Thursday 5 January 2012

Hamad Rashid Bado ni Mbunge?

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, na wenzake wanne, wamepinga kufukuzwa uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa madai kwamba kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa Chama hicho Taifa kilichofikia uamuzi huo ni batili kwa vile kilizuiwa na mahakama kufanyika.

Pia ameeleza kusikitishwa kwake na kosa mojawapo kati ya makosa 11 ambayo alidai kwamba alisomewa katika kikao hicho cha Baraza Kuu juzi alipoitwa kujitetea kabla ya kutiwa hatiani na hatimaye kufukuzwa uanachama.

Kosa hilo ni la yeye Hamad kupiga picha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambapo alisema kikao hicho kilidai kwamba, kitendo hicho kilitoa taswira mbaya kwa chama na wanachama wa CUF.

Hata hivyo, kutokana na uamuzi huo wa mahakama, Hamad alisema yeye na wenzake wote bado ni wanachama hai na halali wa CUF, nafasi yake ya ubunge bado ipo pale pale na kwamba, bado wanayo mashiko ya kufanya kazi za chama na kuwataka wanaopinga hayo waende mahakamani.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, kikao hicho kilizuiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kufanyika hadi hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Kesi hiyo namba 1/2012, ilifunguliwa mahakamani hapo na Hamad na wenzake 10 dhidi ya wadhamini wa CUF.

Wanapinga ama kusimamishwa au kufukuzwa uanachama na kikao hicho, hatua ambayo wanadai ingewapokonya haki yao ya kikatiba na hivyo kuhatarisha hadhi yao halali ya uanachama.

Amri ya kuzuia kufanyika kikao hicho, ilitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Augustine Shangwa, juzi, saa 3.40 asubuhi, chini ya hati ya dharura baada ya kusikiliza maombi ya upande mmoja (wa Hamad na wenzake).

Walalamikaji wengine katika kesi hiyo, ni Shoka Khamis Juma, Doyo Hassan, Juma Said Sanani na Yasin Mrotwa, Kirungi Amir, Doni Waziri, Mohamed Faki Albadawi, Tamim Omar Tamim, Nanjase Haji na Mohamed Massaga.

Hamad alitangaza msimamo wao huo jana, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya Baraza Kuu kuwafukuza uanachama yeye na wenzake wanne. Hao ni Doyo, Shoka, Sanani na Mrotwa.
“Sisi sote hapa tunaheshimu maamuzi ya mahakama. Sasa kwa sababu tunaheshimu uamuzi wa mahakama, kwa order hii ya mahakama iliyotolewa saa 3.40, maamuzi yote yaliyofanyika pale bado ni batili.

Kwa hivyo, bado sisi ni wanachama hai na halali. Wanasheria wananiambia hivyo. Bado nafasi yangu ya ubunge ipo palepale. Wasifikiri kama wameichukua na mashiko bado ninayo ya kufanya kazi za chama na wenzangu wote. Wanaopinga hilo waende mahakamani,” alisema Hamad.

Alisema kufuatia amri hiyo ya mahakama na wakati wanasubiri uamuzi wa mahakama katika kesi ya msingi, yeye na wenzake wote wanakusudia kukutana ili kujadili na kufikia maamuzi ya nini cha kufanya.
“Leo (jana) nimepata simu 15 kutoka mikoani mpaka Charles Mwera amenipigia simu kutoka Mara akiniambia tunaomba tukutane tufanye mashauri haraka. Sasa mimi sitaki kuwa dikteta. Na sitaki niwaamulie wenzangu,” alisema Hamad.

Hata hivyo, alisema anaamini wanachama wa CUF popote walipo wameguswa na uamuzi huo uliochukuliwa na Baraza Kuu dhidi yake na wenzake.

“Tanga jana wananiambia wameshafikisha kadi 100 kukusanya. Temeke kadi 600, Mwanza wanaandaa maandamano makubwa, na kadi zinaendelea kukusanywa. Zinaanza kurudi. Watu wanahama chama. Wananiambia tangaza chama tukajiunge.,” alisema Hamad.
Aliongeza: “Inasikitisha sana kile nilichokisema. Nilisema watu wana nia ya kuua CUF. Sisi tunaoimarisha CUF ndio tunaonekana maadui, lakini wanaoua CUF ndio wanaoonekana watu.”

“Tanga wameniambia mpaka jioni leo watakuwa na kadi 2,000, Mwanza sijui zitakuwa ngapi, Morogoro wamenipigia simu hawajui ngapi.”
Alisema amesikitishwa kwa kunyimwa muda wa kujipanga ili kujitetea alipoomba suala hilo kwenye kikao hicho kujitetea.
Hamad alisema alisikitishwa zaidi kuona haki hiyo ya kisheria ikikataliwa kutolewa kwake hata na Abubakar Khamis (Waziri wa Sheria na Katiba), Twaha Taslima (wakili wa kujitegemea na mwanasheria wa CUF), Ismail Jussa (mwanasheria kitaaluma) Ladhu na Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema baada ya kupokea hati ya amri hiyo ya mahakama, alimwandikia barua Maalim Seif kumuomba apokee nakala halisi ya uamuzi huo wa mahakama.

Hamad alisema katika barua hiyo alimweleza Maalim Seif kuwa karani wa mahakama alifika ofisi kuu ya CUF Buguruni, jijini Dar es Salaam kuwasilisha amri hiyo, lakini ofisa wa chama, Mikidadi alikataa kuipokea.
“Kwa kuwa sisi ni wadau wa shauri hili, na kwa kuwa mimi nimepewa nakala, naomba niwasilishe rasmi kwako rasmi kama sehemu ya pingamizi za awali,” alinukuu sehemu ya barua hiyo.
Alisema alimkabidhi mmoja wa maofisa wa CUF aliyekuwa katika kikao hicho barua hiyo na kumuomba amkabidhi Maalim Seif majira ya saa 7.45.
“Baadaye dakika 15 wakaniita ndani kuniambia ombi langu la kutaka nipewe muda. Wakasema tumekataa kukupa muda, kama unataka ujieleze tu hivyo hivyo, kavu kavu,” alisema Hamad.

Aliongeza: “Nikasema sababu yangu ya kukataa bado iko palepale. Lakini sasa nina sababu nyingine ya msingi zaidi, ya court order (amri ya mahakama) hii hapa, inayosema hiki kikao kisiendelee kufanya maamuzi yoyote mpaka shauri la msingi litakaposikilizwa mahakamani tarehe 13 Februari, 2012.”
“Kwa sababu hiyo ya pili sasa, mimi naheshimu maamuzi ya mahakama, sina sababu ya kuendelea na nyinyi tena. Wakaniambia basi kwa heri. Nikatoka nikaenda zangu.”

Alisema hati rasmi ya amri hiyo ya mahakama waliipeleka ofisi kuu na ilipokelewa na mlinzi waliyemkuta.
Hata hivyo, alisema pamoja na hivyo, aliporudi kwenye kikao alielezwa na Shoka kuwa tayari walikuwa wamekwisha kufukuzwa uanachama.

“Nikasema loh! Tumekufa! Tumekufa! Kama kuna kiongozi mwandamizi wa serikali, Makamu wa Rais, anakataa kuheshimu maamuzi ya mahakama, huyu mtu angekuwa rais siku moja ingekuwaje? alihoji Hamad.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alipoulizwa jana na NIPASHE, alisema hadi wanamaliza kikao hicho juzi hawakuona amri yoyote ya mahakama.

“Ninachosisitiza ni kwamba mahakama haijaleta amri yoyote kwa chama. Na hivi ninavyoongea hatujapokea chochote kutoka mahakamani. Sie ni chama na chama hiki kinaongozwa na  katiba na katiba imefuatwa katika kila jambo. Kwa hiyo, maamuzi ni halali na yanafuatwa na tunayasimamia,” alisema Mtatiro.
Aliongeza: “Rais wa Zanzibar amewahi kuapishwa na Jaji Mkuu na hatukumtambua kwa miaka kadhaa ijekuwa Hamad Rashid? Akirudishiwa  ububge na mahakama atakuwa  mbunge wa mahakama.”

Mtatiro alisema mbali na Hamad na wenzake wanne kufukuzwa uanachama, alisema Doni, Massaga, Albadawi na Nanjase walivuliwa uongozi wakati Kirungi, Tamim na Ayubu Kimangale walipewa karipio kali na Yusuph Mbungiro na Ahmed Issa walipewa pole kwa kuingizwa kimakosa katika kadhia hiyo.

TENDWA APONDA
Msajili wa Vyama Vya Siasa, John Tendwa, alikerwa na vyama vya siasa kuwafukuza hovyo wanachama wao.
Alieleza kukerwa na tabia ya vyama vya siasa kutumia taratibu na kanuni za vyama vyao kuwafukuza uanachama wabunge wao na hivyo kuipa serikali gharama wa  kuitisha uchaguzi mwingine.

Alifafanua kuwa kuitisha uchaguzi kwa jimbo moja ni zaidi ya Sh. bilioni 19 na kutaka sheria aiangaliwe upya kwa kuwa hali hiyo inaipa mzigo serikali pamoja na kuwanyima haki wapiga kura waliomchagua mbunge wao.

Alisema kufukuzana uanachama kunawafanya wabunge na viongozi wengine wa vyama vya siasa kukosa ubunifu pamoja na kushindwa kutoa mawazo mapya ambayo yatasaidia kukijenga chama kwa kuwa watakuwa wanaogopa kuitwa wasaliti.

CHEYO ATETEA
Mwenyekiti wa Chama Cha United Democratic Party (UDP), aliunga mkono kutimuliwa uanachama kwa mtu yeyote anayetaka kuleta mapinduzi ndani ya chama.
Alisema kama mwenyekiti wa chama aliyechaguliwa muda haujamailizika na akajitokeza mtu anataka kuleta mapindunzi ni vyema akatimuliwa.

Cheyo alifananisha msaliti yeyote katika chama sawa na mtu anayetaka kumpindua Rais na kusema kuwa mtu wa namna hiyo adhabu yake ni kunyongwa.
Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment