Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho
akiendesha kikao cha baraza hilo kinachoendelea katika ukumbi wa Mbweni
nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho ameitaka
Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kutoa taarifa katika baraza
la mawaziri suala la Tanzania kuwasilisha ombi la nyongeza masafa ya
bahari kuu kwenye Umoja wa Mataifa. Kificho alisema hivyo baada ya
Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna kusema
kwamba yeye kama wizara taarifa anayo hiyo lakini katika baraza la
mawaziri hakuna taarifa ya jambo hilo iliyowasilishwa.
“Nakuomba waziri mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna kuleta taarifa hiyo
baraza la mawaziri kwa ajili ya kuifanyia kazi pamoja na wajumbe wa
baraza la wawakilishi” alisema Spika Kificho.
Kificho, aliwaambiwa wajumbe wa baraza hilo wasubiri na kuiagiza
Serikali kulifuatilia suala hilo kikamilifu ili wananchi wa Zanzibar
wajue lengo la hatua hiyo kwa serikali ya Tanzania.
Alitoa agizo kwa serikali kutoa maelezo juu ya upande mmoja wa
Muungano kupeleka maombi hayo kwa Umoja wa Mataifa bila kuushirikisha
upande wa pili.
Aliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatilia jambo hilo
kabla ya maamuzi ya Umoja wa Mataifa hayajatolewa kuhusiana na suala
hilo kwani suala hilo linahusu pande mbili na wananchi wa Zanzibar wana
haki ya kujua mwenendo wa mambo katika nchi yao.
Awali Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu
alitoa taarifa mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha ombi katika umoja wa
mataifa kuomba kuongezewa masafa zaidi ya maili mia mbili katika bahari
kuu.
Jussa alitoa hoja ndani ya baraza la wawakilishi akiwataka wajumbe wa
baraza hilo lijadili suala hilo kwa uwazi hasa kwa kuzingatia suala
hilo lina athari kubwa kwa wazanzibari iwapo litafanikiwa.
Alisema hatua hiyo ya Serikali ya Muungano ni nzito na inayogusa
wananchi kwa hiyo, ilitakiwa kuangaliwa vizuri kwani waathirika wakuu
huenda wakawa zaidi ni wazanzibari.
Jussa alifahamisha kuwa kwa mujibu wa taarifa iliyotoka ndani ya
vyombo vya habari ombi hilo linawasilishwa jana katika ofisi za Umoja wa
Mataifa huko New York, Marekani.
“Waheshimiwa wawakilishi hoja hiyo imetugusa sana wananchi wanzanzibari
tunaomba muichangamkie, hatutaki mambo ya hewala bwana, hoja ya serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusema kuwa Zanzibar imeshirikishwa
kwa vile mjumbe mmoja kutoka Zanzibar anaonekana katika picha ya pamoja
na mama tibaijuka katika kuwasilisha ombi hilo la umoja wa mataifa
hatuitaki wala haitoshelezi” alisema Jussa katika kikao hicho cha baraza
la wawakilishi kinachoendelea huko Mbweni Zanzibar.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rasi, Ali Mzee Ali, alisema
kuwa ingekuwa jambo la maana suala kama hilo likapigiwa kura kutokana na
umuhimu wake kitaifa na sio kuamuliwa na upande mmoja.
Suala la masafa ya bahari kuu limekuwa na mgogoro kati ya Zanzibar
pamoja na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kiasi ya baraza la
wawakilishi kupitisha azimio kuhusu jambo hilo, ambalo limeingizwa
katika orodha ya kero za muungano.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Shamuhuna alisema kwamba wizara yake inayo
taarifa kamili ya suala hilo ambapo alitakiwa yeye kufunga safari kwenda
umoja wa mataifa kuwasilisha ombi hilo pamoja na waziri wa ardhi,
nyumba na maendeleo ya makaazi wa jamhuri ya muungano Bi Anna Tibaijuka.
Hata hivyo Shamuhuna alisema kwamba kutokana na kutingwa na kazi
nyingi alimtuma afisa wake kufuatana na ujumbe huo kwenda katika safari
hiyo.
“Ujumbe huo kwa sasa upo katika umoja wa mataifa na tayari
unatarajiwa kuwasilisha ombi hilo ambapo Tanzania baadaye itapangiwa
tarehe kwenda kusikiliza shauri lao”.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar baadhi yao wamehoji hatua
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupeleka maombi Umoja wa
Mataifa (UN) kuomba kuongezewa ukubwa wa eneo la bahari na kutaka
ufafanuzi wa suala hilo kuwasilishwa ndnai ya kikao hicho, hatua ambayo
kimsingi Spika Kificho alikubaliana nao wajumbe hao na kuiagiza serikali
kuwaislisha suala hilo barazani hapo.
Tanzania inawasilisha ombi la kuongezwa zaidi masafa ya eneo la
bahari kuu kutoka mia mbili na sasa kufikiya mia nne, kama shauri hilo
litakubaliwa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, anaelezwa kuwasilisha hoja hiyo na kuiwasilisha Umoja wa
Mataifa (UN) huko New York Marekani.
Shamhuna anauza nchi yetu kwa thamani ndogo ya kutegemea urais 2020, ila wazanzibari mujuwe hivi ni vita anavoviandaa baada ya wao kuondoka katika dunia hii, kwani wanatakiwa wajuwe wao hawatokaa hapa milele, Allah atakwenda kuaadhibu kwa kuigawa nchi tukufu ya kiislamu kwa watanganyika na pia umwagaji damu utakaofuata pia wao watakuwa questionable kwani watoto wetu nna uhakika hawatokubali
ReplyDelete