba hizo mbili ni sawa katika ukubwa wake.
Tatu, Profesa Tibaijuka ajue kuwa Hoja ya Jussa haijakataa uwepo wa
mipaka ya Tanzania, lakini ilichokuwa ikitaka ni pande mbili hizi
kufahamiana ndani ya mipaka ya Tanzania haki za Zanzibar ni zipi kwa
sababu katika bahari kuna suala la uchumi, uvuvi na uwekezaji mambo
ambayo yote si ya Muungano,
Bila ya kwanza kumalizana ndani kujua haki za Zanzibar itakuwa kama
vile suala la Jumuia ya Afrika Mashariki ambapo katika Mambo 14 ya
Afrika Mashariki ni 3 tu ambayo ni ya Muungano na kwa hivyo Tanzania
inaisemea na kuichukulia maamuzi Zanzibar katika mambo 11 ambayo si ya
Muungano.
Profesa Tibaijuka ni Waziri wa Ardhi, Makazi na Nyumba mambo ambayo
yote si ya Muungano, anapataje haki na uwezo wa kwenda kuiwakilisha
Tanzania na kuisemea Zanzibar wakati katika wizara yake suala la bahari
halimo.
Na hata kama lingekuwemo basi bahari si suala la Muungano na kwa
hivyo pande hizi mbili zingebidi zikae upya kuamua kufikiria iwapo ipo
au hakuna haja ya kulitia suala hilo katika Mambo ya Muungano.
Au kwa wakati huu kwa kuwa si la Muungano pande hizi mbili
lingelikabili vipi suala hilo kama ajenda ya Muungano. Kwamba mawaziri
wameshiriki na Serikali kutoa wajumbe hakulifanyi jambo hilo liwe halali
kama ambavyo hakulifanyi jambo hilo liwe la Muungano.
Pia Professa Tibaijuka kama angemfahamu Jussa na kwa hivyo mawazo ya
Wazanzibari ni kuwa hawaamini jambo lolote linalofanywa na Serikali ya
Muungano kuhusiana na Zanzibar na kwa hivyo chochote kile kinapaswa
kufikiwa maamuzi na hata kukatibiana na mapema.
Sijui kama Professa Tibaijuka anajua kuwa shaka hii ni kubwa na
imeonekana katika mambo kadhaa wa kadhaa na kama anataka afaidi mtizamo
wa Wazanzibari juu ya wanavyouona Muungano na pingamizi zake asome
makala ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud “ Masuala ya
Muungano Yasiokuwa na Majibu.”
Hadaa, mbinu na hila mbali na udhaifu katika utekelezaji na maamuzi
umeonekana katika mambo mengi kiasi ambacho inatisha na Muungao huu
umekuwa ukenda msege mnege na kupindana mkono kuliko ridhaa ya upande
mmoja.
Maamuzi kadhaa yanayofanywa kwa kuwa hayana mashiko ya kikatiba na
sheria katika zile zinaozoitwa kero za Muungano, yamebaki kama yalivyo
na kwa kweli asilimia 95 ya kero za Muungano ni zile zenye kuibana na
kuikandamiza Zanzibar.
Waziri Professa Tibaijuka ambaye ni mgeni sana katika kilinge cha
Muungano alipaswa afahamu taswira yote hii na asione malalamiko ya Jussa
ni ya kuzuka tu na yasiokuwa na mashiko.
Kwa kumalizia hata kama Serikali ya Zanzibar ilishiriki basi wananchi
wanasema wamefanyiwa khiyana na Serikali yao na kwa kupitia kwa Baraza
la Wawakilishi wanataka Serikali yao ijue kuwa ilifanya makosa kushiriki
katika mchakato huo bila ya kwanza kujua nafasi ya Zanzibar.
Profesa Tibaijuka fikiri jambo moja tu juu ya Serikali ambayo unasema
ilishiriki katika mchakato huo. Wewe ni Waziri lakini uliyepewa
kufuatana naye kwenda New York alikuwa ni Mkurugenzi Ayoub Muhammed
Mahmoud wakati Wizara hiyo ina Naibu Waziri mzima…wewe ulijisikiaje
kufananishwa na Mkurugenzi kuwa ndio colleague wako?
Kwa hili Ismail Jussa hana haja ya kuomba radhi. Ni kama alivyosema
Muhammed Ghassany mwandishi wa habari wa Zanzibar. Mwizi anakamatwa
amemebeba vitu vya watu anasepa navyo na alipokabiliwa akasema, “Mwizi
mie…niombeni radhi.”
No comments:
Post a Comment