Tamko hilo amelitoa alipokuwa akizungumza
katika mahojiano maalum kuhusu maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya
Zanzibar huko Ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar jana.
Alisema kuwa na mfumo wa kutoa urais kwa zamu ni mwanzo wa kuligawa taifa na kuvuruga umoja wa kitaifa wa Tanzania.
“Ni hatari kuwa na mfumo wa kutoa urais
wa muungano kwa zamu kwa sababu ni mwanzo wa kuligawa taifa vipande,”
alisema Waziri Aboud.
Alisema utaratibu unaotumika sasa wa
kupata mgombea wa nafasi ya urais kwa kuzingatia sifa na uwezo bila ya
kuangalia anatoka upande gani wa muungano ndiyo unafaa kuendelea
kutumika kwa sababu umesaidia kuimarisha muungano.
Aidha, alisema kwamba mawazo kama hayo
hayafai kupewa nafasi kwa sababu ni mwanzo wa kuanza kujenga ubaguzi
jambo ambalo kinyume na misingi ya umoja wa kitaifa.
“Kama leo tukisema kuwepo na zamu ya
urais wa Muungano baina ya Tanzania bara na Zanzibar badaye wataibuka
watu wakitaka kuwe na zamu urais wa Zanzibar baina ya visiwa vya Unguja
na Pemba". alisema.
Alisema kutokana na Tanzania kuwa na
mikoa mingi kutaibuka watu wakitaka zamu ya kutoa urais katika mikoa yao
kama Mwanza, Tabora, Rufiji, Kigoma na kuwa mwanzo wa kuzorotesha umoja
wa Watanzania.
Waziri Aboud alisema utaratibu unaotumika
sasa ni mzuri kwa sababu umesaidia kupata viongozi wanaofanyakazi bila
ya kuzingatia wanatoka upande gani wa Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Waziri Aboud alisema katika kipindi cha
miaka 48 ya Mapinduzi, Muungano umeleta faida kubwa katika kuimarisha
amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.
Alisema Muungano umesaidia kujenga
misingi ya kiuchumi kutokana na wananchi wa Zanzibar wapatao milioni 1.2
kupata nafasi ya kulitumia soko la biashara la Tanzania bara la watu
milioni 40.
Hata hivyo alisema wakati huu wa kuelekea
mchakato wa mabadiliko ya katiba ya muungano ni vizuri wananchi
wakapata nafasi ya kujadili na kuamua wanataka katiba ya aina gani kwa
maslahi ya maendeleo ya nchi na vizazi vijavyo.
“Upande wangu mie binafsi napendelea mfumo wa serikali mbili ndiyo umesaidia kuimarisha Muungano wetu,” alisema.
Chanzi: Nipashe
Duh!!! Huu mtihani wetu wazanzibari, yaani tunaambiwa tuwe kitu kimoja katika kipindi hichi cha kuelekea kwenye katiba mpya lakini kinyume chake hao ambao ni viongozi wa kutuunganisha kwenye kuelekea kwenye kutetea maslahi ya Zanzibar ndio hao kila mmoja ana misimamo yake, huu ni mtihani kwa wazanzibari,
ReplyDeleteLabda niwaulize huyu maalim haya mawazo kayatowa kichwani kwake bila ya kushauriana na hawa akina Mohammed Abood au hawa akina Abood wanaendeleza zile siasa za kutegana kwa ajili ya kujijengea maslahi binafsi bila ya kuzingatia maslahi ya ZAnzibar?
Allah aibariki Zanzibar na awabariki na watu wake na atuepishe na viongozi ambao wanaweka maslahi yao mbele bila ya kuzingatia maslahi ya Zanzibar na Uislamu kwa ujumla