Wednesday 29 February 2012

Maalim Seif: SUK ni imara, Zanzibar ni shwari

Na Joyce Mmasi
NI zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu Wazanzibari wafungue kurasa mpya za maisha ya kisiasa pale walipofanya mabadiliko ya katiba na kuruhusu nchi hiyo kuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa na vyama viwili vya siasa ambavyo ni CCM na CUF.
 
Kuundwa kwa serikali hiyo kumeleta matumaini kwa wananchi wa nchi hiyo ambapo wengi wa Wazanzibar wamekuwa wakiiunga mkono serikali hiyo kwa kile wanachosema imerejesha maelewano, upendo, amani na kutokubugudhiana kama ilivyokuwa mwanzo.
 
Macho na masikio ya wapenda amani duniani kote wamekuwa wakifuatilia maendeleo ya serikali hiyo kwa kuangalia matokeo yake kufuatia kuundwa na hatimaye kuanza kuwatumikia wananchi wake hadi sasa ambapo imetimiza mwaka na zaidi sasa.
 
REDET ni Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia  Tanzania wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Ukiwa miongoni mwa wafuatiliaji wa maendeleo ya serikali hiyo ya Umoja wa kitaifa, Mpango huo umefanya semina ya siku mbili mjini Zanzibar kwa ajili ya kuangalia hali ya kisiasa katika visiwa hivyo ambapo mada kuu katika mjadala huo uliowahusisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, wasomi, wanasheria, watendaji wa serikali na watu wa kada mbalimbali ilikuwa   “Uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar”

Makamu wa Rais wa serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni miongoni mwa wanasiasa aliyechangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa mpango wa kuundwa kwa serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa, ndiye alifungua semina hiyo.

Mwaka mmoja wa SUK Zanzibar
Akifanya tathmini ya mwaka mmoja wa serikali hiyo, Maalim Seif anaanza kwa kutamka kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni imara na kuwa uimara wake unaongeza mafanikio ya wazanzibar na maslahi ya Watanzania wote.
 
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imetokana na matakwa ya wananchi wenyewe wa visiwa hivi, baada ya kuona mfumo uliopita yaani mfumo tenganishi hauna faida kubwa katika kujenga umoja na kukuza maendeleo ya Wazanzibari, ” anasema.
 
Licha ya uimara wa serikali hiyo, Seif anaweka angalizo kwa kusema kama ilivyo katika mataifa mengine, mfumo wowote mpya unapoanzishwa huja na changamoto mbali mbali, hivyo kuhitajika marekebisho ya hapa na pale, ili kuufanya uweze kufanikisha malengo yaliyokusudiwa tangu mwanzo.
 
“Uzuri ni kwamba Zanzibar ina fursa nzuri ya kuweza kujifunza kupitia sehemu nyingine za dunia, ambazo zina serikali zenye mfumo wa aina hii” anasema.

Anaendelea kusema kuwa, jambo la kutia moyo kwa kila aliyeuunga mkono uamuzi wa kuwa na serikali hiyo ni kuwa, katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa serikali shirikishi wazanzibar wanashuhudia faida nyingi.

“Faida moja kubwa ni maelewano makubwa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar. ..... kabla ya kuja kwa utaratibu huu tulikosa maelewano, hali iliyokuwa imesababishwa kwa kiasi kikubwa na kutofautiana kwetu katika itikadi za kisiasa na kukosa mashauri ya pamoja katika kuendesha nchi yetu na kujiletea maendeleo” anasema.
 
Anasema, Zanzibar iliyo chini ya mfumo wa serikali shirikishi wananchi wenye itikadi tafauti pamoja na viongozi wao, wanakaa pamoja wakishirikiana katika kila uwanja wa maisha na zaidi katika mambo ya kuwaletea maendeleo yao.

“Sina budi kukiri kwamba changamoto za hapa na pale zinatokea na hazitaacha kutokea, lakini kutokana na utaratibu tuliojiwekea kuweka maslahi ya wananchi wetu mbele, changamoto zinapojitokeza tunakaa pamoja kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka” anasema.
 
Maalim Seif anasema, Serikali ya Umoja wa Kitaifa badala ya kupoteza muda mwingi kushughulikia kutatua migogoro, muda karibu wote unatumiwa kufikiria, kubuni na kupanga mipango ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi ambapo anasema tayari wawekezaji wa ndani na nje wamevutiwa na hali hiyo na wamo katika mazungumzo na taasisi husika kuwekeza nchini humo.

Anaongeza kuwa, mafanikio ya makubaliano ya muafaka yalianza kuonekana katika uchaguzi wa 2010 ambao anasema ulionesha maendeleo makubwa katika uwanja wa kampeni, kwa vyama vyote kutumia haki yao ya kufanya kampeni bila ya vizingiti.

“Kampeni za 2010 zilikuwa za kiungwana. Pamoja na kuwa na hamasa, lakini kwa kiasi kikubwa hapakuwepo na malumbano, matusi wala kushambuliana. Kila mgombea alijikita katika kutetea sera na ilani ya uchaguzi ya chama chake na kujenga hoja za kuwashawishi wananchi watoe kura zao kwa mgombea na chama chake....   Haya ni maendeleo mazuri na ni wajibu wetu sote kuyaendeleza na kuyafanya kuwa bora zaidi” anasema.

Hali ya kisiasa Zanzibar baada ya SUK
Maalim Seif pia anaizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar baada ya kuundwa kwa serikali hiyo ambapo anasema ni shwari na kwamba ile tabia ya kupingana kwa sababu za kisiasa inaelekea kwisha kabisa, jambo analosema litawezesha serikali kufanya maamuzi kwa haraka na ambayo yatakubalika kwa wananchi wa mirengo yote mikubwa na viongozi wao.

“Kwa ujumla hali ya kisiasa ya Zanzibar hivi sasa ni shwari, na wananchi wanafanya shughuli zao za kisiasa, kijamii na kimaendeleo bila ya bughudha yoyote. ni maendeleo makubwa tukilinganisha na tulikotoka” anasema.

Anasema kuwa na Serikali ya Umoja  wa Kitaifa katika mfumo wa vyama vingi ni hatua kubwa sana, ambayo inaonyesha upevu wa kisiasa ambao utaiwezesha nchi hiyo kusonga mbele kimaendeleo kwa kasi zaidi.

Ile tabia ya kupingana kwa sababu tu za kisiasa imepungua sana na kuelekea kwisha kabisa, jambo ambalo litawezesha serikali kufanya maamuzi kwa haraka na ambayo yatakubalika kwa wananchi wa mirengo yote mikubwa na viongozi wao.

Anasema kutokana na matokeo hayo, sasa wawekezaji wanavutiwa na hali ya amani na utulivu ya Zanzibar, ambayo hujenga mazingira bora katika shughuli za uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa jumla.

Changamoto wanazokabiliana nazo
Anasema licha ya mafanikio hayo, zipo changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo na kusema miongoni ni kuwa wapo baadhi ya viongozi na watu ambao hawafurahishwi na Maridhiano ya Wazanzibari.

“Watu hao ni wachache. Baadhi yao wamekuwa wakijaribu kutia fitna ili kuvuruga maelewano, kwa bahati mbaya yako magazeti machache yanayotolewa Tanzania Bara ambayo yamepania kuleta chochoko ili kuvuruga kuaminiana kulikojengeka......Hata hivyo, kwa vile walio wengi wanaona umoja wetu huu una faida kuliko hasara watu hao hawatafanikiwa” anasema.

Anaeleza changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni katika kukidhi matarajio makubwa ya wananchi juu ya serikali yao, pengine kuliko hali halisi ilivyo ambapo anasema, wananchi wengi wanatarajia serikali yao itaweza kutatua kwa muda mfupi kero kubwa zinazowakabili katika maisha, kama vile mifumko ya bei za bidhaa muhimu na kuwepo hali ngumu ya maisha.
 
Hata hivyo anasema tokea serikali hiyo ilipoanza kazi imekuwa ikichukua hatua kubwa kuhakikisha ugumu wa maisha ya Wazanzibari unapungua, na wananchi kote Unguja na Pemba wanapata nafuu katika maisha.

“Uhaba wa fedha serikalini pamoja na hali isiyotarajiwa inayojitokeza ulimwenguni, kama vile kupanda kwa bei ya mafuta mara kwa mara, kushuka thamani ya shilingi dhidi ya dola, uharamia katika bahari yetu ya Afrika Mashariki, pamoja na majanga ya ukame na mafuriko katika nchi tunazozitegemea zaidi kununua bidhaa za vyakula, vitu hivi baadhi ya wakati huchangia kutofikiwa malengo yetu’ anasema.
 
Anaongeza kuwa serikali inachukua juhudi kubwa kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi ambapo wakati mwingine serikali hulazimika kupunguza kodi za bidhaa zote muhimu, kwa kuzingatia hali za maisha ya wananchi wetu.

No comments:

Post a Comment