18th February 2012
Tume
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetangaza kwamba itaanza kuhakiki vyeti
vyote vinavyotolewa na vyuo vikuu nchini na vya nje, pamoja na
kuvisajili ili kutambua vyuo vinavyotoa elimu ya juu kiholela.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Sifuni
Mchome, alisema imeamua kujaribu kujikita katika mfumo utakaoiwezesha
kufanya mabadiliko mbalimbali ili kuboresha utoaji huduma zake.
Profe. Sifuni alisema kuwa katika
utaratibu utakaoanza hivi karibuni, suala zima la ithibati litaangaliwa
kwa umakini, kwani TCU inataka kuhakikisha programu zote zinatolewa
kwenye vyuo vikuu vinavyotambulika na kwamba taarifa kuhusu utoaji elimu
ya juu kiholela itatolewa hivi karibuni.
Aidha, alisema kuwa programu zote
zitakazotolewa na vyuo vya juu ni lazima zithibitishwe na Tume hiyo na
kama zinatolewa nje ya nchi zitambuliwe ikiwa ni pamoja na shahada na
stashahada.
Alisema katika kutambua shahada ya
kwanza, ya pili na ya uzamivu, Tume hiyo imewasiliana na wataalamu ili
wasaidie kuweka kumbukumbu na mawasiliano kati ya TCU na wahitimu wa
vyuo, ambapo baada ya mhitimu kujaza fomu ya kwenye mtandao ili kuomba
cheti chake kitambulike, atatakiwa kupeleka cheti chake halisi ili
kikaguliwe.
Aliongeza kuwa baada ya kukaguliwa, TCU
itatoa cheti kitakachoonyesha kuwa cheti cha mhusika kimekaguliwa, na
cheti hicho kinaweza kutumiwa na mhitimu sehemu yoyote na endapo
watakitilia mashaka cheti chake ataweza kuwaonyesha cheti cha
uthibitisho kutoka TCU.
Alifafanua kwamba lengo la utaratibu huo
ni kuwasaidia wale wenye vyeti vya nje kuvisajili kwa muda mfupi, ambapo
itachukua wiki mbili cheti kusajiliwa.
VYA WALIO KAZINI PIA KUKAGULIWA
Akijibu swali kuhusu wale ambao tayari
wapo kazini na wana vyeti kutoka vyuo vya nje ambavyo havijatambuliwa na
TCU, Profesa Mchome alisema wamekwisha kupokea maelekezo kutoka kwenye
Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kuwa pia vyeti vyao vinatakiwa
kusajiliwa.
“Kwa wale wafanyakazi walio na vyeti vya
nje, na ambao wapo kazini, lakini bado TCU haivitambui vyeti vyao,
tutatangaza na kutoa muda ili wote wavilete tupate kuvitambua” alisema.
UDAHILI 2012/13
Profesa Mchome pia alitangaza kuanza kwa
muda wa udahili wa wanafunzi kwa msimu wa masomo wa 2012/2013, ambapo
watahiniwa wamegawanywa katika makundi matatu, ambayo ni waombaji wa
moja kwa moja, waombaji wasio wa moja kwa moja, na waombaji wenye sifa
zinazolingana.
Alisema kwa waombaji wa moja kwa moja,
wanatakiwa kuanza kuomba udahili kuanzia Aprili 23 mwaka huu kutegemea
na matokeo ya kidato cha sita kwa wale wote waliomaliza kidato cha sita
mwaka 2010, 2011 na 2012, pamoja na wale walio na stashahada za ualimu
mwaka 2010, 2011 na 2012.
Kundi la pili ni waombaji wasio wa moja
kwa moja wanaotakiwa kuomba kuanzia Aprili 1, mpaka Aprili 30, 2012
waliomaliza kidato cha sita, wenye stashahada za ufundi na wenye
stashahada za ualimu waliomaliza sio chini ya miaka miwili iliyopita.
Kundi la tatu ni wenye sifa zinazofanana na hizo, ambao wanaweza kuomba moja kwa moja.
Hao ni wenye stashahada zinazotambuliwa
na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE), ambao hawapo kwenye kundi la
kwanza wala la pili la waombaji.
Wengie ni wenye stashahada kutoka nje ya
Tanzania ambazo zinatambuliwa na NACTE na wengine wenye shahada ambao
wanataka kujiunga na programu nyingine za shahada kama uchumi na
biashara
Wengine ni wahitimu wa kidato cha sita na wana vyeti vyenye sifa ya kuwaruhusu kujiunga na vyuo vikuu.
Profesa Mchome alisema TCU imeamua kuweka
viwango vilivyo sawa katika ufundishaji hasa katika masomo ya biashara
na mfumo wa kutambua tuzo za vyuo vikuu ili kuleta ulinganifu kwa vyuo.
Aidha, alisema TCU ina mpango wa
kuviunganisha vyuo vyote vilivyopo chini ya NACTE na TCU ili viwe na
mfumo mmoja utakaovitambulisha.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment