Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv. Spice
Islanders 1 imependekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Mustafa
Aboud Jumbe pamoja na wahusika wengine wachukuliwe hatua za kisheria na
kinidhamu kutokana na uzembe waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli
hiyo
Akitoa mapendekezo ya Ripoti hiyo leo katika Ukumbi wa Wizara ya
Habari Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi
Abdulhamid Yahya Mzee amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeyakubali
mapendekezo ya ripoti hiyo na kusema itaiachia Mahaka na Jeshi la
Polisi kutimiza wajibu wao
Dk.Abdulhamid amesema miongoni mwa watu ambao walibainika na makosa
katika ajali hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Mamalaka ya Usafiri wa
Baharini Zanzibar Haji Vuai Ussi,Mkuu wa kituo cha usimamizi wa usalama
wa vyombo vya baharini wa Shirika la Bandari,Usawa Khamis Said na Kaimu
Mdhibiti wa Bandari ya Malindi Sarboko Makarani Sarboko.
Wengine ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku
Hashim Ayub ambaye ni Mwakilishi na Mbuge wa Jimbo la Muyuni,Salim Said
Mohammed, Makame Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.
Dk.Abdulhamid amesema wahusika wote waliotajwa katika ripoti hiyo
ikiwa ni pamoja na Captain wa Meli hiyo Said Abdallah Kinyanyite na
wasaidizi wake,Afisa usafirishaji wa Shirika la Bandari Hassan Mussa
Mwinyi na Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya Usafisiri wa Baharini Juma Seif
Juma watachukuliwa hatua za kisheria kulingana na makosa yao
Mrajis wa meli Abdallah Mohammed Abdallah, Afisa Usalama wa Mamlaka
ya Usafiri wa Baharini Simai Nyange Simai, na wasimamizi wa watatu wa
uingiaji wa abiria katika meli hiyo Yussuf Suleiman Issa,Shaib Said
Mohammed na Juma Abdallah Hussein nao wachukuliwe hatua za kisheria na
kinidhamu.
Wengine ni Afisa Mkuu wa Mv.Spice Abdalla Mohammed Ali,Mhandisi Mkuu
wa Meli hiyo Khamis Ahmada Hilika, Mabaharia wote wa Meli hiyo pamoja na
Askari wa Bandarini waliokuwepo zamu katika kupanga abiria siku ya
tukio ambao ni Sajent Jumbe Muhaji na Koplo Juma Abdulla.
Akizungumzia juu ya fidia kwa wahanga wa ajali hiyo Dk.Abdulhamid
amesema jukumu la kuwalipa wahanga hao liko mikononi mwa wamiliki wa
meli hiyo kwa mujibu wa sheria na kwamba vigezo vya kulipwa wahanga
vitafuata utaratibu maalum uliowekwa ambapo kwa waliofariki watalipwa si
chini ya Sh Milioni Kumi
Kwa waliopata ulemavu watalipwa asilimia 75% ya Fedha watakazolipwa
waliofariki dunia ambapo waliokuwemo katika meli hiyo bila kupata
ulemavu watapata asilimia 50% ya kiwango hicho.
Kuhusu fedha za michango ya maafa ambazo zimetolewa na taasisi
mbalimbali Dk. Abdulhamid amesema fedha hizo zitagawiwa kwa wahusika
chini ya utaratibu maalum utakaowekwa na Mfuko wa Kamati ya maafa uliopo
chini ya Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais
Aidha Dk.Abdulhamid alisema ripoti hiyo itawekwa wazi na kupatikana katika mitandao na Maktaba kuu ili wananchi waweze kuisoma.
Ripoti ya Tume hiyo iliundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kufuatia kuzama kwa Meli ya Mv.
Spice Islanders 1 tarehe 9/09/2011 katika Mkondo wa Nungwi kuelekea
Pemba ambapo inasadikiwa ilikuwa na abiria 2470 na tani kadhaa za mizigo
No comments:
Post a Comment