Thursday 12 January 2012

Tunahitaji mapinduzi ya uchumi, maisha Z’ bar

Thursday, 12 January 2012 10:00
LEO ni siku ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Siku hii ni ya kukumbukwa kwani ni siku ambayo wananchi wa Zanzibar waliuangusha utawala wa Kisultani ambao ulikuwa ukiwakandamiza na kuwanyonya katika nchi yao.

Tunachukua fursa hii kutoa pongezi kwa Wazanzibari na Watanzania kwa jumla kwa kuadhimisha siku hii muhimu, lakini pongezi zaidi kwa kudumisha amani na udugu miongoni mwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa miaka yote 48.

Sote tunafahamu kwamba safari ya miaka 48 aliyoianzisha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, haikuwa rahisi kwani kumekuwapo changamoto nyingi za hapa na pale kiasi cha kutishia umoja wa kitaifa wa Wazanzibari.

Yote hayo yalikuwa mapito, lakini jambo kubwa la muhimu hii leo ni kujadili jinsi ya kusonga mbele na kuhakikisha haturudii makosa ambayo kutokea kwake kulisababisha matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kugharimu maisha ya Watanzania wenzetu kadhaa.

Mara nyingi maadhimisho ya aina hiyo, hasa ya kiserikali hutumika kwa kuandaa sherehe na shamrashamra za hapa na pale, huku wengi wakizitumia kwa mapumziko nyumbani ambako hutulia na familia zao.

Sisi wa Mwananchi tunaiona sikukuu hii ya kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kuwa, ni siku ya kutafakari tulikotoka, tulipo na tunakokwenda kwa maana ya kila mmoja wetu kujiuliza ni upi mchango wake katika miaka yote hiyo.

Lakini pia ni wakati wa watawala waliopo sasa kubaini changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii ambazo zimekuwa ni vikwazo vinavyowazuia Wazanzibari kusonga mbele kimaendeleo kiasi cha kuwafanya baadhi yao kuishi katika maisha ya umasikini na ufukara wa hali ya juu.

Tusiwe na choyo kwa vizazi vijavyo, bali tuwe na upendo na ukarimu kwa kutumia siku hii, kutafakari na kuchukua hatua za dhati dhidi ya matatizo yaliyopo, tukiutazama ustawi wa Zanzibar miaka 48 ijayo kwa ajili ya watoto wetu na wajukuu zetu.

Leo tunaiona Zanzibar na kuifurahia kutokana na msingi uliojengwa na wasisi wake, ambao walikuwa na mtazamo kwamba baada ya miaka 48 tutakuwa na nchi yenye asali na maziwa.

Lakini inawezekana pale walipoachia wao, tuliopo leo tumeshindwa kupiga hatua ya kuridhisha na ndiyo maana bado kuna malalamiko kutoka kwa Wazanzibari ambao hawaridhishwi na mambo yanavyokwenda.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na vyama vya CCM na CUF kwa pamoja ina changamoto kubwa ya kujiuliza kwamba, katika idadi ya miaka inayokaribia nusu karne Wazanzibari wamevuna nini au wana nini cha kujivunia?

Pia tujiulize mapinduzi yalikuwa na maana gani Januari 12, 1964 na leo hii 2012 miaka 48 baadaye, mapinduzi haya yana maana gani kwa Wazanibari? Bado yana maana ile ile ya miongo yapata mitano iliyopita au maana yake imebadilika?

Kadhalika tujihoji, kama lengo la mapinduzi lilikuwa ni kuwakomboa wanyonge kutoka katika minyororo na utumwa chini ya utawala wa Kisultani, je lengo hilo limefikiwa? Hivi leo  minyororo na utumwa wa Wazanzibari ni nini au ni upi?

Maswali hayo na mengine mengi yanapaswa kupatiwa majibu kutoka kwa viongozi wetu wa sasa. Tena majibu sahihi ambayo siyo tu kwamba yanawatia moyo wananchi wa Zanzibar, la hasha, bali majibu ambayo utekelezaji wake utaleta nafuu kwa maisha yao, sasa na siku zijazo.

Kwa jinsi hali ilivyo sasa, tunahitaji Mapinduzi mapya Zanzibar na haya si mengine bali ni mapinduzi ya kiuchumi yatakayomwezesha kila Mzanzibari kuishi maisha bora yanayolingana na thamani ya utu wake. Inawezekana iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake. Mungu ibariki Zanzibar.
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment