MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Iddi amesema mabadiliko yanahitajika katika nyanja mbali
mbali zikiwemo za kiutendaji ili kuondokana na utaratibu wa kufanyakazi
kwa mazoea ambao hauna tija.
Balozi Seif alieleza hayo jana
ukumbi wa hoteli ya Bwawani kwenye ufungaji wa mkutano wa pili wa hali
ya siasa visiwani Zanzibar, ulioandaliwa na Mpanago wa Utafiti na Elimu
ya Demokrasia Tanzania (REDET) wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema baada ya utulivu wa kisiasa
ulioletwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa
Umoja wa Kitaifa, jambo la msingi linalohimizwa ni mabadiliko katika
utendaji na kuacha na tabia ya kufanyakazi kwa mazoea ‘business as
usual’.
Alifahamisha kuwa tabia hiyo
haitaleta maendeleo ya haraka kwa wananchi ambao wamekuwa na shauku
kubwa ya kupiga hatua za maendeleo mbele baada ya kuwepo kwa utengamano
wa kisiasa miongoni mwa Wazanzibari.
Balozi Seif alisema serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa, inafanyakazi kwa
kuweka mbele maslahi ya wananchi kuliko maslahi binafsi. “Hakuna jambo linaloamuliwa na
mtu mmoja peke yake bali serikali nzima chini ya uongozi wa Baraza la
Mapinduzi. Tukisema huu ni uamuzi wa serikali uamuzi huo umefikiwa
katika misingi hiyo”,alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kuwa hakuna kitu
kilichoundwa na mwanadamu ambacho hakiwezi kuboreshwa, hivyo changamoto
zinazotolewa na wadau zinazoikabili serikali zitafanyiwa kazi. “Serikali itakuwa makini
kuangalia mapendekezo hayo ili yaweze kuboresha si serikali tu bali hata
taasisi nyengine zinazohusiana na utendaji wa kazi wa serikali
yenyewe”, alisema Balozi Seif.
Aidha aliwaeleza wajumbe wa
mkutano huo kuwa kuunda kwa serikali ya Umoja wa kitaifa imeamuliwa na
wananchi wenyewe kwa kura ya maoni ambapo hivi sasa imekupo faida kubwa
ya ushirikiano na kuaminiana miongoni mwa wananchi ikilinganishwa na
hapo awali.
Alisisitiza kuwa pamoja na
mabadiliko katika serikali kuhitajika, lakini hayapaswi kuwa ya haraka
mno kwani huku akitolea mfano nchi ya Urusi ambayo ilitaka kufanya
mabadiliko ya haraka.
Katika mkutano huo wa siku mbili
wataalamu mbali wa sheria walipata nafasi ya kuwasilisha mada ambapo
walionesha changamoto inayoikabili serikali ya Umoja wa Kitaifa katika
kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Katika mada yake Kaimu Katibu
Baraza la Wawakilishi Yahya Khamis Hamad alisema serikali ya Umoja
iliyopo Zanzibar inatofautiana na ile ya Kenya na Zimbabwe ambazo
ziliundwa baada ya machafuko yaliyotokana na uchaguzi.
Alisema serikali hizo ni za muda
wakati ile ya Zanzibar ni ya kudumu iliyobainishwa katika katiba baada
ya wananchi kuridhia katika kura ya maoni.
No comments:
Post a Comment