Tuesday 21 February 2012

Zanzibar yapokea ripoti ya mgawanyo wa fedha za muungano

ZANZIBAR tayari imepokea ripoti ya Tume ya Pamoja ya Usimamizi wa Fedha kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotokana na washirika wa maendeleo kwa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema hayo jana wakati alipozungumza na gazeti hili.
Alisema tume hiyo tayari imewasilisha ripoti yake kwa pande mbili za Muungano kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotokana na washiriki wa maendeleo pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imepokea taarifa ya tume ya pamoja ya fedha kwa ajili ya kuifanyia kazi...ngazi muhimu zote tayari imepitiwa na Zanzibar imeridhika nayo,” alisema.
Alisema ripoti hiyo imepitiwa na vyombo vya juu vya SMZ ikiwemo Baraza la Mapinduzi ambalo hujumuisha mawaziri wote wa Serikali.
Hata hivyo, Omar alisema Zanzibar kwa sasa inasubiri kukamilika kwa taarifa hiyo kwa ajili ya utekelezaji wake kutoka kwa upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo bado Baraza la Mawaziri halijakaa kuijadili.
Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Serikali zote mbili na mwenyekiti wake William Shelukindo.
Kwa muda mrefu kumekuwepo na malalamiko kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotokana na washirika wa maendeleo ikiwemo za misamaha ya madeni pamoja na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
Zanzibar imekuwa ikilalamika gawio inalopata la asilimia 4.5 kwamba ni dogo na limepitwa na wakati na halilingani na matumizi halisi ya SMZ katika shughuli zake.
Chanzo: Habari leo

No comments:

Post a Comment