Saturday 14 January 2012

Kamati kuu CCM yampitisha Raza jimbo la Uzini

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete (kulia), akiendesha Kikao cha Kamati Kuu ya CCM Taifa kilichokaa jana Mjini Zanzibar kwa ajili ya kujadili na kuchagua mgombea atakayekiwakilisha Chama cha Mapinduzi CCM katika uchaguzi mdogo wa Uwakilishi katika Jimbo la Uzini,

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemteua mwanachama wake, Mohammed Raza Daramshi kuwa mgombea wa Uwakilishi jimbo la Uzini mkoa wa kusini Unguja. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema kwamba kikao hicho kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kimempitisha Raza baada ya kuridhika na sifa zake.

Nape alisema, Kamati Kuu pia imemteua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk. Aman Karume kufungua kampeni za CCM za kuwania jimbo hilo ambazo zitafanyika Januari 28, mwaka huu katika Uwanja wa mpira wa Ghana.

Alisema wakati kampeni zitafunguliwa na Dk. Karume, ufungaji kampeni hizo utafanywa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwenye Uwanja wa mpira wa Tunduni.

Uchaguzi mdogo wa uwakilishi jimbo la Uzini unafanyika kufuatia kufariki dunia aliyekuwa mwakilishi wake kwa tiketi ya CCM, Mussa Khamis Silima aliyefariki kwa ajali ya gari, Septemba 23, mwaka jana.

Kuhusu minong’ono kwamba Raza ana utata katika uraia wake, Nape alisema Kamati Kuu imelitaza jambo hilo kwa makini lakini haikuweza kulipa uzito wa kumyima Raza nafasi ya kugombea kwa kuwa hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kuthibitisha hilo.

“Bado tunao muda wa kutosha, kama yupo mwenye ushahidi wa kutosha kuhusu hili anaweza kuleta ushahidi, ukiwa na uzito hatutaupuuza”, alisema Nape.

No comments:

Post a Comment